10/06/2018

Jando (2)

Kama tulivyoandika katika kichapo cha kwanza (jando 1), wasungo wanatahiriwa porini, pahala ambapo si mbali kutoka kijiji. Huko ndiko wanaume pekee wanapojikusanya. Mwenye shughuli, ngariba na wafuasi wake huzunguka kitanda cha mayowe ambacho kimefunikwa na mkeka. Kitanda hicho kitakwenda kutumika tena porini penye utagala ambapo nyakanga atakilalia. Kabla ya wasungo hawajafika, kuna kaida na kanuni mahususi ambazo zinapaswa kutekelezwa. Ni hatua ambazo zinaonekana wazi katika video ya kwanza. Tunaona kwanza jinsi msaidizi wa ngariba anavyotayarisha jogoo yule ambaye atasogezwa kwenye mvungu wa kitanda ili kuhakikisha kwamba hakuna uhasidi. Huyo jogoo huchinjwa endapo mvungu huo haukaliki. Kisha ngariba anaomba ruhusa ya kutahiri. Ndio maana anawaita washiriki na wahusika wote wa shughuli. Hapo tunaelewa dhahiri kwamba tupo katika mapokeo fulani ya jando, ambayo yanaitwa, katika vijiji vya Kilwa, tarehe ya kina ncheni. Hiyo jando ni ya watu wa pwani tu ambao hufuata mapokeo ya Waswahili. Mbali na mavazi ya ngariba — kilemba na joho — na vifaa vyake — kipenga, kisu na mkoba wake — kitanda pia ni kipengele kikubwa cha jando ya kiswahili. Tofauti na bara, hususan katika tarehe ya ngariba wa vijiji vya Ngindo, ambapo mafundi wa tohara huvaa njuga, shanga na ngozi ya chui na hujipaka rangi nyeupe ya kipaji inayoitwa ungigo. Pia, ngariba wa bara hawatumii kipenga bali firimbi. Isitoshe, hawatumii kitanda bali wanatahiri chini, juu ya mkeka. Katika sehemu ya pili, tunasikia ngariba anavyoita wakuu wa nasaba zenye maana katika jamii ya kiswahili, mathalan ni Washirazi, Wamalindi na Masharifu. Wao ndio wanaobeba haki ya kuhalilisha shughuli hiyo huku ngariba akikabidhiwa kisu kutoka mwenye shughuli ambaye ni mzazi wa chando (mtoto wa kwanza atakayetahiriwa). Hatua hiyo ya mwisho kabla ya kutahiri inafuatwa na dua la kiislamu.
08/06/2018

Jando (1)

Katika enzi za kale, katika sehemu nyingi za Afrika, watoto walipokuwa wametimia umri fulani walikuwa wanapelekwa jandoni. Kwa kiswahili, tunasema kwamba watoto wanakaa kitako, ama kuwa wanakwenda kuhitiniwa ama kutahiriwa. Kwa kifupi, Uswahilini, watu husema kwamba wasungo wanakwenda kwenye ikidi. Siku hizi jando, kwa maana ya jando ya jadi, imekufa. Mimi mwenyewe na mwenzangu Ryo Nakamura kutoka Chuo Kikuu cha Fukuoka Japan, tuliwahi kuhudhuria shughuli hizo ambazo, wakati ule, zilikuwa zinahusisha watoto wa Kilwa na vijijini vyake. Katika shughuli hizo kulikuwa na hatua kadha ama tuseme vidato vichache vya kutimizia tokea siku yenyewe ya tohara hadi siku ya kukuwira yaani kurukwa kwa jando. Kwa jumla, watoto walikuwa kwanza wanatahariwa na fundi anayeitwa ngariba. Ndiye aliyekuja kutahiri wasungo kwanza kabla hawajafikishwa porini katika utagala (kumbi kwa kiswahili cha kamusi) ulioongozwa na nyakanga. Nyakanga ni kiongozi ambaye, kutokana na ufundi wake katika mambo ya uganga, hutoa mafunzo mengi yanayoambatana na maswala ya itikadi, usuli, tabaka la kijamii na mawasilianao ya kijinsia. Ndipo utagalani wari walipotawishwa muda mwingi, takriban miezi miwili, huku wakifundishwa jinsi vile wanavyopaswa kuzimudu asasi muhimu za jamii, ikiwemo lugha, maadili ya kienyeji na mambo mengineyo.

Katika michapo ya leo na ya siku zijazo, nimeamua kuchapisha vichache tu, vile vya kazi yetu tuliyofanya na mwenzangu Ryo Nakamura, ambaye ndiye aliyepiga filamu. Katika video hizi ndogo, tunaona jinsi ambavyo jamaa wote wa kijiji wamekusanyika uwanjani — katika mzunguko wa kijiji —, huku wakiwa wamepangana vizuri ili kumlaki ngariba. Ngariba yupo katikati, kivulini kwa mti, anaimba mwimbo uitwao « Alimanguto », huku akitegemea kufupwa au, kwa kiswahili cha mjini, kutunzwa. Watu wanamwendea, wanatoa senti chache, kisha wanarudi katika msururu wa watu. Katika nyimbo nyingi ambazo huimbwa, tunazikuta hizi zifuatazo :

1- Anapoingia Ngariba kijijini, siku moja kabla ya shughuli ya kutahiri, mwimbo huo unasikika :

Ori ! gae gae karitira
Ori ! gae gae karitira
Na mwari paranda

Ori ! Gaegae (baibui mkubwa sana) kaingia
Ori ! Gaegae (baibui mkubwa sana) kaingia
Mwari atakwenda porini

2- Asubuhi mapema, siku ile ya kutahiri, nyimbo hizi huimbwa :

Pambano ndipo pao
Ndipo pao unyago
Ndipo pao unyago

Hapo ndipo penyewe
Hapo ndipo shughuli

3- Kisha penye uwanja pale :

Ngariba :
Alimanguto leo !

Kiitikio :
Alimanguto mwanangu mwanja
Kisimani utamtuma nani ?
Kutuma utantuma nani ?
Kuchapa utanchapa nani ?
Kutukana utantukana nani ?
Kumfyonya utanfyonya nani ?

4- Anapokwenda kutahiri, ndipo ngariba anapoimba :

Tukimure kincheni nnore
Nnore tukimure kimasimba

Tuchapie, tucheze, mkaone
Mkaone tunacheza kisimba

5- Kisha :

Mwanjenu mwanja, mwanja
Nyaura malawi

Mwenzenu naondoka, naondoka
Wari, natangulia !
                                                                                 

01/06/2018

Ufaransa nchi ya mabwege ?


Hivi karibuni tumeshuhudia mkasa wa ajabu. Mkwezi kutoka Mali aliyekuwa ameingia Ufaransa kinyume na sheria ameonyeshwa kwenye runinga na mitandao ya kijamii huku akipanda kwa mikono mitupu ghorofa za jengo moja katika mtaa fulani huko Ufaransa. Alifanya vile kwa sababu ya mtoto mmoja aliyekuwa amejikuta ananing’inia penye ghorofa ya nne, nusura kuanguka chini kutoka roshani ya juu. Ndipo mkwezi huyo, kutokana na ushujaa wake, alipoamua kumwokoa mtoto huyo.

Tukio hilo hapa Afrika lisingeguswa, mbali na kushangiliwa, hata kidogo penye baraza za Waswahili wala mtu huyo asingepata sifa yoyote, kwa sababu moja kuu : Afrika wakwezi wako chungu nzima. Na wengi wana kupuu… Ndio maana hatuna budi kujiuliza, kwa nini jamaa huyo ametunukiwa kila kitu, hadi kupewa uraia (wengine wengi wameshasema kwamba atapata mke pia). Maana yake nini ?

Kwanza, msomaji ukiwa na mpango wa kukimbilia Uzunguni, shurti usiwe mtu mwenye akili nyingi, usiwe mtu ambaye umebobea katika taaluma za ndani, sijui usanii au sayansi. Hapana, ujasiri fulani utatosha. Msomaji usikonde, wewe pia unaweza ukafaulu : nenda kila siku penye klabu ukatunisha mishipa yako, ndipo huenda utakapopata nafasi ya kupata visa ya kuingia kwa Mamtoni. Kusoma ? Acha tu, kumepitwa na wakati. Wafaransa ni mabwege, hawajui lolote. Isitoshe, wanaacha watoto wao katika hali ya hatari. Katika nchi za Afrika zenye lugha ya kifaransa, mpaka leo hatuachi kucheka, mbavu zinawauma watu. Kejeli na dhihaka chungu nzima zinarushwa. Kama katuni hiyo ifuatayo :

Ufaransa : tayarisheni madokumenti, tuko njiani,
tunakuja !

Pili, huyo kijana mkwezi amepewa taadhima kubwa sana. Mpaka rais ya Ufaransa amemkaribisha ndani ya Ikulu, ambapo siku hizi ni kibanda cha mabwege wanaotawaliwa na Vizito vya Yuropa, si mnamfahamu mama Merekeli ambaye siku hizi anapiga mnada mkubwa sana ? Yeye ndiye aliyeanzisha biashara hiyo ya kuingiza katika nchi za Ulaya watumwa kutoka Afrika. Utumwa mpya lakini, si ule wa zamani. Siku hizi huo utumwa ni halali, hamna shida. Human righti, bwana ! Watumwa hawa wanatakiwa kuhitimu shahada yao ya kupiga domo-kasia ndani ya mashua ya kuvukia bahari ya Mediteranea. Wakishavuka bahari hiyo, pale ufukeni watawakuta wale mabwege wakiwasubiri na hundi, chakula na misaada mbalimbali. Hamdulilah !

Uhispania tayari kupokea "wahamaji"
"Poa, stroberi zetu zitachumwa"
Tatu, usiwe na taharuki kama hujapata kibali chako. Iko siku, utapata. Tufanye mambo kwa zamu na nidhamu. Utapata kwa sababu Ufaransa tayari ni nchi ya kiafrika. Na kama umesoma darasani kwamba Afrika ina nchi 54, ujisahihishe sasa, ziko 55, pamoja na Ufaransika. Hiyo ni dhahiri. Wacha nikufahamishe. Hapa Afrika mtu yeyote mgeni, awe msomi, mtu hodari sana katika taaluma au ujuzi fulani, ama, kwa mfano, awe na umahiri fulani katika kuimudu lugha mojawapo ya kiafrika, huku akionyesha kwamba anajua kimakonde au kiswahili kushinda hata mwenyeji, basi thubutu, kupata uraia haiwezekani. Huyo mgeni hatakiwi, kama alivyo mgeni msomi huko Ufaransa siku hizi, kunradhi Ufaransika. Na kweli ukichambua zaidi, mfano Tanzania, utagundua kwamba Mbanyani tu kutoka Kariakoo ndiye ambaye hupata uraia wa Tanzania, pengine kupitia hongo na ubani chungu nzima. Huyo ndiye mkwezi wa Tanzania.

                                   

Jamaani, msikonde, visa zitapatikana. Na kama mnataka kupeleka watoto wenu huko Juu, kwanza msisahau kwamba Ufaransa nako ni nchi yenye shule (za mabwege) huko kwenu. Mkazitafute basi, just in case unataka kujifunza maneno mawili matatu ya kifaransa… yatatosha hayo, si unajua Ikulu siku hizi, wanataka kuajiri mfua dafu !

Lakini mkitaka kupata vibali haraka haraka, msomaji unaweza kufululiza barabara ya Ali Hassan Mwinyi rodi mpaka utalikuta jengo la Ubalozi wa Ufaransa… lakini usijaribu kuchupia ukuta wake ! Usifanye haraka…

Picha hizo za chini zikionyesha jamaa wa nchi mbali mbali za Afrika magharibi wakiwa sasa wanafanya mazoezi huku wakijaribu kupanda majengo… just in case !