10/01/2013

HISTORIA FUPI YA KILWA KATIKA MAANDISHIKilwa Kisiwani ni jina la kijiji kikubwa kwenye Kisiwa cha Kilwa karibu na mji wa Kilwa Masoko katika Mkoa wa Lindi, Tanzania. Ndipo mahali pa mji wa Kilwa ya kihistoria iliyokuwa mji mkubwa kabisa kati ya miji ya Waswahili katika pwani la Afrika ya Mashariki wakati wa karne za 12-15 BK. Kwa hivyo, Kilwa ilikuwa mji mkuu Afrika mashariki kabla ya wazungu hawajafika kwenye bahari kuu la Hindi. Kwa mujibu wa tariki ya Kilwa ambayo ni miongoni mwa matini ya kizamani sana yanayotoa historia fupi kuhusu sehemu hii ya Tanzania, Kilwa ni mji ulioanzishwa na kusimamishwa na wahamiaji kutoka Shiraz, huko Uajemi kwa siku za leo. Ni dhahiri kwamba matini haya ambayo jina la mtunzi wake limepotea ni aina ya masimulizi ya kusisimua akili ya msomaji kwa kuwa na hadithi ya kibuni. Kwa hivyo, ingawa yana maudhui ya kuvutia sana kutokana na ushuhudio wake muhimu sana, tariki hizi hazisomeki kama insha ya kisayansi ambayo itakuwa imeandikwa kufuatana na nadharia tete yenye uthabiti. Mintarafu asili ya wahamiaji wa kwanza ambao walifika Kilwa, hatuna uhakika kwamba walikuwa wanatoka Uajemi, kama inavyodaiwa na tariki hii. Hapo tuwe makini sana.
Kwa mujibu ya tariki hizi, inasemekana kwamba Sultani mmoja aliyeitwa Hassan bin Ali kutoka Shirazi ndiye aliyehama kule kwao wakati wa kuibuka aina ya mgogoro kati ya watu wake. Sultani huyo akaamua kuondoka na watoto wake sita. Kuondoka kwao huko kwenye bandari ya Siraf, walisafiri kwa jahazi saba kuelekea Afrika mashariki. Hapo inaaminika kuwa kila wakipita kwenye bandari ya kanda ya pwani, mmojawapo alivunja safari yake huku akiaamua kuweka misingi ya mji wake. Ndiyo asili ya miji saba ambayo tunayo mpaka leo kwenye kanda ya pwani ya afrika mashariki : Mandakha, Shaughu, Yanba, Mombasa, Pemba, Kilwa na Hanzuân. Sultani mwenyewe alikuwa wa mwisho katika kusalia katika msafara huu, naye akakaa kisiwa cha Hanzuani ambacho kipo Ungazija. Mikasa hii na tukio hilo limejitokeza katika miaka kuanzia 957 mpaka 985 baada ya K. Inaaminika kwamba Kilwa wakati ule kilikuwa kisiwa kilichomilikiwa na wenyeji waitwao wamuli. Kwa kuwa walikuwa hawana nguvu nyingi, walikubali kukiuza kisiwa chao kwa kukubali kupewa vipande vya ntandio. Hapo ndipo Ali bin Hussein alipochukua kisiwa hiki kwa ajili ya kukaa ikiwa ni pamoja na kujenga majumba ya kujitetea dhidi ya watu wa bara na miji mingine ya pwani.

Kati ya mwaka 957 hadi 1131, Kilwa uliwahi kupambana na mji jirani uliokuwa unaitwa, kwa enzi zile, Shagh. Ghasia zile zikakolea, zikawa zikageukia zikawa vita kwa ajili ya kutawala himaya kubwa. Kilwa ukawa na sifa za fahari katika pande zote za Afrika mashariki kutokana na nguvu zake na mali yake ambayo ilikuwa inatoka bara la Afrika, pahala panapoitwa Sofala. Dhahabu ya Sofala, ambayo ilikuwa ni baadhi ya madini iliyopatikana kwa wingi wakati ule, ilikwenda kuchukuliwa na kuletwa Kilwa kwa njia ya kutembea kwa miguu. Misafara hii ilikuwa changamoto kubwa sana katika kutajirisha himaya ya Kilwa. Hapo yupo mwandishi mwingine katika lugha ya kiarabu, Al-Mutahar bin Tahir al Makdisi, ambaye vile vile anatoa ushahidi mzuri wa kwamba nchi ya zenj – ambayo ni sehemu hii ya kanda ya pwani kwa enzi hizo – ilichangia sana katika usafirishaji wa dhahabu kutoka Kilwa kwenda Uarabuni kuanzia karne hii ya 10. Kwa kifupi, wataalamu wa historia wamekubali kusema kwamba kilele cha Kilwa katika kujifaharisha kilianza karne 12 ikadumu hadi karne 15. Kilwa ikawa muhimu zaidi kuliko Mombasa. Biashara yake ilikuwa dhahabu kutoka dola la Mwene Mtapa (Zimbabwe), pembe za ndovu, chuma, nazi pamoja na kununua bidhaa kutoka bara Hindi na Uchina. Sarafu ya dhahabu kutoka Kilwa imepatikana huko Zimbabwe Kuu.
Baharia maarufu ambaye pia alikuwa ni mwana historia hodari sana, Ibn Battuta, anathibitisha vilevile kwamba dhahabu ilikuwa inapatikana pia katika eneo lililoitwa Yufi, nchini mwa Limi (nchi ya kiajabu ambayo wataalamu wengine wanakisia ni pengine Nigeria). Zama zile zilikuwa za kudhabiti utawala wa Kilwa ambao ulipanua mpaka Mafia, Zanzibar na Pemba. Sultani Suleiman bin al-Hassan (1170-1189) aliwahi kukarabati majengo makubwa ya Kilwa kisiwani. Anajulikana sana kwa ujenzi aliouanzisha chini ya utawala wake ambao unaitwa Husuni mdogo. Enzi hii bado ilikuwepo chini ya nasaba (dynastie) ya Shirazi mpaka mwaka 1277, ambapo ni kipindi cha awamu nyingine iliyojitokezea katika nasaba ya Mahdaliya ambayo ilitoka Hadramau, Yemen. Karne 14 na mwanzoni mwa karne 15 zilikuwa nyenzi za fahari kubwa sana kwa sababu ya kufaidi na kujiimarisha kipindi kile cha nyuma ambacho Sultani Al Hassan bin Suleiman II (1331-1332) alipopata nafasi ya kuongeza nafasi ya kuswalisha swalat al ijumaa ikiwa ni pamoja na kujenga kasri inayojulikana kwa jina la Husuni Kubwa. Kipindi kile kilikuwa cha kuagizia vyombo vingi kutoka nchi za kigeni, hususan ghuba ya Uajemi na Uchina. Viongozi wa awamu zile waliwahi pia kutengeneza sarafu zenye chapa na vitu vinginevyo vya shaba. Lakini kati ya 1466 hadi 1476, Kilwa iliingia katika kipindi cha kuyumba yumba kwa sababu ya vita ya ndani. Kutokana na hali hiyo ya kufarakiana katika kugombea nafasi ya kutawala, Kilwa ilipoteza baadhi ya majimbo yake, ikiwa ni Zanzibar pamoja na Sofala.

Wakati Vasco de Gama, baharia mashuhuri kutoka Ureno, alipopita katika eneo la Kilwa mwaka 1498, mji huu ulikuwa umeshapoteza sera yake. Wareno walijikalia kwa kipindi kirefu, takriban miaka mia mbili, huku wakijenga aina ya gome ambalo linaitwa Gereza. Uharibifu wa Kilwa ukawa mbaya zaidi wakati mapigano kati ya makabila yalipozuka bara kutokana na mashambulizi ya watu waliokuwa wanijiita Wazimba (kutoka Zimbabwe). Vita kubwa ilitokezea Kilwa mwaka 1587 ikawa ikabadilisha ramani ya kiutawala katika sehemu hii ya Afrika. Kuanzia hapo Kilwa ulishindwa kurudi katika hali ile ya mwanzo, ukatumika tena kama kituo cha biashara. Kuja kwa Wareno katika Karne ya 16 ilivuruga biashara ya watu wa pwani. Kilwa ikarudi nyuma. Katika karne za 18 na 19 hali yake ikawa nzuri tena kutokana na biashara ya watumwa iliyofanyika wakati waomani walipopata fursa ya kutawala eneo lote la pwani. Hapo ndipo Kisiwani ilipopata jengo kubwa linaloitwa Makutani ambalo lilitengenezwa upya mwaka 1776. Lakini ijapokuwa Kilwa iliwahi kufufuka kiuchumi kipindi kile, haikushinda sana katika kujitetea wakati majambazi wa baharini watokao Madagascar, Wasakalava, walivamia Kilwa na Mafia, hasa mwaka 1822. Wakaazi wengi wa Kisiwani walihamia mji wa Kivinje ili kujinusurisha. Biashara ya watumwa iliposimamishwa ndipo utajiri wa Kilwa ulipoanguka. Leo hii Kilwa Kisiwani ni kati ya Hifadhi ya Kiutamaduni muhimu sana za Tanzania, nayo imeandikishwa katika orodha ya UNESCO ya « Urithi wa Dunia » (World Heritage).

Makala hii imeibwa ikahamishwa kwenye tovuti ya Jamii Forum HAPO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni