15/01/2013

UROGOLOJIA WA KARL MARX


.

Kuhusu : « Historia ya mswahili na fungamano za kiitikadi na kiuchumi », Ibrahim N. Shariff, Alamin Mazrui, kutoka katika Historia fupi ya Zanzibar, K.S. Khamis, H.H. Omar (hariri) © idara ya Nyaraka, Makumbusho na Mambo ya kale, Zanzibar, 1994 : k.130-142.Hivi karibuni nimetoa kijitabu kidogo kutoka kwenye rafu yangu nyumbani. Kijitabu hiki kilikuwa kimefunikwa na vumbi na takataka nyingine kwa kutokusomwa. Kwa kuwa nilikuwa sijakisoma, na kweli hakina kivutio ukichungulia sura yake, nikaanza kukikong’ota na kukipangusa nikakifunua chapu chapu huku nakifikia mwishoni mwake. Nikakuta makala moja ya Profesa Shariff ambaye si mgeni kwangu. Pepa hii inaitwa « Historia ya mswahili na fungamano za kiitikadi na kiuchumi ». Kwanza kilichonishangaza ni kuona kwamba Profesa huyu maarufu anajua kusoma na kuandika kwa kiswahili. Nilikuwa mbali sana kwani nilifikiri kwamba Tanzania mtu yeyote akiwa na education, lazima atumie kiengereza (cha kibiashara ? au kibepari ?). Isitoshe, hapo hatuna budi kumvesha kilemba Profesa yetu kwa kutotumia mabombastiki kama ilivyo kawaida wakati maprofesa waliopanuka kichwani wanapotoa mihadhara ya kitaaluma. Kiswahili chake hakina maroroso, hata mimi mlami nimeingia laini, mambo poa.
Ili mradi msomaji aelewe vizuri kinachoongeleka katika makala hii, nitaanza kuchana sehemu ndogo ya utangulizi wa kitabu hiki ambacho kimekusanya matini mbalimbali ya waandishi maarufu wa Tanzania na maeneo mengine duniani. Mtangulizi anaandika :
« ... wasomi hao wanaona, kwa bahati mbaya kasumba iliyoletwa na Wazungu, bado inaendelezwa na tabaka tawala za mataifa huru yanayotumia sana kiswahili ili kufanikisha malengo yao ya kisiasa. Wakati nchini Kenya Waswahili wametumbukizwa katika kapu la makabila mengine ili kuua utambulisho wao, katika Tanzania utambulisho wa Mswahili umegubikwa na kugaiwa taifa zima na hivyo Watanzania wote wamefanywa kuwa ni Waswahili, jambo ambalo kwa madai ya Wasomi hao si haki. Wasomi hao wanamalizia kwa kuonyesha msimamo wao unaothibitishwa na maandishi ya kale kuwa waswahili wapo na wameelezwa kuwa ni jamii ya watu maalum waliokuwa washupavu katika kulinda haki na uhuru wao » (uk. IX, X).
Hapo kwa kweli msomaji tuko kwenye kitimoto !
Kabla sijaendelea kudadangia mahoja kadhaa yaliyomo ndani ya makala hii, msomaji anapaswa kwanza kudokoa dokoa baadhi ya maneno yanayotumika hapo katika dondoo hili ambayo yanaonyesha wazi kwamba kitabu hiki kinatumia msamiati maalum (« kasumba (ya kikoloni ?), watu ama wanatumbukizwa au wanagubikwa »). Tukichambua zaidi tini lile la Bwana Shariff tunahisi kwamba kihistoria lina vishawishi vingi vya kuweza kumzuga msomaji na kuteka akili zake hasa kama msomaji hana kipaji chochote katika fani hii. Kwanza bwana Shariff anajipa utukufu mkubwa sana kwa kuanzisha makala yake kama hiyo :
« Utambulisho wa waswahili umezusha mjadala mkubwa miongoni mwa wataalamu kwenye mikutano iliyofanyika hapa afrika ya Mashariki na nchi ya nje ».
Hapo msomaji sitaficha mshangao wangu mkubwa kwa kusema kwamba utaalamu kama huu, ingawa pengine una faida yake katika vikao na taasisi mbali mbali ya Tanzania na nchi za kigeni, hauna ufahari wowote wala sifa yenye ufanisi kwa kukosekana wasomaji, washiriki au washabiki, hasa katika nchi za Ulaya. Msomaji lazima ajue kwamba Ulaya mtu kwa kawaida anazingirwa na mamilioni ya vitabu venye thamani kubwa wala hajaona kivutio chochote kuhusu « mjadala huu mkubwa ». Hata vitabu vya waandishi maarufu wa Tanzania kama vile vya Ibrahim Hussein au Kezilahabi ambavyo vinastahili kupewa umaarufu duniani, havijapata nafasi hiyo. Kwa hivyo midahalo ya kihistoria kuhusu Tanzania, bado...
Pili hatuna budi kumhadharisha msomaji kwamba kihistoria makala hii haina uthibisho wa kutosha, aidha umewekwa juu ya misingi ya aidelojia. Mathalan kwa kutaja tariki na madondoo ya wafanya biashara wa zamani, bwana Shariff anaonyesha wazi kwamba anataka kuelekeza na kuongoza akili ya msomaji asije akaelewa historia husika kama inavyotakikana. Na kweli katika kutaja maneno ya wafanya biashara wa zamani, wawe waarabu au wazungu, ingalibidi awe makini sana kwa kuwa maneno hayo yanaakisi mitizamo na muono wa watu wa enzi zile, sio kwamba yanatuletea ufahamu halisi wa muktadha wa kisiasa jinsi ilivyokuwa wakati ule. Kwa mfano, maneno ya bwana Stigand yanaonyesha kwamba mwenyewe ni gozi, lakini yanaleta ufahamu gani katika kupima na kusoma historia ya Afrika mashariki ? Na yanaleta ufahamu gani kuhusu « itikadi za wazungu » wa enzi ile, kama anavyodai Profesa yetu ?
Kwa kifupi, tukitaka muhtasari wa maelezo yake, hatuna haja hapo ya kudodong’oa mahoja yake yote kwani ni dhahiri kwamba yanalenga lengo mmoja tu, nalo ni kuonyesha kwamba wazungu waliokuja kuitawala sehemu hii ya Afrika mashariki zamani walikuwa ni watu gozi wa kuletea kinaa wakati waarabu walikuwa hawana noma. Kihistoria, makala yake haizidishi ufahamu wa Afrika mashariki, haina upya ila imezidiwa na ubatilifu. Hata hivyo, kwa msomaji tunaweza kuifupisha kama ifuatavyo. Bwana Shariff anasema kwamba :
·      waswahili (yaani watu wa mwambao) walikuwepo kabla ya wazungu hawajafika : enzi ile ilikuwa ya utamaduni wa hali ya juu, hata Shakespeare ni ruya ya mtoto.
·      wakaja wazungu, wakatawala kiukoloni, wakatunga sheria kali, wakapuuza wenyeji kwa kuwadharau na kuwabagua, waswahili wakawa watu duni. Kila kitu kikaangamia.
·      wazungu wakaondoka, uhuru ukapatikana, lakini uswahili (yaani utambulisho wa watu wa pwani) ukatoweka Tanzania, na ukawa kama mofa ndani ya jani la mgomba huko Kenya, yaani si lolote si chochote.
·      ingawa kwa watu wengi siku hizi mzungu ni posho na mshiko, yaani mzungu ni mtalii mwenye kaptula anayejikrimu kwa sababu ya jua kali la kiswahili, kwa mujibu wa Prof I. uzungu bado ni sumu uliomo ndani ya fikra ya watu, umejikita (kwa mujibu ya maneno yake babu). Wapwani (pole, waswahili), na wabara ( ?) hutengana kwa sababu ya mzungu ?
Kwa kufindikiza (samahani msomaji kwa neno hili la kinabo) hapo, nitaongeza moja la kwangu kwa kuwa ni dhahiri kwamba mzee Shariff amejizuia kidogo lakini bila shaka angalikubali hilo : Tanzania ukatili na ufisadi bado vipo, kama vile ugoni wa madenti, uchawi dhidi ya maalbino, utapeli wa kiserikali, uchafuzi wa mazingira, n. k. Unajua kwa nini, msomaji ? kwa sababu ya mzungu. Profesa Shariff angeichana kauli hiyo katika pepa yake isoyokuwa na maroroso. Yes. Kanaandika kwa kiswahili, tena ! Duh !
Makala hii imejaa vichekesho ambavyo si lazima vyote vitajwe hapa. Kwa mfano tunapasua kichekesho kikubwa hapo anaposema :
« ...wareno ndio walioweka msingi wa mbabaiko ulioendelea mpaka sasa kati ya kumtafautisha mswahili, mwarabu na mahusiano yao » (uk.135).
Lingine hapo :
« ... si captain Stigand peke yake ambaye alikuwa mkaburu bali wakati na mazingira yenyewe yalikuwa ni ya kigozi na kikaburu... » (uk. 138)
Tena imeandikwa kwa rangi nyeupe na nyeusi !! Stigand, eti ni mzungu ! Kwangu kabla ya kuwa mzungu, ni mpumbavu. Jina lake na sifa zake visingetajwa katika kitabu hiki kinachojitia hadhi ya kupambana na mahoja makubwa kama hayo. Sio kwamba nataka kukanusha kwamba alikuwa ni mbaguzi, lakini Stigang alikuwa ni mtu wa kawaida, si Leonard de Vinci wala Shakespeare ! Inakuwaje mheshimiwa Profesa, tena si Profesa Juha wala Kalulu, amekubali kujitia makaa mpaka kumtaja habisi huyu ? Hata kama Stigand alikuwa mbaguzi kishenzi, muuza chapati wangu pia ni gozi ! Ugozi ni jambo la kawaida katika dunia hii. Huyo Stigand mwenye hadhi kubwa sasa kwa sababu ya Prof Shariff anastahili kutajwa katika makala hii, mboni ? Kwa nini Prof yetu kanamgaia hidaya hii ya kuweza kufufuka ilhali mpumbavu huyu kafa zamani, tena fofofo ? Profesa mwenzetu amefanya utafiti mkubwa, bila hata kutumia nadharia, walahi ! Tokeo limepatikana hapo : gozi Uzunguni lipo. Hivyo ? Afrika je ? Babu kajitahidi.

Hapo ndipo yananijia maswala chungu nzima. Mojawapo ni hili : hadi lini utamaduni, vitambulisho, ngozi, nywele, kucha, uzeruzeru vitakuwa chanzo cha kutenganisha watu na kuzidisha ufisadi baina ya watu duniani ? Mboni katika dunia yetu hatugombani tena kisanii, kihekima, kishairi ? Mzee Shariff anadai kwamba wakoloni walizusha au walififiliza sifa ya makabila mbalimbali yaliyosthahili kuwepo au kutokuwepo. Ya nini ? Si ilikuwa enzi ya ukoloni ambayo sasa imepitwa ? Eti waswahili wapo ! Sawa, hata kama si kweli, kimezidi au kimepungua nini hapo ? Mimi ni mfaransa lakini ningalikuwa na kitambulisho hiki pekee, ningalikuwa mnyonge. Hapo nilipo Ufaransa, nchi ya falsafa, riwaya, ushairi na usanii wa aina nyingi tangu karne 11, watu wengi katika wasomi (ambao wanampuuza kina Stigand) bado wanabaki mdomo wazi wakiambiwa kwamba wasanii wa kifaransa wako. Ingawa tunao washairi, hatuna ushairi wa kifaransa. Usanii huu wote umekopea lugha na tamaduni nyingi zikiwemo Ugiriki, nchi za kiarabu, Asia, na kadhalika. Sio kwamba wafaransa ni mabastadi – ingawa ningalikubali vijembe vya Stigand laiti angalizumgumzia wafaransa badala ya waswahili – kwa kuwa tunajisikia vizuri na kasoro hilo. Katika urithi wetu, hapa Ufaransa, tunajiona vizuri kwa kuweza kusema kwamba Mohamed Dib, Edmond Jabès, Andrée Chedid, Hampaté Bâ ni miongoni wa wasanii tunaoweza kuhesabu katika kasumba yetu. Wala hatujali kama ni waarabu au waafrika wala mtu wa mwezini. Homere, Aristote na Plato si wagiriki, ingawa walizaliwa Ugiriki. Usanii, falsafa, ushairi havina ukabila wala utambulisho. Hapo nahisi kwamba tuko wengi (wafaransa, waswahili, wananiu, waglagla...) katika kukiri kwamba tunatofautiana na mzee mheshimiwa Profesa Shariff kwa sababu kihistoria tuko wengi tunaokubali kujiangalia katika macho ya wageni. Hapo nitachukua njia ya mkato katika kuuliza : je, nini ni muhimu katika jamii, kuwa na hekima (kif. culture de l’esprit, kieng. wit ; kigiriki : paideia) au kuwa na kitambulisho ?


Ni dhahiri kwamba makala hii isiyokuwa na misingi ya kihalisi, kwa upande mwingine ina vivutio kadhaa. Kimojawapo kinarudi kila mara katika mjadala wake kama dhana ya kirumba nayo ina uthabiti wake imara. Prof Shariff anasisitiza kwamba kila jamii hutegemea sana mazingira yake na historia yake, nazo ni muktadha wake, katika kuzusha itikadi zake. Kwa mfano anatueleza kwamba wakati wa ukoloni, itikadi za wareno zilikuwa tofauti na zile za kijerumani. Hapo hatuna budi kumwunga mkono Bwana Shariff. Lakini pia inabidi tujiulize hapo : waswahili na waarabu walikuwa na itikadi gani ? Hapo msomaji anahisi kwamba mwandishi hajasogeza utathmini wake kwenye mstari wa mbele au huenda kwamba mawazo yake yote yamechukuliwa na nadharia kinyongo. Hapo tunapofanya uchambuzi tosha, wala si wa kina sana kwa kuwa ni dhahiri kwamba Profesa Shariff ni msomaji maarufu wa Karl Marx, tunagundua kwamba Profesa yetu anataka kuthibitisha kwamba mtawaliwa yeyote katika dunia hana itikadi yoyote. Ina maana kwamba waarabu – kwa kutokuwa na itikadi - hawakutawala Afrika mashariki ? Au utawala wao ulikuwa wa kupigana denda kama wanavyofanya wazungu ? Wakubwa, yaani wakoloni (vigogo wa siku hizi je ?), ndio watu wenye itikadi haswa. Hapo msomaji hatuna budi kukiri kwamba tumejitosa katika bahari ya aidolojia tupu. Ama kweli political correctness haina mipaka.
Jambo hili lisingekuwa la kuzingatia hapo ikiwa Prof Shariff angetumia dhana badala ya kauli. Kwa maneno mengine angesoma Plato kuliko Karl. Au pengine mzee Shariff hajatoka katika pango la Plato ? Katika kughushi maelezo yake kwa kuyatilia kaputi, yaani kwa kufunika itikadi za msingi zilizomo ndani ya hoja yake, anatuchukua kimzobezobe. Ndipo itikadi yake inapojidhihirisha. La kushangaza ni kwamba itikadi yake inafanana na nyingine ambayo imejikita sana ndani ya fikra za waswahili ( ?) nayo ni urogolojia (itikadi ya uchawi). Urogolojia na umarxisti zinafanana kinamna fulani na zinapishana kwenye krosi ya itikadi kwa kufuatilia nadharia tete moja kama ifuatayo : likitokezea tatizo au maafa ya aina yoyote katika jamii, ufafanuzi unapatikana papo kwa papo, wala hauna haja ya kwenda kutafutwa katika undani wa mambo. Hapo Bwana Shariff anatusaidia mfano mzuri : Tanzania na nchi nyingine zinanyanyaswa kwa sababu ya ubepari na ubeberu (chanzo cha nje). Sio kwamba watanzania hawaendelei kwa sababu hawana nidhamu wala elimu (chanzo cha ndani), au kwa sababu mfumo wa siasa Tanzania umeborongwa kwa rushwa nyingi, hapana. Chanzo cha matatizo yanayoikumba nchi hii kinapatikana katika shinikizo za kipebari au katika mazingira haya ya ukoloni mamboleo ambazo zinatoka katika sababu ya nje. Maelezo hayo yanafanana na mengine ambayo ni ya baraza ya kimtaa na huzungumzwa kila siku hapa na pale Tanzania, nayo ni urogo. Hapo unakuja mfano mwingine : endapo mkaazi wa kijiji chochote wa nchi hii hajachuma chochote katika shamba lake, si kwa sababu ya uvivu au uzembe wake bali ni kwa sababu ya mtu mwingine (chanzo cha nje) mwenye choyo na husuda za kuweza kuwaangamiza wenzake. Usiseme kwamba mkulima huyu ameshindwa kwa kutokuwa na akili (chanzo cha ndani), au kwa kuwa hajasoma, hapana. Bila shaka, yupo mrogi mwenziwe anayetaka kumnyanyasa au kumroga. Wamarxisti na waliorogwa wa nchi zote, tuwe pamoja katika kupambana na ubepari au uchawi, huo utashindikana na kisha utakoma, jii !
Hapo nitakuwa sina zaidi kuhusu makala hii ila natumaini kwamba msomaji atafahamu vizuri kwamba msomi yeyote anaweza akawa mtatanishi wa hali ya juu wakati usomi wake umeingiliwa na siasa na itikadi. Kwa kumalizia hapo nitapenda kuchukua fursa hii ili kumpongeza Profesa yetu kwa kututunukia mafinyufinyu kibao. Tunafikwa na mshangao mkubwa kwa kuwa Profesa Shariff amejulikana sana katika dunia yetu kwa kuwa na msimamo wa kimarxisti tangu kuzaliwa kwake. Bila shaka hapo tunahakikishwa kwamba hakunyonya maziwa ya kibepari jandoni. Wakati dunia yetu inazidi kuzinguka kavu kavu, na kweli mambo yanazidi kwenda songombingo, wakati watu hutafuta riziki yao kwa kupuyanga puyanga kama kuku, wakati kila kukicha tunaamka katika dunia inayozidi kwenda mrama, yaani haina suka wala konda, yeye bado yumo, humo humo, katika sanduku ya hirizi ya Karl. Ama kwa kweli, mzee Sharif ni mswahili... Tumfagilie baba ntilie mwenzetu, wawaa !
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni