06/09/2013

HIFADHI YA AMANI KATIKA MILIMA YA USAMBARA


Kutokana na ongezeko la watu duniani ambalo ni tishio kubwa sana inayoweza kuathiri mazingira yetu, si rahisi kuona tena eneo la mazingira asiliya ambalo halijaguswa na binadamu. Sisi sote, mbali na uraia au asili yetu, tumefikwa na changamoto kubwa sana kwa sababu nafasi ya kuishi katika mazingira safi yenye utajiri kiasiliya inazidi kupungua kila siku. Sisi sote tunataka kukaa katika nyumba nzuri, kupata umeme na maji, kuendesha gari na kupanda ndege, kustawisha mimea na kuchuma mazao mengi kushinda mahitaji yetu, na hali kadhalika. Wakati wa kupendelea hivyo, tuna kawaida ya kujiangalia tu kiubinafsi huku tukipuuza viumbe wanaoishi katika mazingira yetu kwa kufikiri kuwa hawana faida. Hilo ni janga kubwa sana ambalo linatukabili sasa kwa sababu mara nyingi tunakosa elimu ya kutosha.

Kwa bahati nzuri, Tanzania bado ina sehemu asiliya ambazo zinaelekea kuwa hifadhi nzuri, lakini tukizingatia hali jinsi ilivyo kwa mtizamo wa juu juu tu. Hususan hifadhi ya Amani, katika safu ya milima ya Usambara ni miongoni mwa misitu ya asili ambayo serikali ya Tanzania imeamua kuitilia maanani kwa sababu ya thamani baioanuai yake kubwa. La kusisitiza kwanza ni kwamba eneo hilo, pamoja na kwamba lina sehemu nyingi za mazingira asiliiya, vile vile lina watu wengi ambao huishi huku tangu zamani. Si la kushangaza basi, hasa katika muktadha hii, kuona kwamba sura ya milima yake ina vipande vipande vya mashamba ya mchai, ambavyo ni tange zinazomilkiwa na watu, pamoja na miti mingine ya kuleta mapato kwa wakaazi wake. Ina maana kwamba maeneo makubwa sana ya asiliya tayari yameshapotea kusudi binadamu aweze kuchuma mazao yake ya kilimo (hasa mchai, mkarafuu, muwa, mdalasini, mahindi na kadhalika). Siyo kwamba wakaazi hawana haki ya kushughulikia shughuli zao za asili (kulima, kukata kuni, kuchuma miti ya porini, na kadhalika), ila msomaji aelewe kwamba binadamu akizidi kukiuka mipaka ya majukumu yake, yaani akizidi kutumia ardhi anakoishi kupita kiasi, athari juu ya mazingira kwa jumla itakuja kuwa ya kiangamizi.


Kwa kifupi, changamoto kwa siku hizi ni hilo : kutunza mali ya watu bila ya kuangamiza yaliyobaki katika mazingira asiliya. Na kutokana na hali hiyo ya utele, utele wa watu, utele wa nyumba, utele wa gari na kadhalika, imekuwa kama kwamba dunia imekuwa finyu zaidi kila kukicha, kiasi cha kukatisha tamaa ya wataalamu ambao wanajitahidi, kila siku, kuwaelimisha watu ili watunze mazingira yao. Kinachobidi sasa ni kujipatia muamuzi mwafaka ambao itakuwa aina ya suluhisho endelevu kwa watu ambao wamebahatika (ingawa hawajajua kwamba ni bahati) kuishi katika mazingira asiliya mithili ya milima ya Usambara. Watu wana haki ya kuzalisha mazao yao ya kilimo lakini pia wanapaswa kukiri kwamba wanyama wadogo kama vile spishi fulani ya ndege au reptilia ambao ni waendemiki wa Usambara wanastahili kuishi na kuwepo kwa enzi zijazo. Je kweli hilo litawezekana wakati tunaambiwa kwamba asilimia 50 ya misitu imeshapotea ?

Wanyama wa msitu

Wanyama wengi huishi katika milima ya Usambara. Katika jamii ya mamalia, eneo la Amani limesharekodi aina 60 ya spishi mbali mbali, kuanzia panya mdogo hadi nguruwe msitu. Mtembezi huenda atakutana na « nyani wa njano » (kg. yellow baboon, kl. Papio cinocephalus), ni rahisi kumkuta kutokana na tabia yake pole sana. Pamoja na nyani huyo, wanyama wengine wanaoonekana kwa wingi ni kama : mbega (kg. Angola pied colobus, kl. Colobus angolensis), kima bluu (kg. Blue monkey, kl. Cercopithecus mitis), nende mwenye miguu mekundu (kg. Zanj sun squirrel, kl. Heliosciurus undulatus), nende wa milimani (kg. Tanganyika mountain squirrel, kl. Paraxerus lucifer), nende wa pwani (kg. red-bellied coast squirrel, kl. Paraxerus palliatus) nende anayepaa (kg. Lord Derby’s Anomalure, kl. Anomalurus derbianus), koni (kg. black and rufous elephant shrew, kl. Rhynchocyon petersi), kuhe (kg. giant pouched rat, kl. Cricetomys gambianus), komba wa Usambara (kg. Usambara galago, kl. Galagoides species)

Ndege adimu

Ndege katika hifadhi ya Amani wako wengi. Wengi hupatikana katika sehemu mbali mbali za Afrika pamoja na nchi nyingine. Wengine ni adimu sana ama wamezoeleka sana kuishi katika milima hii tu. Ina maana kwamba wanapatikana hapa hapa tu duniani, yaani ni ndege au wanyama andemiki. Wengine wameadimika sana kiasi cha kukumbwa na hatari kubwa ya kupotea kabisa. Mmojawapo ni aina ya ndege mwenye mdomo mrefu anayeitwa « kolokolo domo-refu » (kg. Long-billed forest warbler, kl. Artisornis moreaui ) ambaye yupo katika milima ya Usambara ikiwa ni pamoja na sehemu ndogo ya Msumbiji. Kwa hivyo tunapaswa kuwa makini sana katika kuhifadhi mazingira yake endapo tunataka ndege huyo aonekane tena kwa vizazi vijavyo.


Katika takriban aina 350 ya ndege ambao wamerekodiwa katika milima ya Usambara, 12 wako kwenye takwimu ya ndege walioko katika hatari ya kutoweka duniani. Miongoni mwao wapo « bundi wa sokoke » (kg. Sokoke scops-owl, kl. Otus ireneae), « bundi wa Usambara » (kg. Nduk eagle-owl, kl. Bubo vosseleri), « nofi wa Tanzania » (kg. Nicoll’s weaver, kl. Ploceus nicolli), « chozi milia ya kijani », banded green sunbird (kl. Anthhreptes rubritorques), « chozi Amani » (kg. Amani sunbird ; kl. Anthreptes pallidigaster).

Angalia hapa : Ndege wa Tanzania

Reptilia na viumbe wengine :

Milima ya Usambara imejaaliwa kuwa na karibu jamii 30 za reptilia, wakiwepo vinyonga, nyoka, kenge na mijusi. Takriban jamii 16 za reptilia hazipatikani mahali pengine popote duniani. Miongoni mwao, ndio vinyonga wanaoonekana kwa urahisi

sana, hasa usiku. Wako aina mbali mbali, wenye au wasio na pembe, wadogo kwa wakubwa kiasi.

Kama mtapenda kusoma na kujua zaidi, hii tovuti ifuatayo inatoa taarifa nyingi, kwa kiengereza :

Angalia hapa : Amani Nature Reserve

Amphibia kama chura wapo wengi pia. Amphibia hawapungui chini ya spishi 40. Wengi katika hawa ni waendemiki wa milima ya Usambara wala hawapatikani kwingine duniani. Miongoni mwa chura, wasayansi wana kawaida ya kuainisha kila spishi kufuatana na etolojia yake. Hususan chura wa maji (aina yaXenopus) huishi ndani ya maji tu wala anashindwa kutoka nje. Tofauti na wengine (jamii ya hyperoliidae)ambao huishi juu kileleni kwa miti.


Mwisho katika viumbe hawa wa kiajabu ni vipepeo. Wako wengi sana na mtembezi hawezi kuwakosa katika matembezi yake. Msomaji anaweza kuangalia tovuti hii ifuatayo kuhusu vipepeo wa Tanzania ambao takriban 130 wanapatikana Tanzania pekee wala hawapo nchi nyingine duniani.Kuhusu vipepeo, hapa.             
             


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni