26/11/2013

Nafasi ya ilhamu katika kutunga riwaya

Majuzi tu, katika wilaya ya Tanga, nilikutana na rafiki mmoja mtanzania ambaye ni mwalimu wa hesabati katika shule za sekondari. Tulizungumza mambo mengi sana lakini swala moja liliibuka katika maongezi yetu likatubana sana hadi tukaamua kuligusia tena siku nyingine. Mada hiyo iliambatana na ubunifu katika fasihi andishi. Nayo ilianzia katika swala la rafiki yangu liliyokuja kama ifuatayo : mara nyingi sisi watanzania tunaambiwa kwamba hatuna kumbukumbu nyingi kuhusu waandishi wetu wa zamani, akiwepo kwa mfano mwandishi maarufu mwenzetu Shaaban Robert. Hiyo ni sahihi lakini je, kutunga kitabu cha riwaya au tamthilia kuna maana au umuhimu gani ? Na hasa, ina matumizi gani na faida gani kwa wananchi ? Na kweli, swala hilo lina uzito mwingi kwa sababu haliathiri ubunifu katika uwanja wa fasihi pekee bali linatufanya tuelekeze fikra zetu kwenye maudhui mengine ya kiutamaduni kama vile falsafa na usanii mbali mbali ambazo, kwa mtizamo wa juu juu, hazina faida wala thamani yoyote. Tukichambua zaidi tutagundua pia kwamba hesabati — au sayansi nyingine — haina faida yoyote kwa kuwa kazi ya msingi ya hesabati ni kuhakiki kitu ambacho hakina dhima wala kazi yoyote kwa muda wa papo kwa papo. Taaluma hizi zote hazitumiki kwa maana ya kwamba hazina matumizi ya kukinaisha mahitaji yetu ya kileo katika harakati zetu za kimaisha. Ndipo inapokuwa dhahiri kwamba ujuzi ni kitu cha bure.

Sawa, aliendelea kusema mwandani wangu, lakini riwaya inathibitisha au inataka kuthibitisha kitu gani ? Nikaona kwamba ni kweli kuwa fasihi kwa jumla haina tijara, pengine kwa sababu ni mchezo au kwa neno lingine ni burudani, yaani ni usanii wa kiujumi (aesthetis) usiokuwa na faida wa kiuchumi. Lakini bila shaka tunaweza kuainisha burudani ya aina mbali mbali. Burudani ya kutunga riwaya inatakiwa mwandishi awe na umahiri, ubunifu, ufundi na ilhamu nyingi katika kubuni. Burudani tulizo nazo siku hizi kupitia vyombo vya habari au runinga au sinema hazina sifa hizo au tuseme muundo huo unaotakikana katika ubunifu wa fasihi. Burudani iliyomo ndani ya usanii huo wa fasihi inataka mbunifu awe makini sana, hasa katika kutumia ilhamu yake. Na hilo ndilo linalothibitisha kwamba Shabaan Robert si mtu wa kawaida. Ningalisema kwamba si Kezilehabi, si Mohamed Said, si Mbwana, na kadhalika. Nachotaka kusisitiza hapo ni kwamba usanii huo, kwa kutumia ufundi wa kipekee, unaegemea utamaduni wa kibinafsi. Nayo ilhamu ni bahari yake kubwa.

Hapo ndipo rafiki yangu alipokatiza maneno yangu huku akisema kwamba hata msayansi wa fani yoyote hutakiwa kuwa na ilhamu. Na ni kweli. Linaturudisha nyuma sana katika karne zilizopita, wakati mfalsafa maarufu Pascal alipowahi kuchanganua namna mbili za kufikiri : kufikiri kupitia njia nyepesi na kufikiri kupitia jiometri. Cha kustajaabisha ni kuona kwamba Pascal anasema kuwa mwelekeo au mkabala unaotumika katika kufikiri kupitia jiometri ni rahisi sana kuliko njia ile nyingine ambayo inatumika katika kutunga kitabu cha fasihi. Kwa sababu moja tu ambayo ni rahisi kuelewa tukisoma Pascal kwa makini : vigezo vya kufikiri kupitia njia nyepesi ambavyo viko vingi vinatumika kila siku katika maisha yetu ya kawaida ; lakini kuzitumia kama ipasavyo katika vipengele vyake vyote kwa ajili ya kubuni kunataka mtu awe na akili tambuzi na ung’amu uliyokamilika.

Mwandishi wa fasihi naye pia ni msanii ambaye hutambua mambo — anaonyesha, anadhihirisha — si mtaalamu anayethibitisha. Ndiyo maana tunaweza kumhusisha katika kile kikundi cha watu wenye akili ya kupitia njia au mbinu nyepesi. Na katika mchakato huo wa kubaini mambo mwandishi fasihi ni mbunifu wa hisia. Tusimchukulie kama mtu anayeeleza misingi ya matukio, au tuseme visababi vya mkasa fulani. Kazi yake si kueleza au kupambanua, yaani kugundua kwamba tukio hili limesababishwa na tukio ile. Mwandishi wa riwaya ni msanii ambaye anajitahidi kumletea msomaji wake katika mazingira ya hisia fulani inayofanana na ruya, hisia za pupa au jazba. Hatumii nadharia wala dhana. Ingalikuwa ni kinyume na dhamira yake kuu ya kuzusha hisia kwa njia ya kuambukizwa ilhali tafakari, kwa kumtwisha mbinu ya nidhamu na taamuli, ingalimfikisha kwenye msimamo usiofaa katika kazi yake ya kubuni.

Swala hili linatuongoza kwenye uwanja wa ilhamu na umahiri. Kwa kiwango kikubwa ilhamu — ambayo mara nyingi haichukuliwi na wahakiki kama ni kigezo kikubwa sana katika kukuza umahiri wa kutunga kitabu cha fasihi ­— ni chanzo kikubwa katika ubunifu. Hapo hatuna budi kutilia mkazo juu ya uhusiano mzito baina ya ilhamu na ubunifu wa kifasihi. Sifa ya kitabu cha fasihi inahusiana na jinsi mwandishi alivyojikita katika swala hili la kubuni kupitia tabia hii hanamu ya akili yake. Kwa kuwa msanii wa fasihi si mtaalamu mwenye nia wa kutufahamisha dhahiri kinachoendelea katika maisha ya binadamu — si kazi yake kupiga kampeni au kuhamasiha wasomaji wake wafanye au wasifanye kitendo fulani, si kazi yake kutuhimiza tujiepushe na kitendo hiki kibaya au tuwe wangalifu wakati tunavutiwa na mtizamo huu hasi, na hali kadhalika — basi ni wazi kwamba fasihi si insha, riwaya si kitabu cha sosholojia, tamthilia si sheria, shairi si siasa na kadhalika. Ikiwa nataka kuandika kitabu kuhusu ukimwi au mauaji wa maalbino, nitaandika insha au vipeperushi au matini ya kisosholojia. Sitaandika riwaya.

Ilhamu ni kitu gani ? Na inatokea wapi ? Tukiangalia katika mapokeo ya kifalsafa mbali mbali au katika mapokeo ya kifasihi kadhaa tunakuta mitizamo mengi sana. Hapo katika nafasi ndogo ya makala hii hatuwezi kuipitia yote lakini tunaweza kuikusanya katika mikondo michache. Kwa wahenga wa Uyunani wa kale, mtu alikuwa anafikwa na ilhamu wakati mizuka ya aina mbali mbali inapomshukia msanii. Tunasema kwamba msanii amejaaliwa au amebarikiwa na taswira au hisia ambazo ni kichocheo kikubwa katika kubuni kwake. Ni kama kuwezwa na athari ya nje — iwe ni miungu, mizimu, koma ya wazee waliokufa, roho mtakatifu, n.k. Athari yake wakati mwingine huanzia katika nafsi zetu. Ulaya wataalamu wa saikolojia wameunda dhana mbalimbali kama vile ung’amu fiche ambao, kwa mujibu wa S. Freud, hutuvamia dhidi ya matakwa yetu wakati tunateleza kimatendo katika pirika zetu za kimaisha. Kwa kifupi, ilhamu hutujia wakati tunaghumiwa na yaliyopo katika mazingira yetu kwa jumla au katika nafsi (undani) yetu, wakati tunapojiamulia kujitenga na dunia iliyoshikika, au wakati tunapotoroka kimawazo katika mazingira tuliyo nayo, ama wakati tunapoyapuuza maswala makubwa ya kisasa, na kadhalika. Kwa sababu msaani ni mtu ambaye hukubali kuchokozwa na kuvamiwa na kilichomjia kupitia ilhamu na ughushi, si jambo la ajabu kuona kwamba ubunifu katika nyanda zake unachukua upeo mkubwa sana. Katika mapokeo ya fasihi, kauli hiyo ni dhahiri : kutoka Shakespeare hadi Wole Soyinka, kutoka Molière hadi Octavio Paz, kutoka Dostoievski hadi Kezilehabi, na kadhalika, tunagundua kwamba fasihi si bahari kubwa tu, bali ni anga isiokuwa na mwisho. Ndio maana mara nyingi tunasikia — hasa katika jamii zisizokuwa na mapokeo ya kifasihi — kwamba kutunga kitabu cha kifasihi ni kazi ya kuunda uwongo, udanganyifu na ulaghai. Ama kweli fasihi ni kazi bure ambayo gharama zake ni kubwa sana. 

Ilhamu ni kiini cha ubunifu. Nduni zake na madhehebu yake ni nyingi, kitu ambacho kinapaswa kutiliwa maanani endapo tunataka kuelewa kuwa utungaji ni kitu au kitendo cha bure : ingawa mwandishi fasihi si mtu wa kawaida kutokana na baraka hii ya kiajabu ambayo husogezewa nayo kwa muktadha wake (lakini waandishi wengine hawana ile ilhamu na muono za kuweza kumridhisha msomaji — kitu ambacho kinatusaidia kutenganisha tungo zuri na baya —) hatuna budi vile vile kuzingatia kwamba kuandika maandishi ya kubuni kunataka ufundi katika hoja ya muundo. Ilhamu pekee haitoshi.


Marejeo :

Pascal « Mawazo » (kif. Les Pensées ; kiz. : HAPA

Haji Gora « Kimbunga »

Hugo « Maangazo » (kif. Les méditations ; kiz.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni