15/12/2013

Ilhamu : kwa nini fasihi haitaki uhakiki wala uchambuzi wa kigalacha

« Ninamhitaji Mjerumani kwa ajili ya kukamilisha mawazo yangu »
Paul Valéry (1871–1945, mshairi wa kifaransa, mtungaji insha)

Wataalamu wengi husema kwamba neno hili ilhamu, katika lugha za kiulaya, limeibuka karne 12. Ni neno ambalo linajitokeza katika istilahi ya kikristo. Ingawa neno lenyewe halipo kabla ya hapo, dhana nayo ilitumika katika jamii ya kilatini pamoja na kiyunani. Katika kilatini, inspiratio ni neno ambalo linamaanisha pumzi inayopulizwa kama ile inayotoka katika kinywa cha binadamu. Tukichambua zaidi tunakuta kwamba ilhamu ni spairo yaani, kwa kiyunani, kuhaha au kupapatika. Neno hilo limekuwa karibu sana na jingine yaani enthusiasmos. Dhana hizo zilitumiwa na Plato katika vitabu vyake mbali mbali kama Ion, Phaedo au Cratylus. Mwana falsafa huyu anaitumia katika maana yake mbili : upepo au pumzi fulani na jazba ile inayosababishwa na hali ya kupapatikia malaika, tarishi ya mungu au miungu. Maana hiyo tunaikuta pia katika maandiko kadhaa ya BibliaYeremia (I, 9), kwa mfano, alipowahi kuguswa kinywa chake na Mwenyezi Mungu alisema : « Kisha Bwana akaunyoosha mkono wake na kugusa kinywa changu, akaniambia, “Sasa nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako. Tazamaleo nimekuweka juu ya mataifa na falme ili kung'oa na kubomoa, ili kuharibu na kuangamiza, ili kujenga na kupanda. » Petro (2-1-21) pia husema : « Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu. » Daudi vile vile hutoa maelezo hayo hayo : « Roho ya Bwana ilinena kupitia kwangu, neno lake lilikuwa ulimini mwangu. » (2 Sam. 23:2).
Miongoni mwa tanzu za fasihi, ushairi ndio utanzu unaojengeka kwa kufuata madhehebu hii ya ilhamu kama ilivyotokezea katika mapokeo tuliyopitia hapo juu. Jambo hili linaeleweka wazi : ushairi ndio usanifu usiotegemea sana hali ya kufananisha au kushirikisha maana yake na kitu kilicho katika dunia ya kushikika. Uhalisia si dhamira yake kubwa. Ndiyo maana mashairi ya kisimulizi ambayo yanalenga kupasha taarifa moja kwa moja, yaani bila hata kufinyangwa na utaratibu huu wa kiilhamu, katika mapokeo ya kifasihi mengi, hayana sifa ile ya kuweza kuvutia wasomaji au wasikilizaji wengi. Aristote aliwahi kuudhihirisha mchakato huu kwa kutumia neno la kiyunani mimesis. Pengine kwa kuwa ushairi, kihistoria, unachukua asili yake katika ubunifu ya kitakatifu. Si jambo la kushangaza kuona kwamba, kwa mfano katika kijerumani, neno hili mshairi yaani Dichten lina asili yake ya kugongana na neno la kilatini dictare ambalo lilijiri kutumiwa na wahenga wa Kanisa ya kikristo kwa kumaanisha kwamba ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hupuliza ilhamu ya maandiko ya kidini : washairi hutunga kama walivyotunga mitume wa zamani, kwa kuandika huku wakipuliziwa pumzi ya uhai na Baba mtakatifu (Mwanzo (2-7) : « Bwana Mungu alimwuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, mtu akawa kiumbe hai. »).

Katika historia ya dhana au miongoni mwa wana falsafa kutoka enzi za wahenga wa wayunani hadi leo, tunaweza tukataje angalau vipindi vinne ambapo watu waliichukulia ilhamu kama jambo la kutilia maanani sana. Enzi za zamani sana za Ugiriki, kipindi cha Mzao (Renaissance), kipindi cha nathari ya romansia na kile cha uhalisia bwete (surrealism). Wakati wa enzi za kale, karne 8 kabla ya Y.K, ndiye Homer aliyeanzisha kitabu chake maarufu Odyssey kwa kuimba kianzio hiki kinachoshabihiana na dua   : « nakusihi malaika ukanisimulie visa vya shujaa yule mwenye ujanja mwingi, ambaye alihangaika sana hadi alipoangamiza mji wa Troy, kisha akawahi kutembelea miji mingi ya dunia, akasoma tamaduni zao, akaona uchungu baharini akapambana na shari kuu akajihami mpaka aliporudi nyumbani na wenzake ». Katika utangulizi huu, tunanogewa na utamu wa maneno ambayo yanachanganya dua, falaki, hoja na muhtasari wa matukio tutakayokumbwa nayo tukiingia katika utenzi huu mkubwa wa Odyssey. Mtunzi huyu Homer ni gwiji mkubwa wa kutumia maneno kisanaa ili tuvutiwe na mikasa ya kiajabu ya Ulysses ambaye ndiye shujaa wa simulizi hii maarufu. Kama alivyotueleza Plato katika Ion, mtenzi au mshairi si msanii kamili bali ni mshenga au wakala wa mailaka au miungu ambao ndio waliomkabidhi tunu ya kiubunifu.

Katika mapokeo ya usanii wa kuchora, tunakuta tungo nzuri zinazowakilisha mwenye ilhamu kama vile mshairi katika hali ya kupokea ilhamu. Mara nyingi tunamwona huku akiinamia chini, au amekaa kimya katika msimamo wa kutotikisa wala kusuka suka mwili wake. Yupo kimwili tu, kindevu katika kiganja chake, kama kwamba kitu cha kigeni kimemvaa. Ukimwangalia kutoka nje, utasema kwamba ameganda kama mwari kiputu wakati wa unyago au kama mjane ambaye amehemea kupindukia. Lakini pia tujue kwamba katika nafsi yake, mwenye ilhamu amefikwa na mawazo mengi yakiwemo fantasia, sisimko, jazba, yaani mambo yenye uajabu ajabu. Anaelea katika mikondo ya taharuki. Au pengine anasujudia wahenga wake huku upepo mzuri ukipeperusha nywele zake, na muono wake umekazia upeo wa macho. Hapo ndipo aina ya uchoraji mzuri wa msanii mmojawapo maarufu kutoka Ufaransa anayeitwa Fragonard (1732–1806).

Uchoraji huu unatukumbusha kwamba ilhamu ni kitendo kilicho karibu sana na hali ya kuchagawa au, kwa kutumia neno jingine, kusikilwa. Kwa kusema vile, nataka kusisitiza kwamba kupatwa na ilhamu ni kama kupandishwa au kurushwa nje lakini kwa kubaki hapo hapo. Nayo hali ya mshairi inadhihirisha kwamba ilhamu inaegemea utulivu pamoja na taharuki, yaani ukimya pamoja na kiherehere. Anatakiwa kujiharakisha kwa undani pamoja na kukaa bila ya kutikisika. Imekuwa kama kwamba msanii ni mtu mwenye uwezo wa kujiachilia, pengine kwa kuwa hujisahau, hadi kufikia hatua ya kujikuta katika hali ya kuchanganyikiwa, mara akimiliki alicho nacho mara akikubali kunyimwa miliki yake kwa kutaka kulaki sisimko jipya. Katika harakati hii msanii hupirikana na alicho nacho ndani yake, hupambana na yale yaliyomo moyoni mwake hadi kupachikwa kipaji kile kinachomwezesha kusanifu kitu kipya.

Ilhamu ni kipaji anachopewa msanii — naye si mtu wa kawaida — akiwa amekabidhiwa kipawa hiki kutokana na mwelekeo wake maalum wa kuweza kupokea anayoshushiwa kutoka nje — iwe jambo la kidini, hususan kupitia matambiko ya kipito, kisasili, falaki au dua, au kwa kutumia aina ya mbinu au chombo kingine, iwe ni dawa, vinywaji au uraibu wa kulevya, au kupitia matini au maneno ya wahenga wa zamani — yote hayo yanathibitisha kwamba fasihi ni kubuni katika muktadha ya kiajabu. Inamwongoza msanii kwenye maarifa, lakini maarifa isiyoshikika ambayo si ya kihalisia. Hapo tunaweza kufahamu kwa nini uhakiki ni mkabala ambao hautoshi katika kuchambua fasihi : kwa kuchukulia kwamba uelewa wote unapaswa kupitia kwenye mbinu za kisayansi, bighairi asili ya kifundiro cha akili ya binadamu, uhakiki unajidai kuwa ni uelewa wa kisayansi pekee ambao una uwezo mkubwa kushinda uelewa wa aina nyingine, ikiwemo uelewa wa kidini, licha na uzoefu wa kisufi (mystical experience) au hisia za kitaharuki. Usanii kwa jumla hautegemei matumizi ya akili pekee bali unakiuka mantiki, ufahamu na ufafanuzi.

Marejeo :

Biblia : HAPA  
Homer, Odyssey : HAPA
Plato : HAPA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni