10/12/2013

Ya nini tusome na tuandike wakati porojo zipo ?

Hivi karibuni nimekuta makala moja kwenye blogu ya Profesa Joseph Mbele ambayo imenivutia sana kwa kuibua swali ambalo linatukabili sisi sote ambao tunasomesha shuleni au chuo kikuu. Kwa kuwa mimi mwenyewe ni Profesa katika uhakiki wa fasihi ya kifaransa, ningependa kugusia baadhi ya hoja zilizopo katika mjadala unaoambatana na umuhimu wa kusoma vitabu.

Kwa kawaida, tunasema kwamba hatusomi kwa sababu mbili : kwanza tunasema kuwa vitabu ni ghali mno, hatuna uwezo huu wa kununua kitu ambacho ni burudani, na burudani si lazima ; pili, hatuna utamaduni huu unaotakikana ili tukubali kukaa muda mrefu katika hali ya upweke huku tukisoma kitabu. Pamoja na kwamba maelezo haya yanakubalika, vile vile yanapingika tukiangalia jinsi vile baadhi ya waandishi mashuhuri duniani walivyokabili hali ya ufukara mkubwa katika maisha yao.  Nisitaje pia wateja wa vitabu huku uzunguni na kwingineko ambao watakubali kupunguza mahitaji yao ya kila siku ili wajipatie kitabu. Mshairi maarufu Ufaransa aliyeitwa Baudelaire aliandika maneno hayo ambayo ni ya kushangaza kwa sisi ambao tunaishi katika tamaa : « Mnaweza kuishi siku tatu bila hata mkate ; bali kama hamna ushairi, maisha hayaendi ; na wale wanaokataa wanakosea : hawajitambui »

Pengine kuna sababu ya tatu, nayo inatupeleka katika kuchambua hali ya lugha yenyewe, nayo ni kiswahili. Kuhusu hadhi au sifa ambayo hupewa lugha ya kiswahili, sidhani kwamba nitakosea kwa kusema kwamba kiswahili hakijapewa nafasi ya kutosha katika swala hilo la fasihi andishi. Vitabu vyenye thamani ya kutosha vipo, lakini je, vinatumika ? Msomaji ajaribu kujipatia kitabu kimojawapo kilichopo katika mlolongo wa picha kwenye ukurasa wangu, hapa upande wa kulia. Na hata kama vipo katika maktaba, nani na watu wangapi wanaweza kuvisoma ?

Jawabu nitaliacha kwanza niruke kuelekea chemchemi panapopatikana maudhui ya hoja yangu ya leo : nini haswa kinachohitajika ili watu wapende au wapatwe na ashiki ya kusoma ? Kwa muhtasari, leo nitajaribu kuzingatia vipengele vitatu. Kupenda kusoma kunataka msimamo maalumu :

- kupenda kujing’oa katika hali ya kisasa na kipahala (yaani kutopenda kushughulikia mambo ya kileo tu, kutopenda kuishi na wakati) na kijitosa ndani ya bahari ya uzushi wa kimawazo.

- kupenda kuishi katika hali ya upweke ambao ni kinyume na ukiwa na ukimwa !

- kujitahidi sana katika kujitenga na jamii ambayo kwa jumla ina msimamo wa uratibu wa mwafaka na uthabiti wa ubinafsi. Swala hili linataka mtu awe na nia kali, awe madhubuti katika kuacha na tabia yake ya kuendekeza mwelekeo wa silka : maumbile yetu inapenda kwenda katika mharara wa uzembe, uvivu, jazba, hisia mbaya na kadhalika.

Kuhusu kiswahili mara nyingi hatuna budi kutambua kwamba sifa ya lugha hii inategemea sana maoni ya watu. Nikisema vile nataka kusisitiza kwamba maoni ni kitu ambacho mara nyingi huchukuliwa ni kitu kizuri. Chambilecho bin fulani, maneno ya mtaani ni kweli ! Kinyume na kauli hiyo tunakuta vitabu vingi katika mapokeo ya falsafa au fasihi ambavyo hurudi nyuma katika mkondo huo. Maoni, tukifuata Descartes kwa mfano, ni kauli ambayo haijapitishwa katika uchanganuzi, yaani uhakiki. Kwa hivyo kauli yangu itajidai kuwa ni kweli tu hata kama akili zangu hazijahangaika ili kuthibitisha kwamba inakalia juu ya ukweli au juu ya hitilafu. Ina maana kwamba mawazo yetu yote ya papo kwa papo ni maoni tu, yaani mchunko (cliché) au kwa maneno mengine mawazo ya watu. Kimsingi, maoni ni imani au itikadi, wala sio wazo kamili.

Hilo ni tatizo kubwa ambalo jamii inakubaliana nalo tangu zamani. Plato, mwana falsafa maarufu, alikuwa ni mwasisi halisi katika kuvuta akili za wanafunzi wake juu ya hatari ya maoni. Alichora taswira nzuri katika kitabu chake kinachoitwa Jamhuri kwa kuzingatia sana swala hilo la maoni ; kwa kifupi, tutashinda maisha yetu yote katika pango, yaani katika giza, endapo hatujui namna ya kuelekeza akili zetu penye nuru. Kama tunataka kutoka katika pango hilo la maoni, inabidi tuhangaike, yaani tutumie mbinu, stadi, mikabala, na kadhalika, kupitia usuhulishi ya wahenga waliokufa zamani. Na mbinu hizo, tunazipata katika chombo kimoja tu : katika vitabu, haswa vile vya falsafa na fasihi. Waswahili husema, ukitaka cha mvunguni shurti uiname, yaani uhangaike.
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni