24/01/2014

Mhakiki : kunja mkia, wafasihi wapite mbele !

« Sipendi wataalamu. Naona kwamba kuwa mtaalamu
ni kama kudhoofisha mtazamo wangu »
Claude Debussy (1862-1918 : mfaransa, msanii wa muziki, mwandishi wa insha)Uhakiki wa fasihi una kazi nyingi. Mhakiki ni mtaalamu katika kuchambua vitabu vya aina mbali mbali, hasa katika mawanda ya usanii wa kifasihi. Tuthubutu kuuchukulia uhakiki kama ulivyo, na tuumakinikie katika misingi na chimbuko zake. Ni taaluma ambayo inajidai kuwa na uwezo wa kupanua wigo wa fasihi. Je, kweli uhakiki umetoa mchango mkubwa katika kusaidia watu wasome zaidi na wavutiwe zaidi na vitabu vya fasihi, kitu ambacho ni dhima yake kuu, au haujaleta mafanikio yoyote katika ukuaji wa fasihi ? Kikubwa cha kutilia maanani ni kwamba, hasa katika nchi zile zilizoendelea sana katika usanii huo, kusoma kwenyewe kumepungua na kunazidi kupungua ilhali uhakiki unajiendeleza. Tujiulize kwa nini. Na tusisahau kwamba fasihi ni usanii, yaani ni ubunifu wa akili ya binadamu ambao kwa kawaida hunogewa na watu kwa sababu ya ulimbwende wake na haiba za fani zake. Fasihi ni kitu cha kiujumi, na ujumi ni jambo la kuvutia kwa sababu ya nakshi zake kwanza, la kufanya mpenzi wake avamiwe na uzuri wake. Tusisahau kwamba mkwara hautakiwi mafuta na chakula chema hakihitaji kawa !

Mhakiki maarufu wa kifaransa, Roland Barthes (1915-1980), anatoa mifano mizuri sana katika kitabu chake kiitwacho Insha ya kiuhakiki (Essais critiques, 1964).
Hapo nitachukulia alichosema kuhusiana na hoja ya mhusika katika riwaya, akisisitiza kwamba mhusika yeyote katika tungo la kifasihi hastahimili mfanano wowote na mwandishi mwenyewe aliyemwumba — akitaja mfano wa mhusika mkubwa katika riwaya mashuhuri ya Proust (1871-1922) anayeitwa Charlus huku akisema kwamba mhusika huyu hawezi kusabihiana na Montesquiou ambaye alikuwa ni rafiki ya Proust — ila mhusika huyu ni miongoni mwa sanamu zilizotumika katika kutunga riwaya ambazo zinachangia kujenga msuko wa wahusika wa kitabu hiki kiitwacho « A la recherche du temps perdu » (. Kwa kuwa wahusika wote wa riwaya hii wamefinyangwa vizuri kwa kufuatishia ufundi huu wa kifasihi ambao Proust ameusarifu kwa umahiri mkubwa, Barthes anajidai kwamba tungo lolote katika fasihi kwa jumla linastahili kuchambuliwa kwa kuongoza uhakiki kwenye undani wa tungo tu. Wahusika wote, katika riwaya, wamenaswa katika mfumo wa sanamu ambao ndio unaokarabati maana ya muonekano na tabia zao. Kwa mantiki hiyo, mhakiki asichukulie taathira za nje, kwa mfano wasifu wa mwandishi, kama ni nadharia tete muhimu inaotusaidia kufafanua riwaya yake. Mhakiki huyu anaongeza kwamba hatuwezi kuchukua mazingira na jamii ya mtungaji kama ni vigezo vikubwa katika kutoa ufafanuzi halisi wa fasihi. Maana ya riwaya yoyote isakwe katika maudhui yake pekee. 


Huo ndio mtindo wa « uhakiki mpya » uliozuka katika miaka 1960 huko Ufaransa. Nao ulikuja kupingana na mtindo mwingine uliotawala mapokeo ya uhakiki tangu mwisho wa karne 19 ambao ulianzia wakati wa nathari ya uhalisia asiliya (naturalism). Cha kuzingatia hapo ni kwamba uhakiki, kabla ya hapo, haukuchomoza kama ni stadi ya kitaalamu ya kuweza kupanua wigo wa fasihi. Ni jambo la kushangaza, hasa Ufaransa, ambayo ni nchi iliyojikita katika ubunifu wa kifasihi tangu karne 11. Aidha, ubunifu huo wa kifasihi ulishitadi mfululizo mpaka leo kiasi kwamba fasihi katika nchi hii imesadifu matakwa ya nyakati hizi nyingi, hadi ilichukuliwa na wananchi kama ni chombo murua katika mapambano ya kisiasa au ya kielimu. Si uhondo tu, bali ni changamsho na kichocheo kikubwa katika kuibua itikadi au imani dhabiti mpya katika jamii. Katika historia hii ya kisanii, uhakiki ulijitokezea hivi karibuni tu, katika mandhari ya siasa mpya — baada ya kuzaliwa kwa jamhuri na demokrasia, kujengwa kwa serikali ya dola yenye nguvu zote (mpaka kuundwa kwa wizara wa kiutamaduni) — ikawa mhakiki ni mtumishi wa umma, na mamlaka yake yote yameshamiri katika mikono ya serikali. Mhakiki ni profesa mtegemezi au mtashi wa serikali wakati mfasihi ni mtu huria anayejitegemea katika kujitarazaki na kusanifu vitabu vyake. Wengi katika wasanii maarufu sana duniani waliacha kazi zao za kubuni kwa sababu ya kupatwa na dhiki nyingi katika maisha yao au kwa sababu waliwahi kuajiriwa na serikali — mfano wa kujulikana sana ni ule wa Racine (1639-1699), ingawa msanii huyu aliwahi kuishi chini ya ufalme wa Louis XIV, ambaye alikoma kutunga tamthilia alipoajiriwa na mfalme wake.  

Serikali ina nguvu nyingi : si kuajiri au kuachisha kazi msanii tu, bali ni kumnyamazisha au kumwathirisha — lakini kama vile bwana anavyojisuhubisha na kijakazi wake — kiasi cha kumpa majukumu mengi sana hususan yale ya kuhakiki au kusoma ubunifu, tabia za watu, desturi na mila za jamii, na kadhalika. Uhakiki ni kozi mpya, kama nilivyosema hapo juu, nao umekabidhiwa hadhi kubwa sana katika vyuo vikuu kiasi cha kutufikirisha kwamba, na kweli ni jambo la kuwa na hofu nalo, fasihi itakuja kujinywea au kusinyaa sana katika masuguano hayo ya kihakiki. Zoezi hili tunaliona katika tahakiki mbali mbali za huku Ufaransa : riwaya ya Proust si kitu, Barthes ndiye mtaalamu
anayejua kila kitu, kwa jumla na fusuli, kuhusiana na kitabu kile alichobuni. Anasogeza uhakiki wake hadi kusema kwamba « mwandishi amekufa », si lazima tuwe na nadhiri ya wasifu wa Proust ili kuelewa kitabu chake maarufu. Matokeo yake tunazinduka nayo kila kukicha katika shule zetu au vyuo vikuu hapa na pale : wanafunzi wengi hupendelea kusoma tahakiki kuliko vitabu vya kifasihi, pengine kwa sababu hufikiri kwamba uhakiki ni mkabala au mbinu ya kuweza kufupisha yale wanayotakiwa kujua ili kupasi mitihani yao, au labda kwa sababu wameshakubali itikadi hiyo ya kwamba sayansi ya kiuhakiki imepiku katika kukosoa fasihi. Katika muktadha hii, kwa nini wasome vitabu vyote vya Shabaan Robert ilhali kurasa kadhaa za makala ya mhakiki fulani zimeshakashabi kiini chake ? Na kwa kuwa mhakiki hutumia nadharia nzito — kitu ambacho kinaelekea siku hizi kuwa ni hirizi kubwa — mara nyingi anapewa cheo hiki cha usayansi. Si kujigonga tu au kujivesha kilemba cha ukoka ? Lakini hapo tuna haki ya kujiuliza : je kweli mhakiki ana ustadi huu wa kumwezesha aonelee sayansi kuwa ni kitu cha kusomea fasihi ? Katika kuchambua na kupambanua kwa kujifanya mjuzi wa kila kitu, yupo kama spanaboi na vifaa vyake akijaribu kutuni injini ya gari au kama mhandisi anayejua misingi yote ya ujenzi wake. Katika kusoma na kukosoa kitabu cha fasihi, kazi yake inamwinua hadi kujivunia kile alichokiandika, kitu ambacho kinampa pawa ya kumchezea shere mwandishi, tena kwa kujishua kwa makeke yale ya kujifanya mtaalamu nguli wa kurekebisha na kukarabati kilichobuniwa na msanii — ili pengine kudaka na kusawazisha makosa na hitilafu zake — eti kwa sababu anajidai kuwa mtetezi wa fasihi.


Na kweli, katika historia ya kidhana, uhakiki ni binti ya Marx, Freud na Saussure ambao ni wana falsafa waliobobea sana katika kuanzisha mtindo huu wa kuziba kila mwanya wa kuweza kutupa uwezo wa kupinga ukiritimba huo wa uelewa. Neno hili sayansi huchukuliwa na watu wengi kama kigezo ambacho hakijadiliki wala hakiyumbiki. Ni sawa ya kusema kitu hiki kinachoshikika ni kweli, kwa sababu kipo katika nususi ya mambo, wala hakina nduni ambazo hazieleweki. Uhakiki unajiwakilisha kwa kujipa joho la sayansi yenye dhamiri bayana ya kukidhi mahitaji yetu katika kutatua matatizo yote ya kifasihi. Ikiwa ni hivyo, hatuna budi kubaini kwamba uhakiki unabamba milango yote ya kupitisha upendo wenye uraibu ndani yake au ushabiki wa dhati, hususan ule unaoakisi maumbile yetu ya kupenda kwa kutumia harakati za hisia zetu bainifu. Badala ya kutia shime au kuhimiza wasomaji wasome zaidi, hasa miongoni mwao tunakuta wachipukizi katika kusoma, uhakiki huwa unatuwekea katika hali ya kuamini kwamba kusoma ni kujua matumizi ya mbinu zinazotumika katika maabara (je, katika kitabu hiki, kuna tamathali ngapi, taswira au ishara zipi, n.k. ? « haya wanafunzi, chukueni kalkuleta zenu ! »). Je ni kweli kwamba tahakiki tuliyowahi kusoma zimetuendekeza zikatupa moyo mpevu wa kutaka kusoma vitabu ? Au tahakiki zile zilitushiba mpaka zilitukifu ? Kuwa na hamu ya kusoma inabidi mtu azoeleke tangu utotoni mwake, na mara nyingi azoeleshwe, tena ajue kwamba hamu haiji bila ya kupenda. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni