05/02/2014

Eti vitabu viuzwe kwa kilo ?Siko Tanzania pekee bali katika nchi nyingi za dunia yetu, tunasikia watu wakisema kwamba lazima tusome vitabu. Hapo mimi nitakataa kata kata. Sioni sababu yoyote ya kusoma wala kumhimiza mtu asome. Hapana, musisome. At least, kwa sababu mbili. Kwanza tunaishi katika dunia isiyokuwa na vitabu. Tembeleeni vijiji vyote vya Tanzania na kama kitapatikana kitabu kimoja hapo, mnipigie simu ! Lakini kwa kusema watu wasome, tayari wana vijiji wengi wameshaingiwa na wasiwasi kubwa, wameshajitoa thamani yao wakajiita washamba, punguwani namba uani wasiokuwa na maana, kama si kashkuli ! Kwa malofa hawa, kitabu ni ruya ! Pili vitabu vile vinavyochapishwa na vitoa-vitabu siku hizi si vile ambavyo vinavutiwa kiasi cha kutuwekea katika hali ya kuvinunua. Lakini je, watu wenye uwezo wa kuvinunua, yaani wakaazi wa miji mikubwa, ambao wameshapata maendeleo endelevu ya kufanya mtu aimudu ung’eng’e ule ule wa kuchotea marupurupu, huvinunua ? Kusoma kitabu kunachukua muda mrefu, masaa mengi, kama si siku nyingi, kutegemea na ukubwa wake. Inabidi mtu aache baraza yake, jamaa zake (wakina broo), burudani zake — sijui kutunisha misuli yako kwa kujiweka fiti, kupiga mataputapu ya kila aina, kusakata rumba katika disko, kuchapa uraibu wako wa kila siku (blanti, vidosho, blingbling na kadhalika), yaani ashiki zako zote za kujipatia starehe kibao — pengine kwa sababu kusoma ni kitendo ambacho kinataka bidii, ghera na uwalii. Ndiyo, kujibidiisha, kwa kumakinika. Si mchezo, ule wa kujipweteka katika sofa yako kwa kuchezea rimoti ya kutembeza dividi ya dizim ambayo, kwa bahati mbaya, huenda itakuja kuskwanchi. Dunia yetu ni balaa : lofa angependa kusoma vitabu lakini hana mshiko (wa kwenda mjini kununua vitabu) ilhali kigogo na pedeshee nao wanachukia vitabu vile kwa sababu hupenda kutegemea nundu.

Wote hawa hawajui kinachoendelea katika dunia yetu. Marehemu Prof. Chachage aliwahi kutusaidia dokezo wazi kuhusu swala hilo. Tumetumbukizwa katika pango jipya — ile ile ya Plato lakini kwa kina zaidi — si la utandawazi tu bali la kibisi, yaani jaa la usawa wa takataka. Vifaa vyote vya kukomboa binadamu vimetupwa humo humo vikaharibika, nacho kitabu kimojawapo.
Na kusambaratika kwa vitu aali hivi kama vitabu vya thamani kumesababisha utamaduni wa kusoma kuingia katika tasnia ya vifundiro dufu. Asije mtu kuniambia kwamba bado vipo vitabu vyenye muwala fulani wa kuvitofautisha na vingine, sikubali. Itakuwaje mtu huyu, baada ya kusoma Montaigne au Dostoïevski, anasoma Gaadafi au kitabu cha mtu mwingine ambacho hakina sifa hiyo inayotakikana ya kuwasilisha hekima ya kibinadamu ? Si kama kuchonga msonobari baada ya kutumia mpingo ? Au kujistiri kwa kaniki baada ya kutumia nguo ya bafta ? Sufi si sanda. Asusa ikiwa tamu ni heri kuliko chakula kingi kisichokuwa na ladha. Chakula kilichoiva si matabwatabwa. Niliambiwa na wazee wa Kilwa, zamani kidogo sasa, kwamba kukaa kibahashuli si kukaa kiungwana. Je narudia swala langu : kitu kilichoghalika, ambacho ni ghama kitakuja kuwafiki muktadha mwingine wahsi ? Kitabu hafifu si kitabu aali. Zamani wanafunzi hawakusoma bali walisomeshwa, yaani waliongozwa na walimu wao kusoma kitabu hiki au kile. Tena ilikuwa marufuku kujiamulia kusoma kitabu ambacho hakikuwepo katika mapokeo au riwaya fulani, yaani katika mkondo fulani. Siku hizi, eti tusome ! ikiwa kitabu tunachosoma ni kifufumkunye, je kitafaa ? 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni