11/03/2014

Hifadhi ya mazingira, fasihi na tabia ya kusoma shuleni


Nilipokwenda hivi karibuni kutembelea marafiki zangu wanaoishi katika milima ya Pare karibu na Same, niliwahi kuzumgumza na watu wengi kuhusu swala la kusoma vitabu. Katika pita pita zangu za hapa na pale nilibahatika kukutana na vijana wa shuleni wa kidato cha 4 hadi 6. Nilishangaa sana kugundua kwamba vijana hawa, ambao watajishirikisha katika kikosi cha wazalendo wa Tanzania kesho kutwa, ambao baadhi yao watakuja kukamata usukani wa kuendesha shughuli muhimu katika sekta mbali mbali ya siasa na uchumi, basi hawa hawana hata kivuli cha dhana kuhusu waandishi maarufu waliowakilisha nchi yao ndani na nje ya Tanzania katika miaka ya nyuma, seuze wasanii wanaoendelea kutunga vitabu hadi leo. Inaelekea kwamba mwandishi Said Mohamed ambaye ni mmojawapo katika wasanii hawa wanaostahili kusomwa kwa umakinifu, amesema ukweli alipojibu ifuatayo :

« Chambilecho, gwiji wetu wa fasihi, Profesa Ebrahim Hussein, hakuna fasihi tena kwa maana ya fasihi. Hakuna wasomaji wazingatifu. Hakuna uhakiki kwa maana ya uhakiki. Kuna fikra ya kwamba chochote kile ni sawa. Shairi, riwaya, hadithi fupi au tamthilia ikiwa ina sura ya tanzu inayohusika, basi ni fasihi tu kwa maoni ya wengi. Fasihi haipo. Wasomaji hawapo. »


Ni kweli, watanzania hawasomi wala hawapendi kusoma. Lakini kusema vile haisaidii kitu kama hatujasaili kwa nini. Nakumbuka siku moja nilikuwa natembea katika milima ya Usambara huku nikifuatana na kijana mmoja kusudi anitembeze katika msitu aliyekuwa anaufahamu vizuri. Tukatembea sana, mara tukaona kijinyoka kikivuka njiani kwa kupiga mikambi chapu chapu ili pengine kujiepusha na maafa ile iliyoshaanza kukipata kwa kusikia watoto wakikifurusha kwa kupiga kelele : « tumwue, tumwue ! ». Ndipo nilipowasimamisha huku nikiwauliza :

« kwa nini mnataka kumwua ?  
- si nyoka ? 
- hapana, nikawajibu, ni chakula ! 
- chakula cha nani ? 
- cha kipozi, mwewe, fungo, ngwachiro na kadhalika. Mkimwua mnyama huyo, si mtakuja kuwanyima chakula wanyama hawa ? » 

Watoto wakazubaa na nyoka akawakimbia. Laiti watoto hawa wangalikuwa na walimu wa kuwasomeshea jinsi mazingira ya kiasiliya imepangwa kiajabu katika mpangilio endelevu kiikolojia, basi tukio kama hilo lisingalitokea. Na watoto, badala ya kutaka kuadhiri kinachoitwa na wana sayansi uhusiano wa kiikolojia, wangalienzi uhai kama wanavyoenzi uhai wao.

Isitoshe, baada ya kusoma mitaala mbali mbali ya shuleni za msingi na sekondari, nikaona kwamba si fasihi ya kiswahili pekee isiyofundishwa, lakini pia mbinu na mikabala ya kuhifadhi mazingira bayoanuai. Watoto hawajui kwamba uhai wao unategemea uhai wa mimea, wanyama na viumbe wote wa dunia yetu. Hawajui kwamba nyoka, uyoga wenye sumu, vidudu hatari na viumbe wote wabaya wa dunia wetu wana nafasi zao na wanatoa mchango mkubwa sana katika kuimarisha uwiano unaostahili kuwepo katika mfumo wa kiikolojia. Inajulikana wazi siku hizi kuwa nyuki na popo kwa kuchavusha maua ya miti na mimea husaidia kwa kiwango kikubwa mzao wa miti ambayo tunatumia kila siku katika mlo wetu. Viumbe hawa hutoa dhima kubwa sana katika kusambaza mbegu na sukari ya maua ambayo kama si wanyama hawa miti na mimea mingi isingalipandikizwa kwingine.

« Nyinyi wazungu mnaenzi mazingira kwa sababu ni katika maumbile yenu ! akaniambia kijana mwenzangu niliye naye siku ile, lakini sisi watanzania, hatuelewi kwa nini mnafikiri kwamba miti na wanyama porini ni kama kitu kitakatifu ! Angalia hali ilivyo kuhusu mibuga na hifadhi ya wanyama pori, sisi tumerithi kitu hicho kutoka enzi ya ukoloni lakini ishu hiyo ya kuhifadhi mazingira haipo katika utamaduni wetu… »

Si kweli hata kidogo. Kwanza zamani Ulaya pia watu wengi walikuwa hupenda kuangamiza mazingira yao, na hadi leo wapo watu ambao hupenda kuwinda wanyama hata kama ni marufuku. Pili, swala la kuchukulia mazingira kama ni kitu kikatakifu haliibuki katika hulka zetu bila hata sababu yoyote. Kuenzi mazingira kwa jumla kunafundishwa, na katika nchi nyingi ni kipaumbele katika masomo ya watoto hadi kujikita katika fikra yao. Na kama hatuzingatii swala hilo, iko siku dunia yetu itakuwa mti mkavu. Na wengi katika sisi hatujui kwamba kwa kuuelemea utakuja kutubwaga.

Hapo chini nimebandika baadhi ya vitabu (na viko vingi sana) ambavyo vinatumika kila siku katika shule za msingi huko Ufaransa ili watoto wajifunze kuhifadhi na kuenzi mazingira yao. Kama si hivyo, watoto wangaliendelea kutumia fumbewe na manati yao hadi kufika hatua ya kutaka kutumia silaha ya kuteketeza mazingira yao…


 

 
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni