11/03/2014

Mazingira asiliya katika fasihiKatika fasihi ya kiswahili, si rahisi kukuta mwandishi aliyejitahidi kuelezea mazingira yake ya kiasiliya, jinsi ilivyo, hasa katika vipengele vyake vyote, kuanzia ardhi, mimea, miti, hewa, maua, wanyama na kadhalika. Pamoja na kwamba riwaya nyingi zinastahili kusomwa, ni kweli pia kwamba takriban tungo zote zinazumgumzia mambo yale yale tunayokumbwa nayo, yaani mambo ya kijamii. Binadamu, binadamu na tena binadamu ! Kupendana, kuchukiana, kufunga ndoa, kupeana talaka, kuzaa, kuiba, kufisadi, kuua, kushtakiwa, kufungwa jela, na kadhalika. Furaha na udhia, heri na shari. Imekuwa kama mlimwengu yuko peke yake wala hana mwandani wake ila mwanadamu mwenziwe, hana mvuto mwingine ila ule wa kula, kulala na kufanya mapenzi. Si ubinafsi au ubinadamunafsi ? Matilaba, tamaa, utashi na ashiki. Mhusika yeyote katika riwaya, akitaja mnyama ni kwa sababu anataka kumsaka, kisha kumwinda, hatimaye kumwuza au kumla. Akiangalia mti ni kwa sababu anavutwa na mbao zake ili ajipatie besera au fremu ya kitanda atakachokilalia. Akipishana na mwenzie — mtu maridadi, awe kimanzi au mlimbwende — ni kwa sababu anataka makamuzi. Lakini kuangazia kitu ambacho hana faida nacho — ingawa tunajua kwamba hewa tuna faida nayo… ­— hana habari, hajali wala habali.

Hapo chini nimebandika dondoo ya riwaya maarufu ya Said Mohamed na nyingine za Adam Shafi zinazogusia swala hilo la mazingira asiliya na baadhi ya viumbe tunaoishi nao kwa heri na shari, kisha nimetafsiri matini nyingine kutoka shajara ya mwandishi wa kifaransa wa kiswizi ambaye alikuwa hodari sana katika kuelezea mandhari na mazingira yake.

« Hali ya hewa inaburudisha na mandhari inavutia. Pepo mwanana zinamparamia na kumpuliza Fadhila ili kumpeperushia wasiwasi wake ; lakini wapi, roho haitaki na nafsi haikubali. Hata videge vilivyocharukwa, vilirukaruka mbele yake, kushikamana na mazingira na kukamilisha liwazo na mapumziko kwa mwenye faka. Katikati ya kutojua la kufanya, Fadhila alisadafu kutupa jicho baharini, akatazama hiki na kile kwa mara ya mia na moja toka alipofika hapo. Ingawa alikuwa na tabia ya kupenda mandhari, sasa pwani ilikuwa chapwa ! Ilimchusha isimguse kamwe moyoni mwake. Yote hayo ni kwa vile yule anayestahiki kukaa moyoni mwake hajafika. » Said Mohamed, Arusi ya Buldoza, 2005 : uk. 78. 


« Popo waliojenga masikani yao juu ya mkamasi, pale Mkamasini wameanza kukifurahia kiza wanaruka ovyo ovyo kufurahia kuanza kwa siku yao. Wamechoka kujining’iniza kichwa chini miguu juu mchana kutwa na sasa zamu yao ya kutamba imefika » Adam Shafi, Vuta n’kuvute, 1999 : uk. 242. 


« Miti hiyo ni mirefu, imekwenda juu na huko juu imejimwaga ikatandaza matawi yake yakajenga paa hewani lililokata jeuri ya jua likashindwa kupenyeza miale yake kufikia barabara ile. Hewa hapo ilikuwa burudani. » Adam Shafi, idem, uk. 243.

« Mbayuwayu wametangulia kufika, wanacheza juu ya rusu ya ziwa ambalo limechachuka. Kwa wepesi wao usiokuwa na mshiko, wanateleza katika hewa tuli kwa vikundi vikundi vinavyopendana, mara wakijifanya kutua hadi kugusa viwimbi vya maji, mara wakipaa juu kwa kuchapa hewa kwa mbawa zao, vitu vidogo vyeusi na vizuri vinavyoucheka upepo na maji huku vikipurukusha hali ya hewa. Havina kitu ila kasi yao, harakati zao za kuruka mbio mbio na hizo zinatosha. Angalia michezo yao ya kudeka na kujitapatapa huku na huku kwa uchangamfu, jinsi vinavyokutania, wewe kiumbe maskini ambaye umepaswa kusota chini katika tope mithili ya nyoka ya Eva. Havijinyimi nafasi ya kukumbatiwa na kimande kinyevu, mara vikiganda mbinguni mara vikiwayawaya kama jani lililopeperushwa na upepo. Vinakucheka, kwa kukucheka wewe mlimwengu uliyegongomelewa katika ardhi tasa, vinakucheka wewe ambaye asilani hutawahi kutamwa na raha hiyo ya kukatisha hewa kwa kupiga mbawa. » C.F. Ramuz, Journal, 13 mai 1897 (Shajara, 13 mai 1897)

Mbayuwayu : aina ya ndege anayerukaruka mbio mbio, wengi miongoni mwao husafiri kutoka Ulaya kwendea Afrika ; hujenga kitundu (au kiota) chake cha udongo upenuni mwa nyumba na penye varanda za majengo ya binadamu ; jina lingine, barawai. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni