16/02/2014

Uhalisia katika fasihi : kiini macho au kiini cha ubunifu ?

« Tell all the truth but tell it slant » Emily Dickinson (1830-1886)


Maupassant (1850-1893) katika dibaji ya kitabu chake kiitwacho Pierre et Jean anatutoa katika ujinga kuhusu ubunifu wa riwaya. Pamoja na kwamba dibaji hii ni matini muhimu sana iliyotangulia katika historia ya uchambuzi wa neno uhalisia katika fasihi, Maupassant pia anatukumbusha kwamba riwaya ni usanii ambao unasawiriwa kwa kutumia maneno ya lugha iliyokamilika, si kama kinasasauti ambacho kinatumika ili kunukuu kilichosikika katika mhadhara fulani au katika mazungumzo ya mtaani. Mtunga riwaya ni kama msanii anayechonga sanamu katika gogo au jiwe, au kama mchoraji ambaye anajua kuteua rangi zake kabla hajaanza kuchora. Ile sanaa itakayopatikana si picha ambayo inaakisi dunia halisi.Na msingi wake tunaouona katika riwaya zile ambazo zimetungwa kwa kutumia usimulizi wa nafsi uliobebwa na mwandishi mwenyewe. Hata katika riwaya kama hizo, hatuwezi kusema kwamba msimulizi — ambaye hutumia neno mimi — ndiye mwandishi mwenyewe anayetoa kauli yake, anajitetea dhidi ya kashfa zinazomfika katika mfululizo wa matukio anaohadithia mwandishi. Hilo ni wazi kwamba riwaya ni tungo la kughushi hata kama limeandikwa kwa kutumia mtindo wa ubinafsi. Kwa mfano katika riwaya maarufu wa Tolstoï (1828-1910) The Kreutzer Sonata, hatuwezi kusema kwamba umimi ule ni kauli ya mwandishi mwenywe, ambaye anachukua fursa hii ya tungo lake ili kutubia neno au kukiri jambo ambalo limemjiri katika maisha yake. Umimi katika riwaya hii ni sanamu ya mwandishi lakini siye. Sisi wasomaji tunayemdhania ndiye nd’o siye. Na hata kama katika baadhi ya riwaya tunahisi kwamba mwandishi yupo chini kwa chini katika mpangilio wa visa wake, si kigezo cha kutufikirisha kwamba mwandishi anasanifu maisha yake. Riwaya bora ni tungo ambalo linaficha mtungaji wake. Hata katika vitabu vingine vizuri ambavyo si riwaya, kama kile cha Rousseau (1712-1778) kiitwacho The Confessions, kitabu ambacho mwandishi alijiamulia kusimulia kumbukumbu zake za zamani, tunaona kwamba mwandishi anajitahidi kuzisimamia vizuri hisi zake huku akitumia fani iliyokamilika. Na bila shaka, msomaji ananaswa na muundo huu, kitu ambacho kinaonyesha dhahiri kwamba mwandishi aliyekomaa katika ufundi wake ndiye ambaye anadhibiti hisia na misisimko zake. Lakini wakati Rousseau anapokuja juu kwa kufunua jazba alizokuwa nazo kuhusu mwandani wake fulani, anashindwa kutumia lugha ile ya haya na hekima ya mwanzoni inayotakikana katika usanii kama huo.

Kwa hivyo, msanii mzuri ni msanii ambaye amefaulu katika kugusia wazo au hisia bila hata kuzibeba au kuziwasilisha moja kwa moja. Mguso unaozunguka zunguka kwa kutumia njia iliyo hanamu ni bora zaidi kuliko ule unaojizusha kwa kufuatilia njia iliyonyoka. Taswira tunayojenga katika ufahamu wetu ni nzuri zaidi kuliko ile tunayoiona kwa macho yetu. Na katika riwaya, kivuli cha jambazi kinachoonekana ghafla kizimbani usiku, kupitia mwangaza hafifu wa kibatari, kitatisha zaidi kuliko uso wake hata kama umeduduika. Umati wa watu waliofikwa na kichaa, ujahili na ubedui kwa sababu ya udokozi uliotokea mitaani, utaangaziwa kwa  njia bora kama mwandishi anaelezea kinachopitia katika kichwa cha kibaka anayesakwa. Fumbo ni afadhali kuliko mipasho. Msomaji anataka kutekwa kwa sababu anapenda kutumia akili na uelewa zake kwa kukisia na kufahamu yeye mwenyewe bila hata kuaswa, kuonywa au kuonyeshwa.

Maupassant anaangazia ndani ya ufundi wenyewe, anatoa mapendekezo ili waandishi wasije wakasahau kwamba wanapaswa kuficha mbinu walizotumia ili kuhadaa msomaji. Kwa kusema kuhadaa, najua kwamba nimekosea kwa sababu ningalisema kwamba mwandishi mzuri wa riwaya hana budi kujisahilisha ili ajionyeshe ni mkweli. Kazi ya usanii wa riwaya ni kukurupusha baadhi ya mambo yakinifu ili kubaathisha yale yanayopuuzwa katika jamii. Hivyo Maupassant anasisitiza kwamba mwandishi anapoandika, « lazima arekebishe au abadilishe baadhi ya matukio ya maisha yake kwa sababu anacholenga ni uhalisia wala si ukweli ». Uhalisia ni neno ambalo lina maana mahususi kwake, ya kuzingatia kuwa mwandishi ni mbunifu wa jambo ambalo linaelekea kuwa kweli kwa sababu limeyumkinika tu, yaani lipo katika jamii. Lakini si lazima liwe la kweli. Kwa sababu si kazi yake mwandishi wa fasihi kulenga ukweli. Usanii ni uwongo mzuri. Katika kukarabati uhusika, uhalisia ni kama mtomo unaokuja kufinyanga muonekano wa mhusika, ili picha tutakayofikwa nayo wakati tutakapokumbwa na wahusika katika masomo yetu ionekane ni kweli. Na ikiwa riwaya imetengenezwa kwa umahiri kamili, sisi wasomaji bila shaka tutakuja kunaswa kwa sababu tumesaini mkataba ule wa kukubalia udanganyifu.

Ni Flaubert (1821-1880), mwandishi mashuhuri wa Ufaransa aliyekosoa neno hili « uhalisia » kwa kuonyesha ghadhabu zake kuhusu neno hilo. Katika shajara na barua zake nyingi alizoandika tunaweza kusoma yafuatayo : « watu wengi wanafikiri kwamba ninanogewa na uhalisi lakini si kweli, nauchukia. Na ni ile chuki ya uhalisia iliyonifanya nikaandika kitabu hiki (Madame Bovary) ». Mtunga riwaya huuatili wakati wake anapotaka kuelezea mtiririko wa mikasa iliyozuka katika mazingira yake kwa kutaka yeye mwenyewe kushughulikia matukio aliyowahi kuhudhuria. Ushahidi hautoshi katika kutunga riwaya nzuri. Madame Bovary si riwaya inayasimulia mkasa wa Madame Bovary ambaye aliwahi kuzini nje ya ndoa, hapana. Kitabu hiko ni kijembe kikubwa, ni kejeli kubwa dhidi ya watu wa enzi ya Flaubert walioenzi sana maadili ya kizandiki yaliotawala katika tabaka la juu — mabwanyenye — la jamii ya kifaransa. Hapo tunaona kwamba uhalisia ni singizio la kisanii. Mauzauza tu.Tukirudi nyuma katika historia, tunakuta waandishi wengine maarufu sana kama Flaubert waliosonga mbele zaidi katika kukiuka ukweli wa maisha. Miongoni mwao Cervantes (1547-1616) na kitabu chake maarufu Don Quixote ambacho nacho kimejaa dhihaka na kejeli, za kuonyesha kwamba mtungaji mwenyewe anajiponda (anajipa jina la kughushi Cid Hamet Ben-Engeli) kwa kushughulisha wahusika wake katika pirika za kimasomaso na kihamnazo za kuchekesha kupindukia msomaji. Katika kitabu hiki tunajihakikisha kwamba uhalisia ni gamba la riwaya linaloficha jina la msanii pamoja na maudhui ya tungo lenyewe. Kuwasilisha ni mbinu yenye kidanganyamacho ndani yake, ni mchezo wa kisanii wa hali ya juu ambao wasanii wachache waliwahi kuumudu. Mtungaji mbaya ni yule anayedhania ukweli ni uti wa mgongo wa fasihi, ambaye hufikiri kwamba riwaya haina budi kuchapisha ukweli, kwa sababu riwaya ni copyright. 


Kwa mantiki hiyo, si jambo la kushangaza kuona kwamba watu wengi hufikiri kuwa mtunga fasihi ni mnyang’anyi. Kwa nini tusome riwaya kuhusu tatizo tulilo nalo katika maisha yetu wakati waandishi habari, wana siasa, na hasa wasanii wa filamu wamepiku katika kutengeneza picha halisi ya changamoto nyingi tunapambana nazo kila siku ? Hapo tunapata jawabu zuri kuhusu kupungua kwa sifa ya usanii huu wa kifasihi katika dunia yetu. Na kweli, tuangalie mapokeo ya fasihi yakoje  hapa Tanzania ? Je, tunaye msanii aliyewahi kutunga riwaya inayosimulia hadithi ya kubuni iliyoelezea visa changamani vilivyotokea zamani sana, kwa mfano Groenland, kwa kuumba wahusika ambao si watanzania, kwa kuelezea maudhui yasiyowahusu watanzania wa leo, lakini kwa kugusia matatizo yanayokumba binadamu kwa jumla ? tena kwa umahiri mkubwa na kwa kutumia lugha iliyopambika ? Kwa nini wasomaji wengi duniani wamezoeleka kusoma vitabu vya riwaya vya nchi za kigeni ambazo hazina uhusiano wowote na mazingira au mandhari yao — eti ni kitu hiki kinachoambatana na ule so-called utamaduni ? Kwa nini kitabu maarufu katika mapokeo ya fasihi ya kiulimwengu — si ya kikuyu, au ya kiperu, au ya kifaransa ­— kama kile cha Murasaki Shikibu (973-1014 au 1025) kutoka Japan kiitwacho Semi la Genji — ni kitabu kinachopendeza dunia nzima ? Au kitabu chake hakisomeki kwa sababu Shibiku alikuwa ni mkoloni, hoja ambayo ni kigezo kikubwa sana katika kutenganisha binadamu siku hizi ? (Ah ! kwa nini nisome msanii huyu, si mjapan tu ? Hainipigi mshipa ! Usikonde babu, fasihi yetu ipo… haya, twende kwenye kabumbu, Yanga na Simba si wanacheza leo ?). Waromani wa zamani sana, wakati nchi yao ilikuja kuangamia, hawakujikosesha kwa kusema « mkate na michezo, inatosha ! ». Na kweli jamii hii ya kifahari ambayo imeturithisha baadhi ya tamaduni tunazotumia hadi leo, imekufilia mbali…

Hapo chini naomba ruhusa, mpendwa msomaji, ya kubandika dondoo la hadithi fupi iliyoandikwa na Said A. Mohamed, mwandishi fasihi wa kusifiwa katika kiswahili, ambaye kwangu si mwandishi halisia bali ni mwandishi ambaye angalikubali maneno ya Marcel Proust aliposema : « Fasihi ndiyo maisha halisi » :


« Kitambo kikapita na pale Jabu alipoona nafasi ni nzuri alipiga mbio kumwendea huyu mwanamama na alipofika karibu, nyaku alinyakua ule mkoba wake.
- Mwizi, mwizi…
Watu walimfukuza. Kundi la watu wenye hasira. Jabu tokea hapo hakuwa na mazoea wala maarifa ya wizi wa kupora au wowote. Alitetemeka alipouona ule umma unamfurusha. Moyoni alijaa hofu. Miguu ilimnyong’onyea, akawa hawezi tena kwenda mbio. Ghafla jiwe lilitua kichwani pake na baadaye hakujijua tena — puu, alianguka chini na pumzi zikaziba. Ndipo utazame ulimwengu wa kinyama usiojua sheria. Mwenye gongo, mwenye jiwe, mwenye buti, mwenye panga, umma wote ulianza kumhujumu na kumbakisha mzoga uliotapakaa damu. »

Kutoka katika Arusi ya Buldoza na hadithi nyingine, Dhuluma inamojificha, uk.15-16, Said A. Mohamed, Longhorn Publishers, 2005.


Marejeo :

Rousseau : HAPA

Tolstoy : HAPA 

Maupassant : HAPA 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni