11/04/2014

Kiswahili cha mitaani na fasihi

Watu wengi huamini kwamba lugha ya mitaani huchangia kwa kiwango kikubwa katika kukua kwa kiswahili, na bila shaka mchango wa muziki ya kizazi kipya, ile inayoshushwa na vijana wa kijiweni, ni fasiri au maelezo ambayo baadhi ya wataalamu hutilia maanani sana. Kwa maoni yangu, kauli hiyo si sahihi ingawa ni kweli kwamba lugha yoyote hujiendeleza kwa kukuza msamiati utokao katika matabaka yote ya kijamii. Lakini matabaka yote. Na kiswahili kitakua zaidi wakati matabaka ya juu katika jamii yatatumia lugha hiyo katika nafasi zake zote na katika vipengele vyake vyote. Bila ya kujivuna au kujishua hadhi. Lugha ni lugha. Lakini lugha si chombo pekee. Kwa kusema nafasi na vipengele vyake vyote, nataka kuzingatia mawanda yote ya lugha, hasa katika istilahi zile ambazo, kwa kawaida, watu hawashughulikii nazo, ikiwemo usanii, sayansi, ubunifu na falsafa. Lugha za mitaani hazihusishwi na vipengele hivyo wa hali ya juu bali zinajishikiza na « maisha », ugumu wake, na namna za kupambana na uchungu wake. Kwa kupekua juujuu katika lugha hii ya mitaani Tanzania, hatuna budi kubaini kwamba istilahi ndizo zile zile, tangu zamani, yaani : kujamiana, kuwasiliana, kujitarazaki, kuvaa na kupamba mwili, kupata na kutumia pesa, kupata uzoefu wa ulevi na dawa za kulevya, na namna za kupata uhondo fulani.

Hapo nimebandika mfano wa kielelezo katika usanii wa ujenzi ambacho kilitengenezwa Ufaransa. Kinaonyesha namna ya kutaja baadhi ya sehemu ya majengo kwa kutumia maneno mahususi. Ingawa msamiati huo haujulikani na watu wote wenye kujua lugha hii, maneno hayo yapo, na yanachukuliwa kama ni maneno muhimu ya lugha ya kifaransa, na yanatumika endapo mtu atapenda kuyatumia.


Je, nani, katika wasomaji wangu wa hapa, wanaweza kunisaidia kutafsiri katika kiswahili majina yote yanaotajwa juu ya kichoro hiki kinachoelezea sehemu zote za ujenzi huu bunifu ? Vijana wa mitaani ? Maprofesa wa chuo kikuu ? Wakilishi wa lugha hiyo katika asasi mbalimbali na idhaa za kiswahili duniani ? Kikubwa hapo ni kujikumbusha kwamba lugha za kiulaya zilistawi kihistoria wakati ziliposifiwa na watu wa juu katika jamii, si vijana jobilesi, yaani vidampa. Mukisoma vitabu vya Shakespeare, vya Hugo, vya Boccaccio, vya Cervantes, mtakuta kwamba vyote vimekopea maneno mengi katika « mitaro » au kwenye bomba za miji ya Ulaya, nao wasanii hawa wakayageuza yakawa maneno ya tabaka la juu ! Wasingalikuwepo wasanifu hawa wa lugha fasaha, maneno haya yote ya mitaani yangalikufilia mbali na lugha hizo, kama vile kifaransa na kiengereza, bado zingalikwenda kwa kudemadema ! Ya nini tena ? Mwenyewe Shakespeare alikuwa si supasta wala hakushika maiki ili kushusha mstari. Alikuwa ni msomi wa kweli, kama wenzake katika dunia hii ya fasihi, ambao hawakuwa na kiburi chochote, huku wakisikiliza vijana wa mtaani pamoja na kusoma lugha yao kwa kina na kwa undani, si kifaransa tu, bali kilatini, kigiriki, yaani lugha asiliya zote za kiulaya. Ndipo lugha hizo zilipotajirika, ndipo lugha zikazuka zikawa za kifahari !


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni