09/04/2014

Shaaban bin Robert na wazee wa zamani


Katika miaka ya 1980 hivi, nakumbuka niliwahi kukutana na wazee wengi wenye maarifa asiliya na hekima ya kina ambao takriban wote wameaga dunia yetu leo. Wengi katika hao walikuwa na kumbukumbu nzuri kuhusu historia ya Tanzania, na walikuwa na kipaji kikubwa kuhusu usanii wa kifasihi, uwe fasihi simulizi kama vile mashairi ya manganja (aina ya ngonjera) au fasihi andishi kama vile utenzi wa marehemu Shaaban Robert. La kushangaza ni kwamba wazee hawa wote — na hapo nataka kuzungumzia wazee wa vijiji vidogo vya sehemu ya Pande, mkoa wa Lindi — hawakujua kusoma wala kuandika, lakini wengi walibahatika kuwa na uwezo wa kuhifadhi mashairi mengi ya Shaaban Robert na kuyatoa baadaye kwa ghibu. La kusikitisha ni kuona kwamba siku hizi vijana wengi katika vijiji vile vile, pamoja na sehemu nyingi ya Tanzania (iwe ya visiwani au ya bara), hawajui hata jina la mshairi huyu. Kama wazee hawa wangalikwenda shuleni, je wangalikuwa mbumbumbu kama mzungu wa reli ? Kila siku namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nadhari ya kutodharau wasiokuwa na elimu rasmi ambao mara nyingi huwapiku maprofesa juha na mapostdoktoreti wenye makeke na kitimbakwira kibao.
"Ewe uliye na maya, shauri langu lishike,
Ina matata dunia, kwa kudumu ndani yake,
Mpaka umeondoa, huzuni yako ucheke.
Cheka cheko ni furaha, uache kusikitika ;
Cheka upone jeraha, yaepuke na mashaka,
Na mwili kupata siha, ukianguka inuka.
Inuka juu inuka, chini usigaegae,
Inuka na kisha cheka, kucheza uendelee ;
Endelea na kucheka, na shangwe kuu nanyowe.
Cheko iwe maridhawa, kunjua uso ucheke,
Mungu Muumba dunia, furaha mchezo wake ;
Huzuni itakimbia, kicheko ni dawa yake.
Tena fanya kila siku, kicheko kifululize,
Na mchana na usiku, furaha iendeleze,
Acha msiba kushuku, kukujia jikataze.
Cheka na watu kukicha, na usiku ukariri,
Ucheke jua likichwa, na kisha uwe tayari,
Huzuni yako kuacha, kwa sababu huhasiri.
Cheka sasa kwa furaha ; dhiki ingawa usoni,
Dhiki ni kama mzaha, asiyecheka ni nani ?
Haya cheka ha ! ha ! ndiyo ada duniani.
Cheka mwanadamu cheka, mtu kaumbwa acheke,
Msiba kwake dhihaka, kicheko mtu mwenzake,
Ni mwenzake wa kuweka, huzuni adui yake.
Msiba unazeesha, mtu bado ni mchanga,
Ndiyo sumu ya maisha, inafaa kujitenga,
Mwilini inaozesha, uzikwe chini ya changa.
Cheka uzuie kwisha, maishayo mbio mbio,
Furaha ndiyo tamasha, kiumbe aliyo nayo,
Hata nyota zakumbusha, kuwa nayo hali hiyo.
Mawingu yanapotenga, nyota mbinguni hucheka,
Chini likashuka anga, la furaha kupeleka,
Kwa wakubwa na wachanga, wapate kufurahika.
Cheka kicheko ni dawa, hutia nguvu mwilini,
Moyo ukapata kuwa, ndani na matumaini,
Ndilo jambo maridhawa, kwa kiumbe duniani.
Basi cheka kwa ! kwa ! kwa usafike moyo wako —
Pamoja na malaika, wema mbinguni waliko ;
Cheka usiwe na shaka, itakuja zamu yako."

Shabaan bin Robert, Kielezo cha fasili, Cheka kwa furaha, Nelson ed. 1968 : uk. 15-16.


Hapa chini nimebandika rekodi ya sauti ya marehemu mzee Mawi wa Kilwa Pande aliyekuwa msanii mahiri katika kutunga mashairi ya ghibu na hadithi nyingine za kuchekesha. Mzee Suleiman Mawi alikuwa ni mpenzi na mshabiki wa Shaaban Robert, hata kama hakusoma vitabu vyake. Tumuombe Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Mzee Mawi mpendwa mahali pema peponi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni