27/05/2014

Fedha, pesa, mshiko, mkwanja na kadhalika…Katika lugha ya kiswahili, pesa ni ishu kubwa sana. Eti ni mdahalo ! Umuhimu wake umedhihirika hasa katika msamiati au katika lugha ya mitaani. Hususan kama huna mapene, utashindwa kuwa na mshiko. Na kama huna mshiko, pengine utamhangaisha kibosile chako akudakishe fuba. Si Tanzania tu, hata uzunguni ! Angalia huku Londoni, kama mkojo umekushika, itabidi ujipatie choo biladi ukapate kujisaidia, lakini kwa kutoa mkwanja kwanza, angalau alasiri mbili, yaani mbala moja. Siku moja huko Bongo niliwahi kumwendea Machinga mmoja njiani ili aniuzie fegi moja ya SM : nikampa buku huku nikisubiri chenji zangu. Kuona kwamba mwuza wangu anachelewa kutoa uchache, nikamwambia : bwana wee unisusie goto langu ! Kwa kuwa Mbongo ni mcheshi, yule jamaa akanirudisha jiwe langu. Ingalikuwa ni kisu je ? Kingalifaa ? Mbongo ni mcheshi, na kwa vitimbi vyake mswahili hakubali kuwa mabaga, asilani ! Si sirikali ina matanuzi makubwa siku hizi ? Mboni mlalahoi naye akaukiwe mbumba ?

Katika fasihi vile vile, fedhwaa ni hoja inayoshughulisha wasanii. Tena tangu zamani. Hapo nimekong’oli dondoo ya riwaya maarufu ya Said Mohamed iitwayo Dunia mti mkavu :

« Kwa nini nafsi ya mwanadamu ikakorwa na mali, utajiri, pesa, husuda. Kwa nini jibu la swali lolote likawa ni pesa ? Siku za mwanzo, alijidharau mwenyewe kwa kuuliza swala namna hiyo. Kwa nini ? Labda kwa sababu ya pesa ni uhai, bila ya pesa hakuna uhai. Aliona kwamba ulimwengu umetanzwa kwenye nyavu, milioni za nyavu labda, ambamo ndani, mwanadamu alitapia kujitanzua — kujikomboa labda. Katika tapatapa hii, pesa ndio iliyokuwa utanzuo wa nyavu mojamoja. Wingi wa pesa, ndio wepesi wa kujitanzua, na ukosefu wake, ni hatua ngumu. Na maskini atapigana wee, hata lile analoambulia ni kujitoa kwenye nyavu moja baada ya moja kwa muda mrefu wa mateso na kabisa hawahi kujikomboa kutokana na nyavu milioni hizo kabla hajafa » Dunia mti mkavu : uk. 36.

Hoja hii ya matumizi ya pesa katika maisha ya binadamu imeelezewa katika vitabu vingi, wala si katika lugha ya wakina broo wala kwenye kurasa za mapaparazi wadogo pekee. Tukitupia jicho katika baadhi ya vitabu hivi kwa kuchukua waandishi mahiri ambao wamepata umaarufu katika dunia nzima, swala la pesa halikupuuzwa hata kidogo. Miongoni mwao tunakuta Rousseau, msanii mzuri wa karne wa 18. Mwana falsafa huyo aliandika vitabu vingi sana, kuhusu maisha yake mwenyewe na mambo mengi mengineo kama vile pesa. Namna alivyolijadili swala hilo, kwa kujipima katika nafsi yake, inatuelewesha jinsi matumizi ya fedha yalivyokuwa yana udhia kwake :

« Mtu anapaswa kuelewa vizuri hisia zangu tepetevu ninazokumbwa nazo : nashindwa kupatanisha msimano wangu wa kwanza uliokolwa na ubaghili wa kina na ule wa pili unaodharau fedha kupita kiasi. Kwangu fedha ni kitu ambacho sina raha nacho, kiasi kwamba sitamani kujipatia kile ambacho sijakipata. Aidha ikiwa ninazo, basi nakaa nazo bila hata kuzitumia, kwa kuwa sijui kuzitumia kwa hiari yangu. Lakini ikitokezea sababu nzuri ya kuzitumia, basi nafaidi hadi sina habari kwamba zimeniishia kibindoni. Bali musiniongopea kwa kusema kwamba mimi ni mbaghili, kwa kuwa sina budhara wala gharadhi. Kinyume na hayo, mimi napenda kutumia kwa kujificha : lakini sina ukuu katika kutoa pesa kwa sababu napendelea kujificha. Kusema hivyo ni kumaanisha kwamba pesa sina uzoefu nayo, na naona aibu kuitumia na kuwa nayo. Ningalipata mshahara mzuri wa kuweza kukidhi mahitaji yangu yote, nisingalikuwa na mwelekeo huo wa kutaka kubana matumizi, hiyo nina uhakika nayo. Ningalitumia pesa zangu zote bila hata kujaribu kupata ongezeko la kipato, lakini hali yangu ya sasa iliyo duni kiasi inanitia wasiwasi. Mimi napenda sana uhuru. Nachukia kizuizi, mateso na uonevu. Kadiri pesa zimo kibindoni mwangu, ndipo napozidi kujitegemea. Hunisaidia nijiepushe na hila na hiana, sifa mbaya ambazo zingalichangia nipate kipato kingine, kitu ambacho kingalinichukiza sana ; na kwa kuwa naogopa kuishiwa na pesa, basi naitunza sana. Pesa tuliyo nayo ni chombo cha uhuru wetu lakini ile tunayoisaka inatuonea. Hiyo ndiyo maana kubwa mimi naitunza wala siivizii. » Les confessions, 1782.

Risala hii ya Rousseau si ya kipekee. Ningalikuwa na fursa ya kutaja matini mengine kutoka katika fasihi andishi, kama vile riwaya nyingi ya Balzac, Zola au Peguy, ambao wamezungumzia swala hilo la fedha kwa kina, pengine ningalikiuka mipaka ya blogu hii ambayo si laiki yake kupokea fasili na maelezo mengi. Imenikumbusha shairi moja la Shabaan Robert ambalo nitapenda kulibandika hapo kwenye ukurasa wangu kusudi ukumbuke, mpendwa msomaji, kwamba wasanii katika lugha ya kiswahili wanastahili kupanda juu ya medani ya ubunifu na kugezana kiustaarabu na wenzao kutoka nchi za kigeni. Kila siku mimi nasikitika kuona kwamba watu wengi hujidharaulisha kwa kushua lugha yao, mbali na kutojua kwamba usanii hauna mipaka yoyote.
Udhia wa mali

Mali kitu cha udhia, najua mashaka yake ;
Usingizi hupotea, afadhali iende zake.
Wakati nilipokuwa mkononi nina kitu,
Furaha sikuijua kwa kuzungukwa na watu ;
Wakidai usuhuba, uwapacho hakitoshi,
Na kulia kuwa haba, wakazidi kunighasi.
Mali ni kitu dhaifu, afadhali isirudi,
Iliwaleta elfu, na mia ya mahasidi ;
Waliotaka nakidi, kwa sifa wakanisifu,
Kunipenda kwa fuadi, kumbe si waaminifu !
Mali kitu cha hasama, iweje hali yake, A !
Kutamani nimekoma, nitakuwa mkichaa.
Mali ina uadui, hata kwa ndugu wa moja,
Haliye ni kama hii, kitu hiki cha kioja.
Tangu mali kunihama, sasa ninayo amani,
Lepe zaidi ya pima, nilalapo kitandani.

Kielezo cha fasili, Nelson, 1968 : uk. 8

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni