14/06/2014

Ngoja kwanza nimcharaze mke wangu ! Nimrapue rapuuu !Nakumbuka nilipokuwa nikiishi London, zamani kidogo sasa, nilikuwa na jirani aliyekuwa na tabia mbaya ya kutwanga mkewe kama mtama, angalau siku moja kila wiki, ilikuwa mbinu yake ya « kumsomesha », kama alivyokuja kujitetea baadaye mahakamani alikoshtakiwa. « Mimi  namfirigisa mke wangu ili ashike adabu yake, akishapata mapigo mawili matatu, basi ametulia, na nyumbani kwangu mambo yanakwenda vizuri ». Na kweli, nyumba yake ilikuwa kama kilinge cha mateso, na bwana yule alipoamua kumtesa mkewe, bila shaka aliondokea kuwa subiani wa kutisha. La kushangaza ni kwamba mkewe alikuwa kipande cha mwanamke, lakini mzuri sana, amejaza, mweusi kama mpingo na baridi kama maji ya mtungi. Kwa sura yake ya mviringo alikuwa binti bulibuli, hana mashobo wala maringo. Kinyume na hayo, alionekana bado ni mwari mwenye haya, na mashavu yake yalijaa kama puto, kitu ambacho kilidhihirisha ukarimu wake.

Kila nilipopishana naye kwenye ngazi, alinikabili kwa tabia yake nzuri sana, huku akitabasamu kwa kunionyesha meno yake meupe kama bafta, lakini ilikuwa si vigumu kumaizi kwamba tabasamu ile ilisinyaa kwa ndani, licha ya kufunika mfundo au dukuduku la moyoni. Nilipomwambia siku moja kwamba nitapenda kumkaribisha nyumbani kwangu, angalau tupate kuelewana kiujirani, niliona kwamba furaha ilianza kutembea na kulea ndani ya damu yake, akajishtukia ameganda mbele ya mlango wangu huku akisimama kama mlingoti, kusudi pengine nimkaribishe ndani apate kulikimbia tundu lake la vyuma, lakini mara tukasikia sauti ya bwana ikimwita kwa kutumia lugha ya mchuuzi samaki, na ndiye aliyekuwa mumewe ambaye alishapachikwa jina la mume bugu au, kwa jina lingine, mume shume. Na kweli dume lile alikuwa na makucha na hadi leo, nikikumbuka ujahili wake, bado ninamwonea huruma yule bibi na shufaka haziachi kunivaa. Kusikia fujo alilofanya mumewe siku ile, bimdogo yule hakuwahi kujikurupusha, seuze kusonya, mara uso wake ukampotea bashasha yote ukawa umemjaa wasiwasi, huko juu mbabe yule ameshaanza kumvurumishia maneno makali, tayari ameshajivuta nje ili azoe « mali » yake… hapo ndipo kidege changu kikatimka kwa ghafla kama umeme.Basi siku ile ikawa janga kubwa. Mapigo yakatandikwa, na kwenzi zikasikika. Sijui ilikuwaje, lakini dari ile kwenye ghorofa yangu ikajiwa na mitetemo, chapa mzigo, piga viboko, tandika mkanda. Zingalifumka ngumi hapo ningalipanda ngazi mbili mbili mpaka juu, lakini mfyosi yule alikuwa pandikizi la mtu, aliyezoeleka kufoka kama faru na kumlamba njiti mtu yeyote aliyemtokezea kwa ukaidi wake. Nikafanya subira kisha nikatoa taarifa kwenye kituo cha polisi na mtondogoo wake bwana yule mharabu akapandishwa katika karandinga.Voltaire (1694–1778), alikuwa mwandishi maarufu kutoka Ufaransa. Aliwahi kuandika vitabu vingi, katika mawanda mbalimbali, ikiwemo falsafa, tamthilia, insha, na hadithi nyingi sana, nyinginezo za kufurahisha na kusisimua akili za wasomaji wake. Alitoa mchango mkubwa sana katika kuinua hali ya dhana katika falsafa ya karne ya Nuru (Enlightenment). Katika maandishi yake, muhimu ni Barua za kifalsafa (Lettres philosophiques, 1734), Zadig (1748) na Candide (1759).

« Zadig alisogea kuelekea mipaka ya Misri. Mtumishi wake ambaye alikuwa ni mtu mwaminifu alikuwa ameshafika katika kijiji cha kwanza ambako alijitahidi kumtafutia pahala pa kukaa. Kwa wakati huo, Zadig alikuwa anatembea peke yake kuelekea bustani zilizokuwepo kwenye ukingo wa kijiji hiko. Mara akaona mwanamke mmoja karibu na barabara aliyekuwa akilia kwa kusalia malimwengu na mabingu yaje yakamtoa katika balaa iliyomkusa huku akifuatwa na bwana mmoja mwenye hasira kubwa. Kufikwa na bwana huyo, mara mwanamke akajitupia chini na kumpigia goti. Lakini bwana akamvaa kwa mapigo na masuto mengi. Zadig hapo hakuweza kustahimili stihizai iliyoletwa na mtu ambaye, kwa ujeuri wake dhahiri, alikuwa ni mwivu, pengine kwa sababu bibie alimtoroka. Bibi yule alikuwa akiomba radhi, lakini Zadig alivutwa na uzuri wake kwanza, kwa sababu alifanana na hewala yake Astarte, ikawa akamwonea huruma licha ya chuki alizokuwa nazo juu ya bwana wake. ‘Hebu nisaidie ! alipiga kelele mwanamke huyo huku akimlilia Zadig, njoo basi ukanitolee katika mikono ya hayawani huyo, uniokolee ! » Kusikia kelele hizo, Zadig aliwakimbilia akajidai kuwaamulia na kwa kuwa alikuwa anababaisha kiarabu kidogo akasema : « kama utu unaujua maana yake, nakusihi bwana uzingatie uzuri na unyonge wa bibi huyo, ni hizaya kubwa sana kukalifu uzuri wa kiumbe aliyekamilika kama bibi huyo, isitoshe yupo hapo akikupigia goti na hana lolote la kumsaidia ila machozi yake ». « Ala ! akimjibu bwana huyo kwa hamaki nyingi, hata wewe unampenda, siyo ? basi wewe ndo nitakurabu, ngojea kwanza nilipize kisasi papo kwa papo ! ». Akamwacha mkewe na nywele zake alizozikamatia akatafuta mkuki akijidai kumchoma nao mwandani wake. Katika hekaheka hizo, akijaribu kuchomoa mkuki huo, Zadig naye alimwahi akaukwapua. Nao ukavunjika katika mikono yao. Mmisri akachomoa upanga wake na Zadig hivyo hivyo. Wakapigana. Mmisri akapiga mipigo mingi, naye Zadig akajitetea kwa kutumia ufundi mzuri. Na bibi yule ameshakaa chini kwenye nyasi, anapuna nywele zake, ametulia tuli huku akiwatizama wakipigana.


Kwa ubabe wake, Mmisri alikuwa na nguvu nyingi lakini Zadig naye alikuwa mwepesi kupindukia, akionyesha kwamba anapopiga ndicho kichwa chake kilichouongoza mkono wake, wakati Mmisri akiongozwa na hasira zake ovyo aliendelea kupiga mipigo ya mafamba. Ghafla Zadig alimweza adui yake akampora silaha yake. Kuona vile, Mmisri akapandishwa na mahoka akamrukia Zadig. Zadig alimkwepa akamzuia barabara akamwangusha chini akamshika kidinindi huku akishamwekea upanga wake nusura kumchoma nao. Kwa mbawazi wake, Zadig hakufanya hivyo akamnusurisha. Hapo ndipo Mmisri kwa mori yake ya hali ya juu alipochukua mwanya huo ili kuchomoa jambiya alikuwa nayo akamjehuri Zadig. Kuona kwamba adui yake hajakubali kutubia, Zadig akamdunga upanga wa kifua chake. Mmisri akatoa ukwenzi wa kutisha akafariki dunia. Zadig alimkurubia mkewe akamwambia kwa sauti yake rahimu : « amenilazimisha nimwue, nimekulipizia kisasi, na umeng’atuka katika mikono ya mtu mwenye ubabe kupindukia. Sasa basi, utapenda nifanye nini ? » « Nataka ufilie mbali, wee mshenzi mkubwa, ndiyo umalizike, uage dunia hiyo, wee umemwua mume wangu, ah ! laiti ningaliweza kung’oa moyo wako ! » « Kusema la kweli, mumeo huyo alikuwa ni mtu mbaya, aliongeza Zadig, kwanza alikupiga kwa kutumia nguvu zake zote, pili alijaribu kunitoa roho yangu, tena kwa sababu ulinisihi nije kukuokoa ». « Ningependa anipige tena, alimaka mwanamke huyo kwa kutoa siyahi kali, nilistahiki kupigwa, umesikia, kwa kuwa mimi ndiye niliyemtilia wivu, msalie mtume anipige tena nawe uondoke dunia hii ! »Said Mohamed, Utengano, uk.47-48 (Longhorn, 1980)

Bwana Maksuudi anarudi nyumbani kwake na amegutuka kuona kwamba mwanae Maimuna ametoroka au, kama anavyodai mwenyewe, ametoroshwa na mama yake mzazi Tamima :

« Maimuna yu wapi naseeeemaaaa. Ilikuwaje ? Alaa, ndiyo mambo yako haya ? Nikiondoka mimi, wewe unatawala enn ? Unamtorosha mwanangu na wewe mwenyewe unajiuza siyo ? Yuko wapi Maimunaaa ? »

Maksuudi ilimtoka bakora ambayo ilianguka juu ya kichwa cha Tamima. Tamima alipiga usiyahi mkubwa akaanguka chini. Muda ulipita. Maksuudi alihema kwa ghadhabu na Tamima aligaragara. Baadaye Tamima alipopata upumzi, alitupa mkono pale alipopigwa bakora. Damu ilikuwa ikimchururika.

(…)

Bi Tamima hakujua jengine la maana ; na udhaifu wake, alinyanyuka taratibu pale alipokuwa kapinduka akajivuta kusogea kwa mumewe. Alipofika karibu yake, alianguka na kumpigia goti. Alimsogonea mumewe amlaani bilisi. ‘Ni… nisameeeehe Bwaaana Maksuudi, si kosa languuuuu ; Maimu… na kakimbiaaaa…’ Tamima alilia kwa nguvu. Chozi labda lingalikuwa kinga.

‘Si kosa lako ? Si kosa lako enh ? Si kosa lako enhe, kosa la nani ? Langu ? Sema, kosa langu ? Kosa la nani basi ?’

Maksuudi alitupa bakora yake na sasa aliupapatua ukanda wake kiunoni. Aliuvuta na kuanza kumcharaza nao mkewe.

Raaap ! Ukanda ulitua juu ya mwili wa Tamima.

‘Mtumeee’ alisalia Tamima huku akiangukia meza iliyokuwa na buli na vikombe vya kahawa vya fedha. Hivyo akenda navyo chini pamoja. Maksuudi aliendelea kumpiga Tamima kanda ya mafamba. Tamima hakujua njia ya kujikinga. Maksuudi aliendelea kucharaza. Tamima zilimtoka mtume nyingi. Hakuwa na hila wala rai ya kujiokoa. Pale chini alibaki kusota kitango malele na huku Maksuudi akimrapua kwa ukanda. Akamwandama ukimbi mzima. Vitu vya mapambo vikaanguka. Maksudi aliendelea kumrapua Tamima ; mara kipembe hiki mara kipembe kile na mara amvute mkono amlete katikati ya ukumbi. Ilikuwa hujma isiyokuwa na mwombezi, na Maksuudi alipiga kama mwendawazimu »

Molière « Mganga asiyejijua » (Le médecin malgré lui) :

Katika tamthilia maarufu ya Molière (1622-73) iitwayo « Mganga asiyejijua », tunakuta wahusika wawili, Bwana Sganarelle na mkewe Martine ambao wanapeana maneno mengi hadi Bwana Sganarelle anajikuta katika msimamo wa kutaka kumcharaza mkewe. Hapo ifuatayo ni dondoo la onyesho la kwanza, mwanzoni mwa mchezo huo niliotafsiri hivi karibuni.


SEHEMU YA KWANZA : SGANARELLE, MARTINE.

Porini karibu na nyumba kwa Sganarelle. Sganarelle na Martine wapo kwenye jukwaa huku wakigombana.

SGANARELLE — Haata, nakwambiaje mimi sitaki, nitasema kwanza mimi maana mimi ndiye kiongozi hapa, umesikia ? 
MARTINE — Na mimi nakwambia kwamba nataka kuishi kwa hiari yangu, wala sikuozeshwa ili kuvumilia upumbavu wako ! 
SGANARELLE — Wanawake bwana wanachosha sana ! Kweli mwanamke ni mbaya kulilo shetani, kama Aristote alivyosema.  
MARTINE — Aka, kanajifanya akili sana, eti Aristote ! Si mpumbavu huyu ? 
SGANARELLE — Ndiyo, natumia akili zangu. Utampata wapi mtema kuni anayejua kutafakari mambo kama mimi, isitoshe aliyemtumikia mganga maarufu kwa miaka sita, ambaye amehitimu masomo yake wakati bado mdogo ! 
MARTINE — We una wazimu nini ?  
SGANARELLE — Mwenda wazimu mwenyewe, mzoga mkubwa we ! 
MARTINE — Ah ! laana juu ya siku ile niliyoolewa na lijitu kama hili !
SGANARELLE — Na alaaniwe mshenga beberu yule aliyeniunganisha na mwanamke huyu balaa.
MARTINE — Wewe si mtu wa kuilaumu ndoa hii kabisa. Kwanza shukuru Mungu umepata mwanamke mrembo kama mimi. Pili hukustahili kabisa kunioa mimi ! 
SGANARELLE — Dah ! Lakini kweli ulinistahi sana siku ile ya ndoa yetu mpaka ukanikubalia. Kwa kweli nilijipongeza sana usiku ule wa kwanza. Sasa usinisemeshe sana hapo nisije nikasema… 
MARTINE — Nini tena ? Kitu gani ? 
SGANARELLE  — Acha tu  ! hayo yote tunayajua, kwanza uliharakisha sana kunikubali. 
MARTINE  — Una maana gani unaposema kuharakisha kukukubali  ? Mwanaume anayenishindisha hospitali, mtu mwovu, msaliti na ananijazia choo tuu  ! 
SGANARELLE  — Wee mwongo  mkubwa  ! 
MARTINE  — Unaniuzia kila kitu ndani ya nyumba yangu. 
SGANARELLE  — Si tunaishi pamoja kwa kubana matumizi  ! 
MARTINE  — Umenichukulia hadi kitanda changu  ! 
SGANARELLE — Si utaamka mapema sasa ? 
MARTINE  — Hujanibakishia hata fanicha moja ndani ya nyumba yangu  ! 
SGANARELLE — Enh enh ! Itaturahisishia kuhama ikitokea dharura ? 
MARTINE — Shughuli zako kubwa ni michezo na ulevi tu ! 
SGANARELLE  — Hilo si linatusaidia kupumzisha akili ? 
MARTINE — Sasa unataka nifanye nini wakati tunayo familia ? 
SGANARELLE — Fanya upendacho ! 
MARTINE — Ninao watoto watano mikononi ! 
SGANARELLE — Si uwaweke chini ? 
MARTINE — Wananibana kila saa huku wakitaka mlo. 
SGANARELLE — Watandike viboko basi. Wakati nimeshakunywa na kushiba barabara napenda watu wangu nao wapate shibe zao katika nyumba yangu ! 
MARTINE — Acha ulevi wewe ! Unajidai mambo yatakwenda vizuri kumbe huna lolote ! 
SGANARELLE — Mke wangu, tungamana kwanza chonde chonde ! 
MARTINE  — Ukorofi wako nitauvumilia mpaka lini  ? Unafikiri ukorofi na uhuni wako…
SGANARELLE  — Wee tusije juu mke wangu  ! 
MARTINE — Unataka nifanyeje ili utimize wajibu wako ? 
SGANARELLE — Mke wangu, unajua uvumilivu wangu una kikomo chake nao hauchelewi kukatika sasa hivi. 
MARTINE — Sijali sitishiki mie wala usinibabaishe na maneno yako.
SGANARELLE — Mke wangu, kifaa changu, umechemka sasa kama kawaida yako, haya…
MARTINE — Ngoja…mimi sikuogopi wala nini.
SGANARELLE — Habibi naona unataka kupigwa sasa ! 
MARTINE  — Usinitishe kwa maneno yako.
SGANARELLE  — Kipenzi changu (kwa kubembeleza huku akitaka kumtomasa mashavu).
MARTINE  — Usinishike mlevi mkubwa  ! 
SGANARELLE  — Sasa nitakupiga kweli ! 
MARTINE — Mtambo wa gongo we ! 
SGANARELLE — Nitakukata mtama Martine ! 

MARTINE — Thubutu ! Mshenzi wewe ! 
SGANARELLE — Aaah sasa uko tayari kupigwa (anachukua bakora).
MARTINE — Kwenda zako mwizi mkubwa. Kwanza wewe mwongo, msaliti, mfidhuli, boga, fala, mjinga, zilo mkubwa, mpumbavu na mshhhhenzi kabisa ! 
SGANARELLE (anampiga
MARTINE — Mama yangu weee !... ah ! 
SGANARELLE — Hilo linafaa kukutuliza sasa ! 

SEHEMU YA PILI : Bw. ROBERT, MARTINE, SGANARELLE.

Bw. ROBERT — Eh ! Eh ! Nini tena ? Jamani mwee ! Si balaa hii mbona  hivyo  ? We bwana kumpiga mkeo kama si ujinga ni nini ? 
MARTINE (mikono yake imeshika kiuno chake anaongea na Bw. Robert huku akimrudisha nyuma kisha anamtandika kofi usoni) — Mimi mwenyewe nataka kupigwa 
Bw. ROBERT — Enh ? …haya nakubali 
MARTINE — Inakuhusu nini ? 
Bw. ROBERT — Sawa 
MARTINE — Angalieni mtu asiyekuwa na adabu, anataka kuwazuia wenziwe wasipige wake zao ! 
Bw. ROBERT — Nakubaliana na wewe. 
MARTINE — Haya unalo hapo ? 
Bw. ROBERT — Hapana. 
MARTINE — Kwa hivyo linakugusa ?
Bw. ROBERT — Hata kidogo. 
MARTINE — Hayakuhusu haya wewe ? 
Bw. ROBERT — Sina la kusema. 
MARTINE — Mimi napenda kupigwa, umesikia  ? 
Bw. ROBERT — Nimesikia. 
MARTINE — Sasa inakuumiza wewe ? 
Bw. ROBERT — Sawa sawa. 
MARTINE — Kama si ujinga kuingilia shughuli za watu ni nini ? 
Bw. ROBERT (anamgeukia mumewe Martine naye pia anaongea naye huku akisukumiza, akampiga kwa bakora ile ile akamkimbiza kisha akasema) — Niwie radhi mwenzangu usione wasi wasi kujiandaa kumpiga basi ashike adabu yake, ngoja nikusaidie ! 

Inaendelea…


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni