16/10/2014

Tafsiri sisisi ? Mfano wa « Mwana mdogo wa mfalme »


Hivi karibuni tumebahatika kupata tafsiri ya kitabu cha msanii wa kifaransa Antoine Saint Exupéry kiitwacho kwa kifaransa « Le Petit Prince ». Kitabu hiki ni aina ya riwaya isiyo na thamani kubwa sana, wala haina mnato wala fahari ile ya vitabu vingine ambavyo vilipata umaarufu mkubwa katika mapisi ya kifasihi. Hapo ningalithubutu kusema kwamba katika nchi au jamii ambapo watu huzoeleka kusoma sana, le Petit Prince si kitabu chenye ladhaa ya kisanaa. Kwa hivyo, ni jambo la kushangaza kuona kwamba kitabu hiki hutafsiriwa katika lugha nyingi za dunia wakati hakina fani wala maudhui ambazo huchukuliwa na wasomaji wengi kuwa kweli ni kitabu cha maana. Katika mapokeo ya fasihi huku Ufaransa, ambako msanii Saint Exupéry alikozaliwa, ni kitabu ambacho hakitumiki darasani wala hakipo penye safu ya vitabu vya kutilia maanani. Kinapendezwa na watoto au watu ambao hawajasoma sana, pengine kwa sababu ni rahisi sana kukisoma. Ni dhahiri kwamba ni kitabu kipendwacho na watu ambao hawajapata ufahamu na uzoefu mkubwa wa fasihi. Huenda ni kwa sababu hiyo — kutokuwa na uzoefu wa kusoma fasihi — hasa katika muktadha yetu ya kiutandawazi, mchakato ambao unatutumbukiza katika machachari ya kusahau tunakotoka na kudharau mapokeo ya kisanaa. Fasihi ni aina ya sanaa inayotutoa katika harakati ya kisasa, pirika tulizo nazo za kila siku, shughuli zetu za kuhangaikia kitu fulani au uhondo fulani. Fasihi ni dawa ya kupoza uchungu wetu wa kuishi leo na kufariki kesho.

Sidhani kwamba le Petit Prince ni kitabu kinachobeba jukumu hilo. Kwa wepesi wake ni hadithi ifananayo na lawalawa. Kina sukari nyingi lakini hakina virutubisho. Puleki na thumni zake zinameremeta lakini kwa juujuu ili kubembeleza malimbukeni wa vibuku uchwara. Kina uja uzito lakini hakina uzazi. Kimevimba kiasi lakini kimejaa hamira. Le Petit Prince ni mtoto mdogo ambaye hatafikia hali ya ukongwe. Katika dunia yetu ya vingwagu wanaopenda makorokoro, blingbling na ulimbwende wa kiburi cha hali ya juu, huenda kitabu hiko kitapata nafasi yake, lakini mbali sana na machela ambako fasihi ghaliki hulazwa siku hizi. Ndiyo maana kwamba tafsiri yake si kazi kubwa sana. Wala haihitaji tafsiri fasiri kama kile kitabu cha Sokofile, Mfalme Edipode. Tafsiri yake kwa kiswahili kinaridhisha, kwa maana ya kwamba kinakidhi dhima ya fasihi hiyo yenye uvuguvugu, ijapokuwa mategu na makosa madogo yalitokea hapa na pale, pengine kwa sababu wafasili walijikwaa kwa kutumia nakala iliyokwisha tafsiriwa katika lugha nyingine ya pili (kwa mfano hakuna duma katika tungo asiliya bali ni taiga).

Kuna kitu kingine ambacho kimenikanganya kidogo, nacho ni kichwa cha kitabu hiki kwa kiswahili. Wafasiri wake wamachagua kichwa cha Mwana Mdogo wa Mfalme, kichwa ambacho hakiridhishi kwa kuwa kinagusia vipengele fulani ambavyo havipo katika kitabu cha kifaransa. Nadhani mfasiri amepotosha maana iliyokusudiwa na mwandishi wa kitabu hiko kwa kuongeza kitu ambacho ni kigeni katika hekaya asiliya. Kwa kutumia maneno mengine, ningalisema kwamba maana chanzo kimebadilishwa kwa kudhamiria maana shabaha (au maana lengwa) ambayo kwa matokeo yake hubeba maana nyingine ambayo haikuwepo katika tungo husika. Hivyo itakuwaje mtoto huyo ambaye ni mhusika mkuu wa hadithi hiyo awe mwana wa mfalme ilhali hana ukoo wala nasaba wala jina ? Isitoshe, ufalme wake sio huo tunaozoea nao katika nchi ambazo mpaka leo hutawaliwa na mfumo huo wa siasa. Wala mtoto huyo si mtoto adinasi ambaye kwa adabu na tabia yake nzuri msomaji atasema ni mtoto nemsi. Pengine kwa kuwa huishi katika sayari yake ya kiajabu angepachikwa jina la kisasa Mtoto supasta ! Lakini ukimchunguza vizuri, utamkuta amezamisha mikono katika mifuko yake, amevaa nguo ya rangi ya kijani, amefunga kipepeo chekundu kwenye shingo lake, vitu ambavyo si vya kisupasta. Tungalipenda awe mtoto mwenye uso wa kutabasamu lakini, kinyume na hayo, amesimama cheni kwa kung’ang’anaa huku akionyesha sura ya ukakamavu. Kweli si mtoto aliyezaliwa katika tabaka la juu (hayupo katika umwinyi) wala si mtoto ambaye hupenda mambo ya kisasa mithili ya watu limbukeni au viongozi wetu wasiokuwa na elimu. Pengine ni mtoto wa ajabu aliyetoka katika ndoto zetu. Huenda shani zake zingalikuwa ni za kikwetu ikiwa tungaliishi katika sayari ya mbali sana. Kama ni hivyo, basi hatuna budi kukiri kwamba ubunifu wa kifasihi hapo umetimia kwa kuonyesha kwamba maisha yetu katika dunia haijakamilika, wala haitakamilika kamwe tusipobaini upungufu na walakini za maumbile yetu.La umuhimu sana tunapotafsiri riwaya au kitabu chochote cha kifasihi ni kuhifadhi nia ya mtungaji bila kuharibu maana iliyokusudiwa. Sisemi kwamba kichwa cha hadithi ya Saint Exupéry kwa kiswahili kimepotoka kwa maana ya kutolingana na maana chanzo ya kichwa cha kifaransa, ila nadhani kwamba kimeongeza kitu ambacho kipo katika jamii ya kitanzania tu au kwa baadhi ya watu wa nchi hiyo — hapo nisingalisema ya kiafrika kwa sababu swala hilo la kuzingatia uzito wa ukoo au kiujamaa halipo katika desturi za kiafrika pekee. Lakini mtoto huyo alivyofinyangwa na msanii wake siye mtoto mtegemezi ambaye amechorwa katika mazingira ya kiujamaa fulani. Kinyume na hayo, yuko peke yake, hana asili wala mustakbali, hana damu wala maji. Ni mtoto huria. Juu ya hayo, huuliza maswali mengi sana, pengine kwa kuwa yumo katika harakati ya kujitambua


Toba ! Kwenye intaneti na katika makala nyingi, hata katika zile ziandikwazo na wataalamu na magalacha wa yunivasitiz — wacha na vitoa vitabu vya vizungu vya kiglobishi — tunakuta jina la msanii wetu wa kifaransa likichapishwa na -, yaani Saint-Exupéry, maandiko ambayo si sahihi ! Marehemu aliwahi kurekebisha mara kwa mara watu waliopuuza jina lake, lakini wapi… Na kosa hilo dogo, bado linazidi kufanyika… hata kwa kiswahili ! Nani kasema kwamba utandawazi ni aina ya maambukizi ya ujinga ? Chambilecho, bana !

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni