26/01/2015

Tafsiri haini ? Mifano kadhaa


Tunajua sasa kwamba tafsiri yoyote ni kazi ambayo huingiliwa na udanganyifu na mauzauza. Kwa kuandika udanganyifu, najua kwamba nimeshakiuka mipaka ya maadili ambayo bila shaka msomaji huizingatia sana. Kwa kutumia neno hilo udanganyifu, namaanisha kwamba mfasiri anajua fika kwamba kazi itakayompendeza msomaji ni ile ambayo itaficha juhudi zake za kitafsiriri, yaani ustadi wake ambao ukijidhihirisha sana katika taaluma yake basi matokeo yake utafuja raha ya msomaji. Ni jambo la kutilia maanani hasa katika kufasiri fasihi. Kwa mfano, kutafsiri Shakespeare katika kiswahili ni kazi kubwa sana ambayo aliwahi kupirikana nayo mwalimu Nyerere — ingawa itikadi ya siasa alikuwa nayo ilimdanganya kiasi fulani — ya kuonyesha kwamba ufanisi wa tafsiri upo katika uwezo wa binadamu wala si katika utamaduni wake. Kwa kifupi, mfasiri mzuri ni yule ambaye ameondokana na tabia ya kujipeleka mbele — kama kwamba ndiye aliyetunga kitabu anayetaka kutafsiri — ili lugha anayeitumia katika tafsiri isionekane ya kigeni mno au ya kienyeji kupindukia. Tunakumbuka tafsiri ya Clement Ndulute kuhusu kitabu cha Chinua Achebe (1930-2013) « Things fall apart » ambacho kichwa chake kwa kiengereza kikageuzwa « Shujaa Okonkwo » badala ya « Dunia imepasuka » au « Mambo yamevurugika ». Hapo ni wazi kwamba mfasiri alizidisha, pengine kwa kutaka kuswahilisha hadithi ya Achebe, uwenyeji (wa kisiasa ?) wa kitabu cha Achebe.

Hata hivyo tusisahau kwamba baadhi ya wafasiri wazuri, miongoni mwa wale waliobaki kwenye orodha ya majina ya mabingwa katika historia ya tafsiri ya fasihi, walikuwa hawana ujuzi wa kutosha kuhusu lugha ambayo waliitafsiri. Hapo nitapenda kutaja mfasiri mzuri Mchina ambaye alijitahidi sana kutafsiri kitabu kimoja cha mwandishi maarufu Mfaransa Alexandre Dumas (1824-1895) ambaye aliandika riwaya inayojulikana kama La dame aux camélias. La kushangaza hapo ni kwamba mfasiri huyo, kwa jina lake Lin Shu (1852-1924) hakuimudu sana lugha ya kifaransa, kiasi cha kuomba msaada kutoka wasaidizi wake ambao, kwa kuwa walijua kifaransa, walikubali kwanza kumsimulia hadithi ya kitabu hiko ili baadaye Lin Chu aitafisiri katika kichina. Ijapokuwa ufahamu wa kifaransa wa Lin Chu ulikuwa mdogo sana, hatuna budi kukiri kwamba tafsiri yake ina kivutio kikubwa sana, hadi kuwa na mnato mkubwa mpaka leo. Kilicho wazi hapo ni kwamba Lin Chu alikuwa hodari sana na umahiri wake katika kuandika katika lugha yake ya kuzaliwa ulikuwa wa kina sana, licha ya kuiweza katika vipengele vyake vyote na hasa katika fani zake zote. Wengi katika wasomaji wa kitabu hiko katika lugha ya kichina husema kwamba tafsiri yake imeipiku hadithi asiliya.

Cha kusisitiza hapo ni kwamba mfasiri anaweza kufasiri lugha ambayo anaibabaisha bila hata kuathiri kilicholengwa na mwandishi katika lugha hiyo ikiwa umahiri wake katika kufinyanga fani imewekwa mbele sana. Umbuji au uzuri wa tafsiri ni kigezo kikubwa tunachopaswa kutilia maanani katika kutathmini mafanikio ya kazi kama hii. Hapo nitapenda kutaja tafsiri moja ambayo ilitolewa zamani kidogo na Mkuki na Nyota, nayo ni riwaya ya Mariama Bâ (1929-1981) Une si longue lettre, yaani Barua ndefu kama hii kwa kiswahili. Hapo nadhani kwamba mtafsiri C. Maganga amefaulu sana katika kazi hiyo ngumu ya kutafsiri kitabu ambacho kiliandikwa katika lugha ya kifaransa (kutoka Sénégal). Na kufanikiwa kwake kuna sababu zake mahususi ambazo hutusaidia kuelewa kwamba kazi ya kutafsiri fasihi si kutafsiri lugha (pekee). Ndiyo maana nakataa kauli ya wafasiri wengi ambao huzingatia sana sarufi, uteuzi mbaya wa maneno au upotoshaji wa maana. Fasihi si porojo ya mitaani, mapayuko ya baraza, au maandishi ya mapaparazi au makala yoyote ya insha. Fasihi si ujumbe wala chombo cha mawasiliano.
Kuna jambo moja ambalo haliachi kunishangaa. Hivi karibuni tumeshuhudia uchapishaji wa kitabu ambacho hakipo katika urithi wa fasihi, nacho ni kitabu cha Saint Exupéry kilichotafsiriwa katika kiswahili kwa kupewa kichwa Mwana mdogo wa mfalme. Hapo pia tunaona kwamba kitabu cha Mariama Bâ nacho kimepata bahati hiyo ya kutafsiriwa katika lugha ya kigeni. Lakini je, vitabu hivyo kweli vina rutuba au utamu fulani tunapovisoma kwa kifaransa ? Kwangu kitabu cha Mariama Bâ kimejaa majivuno na mbwembwe, yaani kimeandikwa kimpangilio wala hakina mtiririko ule wa usanifu unaotakiwa katika riwaya. Kwa kutumia maneno mengine, ni kitabu ambacho kimedhihirisha ufundi wa mtungaji kupita kiasi, kama kwamba mwandishi ameamua kuonyesha dhahiri kwamba anaiweza lugha hiyo ya kifaransa kuliko mzaliwa mwenyewe, awe Mfaransa au Mmali au Mkongo.


Nilipoona kwamba kitabu hiko kilitafsiriwa, kwanza nilijiuliza : kwa nini Yambo Ouologuem, au Amadou Kourouma, au Henri Lopès ambao ni waandishi waliohesabika ni wasanii maarufu sana katika historia ya fasihi, bado hawajatunukiwa tafsiri za vitabu vyao ? Kwa nini riwaya ambayo imeingiliwa na mikogo na mbwembwe nyingi imepata kutafsiriwa wakati Le devoir de violence ya Ouologuem kimebaki katika nchi ya mabubu ? Jawabu tunalipata ikiwa tunakubali kwamba kazi ya kutafsiri ni kazi ya kubuni. Hapo ndipo tutakapoelewa kwa nini mfasiri amefanyikiwa kutafsiri kitabu ambacho hakipendezi sana. C Maganga amefaulu kwa sababu ameshinda — pengine kwa kutojijua — kufuta yale yale ambayo msomaji mzoefu wa kifaransa bila shaka amechukizwa nayo wakati aliposoma Une si longue lettre. Kwa bahati nzuri, Barua ndefu kama hii ni kitabu ambacho kimepoteza mikogo yake ya kiasili. Kama wanavyosema wataalamu wa chuo kikuu, matini lengwa (yaani tafsiri ya Maganga kwa kiswahili) ni bora kuliko matini chanzi (yaani tungo la Mariama Bâ). Kwa mujibu ya kazi ya mfasiri, Mariama Bâ amepata nafasi ya kujifaharisha sana, labda kinyume na alichodhania wakati alipotunga riwaya yake. Mwenyezi Mungu ambariki mfasiri wake !

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni