17/02/2015

Ngugi wa Thiong’o, fasihi na siasa


Mimi ni mshabiki wa Ngugi wa Thiong'o. Katekisimu yake ya kimarxisti, naipenda mno yaani. Nimesoma takriban vitabu vyake vyote. Namna anavyopigania haki ya waafrika, hasa wachimba chumvi wale, yaani walala hoi ambao hupiga mzigo saa ishirini na nne, au vidampa wale ambao huonewa na matajiri wenye roho ya korosho. Yaani watu game tough. Chanzo na chimbuko za tafrani hizi zote tunazijua. Someni Ngugi. Atakusomesheni. Ukoloni tu, huo ndio process iliyoua bendi. Yaani Afrika kapigwa bao yakhe, cause unyanyasaji ulivunjilia mbali mitungi yote ya kienyeji. Na bado ! Wanene wameyeyuka, unafikiri ? Still wamejibanza tu, hupiga deo. Na hakuna yeboyebo wa porini asiye na shukrani kwa vile buradha yetu Ngugi anavyopigania haki za kinabo, licha ya mgoroko. Haki ya Mungu. Nakumbuka siku moja tukiwa na washkaji wenzangu wa Kilwa tukipiga msosi, nami nilikuwepo pale kwa sababu ya mhadhara wenye urasimu mwingi wa kikoloni. Gumzo kali likapasuka pale. Nami nusura nikatimka kwa sababu ya ujinga wangu. Kwani wakati huo nilikuwa sijasoma vitabu vya Ngugi. Ya Rabi alizuka pale jamaa wa kikenya, kwa jina lake hapo nimelitia kaputi, naye alikuwa akiishi kwa mamtoni, akasimama pale akatoa hotuba yake ya kikristu hata mashehe wa msikitini na berere berere zao wangalitupilia mbali tasbihi zao. Wote wah ! kuemewa tu, domo wazi, kidole cha tahiyatu juu ya jamaa yetu na mzimu wake Ngugi. Jamaa huyo Mkikuyu kapiku jamaani, kwa kwenda mbele !


Basi siku ile mimi niliuchuna. Na wenzangu wengine walami wamekula jiwe. Kimya jii. Nikamsikiliza vizuri Mkenya mwenzangu nikakubali kusilimishwa jinsi alivyomfyagilia Ngugi. Chapu chapu siku ya pili yake, nikafukizia mjini, mradi nijipatie nami vitabu vya Ngugi. Na kweli vina kishua. Yaani vinatisha kishenzi. Vyote vinatuhusisha, sisi binadamu. Na ukishavisoma msomaji, hakuna jinsi, huna haja ya kutumia vibuti darasani. Masaa yote, mikono juu. Kwa kusoma vitabu vyake mimi nimefahamu mambo mengi ya nchi yangu nilikozaliwa kabla sijajiswahilisha. Yaani Ufaransa ilivyotawaliwa na ukoloni wa waromani si chini ya karne nne (-52/476), jinsi nchi yangu ilivyoshambuliwa na wavamiaji wa kishenzi kutoka Ulaya kaskazini (kutoka karne 5 hadi karne 8), jinsi nchi hiyo ilivyokaribia kutoweka wakati wa maambukizi ya tauni, jinsi ilivyoingiliwa na ufalme wa kiengereza (vita iliyodumu zaidi ya miaka mia : 1337-1453), mbali na vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati wa vita vya kidini (1562-1598), licha ya maangamizi yenye ujeuri wa kibedui kupindukia yaliyozuka wakati wa mapinduzi ya 1789 yaliyosababisha ukimbizi wa maelfu ya watu wenye umwinyi, mbali ya biashara ya utumwa iliyoteka mamilioni ya wazungu kuanzia karne 16 kwenye fukwe zote za bahari ya Mediteranea kaskazini (hapa). Basi nazidi kusimama dede, na kweli namshukuru Ngugi kwa kunisaidia kupanua akili zangu, jinsi Ufaransa ilivyopigwa na misukosuko hiyo kibao bila hata kutoweka. Na sijataja vita viwili hivyo vya kidunia, vya jana tu. Na nchi hiyo, ambayo niliachana nayo miaka arobaini nyuma, bado inajivurumiza mbele ? Kweli binadamu ni mbabe. Na bado Ufaransa ipo ! Tena imepata tuzo za kinobeli si chini ya 50 karne hiyo ya twenty tuliyokuwa nayo, baada ya kukumbwa na hilaki na teketezo hizo zote. Na ubunifu bado upo, unaendelea, thanks to Ngugi. Ngugi ni mtu kindakikindaki. Ni mtemi wa kweli. Hana ugozi, ukaladi, usuriama wala uchotara. Zamani sana kabla hajazaliwa, wenzetu wa Unguja wangalisema ni mtu konki, yaani pure kabisa, maasumu. Iko siku tutamwabudu, wallahi nakuambieni, tutamjengea hekalu yake. Sank yu veri mach.

Wengine wangalinidakiza papo kwa papo « acha michapo bwana » ! Lakini ukweli umo ndani ya mzaha au mas’khara (mjomba wangu wa msikitini amefutika kidole chake sasa kwani mimi mzungu), wala si mzaha wa kikuyu, jamaani, msidharau watu hawa wakubwa. Ngugi kanataka kuandika kwa kikuyu sasa kwa kuamini kwamba kitendo hicho kitawasaidia waafrika kupambana na ukoloni mambo leo. Yupo jamaa mmoja hivi karibuni aliyenijia akinirushia vijembe kwa kuwa ati ninajigamba kuandika kwa kiswahili. Huku akinisengenya vibaya kwa kunikumbusha kwamba kuandika katika lugha ya kigeni ni jambo la kawaida duniani wala yeye haoni sababu ya kufuga majikwezo ! Na mifano chungu nzima ikamtoka midomoni mwake, tena ihusianayo na pre-colonial period. Nami nikapiga fiksi hapo, jinsi nisivyomwamini. Kwani kwangu kabla ya ukoloni, hamna kitu, giza tupu. Si fasihi ilizaliwa karne 19 katika nepi ya upebari huko Uzunguni ? Eti wajapani wa zamani ya kale walikuwa huandika mashairi yao kwa kichina, eti wazungu wa karne 13 na kuendelea walikuwa na tabia ya kubadilishana lugha zao, waitiliano wakiandika mashairi kwa lugha ya kusini kwa Ufaransa,  na tenzi zilitungwa kwa lahaja ya kifaransa ya kaskazini kwa Italia. Na mwenzangu kanichomozea wengine wa siku hizi, sijui Kundera, sijui François Cheng, au Conrad, ama wale wa Ulaya wa kati, sijui Kafka au Canetti ambao wote walikuwa wakiandika katika lugha ambazo hawakuzaliwa nazo. Wengine wakitumia kifaransa, wengine kiengereza, wala hakuna kasumba wala unyanyaswaji ? Si kweli bana, hayumkiniki hayo, uwongo tu ! Na rafiki huyo ni mtu mweusi, yaani mwafrika Mfaransa, anafundisha fasihi ya kizungu kabla ! Nikauliza, kabla ya nini ? Naye akajibu, kabla ya ujinga !Hakuna maoni:

Chapisha Maoni