20/05/2015

Nimetunga riwaya kwa kiswahili...


…nayo inaitwa "Raha ya maovu". Nilianza kukitunga kitabu hiki wakati nilipokuwa nikiishi Kilwa — Tanzania kusini, mkoa wa pwani. Ni kitabu ambacho hakijakamilika kwa maana ya kwamba hakijapata uhariri wala uhakiki. Najua kwamba kimeingiwa na walakini na dosari zake ni nyingi lakini pia kimejaa taarifa nyingi kuhusu desturi na mila za watu niliokuwa nikiishi nao wakati ule. Sina budi kusema kwamba, ijapokuwa kitabu hiki ni aina ya simulizi iliyobuniwa kwa kutumia lugha ya kiswahili, sura nyingi zimetungwa kwa kukopa maneno mengi kutoka lahaja ambayo wazee wengi walikuwa huitumia katika shughuli zao za kila siku. Juu ya hayo, sura ambazo zinazungumzia shughuli za jando zimetungwa baada ya kuhudhuria na kuendesha shughuli za itani yenyewe. Kwa hivyo, sikuwa na haja ya kusaili wazee wala wapiga soga wenzangu wa maskani wa Mtimbangi nilipokuwa nikiishi, kwa kutumia porojo zilizofinyangwa na vidudumtu na wambea, kwa kuwa watu wengi katika wazungumzaji wa baraza yetu walikuwa ni wazushi wa maneno ya gengeni. Kwa kuwa mimi nina akili zangu na macho yangu, ingawa kinyume na watu wengine nadhani kwamba ogani hizo zinatuhadaa, yote niliyodiriki kuyaona ni sahihi. Na hata kama wahusika katika kitabu hiki ni wa kubuni, vituko na matokeo ya kiushirikina ni vya kweli, hususan nyakanga niliyekuwa nikifuatana naye utagalani, mbali na kuwa mfawidhi wa shughuli za kutolea usungo wa watoto waliotahiriwa, pia alikuwa ni mwalimu wangu wa kunifundisha namna ya kuwatisha na kuwachapa hawa wasimaana ili wasije wakafikiri baadaye kwamba dunia ni miliki yao.

Sioni sababu ya kuandika riwaya katika dunia ambayo imetawaliwa na hela. Ndiyo maana nimeichapisha kupitia mtandao huo. Lakini kuna sababu nyingine. Kwa maoni yangu, fasihi imeshalazwa juu ya machela tangu zamani, wakati fasihi ilipoondokea kuwa tasnia — mchakato ulioingiza fasihi katika itikadi ya uhalisia — na wale ambao wanajidai kuandika fasihi siku hizi ni ama tapeli au makorofi. Lakini ukorofi wao haulingani na ule unaotakiwa na fasihi, kwani hakuna mwandishi halisi ambaye hana lengo hilo la kutukumbusha kwamba tunaishi katika dunia ya udanganyifu, ule unaobebwa na vingwagu wa fasihi bushoke ambao hutuambia kila siku kwamba hakuna kitu cha thamani duniani zaidi ya nususi ya mambo, yale yachipukayo kwenye ardhi kavu inayoshikika. Dunia ya mashiko — au ya mshiko ! — si kitu, au ni kitu finyu, hasa tukiwa na ujasiri huo wa kuichunguza kupitia ndoto zetu au ruya zetu, yaani maruerue yetu tuliyo nayo wakati wa mchana ambayo aghalabu hupuuzwa na lumpeni wa fasihi. Fasihi na utagala ni jambo moja. Yaani ni kimbilio. Hakuna mwandishi maarufu duniani ambaye hakuzingatia sharti hiyo. Ila utagala siku hizi umefungwa. Sisi sote tumekataa kukaa kitako ili kuzingatia yaliyopitwa na wakati, hasa kungwe zile ambazo hazina maana yoyote katika dunia iliyofikwa na hadaa ya kihela. Hata lugha mpya ambayo huchukuliwa ni hazina kubwa kwa kiswahili cha kesho — kutokana na kauli ya wataalamu wa kisasa —, basi lugha hiyo imeuzwa. Ati neno la « kibongo » kitalu limeshapotea ! Na lina miaka kumi hivi, si zaidi ! Kiswahili kile cha zamani ambacho kilitiliwa maanani na vijana wa Kilwa katika miaka ya 1990, siku hizi ni chombo lemavu, na wengi husema ni kinyaa na karaha, yaani pukuchaka. Kwa kuwa mimi sipo katika dunia hiyo, sijali kama lugha yangu ni ya kileo au ya kizamani, sio kwa sababu mimi ni mhafidhina au kwa sababu siupendi usasa, la hasha. Ila naamini maneno hayo ya msanii maarufu wa kifaransa wa karne ya 19, kwa jina lake Stendhal, aliyeandika kwamba binadamu hakupewa lugha ili apate kuwasiliana na watu wengine bali aweze kuficha mawazo yake.  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni