03/06/2015

Raha ya maovu aisee...Leo hii, nimeamua kuangamiza rekodi zangu zote za hadithi nilizorekodi zamani kidogo wakati nilipoishi mkoa wa Lindi katika vijiji vya Kilwa visiwani na bara. Kwa jumla ni rekodi za hadithi mia moja na tatu. Maana ya kitendo hiko ina misingi yake halisi. Kwanza, wiki hii nilipata habari kutoka wenyeji wangu wa Kilwa ya kwamba wazee wale waliokuwa hutamba hadithi hizo, basi takriban wote wamefariki. Msiba huo umenikusa vibaya kwa kuwa wazee hawa, mbali na kuwa mababu zangu kilugha, pia walikuwa na ujuzi wa kina juu ya ubinadamu wa wenyeji waliokuwa wakiishi nao zamani kwenye mwambao wa Tanzania. Ujuzi huo siku hizi umepotea kabisa wala hakuna galacha mmarxisti wa Chuo Kikuu, katika wale wale wanaojitwika jukumu la kusambaza kiswahili duniani (kiukoloni ?), ambaye angalikubali kukalia kandi — kunradhi mkeka mkuu — na washamba hawa akawasikiliza (vijijini tunavaa ndatu au kanda mbili, hatuvai sandozi ya ngozi). Kwangu kusikia sauti ya wazee wenzangu kwenye rekodi hizo ni la kunitia huzuni kubwa wala haivumiliki. Afadhali niziangamize. Pili, hadithi hizo za zamani hazina maana yoyote katika nchi za kiafrika zitumiazo kiswahili ambazo zimefikwa na siasa za uchague nazi ukapate dafu. Kama nilivyoandika katika riwaya yangu, lakini kupitia mawazo ya mhusika anayeitwa Kadhi : 

« …wema haukawii kufutika lakini ubaya unakaa katika dunia mpaka inakwisha dunia, kwa sababu ubaya unavuma, kinyume na wema ambao unadidimia. Ndo maana wazee husema ‘tenda wema wende zako !’ Usingoje shukurani. Ubaya una shukurani. Mtu akifanya ubaya, basi roho yake inafurahi, kwa sababu aliyetaka kumtesa mwenzake, basi ameshateseka, sasa anapita kucheka : ‘eh eh ! Kazi yangu ile !’ Anajifurahisha anajikuta yeye yuko katika raha mustajaba. Wengineo wakimchukia yule, kwa sababu ameshafanya ubaya basi wanakongamana wanaarikana kucheka na kufurahi, wanathubutu kuchinja mbuzi, kuku kutokana na yule alivyopatikana, kwa sababu alikuwa anawatia udhia, labda alikuwa anawambia maneno ya haki au ya sheria, basi wale wanachukia, kwa sababu ukweli unauma katika dunia, si mwarabu, si mhindi, si mzungu, si mswahili… »


Tatu, tunaishi katika dunia inayotukuza aidelojia ya kobe unipe na itikadi za siasa ya mkono mfupi. Katika muktadha huo tulio nao Afrika mashariki, aedolojia ya baada-ukoloni imetawala kiasi cha kubamba njia zote za ubunifu. Laiti wazee wenzangu wangalijua kwamba wajukuu wao wangalikumbwa na kizazi laghai ! Hadithi hizo ambazo hazikuathiriwa na ukoloni wa mpito, wala ukoloni mambo leo na ukoloni rudifu, je zina maana ?

Baadhi ya rekodi hizo zilizookoka katika balaa hiyo zinapatikana kwenye blogu hii : 

Meno ya dhahabu...Matoga ya mke wangu...Furukombe, mnyama wa ajabu...Mohamed na farasi yake…Yunihuni...Asili ya radu...

Maoni 2 :

  1. Ninafuatilia kazi zako za ki-Swahili. Ni za thamani sana. Ki-Faransa ninakijua kidogo sana; hakitoshi kuniwezesha kusoma maandishi ya watu mashuhuri, ingawa baadhi yao nimesoma kama yalivyotafsiriwa kwa ki-Ingereza. Mifano ni Moliere, Albert Camus, Chateaubriand, na Frantz Fanon. Shukrani kwa juhudi zako.

    JibuFuta
    Majibu
    1. Asante sana kwa mchango wako Prof Mbele. Nami pia nafuatilia kazi zako kwenye blogu yako wala sitakosea kusema kwamba mengi katika yale unayoandika yananisaidia kujenga ufahamu mzuri wa "dunia hii ya kiswahili". Kuhusu waandishi uliotaja hapo, bila shaka ni miongoni wa wasanii maarufu ambao wangestahili kutafsiriwa katika kiswahili, lakini kama unavyojua ni kazi kubwa sana ambayo hushindikana kwa kukosekana kwa watu wenye kuzimudu lugha hizo pamoja, yaani kifaransa na kiswahili.

      Futa