17/06/2015

« Wapostiko na Wapostidi » katika fasihi ya kiafrika : Mabanckou na Ouologuem


Katika kikundi cha waposti — yaani wanazuoni wenye itikadi ya post studies — kuna mikondo miwili. Ule wa kwanza unajulikana sana, nao unajumuisha wakina Albert Memmi, Frantz Fanon (1925-1961) na vijikuu wao wa siku hizi, wengi wakiwa na itikadi kali ya kimarxisti. Hawa ni wapostiko (watalaamu wa post colonial studies). Pamoja na kwamba wengi miongoni mwao waliathiriwa na aedolojia ya Karl Marx na wafuasi wake (hasa Lenin na Troski), wengine wamepanua fikra zao kwa kusoma Jean-Paul Sartre (1905-1980) na Aimé Césaire (1913-2008). Katika fasihi, Chinua Achebe (1930-2013) na Ngugi wa Thiong’o wako karibu sana na kikosi hicho. Muono wa wasanii hawa ni hasi kwa kukogesha hoja zao katika ufalsafa wa umarxisti na ufalsafa wa « kuwapo » (existentialism). Kwa mabingwa hawa, binadamu hana uhuru kwa maana ya kutokuwa na matakwa na jukumu. Kwa kifupi, nchi za Afrika zimevurugika kwa sababu ya mzungu (akiwa na damu ya kikoloni, kutokana na maumbile yake) au kwa sababu ya uchumi (siyo siasa ya ndani).  

Lakini kuna kikundi kingine ambacho hakijulikani sana, hasa katika kanda hizo za Afrika zitumiazo kiengereza kama lugha ya kitaifa, kinachoshirikisha wasomi kama Hélé Béji kutoka Tunisia, Amin Maalouf kutoka Lebanoni na Dariush Sheyegan kutoka Iran. 

Wasomi hawa wameendeleza muono chanya kwa kutilia mkazo athari mbaya za siasa ya ndani ambazo zinazidi kukwamisha baadhi ya nchi hizo zilizotawaliwa na ukoloni, hasa tangu zilipopata uhuru. Kwa kifupi, vikwazo au vikwamisho hivyo vingaliondoshwa — yaani rushwa, udikteta, utawala mbaya, gharama holela za uendeshaji serikali zikiwamo posho, gharama za safari za kwenda kununua meremeta, pamba na blingbling Uzunguni, mafunzo na warsha za kula kuku kwa mrija (ndani na nje ya nchi), mafuta na vilainisho, viburudisho vya kila aina, ununuzi wa magari sampuli ya shangingi, upangaji holela, gharama kubwa za matengenezo na ukarabati (barabara, majengo na magari), uhamisho holela na mishahara hewa, na kadhalika —, basi nchi hizo zingalipata uhuru. Wasomi hawa wangalipachikwa jina la mapostidi (yaani wasomi wa post-decolonial studies). Kifalsafa, huamini kwamba binadamu ana uwezo (akiwa na msimamo mkavu wenye matakwa na jukumu madhubuti) wa kujikomboa ikiwa amefundishwa vizuri. Katika fasihi, miongoni mwa wasanii kutoka bara ya Afrika ambao wamekoleza imani yao katika mkondo huo, tunakuta Sony Labou Tansi (1947-1995), Henri Lopès, Emmanuel Dongala na Mabanckou, wote kutoka Kongo. Hapo leo nimejiamulia kunakili madondoo machache ya kitabu cha Mabanckou kiitwacho Le sanglot de l’homme noir (Machozi ya watu weusi), jinsi alivyoponda baadhi ya wakilishi wa kikundi hiko cha kwanza. Kinachokosolewa hapo, si mtizamo huo wa kawaida unaoelekeza mapitio kwenye mionzi ya jua tu ili watu wasipate kuona kwenye giza, bali ni propaganda inayozonga mwandishi fulani ili wasomaji wasikumbuke waandishi maarufu walioishi zamani kidogo. Mfano : hapa na pale tunakuta kwamba mwandishi mwafrika wa kwanza aliyeanza kuandika katika lugha yake ya asiliya ni ama Thomas Mofolo (1876- 1948) au Ngugi wa Thiong’o, kauli ambayo si kweli. Lengo hapo ni wazi : tusahau tenzi na shairi zote zilizotungwa zamani sana uswahilini. Mfano mwingine : baadhi ya waposti husema kwamba kabla ya ukoloni, mambo yalikuwa mwafaka na kwamba jamii ya kiafrika zilisambaratika hasa wakati wakoloni walipofika. Kauli hiyo inasigana na ile ya Yambo Ouologuem (kutoka Mali) na washabiki wake. Wana historia wengi pia wamepinga mkabala huo wa waposti ambao huzingatia sana muktadha wa ukoloni wa kizungu huku wakidharau kipindi kile cha kabla ya ukoloni, mathalan biashara ya utumwa iliyofanyika na waarabu dhidi ya waafrika  (hapa kwa kifaransa) au utumwa ulioteka wazungu wa kaskazini kwa mediterranea kuanzia karne 16  (hapa kwa kiengereza ama kwa kifaransa). Hapo naomba kutafsiri madondoo kadhaa ya kitabu cha Mabanckou kama ifuatavyo :

« Wakati riwaya ya Ouologuem Le devoir de violence (Uhayawani ni wajibu) ilipochapishwa mwaka 1968, vijembe na matusi chungu nzima vikaanza kurushwa ili kumfedhesha na kumwumbua mwandishi wake. Riwaya hiyo ambayo imeundwa kiutenzi, inasimulia historia ya nasaba kuu ya watu wa Saïf ambao walitawala himaya kubwa ya Nakem, katika kanda ya Mali. Mwandishi anaelezea jinsi utumwa ulivyokithiri kabla ya wazungu walipofika katika eneo hilo la Afrika. Utumwa huo ulikuwa umeshatapakaa sehemu zote za Afrika huku ukiratibiwa na waarabu na « wakuu wa kienyeji ». Hivyo ukoloni na utumwa vilikuwa si taasisi zilizoundwa na watu wa nje ya Afrika. Katika dibaji ya kitabu chake, Ouologuem anavunja mwiko huo uliogubika historia hiyo akisema : « Ni katika majaaliwa ya Maniga (au golo) kulaaniwa kiasi hicho, wakiteswa na ukoloni uliofanywa na wakuu wa kienyeji, wakateswa baadaye na waarabu waliovamia sehemu hiyo ya Afrika (…) Walipofika, wazungu walichezea mchezo ule wa wakuu wa kienyeji. (…)


 « (…) Riwaya ya Ouologuem ilianzilisha aina mpya ya fasihi ya kiafrika ambayo ilikuwa imefinyangwa na lengo la kujipatia uhuru wa kweli. Ilikuwa mbali ya fasihi ile iliyoshikilia uratibu huo wa mwafaka uliokuwa imeshamiri kote. Ilianzilisha pia tabia na mkabala wa kutaka kujikosoa, ambavyo ni katika vipengele vya lazima ikiwa mtu anataka kukosoa watu wengine. Basi riwaya hiyo yenye ujasiri mpevu ilichapishwa wakati waandishi waafrika kwa jumla walitakiwa watukuze tamaduni za kiafrika na kuelezea kila kilichoendelea kabla ya wakoloni waovu walipovamia bara hiyo ya Afrika kwa kutumia picha zionyeshazo hali ya utulivu na amani. Hawa wakoloni waovu walichukuliwa ni mabeberu waliotakiwa kubeba dhambi zote katika fasihi hiyo, hususan kwa kuwa wasanii wote waafrika walishindwa kueleza kwa nini serikali za Afrika zilikwama baada ya kupata uhuru. »


Kwa kutukumbusha mkasa huo wa zamani kidogo sasa, Mabanckou anataka sisi tuyatafakari kwa kina kilichoitwa kasumba ya kikoloni na athari zake juu ya matumizi ya lugha za kiafrika.

« Tunastahiki kujiuliza kwa nini aedolojia hii inayotuhamasisha tuache kuandika katika lugha ya kifaransa imebebwa na watu wengi siku hizi kiasi cha kugubika swala lingine muhimu, nalo ni umahiri katika fasihi ambao ni kipimio cha pekee kinachopaswa kuwekwa mbele katika lugha zote za duniani. Kwa kujitosa katika mjadala huo waandishi wengi wa bara la Afrika hujipofua kwa kutoona kwamba kigezo kikubwa ni kimoja tu, nacho ni fasihi (…). Hawa wasomi waafrika, kwa kutenda vile, hufanya kimasomaso kwa kupuuza ubunifu ili wajisukumize kwenye msimamo wa kisiasa. Je mtu akiwa mzungumzaji wa kifaransa, kweli hawezi kuwa msanii ? Kiwingu kile kilicholetwa na Ufaransa, je kweli kina uzito mkubwa kiasi cha kutuzuia sisi waafrika tusibuni maandishi kwa njia ya uhuru ? (…) Mimi najiuliza swala hilo la msingi : je, Naipaul, Rushdie, Zadie Smith, Walcott, Danticat, wote hawa wangalichukuliwa ni wasanii wanaokumbatia « aedolojia hii ya kikoloni » kwa sababu huandika katika lugha ya kiengereza, bighairi ya umahiri wao mpana katika ubunifu ? »


Mimi sioni sababu yoyote ya kutofautisha Gurnah na Kezilahabi. Wote kwangu ni waandishi maarufu kutoka Tanzania. Lakini umaarufu wao hauambatani na lugha wanayotumia katika kutunga vitabu vyao, iwe kiswahili au kiengereza, kwa kuwa kinachowatenganisha waandishi hawa ni vile vigezo vya kiujumi pekee, vinginevyo tungalimchukulia Gurnah ni kijibwa cha mkoloni. Afadhali mwandishi anayemudu lugha yake ya kuandika hata kama ni lugha ya kigeni kwake kuliko mwandishi anayetumia lugha yake ya kuzaliwa lakini kwa kutojua masharti ya kimsingi katika kuunda hadithi ya fasihi (na wako wengi Tanzania). Swala si ile ya Ngugi wa Thiong’o anayejitia wasiwasi na kiherehere kwa kuwa hadi leo anazidi kuandika katika lugha ya « mkoloni » wa zamani bali ni kujihakikisha kwamba lugha tunayoitumia katika kubuni riwaya au tamthilia ni lugha ambayo imejitenga na matumizi ya kawaida (lugha ya fasihi si chombo). Swala ni : ina maana gani kulipa swala hilo la lugha umuhimu mkubwa zaidi kuliko umahiri na ujumi unaostahili kuwepo katika fasihi kwa jumla, bighairi ya lugha inayotumika ?


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni