09/08/2015

Tafsiri ya fasihi kama mbinu halisi ya kujikomboa kutoka katika mtego wa utandawazi ?


Hivi karibuni vitabu viwili vya Kezilahabi vimetafsiriwa katika kifaransa. Pamoja na kwamba tafsiri yoyote katika fasihi ni aina ya chamvi (yaani tunu) inayotembea pasi na magusiano yoyote baina ya watu, ni dhahiri kwamba tafsiri ni aina ya silaha ambayo ingalitumiwa na wale wanaosumbukia uhuru kwa dhati. Mfaransa kutoka kijiji chake ambaye hajasafiri wala hajatoka kiamboni mwake, basi sasa ana uwezo wa kutambua kwamba kweli Tanzania ipo duniani, kwa mujibu ya jamaa mwenzetu aliyejitahidi kutafsiri riwaya ya Kezilahabi. Hapo sisi sote tungalimpongeza mfasiri huyo, tukamfupa (au tukamtunza) hela kama inavyofanyika wakati mtoto anapotoka jandoni — lakini wapi, dunia imebadilika, na utandawazi umekwisha kugeuka utandachuki. Hata hivyo, kutafsiri ni kupanua fikra, ni kazi ambayo inachangia pakubwa katika kushirikisha watu wa asili mbali mbali ambao, kwa sababu wanaishi katika nchi mbalimbali, hawana tabia wala satua hiyo ya kukutanisha fikra zao… Lakini je, katika dunia iliyopanuka sana, ambayo mipaka inazidi kupotea kila siku, kutafsiri kuna faida gani ambayo si faida ya kiuchumi ? Huko Ulaya, hususan Ufaransa, kila siku vitabu vya kila aina vinatafsiriwa kutoka lugha nyingi za dunia. Mamilioni ya vitabu vinauzwa kila mwezi, kwa sababu zile ambazo tunazijua vizuri — wafasili wengi ambao ni wenye stadi ya juu katika fani hiyo (na si lazima mfasiri awe mwanazuoni) ; watu kupenda kusoma vitabu vya fasihi, vikiwemo vitabu vitokavyo sehemu zote za dunia ; taasisi mbalimbali ambazo zinathaminiwa na wananchi na zinazohamasisha wataalamu kutafsiri ; utamaduni wa kusoma, na hali kadhalika.Takwimu

Katika dunia yetu, kiengereza na kifaransa ndizo lugha ambazo zinazipiku nyingine zote katika uwanja huo wa kutafsiri fasihi. Kiengereza kinatafsiriwa sana katika lugha zote za duniani wakati kifaransa nacho kinatafsiri lugha nyingi za dunia. Kiengereza kinatembea — na kinatembeza dhana zake — wakati kifaransa « kinasindika ». Katika nchi zote duniani, Ufaransa ni nchi ambayo imechukua nafasi ya mbele katika kutafsiri lugha mbali mbali katika lugha yake kifaransa. Katika vitabu sita viuzwavyo dukani katika nchi hiyo, kimoja kimetafsiriwa. Mwaka 2010, katika vitabu 63052 vilivyochapishwa — ndiyo mpendwa msomaji, hujakosea hapo, nimeandika vitabu 63052 ! Vingapi Kenya au Tanzania ? —, vitabu 9406 vilikuwa ni tafsiri (katika takwimu hii, vitabu viwili (!!) vilikuwa vya Kezilahabi). Na tukiangazia takwimu hizo kwa undani zaidi, tunakuta kwamba katika riwaya tatu, moja imetafsiriwa. Lugha ambazo kwa asimilia kubwa (84%) zinatafsiriwa katika kifaransa ni kiengereza, kijapani, kijerumani, kiitaliano na kispanishi. Ina maana kwamba lugha ndogo ndogo pia (kama kilingana, kithai na kiswahili kwa mfano) hutafsiriwa, lakini kwa uchache (mnamo lugha 50 kila mwaka zinatafsiriwa).

Ina maana kwamba lugha hiyo Kifaransa imeathiriwa sana na mkondo huo mkubwa wa tafsiri. Mfano mzuri wa athari iliyoikumba lugha hiyo tunaikuta katika msamiati wake. Maneno mengi ya kifaransa yanatoka katika lugha mbalimbali ya dunia — hususan lugha za kiafrika —, mbali ya lugha nyingine nyingi kama kilatini na kiyunani. Ni bahati yake, kwa kuwa hakuna lugha tajiri duniani ambayo itakataa kuingizwa na maneno ya kigeni au kutohoa katika lugha nyingine. Kinyume na kinachosemwa hapa na pale katika makala mbalimbali za kiswahili ambazo zinasambaza kauli ya kwamba kutafsiri ni kuvuruga, kupotoa na kuchafua muundo wa isimu ya lugha husika. Kauli hiyo imewekwa juu ya itikadi mbaya inayoamini sana dhana ya usafi au unadhifu wa lugha. Lakini hakuna dhana hizo za « lugha asiliya » wala hakuna lugha iliyo safi kuliko lugha nyingine. Lugha yoyote ni mchakato wa kihistoria. Wazee wangu walioongea kifaransa zamani ya kale wasingaliitambua lugha ninayotumia siku hizi ikiwa wangalifufuka leo. Mimi sijui kifaransa asiliya ni kitu gani.

Pingamizi

Katika itikadi nyingine ambazo zinazidi kuweka pingamizi ya kila aina katika mchakato huo wa kutafsiri fasihi, hatuna budi kugusia aedolojia ya uposti (HAPA) ambayo siku hizi imekithiri kiasi cha kuathiri muono chanya unaotakiwa kuwapo katika kutafsiri fasihi ya kigeni. Badala ya kusema « sisi ndio tunaobeba hilo jukumu la kupunguza sifa na thamani ya fasihi ya kiswahili katika nchi zetu », waposti hupendelea kusema « kiswahili ni lugha ambayo imekwama katika maendeleo yake kwa sababu ya athari za nje — ikiwemo ukoloni mambo leo au utandawazi. Kwa hivyo, « tusiangazie kinachoendelea ng’ambu, sisi tunakalia juu ya mali, hatuna haja ya kutafsiri » (lakini vitabu vingapi vitatafsiriwa, na vingapi vyenye thamani vitaandikwa mwakani ?). Wakati hao husema « sisi tumetawaliwa », je watu wanafanya nini ili kutengeneza muktadha mzuri wa kuweza kuimarisha fasihi husika iliyopo ? Hapo naomba kutaja tena dondoo ya kitabu cha Mabanckou kama ifuatavyo :

« Takriban waandishi wote kutoka Afrika wanaotumia kifaransa kama lugha ya fasihi wanajua lugha zao za kuzaliwa za kiafrika lakini hawazijui kama ipasavyo hasa katika kuandika. Lugha nyingi hizo zimebaki katika hali yao ya awali ya simulizi tu. Viongozi wa nchi hizo wangaliendesha mkakati katika kuendeleza lugha hizo. Kwa hatua ya kwanza, ingalibidi wale watengeneze mbinu zifaazo kama vile sarufi au, kama sarufi ipo, wairekebishe, waisawazishe. Ingalifaa pia kujenga taasisi mbalimbali, kuchapisha kamusi, kutengeneza magazeti, kwa kifupi kuhamasisha watu wainuke wakakubali kutoka katika lugha simulizi — ambayo ni aina ya mchunko (cliché) unaoongoza fikra za watu kuhusu Afrika — wakaingia katika lugha andishi. Kisha wakome kujivuna kwa sababu ati ndio wazee wanaorithisha utamaduni wetu (…). Kuandika katika lugha ya kiafrika haitoshi kwa kuwa kilicho muhimu kwanza ni kumfunza mwafrika yeyote asome katika lugha yake kama vile Mfaransa, Mchina au Mrusi wanavyofunzwa katika lugha zao. »

Hata hivyo, kuna baadhi ya athari ambazo ni kweli kwamba hazisaidii chochote katika kuendeleza usanii kwa jumla. Iko moja ambayo inazidi kila siku kutibua mazingira yetu hasa katika uwanja huo wa usanii — na tafsiri ni aina ya usanii — nayo ni uchumi wa soko huria yenye itikadi kali. Huo mchakato una madhara mengi ambayo tunayaona kila siku katika dunia yetu, nayo kwa mfano Tanzania ni dhahiri. Leo ukitaka kupanda mlima wowote Tanzania, ulipe… ukitaka kukanyaga mchanga wa pwani kwenye mwambao wa Afrika ulipe, ukitaka figo au kama umekosewa na damu kwa sababu umepatwa na saratani ya figo, ulipe (at least, uteke mtoto kutoka Uganda, ukamwue upate chako), ukitaka nyara ya simba, ulipe, n.k. Je kweli katika muktadha hiyo, fasihi na tafsiri zitakuwa na maana ?

Kwa kuhitimisha makala yangu ya leo, narudi kwenye swala la juu. Je, kweli vitabu vya Kezilahabi vitasomwa kwa kifaransa ? Kwa maoni yangu, nadhani kwamba ni jambo muhali. Imekuwa kama tone moja katika maji ya bahari. Hata kama vitabu vyake vina thamani, je vitaonekana katika vichaka hivi vya vitabu vile lukuki ? Vinginevyo naona kwamba kutafsiriwa kwa vitabu vile ni bahati kubwa kwa sababu uwanja huu wa fasihi hauna mipaka (ndiyo maana kauli ya Kezilahabi mwenyewe haieleweki wakati anaposema kwamba yeye huandika kwa ajili ya Watanzania). Kwa kutafsiri kitabu chochote tunajua kwamba tunasaidia kukipandisha kwenye medani ya mchuano mkali sana. Kezilahabi kwa mujibu wa mfasiri wake atakwea ngazi itakayompelekea miongoni wa mabingwa wa fasihi ya dunia. Akifikishwa huko, itabidi aingie katika marumbano. Lakini je, katika utaratibu huu si atayumbishwa ? Swala nyeti ni hilo : je vitabu vyake vina thamani gani ukiviweka kwenye safu ile ya vitabu vingine mashuhuri kama vile vya Murasaki Shikibu, Kenzaburo Oe, Garcia Marquez, Jorge Luis Borges, na vingine vingi tunavyovifahamu sana kutoka nchi za magharibi ?

Somo la ziada hapa kwenye blogu hii.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni