15/09/2015

Mazingira ya mikoko Kilwa Kisiwani


Hapa leo nimefurahi kumkaribisha katika blogu yangu mwenzangu Ryo Nakamura ambaye ni mtafiti kutoka Japani aliyewahi kufanya utafiti mwingi Kilwa. Anafanya kazi katika Research Institute for Humanity and Nature, Kyoto, Japan. Makala hii imeandikwa kwa kijapani na kiengereza kwanza. Nimeitafsiri kwa kiswahili ili Waswahili wapate nafasi ya kuisoma. Haki ya picha, ramani na jedwali zote imehifadhiwa.

1. Utangulizi

1.1 Kusudio

Dhamira ya makala hii ni kuonyesha namna wakaazi wa Kilwa kisiwani, kusini mwa mwambao wa pwani Tanzania, wanavyotumia mikoko. Matumizi haya yanafuata njia mbili : ya kwanza, watu huenda kuchuma maliasili yanayopatikana katika mazingira haya ya kiasili (hapo tunaweza kutumia methali ya ghala) ; ya pili, mazingira haya, ingawa yanatumika kwa ajili ya kuendesha maisha, nayo hutumika kama shikizo ya shughuli nyingine za jumla. Hapo katika tini hii, tutagusia umuhimu wa mikoko katika jamii ya kisiwa hiki ambayo inategemea sana maliasili ya pwani kwa jumla, huku tukisisitiza kwamba maliasili haya yana nyanja na uchumi zenye kikomo.

Kilwa ulikuwa mji mkubwa zamani za kale wakati wa Ufalme wa masultani ambao uliwahi kutawala kisiwa hiki wakati wa enzi za katikati. Enzi hizo zilikuwa za biashara ya kidunia kwa kuwa Kilwa ilikuwa bandari kubwa iliyosifika katika ulimwengu. Katika ‘tariki za Kilwa’ ambayo ni tini mojawapo kuhusu historia ya kisiwa hiki, inasemekana kwamba Ufalme huu ulianzishwa na Sultani Ali bin Al-Hassan katikati ya karne 10 baada ya Mfalme huyu na jamaa zake kuhama walipokaa huko Shiraz, Uajemi. Msafiri maarufu sana kutoka Moroko aliyeitwa Ibn Battuta naye aliwahi kusafiri sana na kukitembelea kisiwa hiki cha Kilwa wakati wa karne 14. Katika maandishi yake anasema ‘Kilwa ni mji mojawapo uliokuwa mzuri sana katika miji yote ya dunia’. Majengo mengi ya enzi hizo yamebaki leo nayo ni magofu ambayo yameandikishwa katika orodha ya UNESCO ya ‘urithi wa dunia’. Tangu nyakati hizo hadi siku hizi tulizo nazo, Kilwa kimepunguza ukubwa wake kikawa kijiji kidogo kinachokisiwa kuwa na idadi ya watu 1000. Shughuli za watu za kujitegemea huambatana sana na mazingira ya pwani ikiwa ni pamoja na mikoko na miamba.

1. Mazingira ya visiwa vya Kilwa (© R.N.)

Kisiwa hiki kidogo kinakabiliwa na mabadiliko ya kijamii yakiwemo shinikizo za kiuchumi katika nyanja za maendeleo, pamoja na uhaba wa usimamiaji wa miundombinu katika mawasiliano. Licha ya shinikizo hizo, Kilwa kisiwani hukumbwa na matatizo yanayotokea katika kuthibitisha majengo ya zamani. Ukarabati wa majengo haya, uhifadhi wa mazingira ya pwani, uwezekano wa upatikanaji wa maligafi, kuongezeka kwa utalii na kadhalika ni miongoni mwa vipengele vinavyopaswa kuzingatiwa katika kutathmini mahusiano wa kijamii baina ya wakisiwani na mazingira yao, hasa mikoko. Makala hii inakusudia kuchanganua mahusiano hayo na kutathmini namna yanavyowiana kwa kutilia maaani kwamba uwiano huu utastahiki kusimamishwa katika enzi za mbele.

1.2 Mikoko Tanzania

Pwani ya kiswahili ina ukanda mrefu wa takriban kilometa 2000, kutoka kusini mwa Somalia hadi kaskazini mwa Msumbiji, zikiwemo kanda ndogo ndogo Malagasi na Ungazija. Mazingira haya ya pwani bado ni uwanja mzuri wa bioanuai uliopatwa na mikoko mingi yenye ikolojia imara sana Afrika. Katika matumizi yake mengi, mikoko huchangia sana katika upatikanaji wa miundo mbinu asilia kama vile ujenzi wa nyumba. Tangu zamani, miti inayopatikana kutoka mikoko ilisafirishwa nje kutoka eneo hili la Afrika hadi nchi za Uarabuni ambapo mali hii inakosekana. Biashara hii si ya kileo bali ni ya zamani sana. Ilichangia sana katika kuathiri mazingira haya asiliya hasa kwenye ukanda wa pwani wa Afrika mashariki. Kwa mfano kisiwa cha Pemba, kilicho mbali kidogo wa pwani wa Tanzania bara, ambacho zamani kilikuwa kinaitwa ‘kisiwa chenye miti’, kimeathirika kiasi kwamba maeneo mengi ya mikoko yaliyokuwepo sasa yamepotea.

Katika miaka 1990, nchi za Afrika zenye pwani zilifuatilia mikakato ya kudhibiti na kuhifadhi mazingira ya fukwe zao zenye mikoko. Misitu ya mikoko hapa Tanzania imehifadhiwa vizuri. Ripoti moja kutoka programu ya kimazingira kutoka shirika la Umoja wa Mataifa katika kuhifadhi mazingira (UNEP-WCMC) inasisitiza kwamba kati 1990 (1 096 km2) hadi 2000 (1081 km2) maeneo ya mikoko ya Tanzania yamebaki katika hali isiyokuwa na uharibifu. Kusini mwa nchi kunahesabika asilimia 65% ya mikoko yote ya Tanzania ikiwemo 730 km2 katika eneo la Rufiji na 1118 km2 katika eneo la Kilwa.


2. Mazingira ya pwani na maumbile yake Kilwa Kisiwani

Kilwa Kisiwani ni kisiwa kidogo chenye miamba mingi ambacho kipo kusini mwa Tanzania, mkoa wa Lindi, takriban km 300 kutoka Dar-es-Salaam kupitia barabara ambayo bado si nzuri. Kina zinguko ya km 23 na kinaukabili mdomo ya mito mitatu kwa upande wake wa bara. Vilevile kinazingukwa na bahari ya India ambayo inajumuisha sehemu mbili, nazo ni bahari ya karibu yenye kina kifupi kinachohifadhiwa na mikoko na bahari kuu vya maji vyenye matumbawe. Kisiwa hiki kina kijiji chake kidogo karibu na ufukwe wake. Wakaazi wake hutegemea sana mazingira yao ili kupata mahitaji yao kwa kushughulikia uvuvi, ukusanyaji wa vidudu wa pwani na kilimo.


                                    

Kisiwa hiki kina vigezo vyake vya kijeografia : latitudo yake ni 9°S. Pamoja na hayo, kipo katika eneo linalopatwa na misimu ya pepo za kudumu kama vile kusi na kaskazi. Kutokana na tabia yake ya kitropiki, Kilwa inapata maji ya mvua inayokadiria 1000 mm kwa mwaka. Usimbishaji huu unagawanyika katika misumu miwili ambayo wakaazi wa Kilwa hunufaika nayo wakati wa kifuku na vuli. Kutokana na hali hii ya kupatikana mvua ya kutosha, familia nyingi hupanda mimea ya aina mbalimbali ikiwemo mtama, muhogo, mahindi, mpunga, mbaazi, karanga, korosho na mingineyo. Ingekuwa jambo jepesi la kuweza kukidhi mahitaji yao endapo watu wangekuwa na vifaa vya kulimisha mashamba makubwa kushinda yale wanaopambana nayo siku hizi ambayo hayazidi eka moja. Ndiyo maana kilimo hiki duni hakizalishi mazao ya kuuzia bali ya kutengeneza chakula cha nyumbani. Bahari ndiyo sekta kuu inayochangia kupata pesa taslimu. Wavuvi hutumia vyombo vya mbao vya aina mbili : cha kwanza ni aina ndogo ya chombo kinachochongwa katika mkuku wa mti na kinachoitwa mtumbwi, cha pili ni aina nyingine kinachoundwa kwa mbao na kinachotumia tanga ya kilatini ili kusafiri.

3. Maeneo matatu ya kiikolojia

Mazingira ya pwani ya Kilwa kisiwani yanagawanyika katika sekta tatu ya kiikolojia (Jad.2) :

Ikosekta ya kwanza inasambaa kutoka kisiwa chenyewe hadi sekta ya bara. Inajumlisha mito, mifungu na maji ya mpito zinazoenea baina ya kisiwa na ufukwe wa bara unaokabili kisiwa. Hapo maji ya bahari haina kina kikubwa na mawimbi yake ni madogo sana. Sekta hii, ingawa ina mikondo ya hapa na pale kutokana na mabadiliko ya kiwango cha maji kwa jumla, inajihami kutoka pepo kali zinazovuma kutoka bahari kuu. Ikosekta hii ina mfumo ikolojia ya kipekee : matope na vifungu vya mwani vinapatikana ndani ya maji.

Ikosekta ya pili inahusiana na sehemu kubwa sana kwa upande wa bahari kuu. Hapo ndipo tunapokuta ukanda wa matumbawe ambao unakinga ufukwe wa kisiwa hiki. Sekta hii ina umuhimu wake kwa kuwa ina maji mengi kadiri tunavyokiuka ukanda huu wa matumbawe kuelekea baharini. Mawimbi makubwa, pepo kali za misimu ni miongoni mwa vipengele vya mfumo ikolojia wa sekta hii. Bioanuai yake inategemea sana mazingira haya yenye matumbawe na mchanga mwingi.


Ikosekta ya tatu inaingiliana na sekta hizi mbili tulizotaja kwani ipo katikati ya bahari kuu na mikondo ya ndani inayoakisi sekta ya kwanza. Maingiliano ya kiikolojia yanayopatikana katika sekta hii yanadhihirisha kwamba hapo ndipo mazingira ya mpito yenye kubadilishana spishi ya ndani na spishi ya nje ya mfumo ikolojia ya kisiwa hiki.

3. Iko-sekta za Kilwa Kisiwani (© R.N)


Tukizingatia jinsi wakaazi wa kisiwa hiki wanavyotumia ikosekta hizi katika shughuli zao za kila siku, tunagundua kwamba sekta ya kwanza ndiyo inayotumika sana kuliko nyingine. Si jambo la kushangaza ikiwa tunatilia maanani vipengele viwili ambavyo hupuuzwa sana katika uchambuzi mwingi ya kiikolojia navyo ni chanzo ya kijamii na historia ya eneo hili la mwambao la afrika mashariki.

4. Bahari ya ndani : mikoko na enzi ya Ufalme

4.1. Mabaki ya Ufalme wa Kilwa

Mabaki yaliyosalia kutoka enzi hii ya Ufalme wa zamani yanavutia sana kutokana na ukubwa wao. Mbali na magofu tuliyo nayo siku hizi ambayo yanaonekana wazi katika mandhari yenye vivutio vingi, historia hii ingali ina umuhimu wake katika maisha ya wakaazi kwa kuwa inachangia katika kukikuza kitambulisho cha kisiwa hiki kidini au kilugha hususan kwa siku hizi ambazo zimekumbwa na maingiliano mengi ya kikabila. Sura hii inalenga kumsaidia msomaji ambaye bado hajatembelea kisiwa hiki kupata picha halisi ya majengo hayo ya zamani ambayo siku hizi ni magofu. Magofu haya yamepewa nafasi kubwa katika matini au maandishi ya kitaalamu. Ijapokuwa yapo mengi, hapo tutafuatilia taaluma ya wanaaekolojia huku wakiainisha majengo yenye asili ya kiarabu na yale yenye asili ya kireno (jed.1) :

Ya kiarabu : zimehesabika misikiti sita, kasri au majumba makubwa tatu, makaburi manne ;

Ya kireno : ipo aina ya ngome ambayo inaitwa Gereza.

        


4.2 Mtawanyo wa magofu Kilwa Kisiwani 

Endapo tunachukua ramani ya kisiwa hiki, tunagundua kwamba magofu hayo yametawanyika katika maeneo matatu makubwa (fig.3) :
Kuzunguka au katika kijiji tunakuta : Msikiti Mkuu (1), Gereza (3), Makutani (4), Msikiti Mdogo (5), Msikiti wa Malindi (7), Msikiti wa Jangwani (9), Makaburi ya Malindi (13).

Nje ya kijiji au porini : Makaburi ya Shirazi (6), Makaburi ya Masheikh Arobaini (10), Makaburi ya Sake (12).

Kaskazini mwa mji, kwenye kilima kidogo kilichopo kilometa mbili kutoka kijiji : Husuni kubwa (2) na Husuni ndogo (11).

3. Mtawanyo wa magofu Kilwa Kisiwani

Katika majengo haya yote, mojawapo ni muhimu sana kwani linaashiria kwamba wakaazi wa kisiwa hiki zamani walikuwa hukaa karibu nalo kwa ajili ya kuswali, ni Msikiti mkuu. Gofu hili bila shaka lilikuwa na umuhimu wake hususan kwa watu wa enzi zile ambao wengi walikuwa na asili ya Uarabuni. Inadhihirisha kuwa kuanzia kujenga kwake (mnamo karne 13) hadi kudhoofika kwa himaya ya Kilwa (takriban karne 15) watu walikuwa huishi katika eneo hili ambalo nalo ni eneo la mikoko. Eneo hili la kaskazini/magharibi la kisiwa hiki linalokabili misitu ya koko mingi upande wa bara, pia ni pahala pazuri sana kwa kuishi kwani lina tabia ya ubaridi mwanana wakati wa kiangazi. Aidha, kwa sababu ya upepo mzuri wa kaskazi, limebahatika kutokumbwa na homa ya malaria kama ilivyo katika sehemu nyingine ya kisiwa hiki au katika vijiji vingine vya karibu karibu huku bara. Isitoshe, ni pahala penye visima vingi vyenye maji baridi mazuri. Jambo la kustaajabisha ni kwamba miji mingi ya visiwa vya kiswahili kama vile Pate, Lamu, Manda, Mombasa na Ibo (Msumbiji) huwa imejengwa kwa kufuata mtindo huu wa kukaa karibu na ufukwe wenye mikoko mingi upande wa magharibi kaskazini.

Hali kadhalika, licha ya faida ya kuwepo katika mazingira yenye vigezo hivi, msimamo wa mji uliwahi kuwasaidia wakaazi wake katika kujitetea kutoka maadui waliokuwa huja zamani kuwashambulia mara kwa mara. Vilevile, wakati maji yanapokupwa, bahari inabakisha madimbwi mengi na mafungu yenye manufaa kadhaa ya kisiasa. Bila shaka, boti kubwa zenye malengo mabaya zilikuwa zinahofia kutia nanga katika maeneo hayo yenye maji haba. Wakati wa ufalme, maskani kuu ya Mfalme ilikuwa karibu na misitu ya mikoko, si kwa ajili ya kuchuma maliasili hii peke yake kwa kuwa ni dhahiri kwamba mji huu wa zamani sana ulikuwa na mfumo wake wa utetezi wenye ufanisi wa kipekee ulioegemea mazingira hii maalum.

                                            

5. Misitu ya koko : matumizi yake ya mahususi na ya jumla

Inaonyesha kwamba kabila nane za mikoko zinapatikana Tanzania (Jad.2) ambazo zote zinaota na kustawi vyema katika kisiwa cha Kilwa. Maliasili ya bahari Kilwa imekua kwa kuegemea sana biaoanuai inayostawi katika mikoko. Hapo katika sura hii tunataka kuchambua matumizi ya misitu hii ya koko kwa kuonyesha kwamba watu hufuata vielelezo vya aina mbili :

5.1 Ruwaza ya kwanza : matumizi mahususi

Katika kielelezo hiki tunakuta kwamba misitu ya mikoko hutumika katika vipengele vyake vyote navyo vinajumuisha boriti, fito, mizizi, majani, mibegu, asali na vitu vinginevyo. Kutoka katika vitu hivi vyote ambavyo vinashughulikiwa, tunaweza kuainisha matumizi ya aina saba katika shughuli za wenyeji. Hapo tumegawanya maliasili hizi kutokana na dhima yao katika shughuli za kijamii :

Misitu ya koko ni chanzo kikubwa cha majengo : wenyeji huenda kukata boriti, fito, pau kwa ajili ya kujenga nyumba zao.

Misitu ya koko inachangia sana katika kupatikana kwa vifaa vya kuunda vyombo vya kusafiri baharini : dau, ngarawa, mtumbwi.

Baadhi ya vifaa vya kuvulia navyo vinapatikana katika misitu hii, kwa mfano fito za kusimamisha mitego ya samaki kama vile wando (au uzio).

Misitu hii vile vile inazalisha maliasili za kimaumbile ambazo hutumika katika pirika za kijamii kama vile kuni na makaa.

Misitu hii ni sehemu nyeti kwa kupatikana kwa utibabu wa kienyeji kama vile mibegu ya Xylocarpus granatum.

Wakati wa kiangazi ambacho ni kipindi cha ukame, wanyama wa kufuga kama vile mbuzi na kondoo hupenda kutembea tembea kando ya misitu hii ili kutafuta majani makavu.

Watoto hupenda kutengeneza vitu vidogo vidogo vya kucheza navyo kama vile pia au vidau vidogo kwa kutumia chuchu za Sonneratia alba, yaani tunda lake.

                             

5.1.1 Miundo ujenzi ya nyumba

Kufuatana na mapokeo ya kijadi katika ujenzi wa nyumba, watu wa Kilwa, almuradi mithili ya watu wengi kwenye mwambao wa Afrika mashariki, hutumia boriti kwa ajili ya kujenga kuta pamoja na dari za nyumba zao (jed.4). Boriti hizi (kutoka Rhiphora mucronata) zina manufaa mengi kwa kuwa zina aina ya rangi ya kimaumbile ndani ya patu zao ambayo inakuja kuongeza imara yao dhidi ya vidudu kama vile mchwa ambao kwa kawaida hula sana mbao. Kwa kuwa ni ngumu sana boriti hizi zimesifiwa sana na watu tangu enzi za zamani sana. La kudhibitisha kauli hii tunalikuta katika majengo ya zamani : mengi yamebaki katika hali nzuri kwa kutumia boriti hizi. Msafiri au mtalii hana budi kutembelea kasri ya Makutani kama atapendelea kujiaminisha kwa macho yake mwenyewe.

Kukata miti kunatakiwa kusajiliwa kwenye ofisi ya mikoko iliyopo Masoko ambayo ndiyo taasisi inayosimamia shughuli hizi. Ndio maofisa wa serikali wanaotoa vibali na ruhusa za kukata miti. Kusimamia kukata mikoko ni kazi muhimu kwani hatuna budi kukumbuka kwamba nyumba moja yenye vyumba vitatu au vinne inataka boriti zisizopungua 700.


Ipo aina mbalimbali ya miti ya koko kutokana na ukubwa wao (jed.3). Yote ina kazi yao kutokana na matumizi yao. Mfano pau, ambayo ni mti wenye diameta baina ya 3.8 hadi 7.5 cm, inatumika sana katika kutengeneza fremu ya viambaza ; boriti nazo zina kazi maalum katika kujenga dari ndani ya nyumba : hapo ni dhahiri kwamba ukubwa wa boriti, ambayo ina diameta kati ya 11.5 hadi 14 cm, unachangia kuhimili paa la nyumba. Msomaji lazima aelewe kwamba mtu mzima anaweza kukanyaga na kutembea juu ya dari bila hata kuiharibu. Boriti ndio mti uliokuwa unasifika sana zamani hadi ikafikia hatua ya kuukata kupindukia katika maeneo mengi ya Afrika mashariki. Huku Kilwa ndio mti uliosafirishwa sana nje mpaka Uarabuni ukawa ukakatwa sana mpaka leo. Ipo ripoti moja inayothibitisha kwamba misitu ya koko kwenye mwambao ya kiswahili imepungua sana kiasi cha kupoteza asilimia 50 ya ukubwa wake wa kiasili. Shughuli hizo za ukataji uliathiri sana misitu hii hasa kwenye maeneo ya kaskazi ya mwambao huu, yaani kwenye kanda za Kenya na Somalia. Kwa bahati nzuri, maeneo ya kusini kama vile yale yaliyopo kusini mwa Tanzania bado yapo mazima.

5.1.2 Vifaa vya kuunda vyombo

Vyombo vya bahari ambavyo kwa kweli ni mbinu muhimu sana katika maisha ya watu wa pwani, huundwa kwa kutumia mbao ya aina nyingi ikiwemo mbao ya koko. Kilwa vyombo hivi ni aina saba :

Mtumbwi.

Ngalawa ambayo haipo Kilwa kisiwani kwa siku hizi ; inaonekana Songomnara kusini kidogo, 5 km kutoka Kisiwani.

Dingi (kutoka kieng. dinghy) ambayo ni chombo kidogo sana hususan kinachotumika usiku kwa ajili ya kuvulia samaki kwa kutumia taa. Ingawa haipo katika visiwa vya Kilwa, inaonekana Kilwa Kivinje.

Mbare ambayo ni aina ya chombo kisichokuwa na mkuku chini yake (yaani tako lake halichongeki likawa halina ncha ndani ya maji).

Dau ambayo haina mkuku ni aina ya chombo cha mbao zilizochongwa.

Mashua inafanana na dau ila inayo mkuku mdogo na hutumia tanga.

Boti pia inafanana na mashua ila haina tezi : hutumia mashine. 

                                    

Katika vyombo hivi vyote, mbare, dau, mashua na pengine boti huundwa kwa kutumia mbao za koko katika baadhi ya vipengele vyao, navyo hasa ni mkuku, mataruma, mlingoti, foromali, tezi, n.k. Hapo inabidi tukumbuke kwamba kuundwa kwa chombo kunategemea sana mazao au nishati zinazozalishwa na miti hii ya koko (jed.4). Kila aina ya spishi ya koko ina faida na utumizi vyake. Kwa mfano, msinzi (Bruguiera gymnorrhiza) inajulikana sana kwa kuwa ni mti mgumu sana katika yote. Kutokana na hali hii, ndio unaotumika katika kutengeneza sehemu zile za vyombo zinazohitajika uthabiti na vifaa imara kama vile mikuku, milingoti na mataruma. Kwa upande mwingine, mkandaa dume (Lumnitzera racemosa) na mkungu (Heritiera littroralis) huwa ni miti ambayo haisaidii sana katika kuunda vyombo kwa sababu ya udhaifu wao katika kazi hii. Miongoni mwa wenyeji, mafundi wa vyombo pamoja na wavuvi wengi huelewa vizuri manufaa na ila za miti hii yote.

5.2 Ruwaza ya pili : matumizi ya mikoko kwa jumla

Ruwaza hii inaambatana na zoezi nyingine ya kienyeji katika matumizi ya mazingira ya koko haswa katika misitu ya ndani yaani katika ikosekta ya 3 ambayo, hapo tunatilia mkazo, ina maji kidogo yasiyokuwa na misukosuko mingi. Aidha, sekta hii ina spishi anuai nyingi. Katika zoezi kuu la kiuchumi katika mazingira kama haya, wenyeji hupendelea kutumia misitu kama ifuatayo :

Misitu ya koko ina nafasi kubwa ya kupatikana kwa nyanja za uvuvi.

Pia ina sehemu nyingi kama vile mito ya kuwatumikia wavuvi kama njia ya kusafiri kwa chombo.

Eneo hili kubwa lina nafasi ya kuzalisha chumvi haswa kwenye ukanda uliopo kati ya misitu ya koko na nchi kavu. Ndipo hapo maji ya bahari yanapokupwa yanaachia masalio ya chumvi inayopatikana wakati wa uvukizaji.

Misitu hii inawapa nyuki nafasi ya kwenda kuranda ndani yake ili kutafuta unga wa asali unaopatikana katika maua ya miti hii, nayo ina faida kubwa kwa jamii kwani inachangia kuinua kipato cha wakaazi wa kisiwa hiki.

La mwisho, tusisahau kwamba wakati misitu hii haina faida ya moja kwa moja kwa watu binafsi, ina thamani kubwa sana kwa kuongeza kingo za fukwe zinazoathirika kutokana na mmomonyoko wa ufukwe na mwinuko wa kiwango cha bahari.

Mazingira haya yana vivutio vingi vya kitalii. Zanzibar matembezi ya wageni katika mazingira haya tayari hufanyika na huleta faida kwa wenyeji. Ili mradi kutoa maelezo zaidi kuhusu matumizi ya misitu hii kama nyanja za kuvulia samaki pamoja na sehemu ya kusafiri, tutaongeza ufafanuzi zaidi katika sura hii ifuatayo.

5.2.1 Nyanja ya kuvulia samaki

Jedwali ya 4 inaonyesha utawanyikaji wa nyanja za kuvulia katika mizunguko ya Kilwa kisiwani. Katika nyanja 66 kwa jumla ambazo zinatumika mara kwa mara katika shughuli za kuvua, sehemu 30 (yaani 45%) zipo katika ikosekta 1 (jed.6). Ina maana kwamba bahari hii ya ndani ina spishi wengi wakiwemo samaki wastani na wadogo, kamba wadogo, majongoo na mazao ya koko. Mathalan, misitu hii ya koko ambayo iko ndani ya mfumo ikolojia muhimu sana ni sehemu ya mazalio nyeti kwa viumbe vyote vya bahari. Uvuvi unaweza ukafaidi katika mazingira kama haya.

Mitego na zana za kuvulia ni za aina nyingi sana. Huku Kilwa kisiwani aina ya zana zisizopungua 41 zinatumika. Katika zana hizi, aina ya mitego 23 (yaani 56%) zinatumika katika mazingira yenye mikoko, ikiwemo bahari ya ndani (jed.5). Zana hizi zinafaa sana katika mazingira haya. Hapo ndipo tuzingatie kwamba zana ya aina yoyote (iwe ya kijadi au ya kisayansi au kiteknolojia) haina ufanisi wowote ikiwa haitegemewi na maarifa na mitizamo asiliya. Kuambatana kwa zana, ufundi na maarifa kunaleta ufanisi mzuri ambao vile vile utakuja kuheshimu hali jinsi mazingira ilivyojengeka kiasili. Kwenye kisiwa cha Kilwa, wavuvi wengi bado huelewa vizuri kila aina ya nduni ya kimaumbile iliyopo katika mazingira husika kama vile pima ya maji, uoto uliopo ndani ya maji, spishi za samaki zinazopatikana, kiwango cha maji, n.k. Kwenye maji haba na katika misitu ya koko isiyopatwa na misukosuko ya maji, wavuvi huweza kwenda kuvua kwa miguu au kwa kutumia chombo kidogo. Aidha, ndipo katika sehemu kama hizi wavuvi wanapokwenda sanjari kushughulikia kuokota kombe na majongoo, kuvua kwa kutumia mitego ya kusimamisha kama vile wando, au vingenevyo kwa kuzimisha madema. Tabia ya kimaumbile iliyopo katika sekta hii ya bahari ya ndani inakubali vizuri shughuli kama hizi za uvuvi ambazo hazina gharama kubwa mithili ya zile zinazosababishwa na matumizi ya vyombo na nyavu. Inaelekea kwamba sekta hii ya shughuli za kiuchumi inatumika tangu zamani sana.

5.2.2 Njia ya kusafiri

Katika eneo la Kilwa, misitu ya koko ina dhima nyingine kuu. Kwa kuwa ni ikosekta yenye hali tulivu na maji shwari, wenyeji hupitisha vyombo vyao katika misitu hii yenye mito na njia ya maji nyingi ili kuunganisha vijiji vidogo ambavyo si aghalabu kupatwa kwa njia nyingine hususan za bahari kuu. Kwa mfano, wakati maji yamejaa, vyombo vikubwa kama vile dau, mashua au boti vinashinda kuunganisha bandari ya Kilwa Masoko na bandari ya Pande Mtandura wakati vyombo vingine vidogo kama vile mitumbwi na mbare hupitishwa ndani ya misitu ya koko, huku vikisheheniwa na bidhaa, vifaa vya kienyeji au mazao ya baharini ambavyo vinasafirishwa hadi sehemu mbali mbali za ukanda huu wa pwani.

                                                                                       


Mawasiliano haya yanatoa picha halisi ya mtandao ya kienyeji ambao unaonyesha wazi kwamba watu wa pwani hii ya Wilaya ya Kilwa huwasiliana vizuri kijamii. Kwa mfano, katika wanawake 101 ambao wameolewa Kisiwani, karibu 63% wanatoka nje ya kisiwa hiki wakiwemo 35% kutoka Pande, 5% kutoka Mavuji, 3% kutoka Masoko na eneo la Mgongo, 3% kutoka Songomnara. Ni dhahiri kwamba uhusiano wa kiukoo umeenea sana katika eneo hili la Kilwa kufuatana na utaratibu wa kwenda kuposa katika vijiji vingine au maeneo mengine. Uhusiano huu wa kijamaa umejengeka tangu zamani nao hunufaika sana mawasiliano haya ya bahari. Aidha, vijiji vyote vya eneo la Kilwa, haswa kwenye mwambao, vinawasiliana vizuri wakati wa matukio ya kidini kama vile ziara ya Pande, licha na mawasiliano ya kiurafiki au kibiashara.


5.3. Uwiano katika matumizi ya misitu ya koko

Uhusiano uliopo Kilwa baina ya matumizi ya hapa na pale na matumizi ya jumla umewiana vizuri. Maangalizi mengi katika dunia huonyesha kwamba kukatwa kwa mikoko mingi huathiri mfumo wa kiikolojia lakini pia kutokatwa kunaleta matatizo katika maisha ya watu wenye kutegemea misitu hii ya koko. Kwa kuwa uwiano unaopaswa kupatikana hapa unakuwa si rahisi kusimamishwa, hatuna budi kubaini kwamba misitu ya Kilwa imebahatika sana kutoathiriwa na watumiaji wake kutokana na shughuli zao za kila siku. Pengine hali hii ina sababu ya kipekee ikiwemo idadi ndogo ya watu wanaoishi kusini mwa Tanzania. La kuzingatia katika eneo la Kilwa ni kwamba ndipo idadi ya watu wanaoishi kwa kila km2 ipo ndogo zaidi kuliko idadi zote nchini (kuna watu 12 kwa kila kilomita ya mraba, kwa mujibu ya censa ya 2002). Aidha, hatuna budi kukumbuka kwamba hali ya uchumi kwa jumla katika eneo la Kilwa haijapewa nafasi ya kuweza kuinua maisha ya watu kama inavyotakikana. Shinikizo hizi zinaelekea kuwa ni vikwazo vya kukanusha maendeleo ya kisasa, lakini vile vile zina nafuu katika kupunguza presha ya kijamii juu ya maliasili ya Kilwa.

Hivi karibuni, maendeleo katika sekta ya utalii na miundombinu yamepewa kipaumbele. Unesco wa Tanzania, pamoja na serikali ya Ufaransa na ya Japani vimejitahidi sana katika kusaidia ukarabati wa magofu ya zamani ya Kilwa. Barabara kuu kutoka Dar hadi Kilwa inakaribia kumalizika ingawa ujenzi huu umeanzishwa mwaka 2000. Daraja ya Mkapa imetengenezwa ikakamilika mwaka 2003. Siku hizi uchimbaji wa mafuta unaendelea kufanyika karibu na Kisiwa cha Kilwa. Tafiti nyingine pamoja na mazoezi mengine kuhusu mwambao huu wa Tanzania vinatakiwa kuendekezwa ili wenyeji wa eneo hili la Tanzania wasije wakaharibikiwa katika uhusiano uliopo baina ya mazingira ya kimaumbile na mazingira ya kibinadamu. Changamoto kubwa inatukabili hapo : kuhifadhi maarifa asiliya ya binadamu pamoja na mazingira ya bahari.


                                  
           
6. Hitimisho : umuhimu wa misitu ya koko katika shughuli za binadamu tangu zamani hadi leo

Tumeona kwamba Kilwa ziko aina mbili ya bahari : bahari ya ndani yenye mikoko na bahari kuu yenye miamba ya matumbawe. Ikolojia ya pwani inagawanyika katika ikosekta tatu nazo zinakubali vizuri shughuli za kibinadamu. Katika ikosekta zote, ndiyo ile ya kwanza inayoshughulikiwa sana kuliko nyingine. Aidha, uchambuzi linganifu unathibitisha kwamba kijiji cha leo na maskani ya kifalme ya zamani vimetumia sehemu ile ile ya kuweka majengo yao, yaani sehemu iliyopo karibu na misitu ya mikoko ya bahari ya ndani. Uvuvi, safari na biashara ya hapa na pale ndizo shughuli zinazofaa kufanyika katika mazingira kama haya ambayo pia ni pahala safi pa kustahimilisha jamii ya eneo hili la Tanzania. Isitoshe, tumeona kwamba misitu hii inazalisha maliasili yenye faida nyingi katika jamii hii kama vile vifaa vya ujenzi, vyombo, zana za kuvulia au kuni na makaa. Kwa hivyo, mazingira haya kwa jumla ni muhimu sana kwa watu wanaoishi kwenye mwambao huu ilhali upatikanaji wa miti nchi kavu utakuja kufika kikomo chake endapo idadi ya watu itakuja kuongezeka.

Bahari ya ndani inatarazaki sehemu nyingi zenye samaki wengi kwa kuwa mazingira haya ni mazalio ya spishi nyingi. Uvuvi mdogo wa mapokeo kama vile kuvua sanjari kwa miguu au katika vyombo vidogo unafaa sana kutumika katika eneo kama hili. Kusema kwamba uvuvi huu haufai kwa sababu ni wa zamani sana au umepitwa na wakati si kauli inayokubalika. Licha ya kwamba inadharau mapokeo yaliyorithishwa na vizazi viliopitwa, rai hii haina msingi. Wa kukanusha rai hili, utafiti wetu unadhibitisha kwamba uvuvi huu una faida mbili : kwanza, hauna madhara wala athari katika mazingira ambayo ni mepesi sana kuathirika (vinginevyo, misitu ya mikoko ingetoweka tangu zamani); pili, mitego na zana hizi za mapokeo zinatega samaki wa aina nyingi, hali inayothibitisha kuwa uvuvi huu una ufanisi wa kukimu mahitaji ya watu bila hata kuharibu maliasili. Zaidi ya 50% ya nyanja za kuvulia zipo katika ikosekta hii ya bahari ya ndani ambazo zinakubali mbinu na zana hizi za kuvulia. Kwa kifupi, misitu ya mikoko ni kiini na himili ya shughuli nyingi za Kilwa.

Bahari ya ndani si kwa ajili ya shughuli hizi za kiuchumi pekee kwani inakubali njia nyingi ya misafara. Katika njia hizi zilizopo siku hizi, nyingi ni za ndani kwa ndani. Ni dhahiri kwamba mahusiano mengi ya kijamii yanaegemea mitandao hii ya mawasiliano. Kwa kuwa jamii imejengeka juu ya mahusiano ya kusaidiana na kubadilishana mazao na habari ya aina mbali mbali kwa kupitia njia hizi za kibahari, hatuna haja ya dhana ya kinadharia ili kukisi kwamba utamaduni huu mkuu wa Kilwa unatoka zamani sana hadi Ufalme wa enzi za katikati.

Maliasili ya misitu ya koko ina faida nyingi kwa watu wa Kilwa lakini tusisahau kwamba pahala pa kuishi pamoja na maliasili vinapungua. Katika visiwa vya Kilwa, mithili ya pahala pengine duniani, viumbe pamoja na vidudu vyenye uhai havidumu milele (katika spishi ambao tayari wameshatoweka hatuna budi kutaja nguva). Lakini kwa sababu ya misitu ya koko tunaweza kubaini kwamba tangu zamani sana Kilwa pamekuwa pahala pa kustawisha jamii, tokea Ufalme hadi leo. Ili kukuza maendeleo endelevu katika miaka ya mbele, ni jukumu letu kuhakikisha kwamba maliasili ya misitu hii itakuja kutumika kwa kuepushana na presha ya kibinadamu ambayo huenda itaongeza utumiaji wa maliasili haya yenye ikolojia muhimu sana.


La ziada :


Jed. 1. Aina ya magofu na asili zao

Asili
Tabia
Jina
Karne
Pahala

Uarabu / UajemiMisikiti
Msikiti mkubwa
Husuni ndogo
Msikiti mdogo
Jangwani Msikiti
Malindi Msikiti
Mvinje Msikiti
11BK
17-14BK
15BK
15BK
15BK
15BK
1
11
5
9
7
17
Kasri
Jumba
Husuni kubwa
Great House
Makutani Palace
17-14BK
14-15BK
15BK
2
8
4

Makaburi
Makaburi ya Shizaji
Makaburi ya Malindi
Mashehe arubaini
Sake
16BK
18BK
18BK
?
6
13
10
12
Ureno
Gereza
Gereza
16BK
3
Jed. 2 Aina ya koko Kilwa

Na.
Spishi
Kabila
Kiswahili
1
Rhizophora mucronata Lam.
Rhizophoraceae
mkoko
2
Bruguiera gymnorrhiza (L.) Lam.
Rhizophoraceae
msinzi
3
Ceriops tagal (Parr) C.B.Robinson
Rhizophoraceae
mkandaa
4
Avicennia marina (Forsks.) Vierh.
Verbenaceae
mchu
5
Heritiera littoralis Dryand.
Sterculiaceae
mkungu
6
Lumnitzera racemosa Willld.
Combretaceae
mkandaa dume
7
Sonneratia alba Sm.
Sonneratiaceae
mpira / mliyana
8
Xylocarpus granatum Koenig.
Meliaceae
mkomafi


 Jed. 3 Miti ya koko na ukubwa (dayameta) wao


  
Kiswahili
Dayameta (cm)
Nguzo kubwa
16.520
Nguzo
1416.5
Boriti
11.514
Mazio
7.511.5
Pau
3.87.5
Fito
chini ya 3.Jed. 4. Matumizi ya miti ya koko katika kuunda vyombo, kutegemea na uthabiti wao

Kiswahili
Jina la kisayansi
Uthabiti
Matumizi
Msinzi
Bruguiera gymnorrhiza (L.) Lam.
+++
mkuku, foromali, ma-
taruma
Mkoko
Rhizophora mucronata Lam.
++
mataruma, mlingo-
ti, boriti
Mkandaa
Ceriops tagal (Parr) C.B.Robinson
++
mataruma, mlingoti
Mpira
Sonneratia alba Sm.
+
mlingoti, mataruma, foromali, mkuku
Mkomafi
Xylocarpus granatum Koenig.
mataruma
Mchu
Avicennia marina (Forsks.) Vierh.
mataruma
Mkandaa dume
Lumnitzera racemosa Willld.
--
hamna
Mkungu
Heritiera littoralis Dryand.
--
hamna

 Jed. 5. Aina ya uvuvi na mbinu zinazotumika katika mazingira ya koko


Vifaa
Kiswahili
Kiengereza
Bahari*
B
C
D
EWavu

Misadaka
GillnetNyavu za kupigia
Gillnet (pressure with stick )
Juya
Seine net (large)Nyavu za kavogo
Seine net (small or middle size)
Nyavu za kokoro
Ring net
Kiniya
Cast netMsembwe
Ring net (pressure)
Nyavu za tandiyo
Scoop net

Mshipi

Mshipi
Handing fishing

Urimasi
Handing from coastMatozi
Long line (small)Kocho
Angling fixed to a pole
Mbinu

Wando wa miti
Fish fence (wood)
Wando wa nyavu
Fish fence (wood and net)
Dufu
Fish fence (wood and canoe)
Uriro
Fish fence (coconuts fiber)
Dema ya kutosa
Fish basket (sinker)Dema ya kufinga
Fish basket (fixed at coast)


Dema ya kugongea
Fish basket (long line)Kuzamia Jongoo
Sea cucumber dive
Kombe
Shellfish gatheringUgonyo
Fish pot
Kaa
Mangrove crab
*dondo : A=bahari ya ndani, B=misitu ya koko, C=bahari ya katikati, D=matumbawe,                         E=bahari kuu

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni