28/09/2015

Nimetafsiri Antigone, mchezo wa Jean Anouilh
Muhtasari wa mkasa wa Edipode na Antigone

Zamani ya kale, alikuwepo Mfalme mmoja wa Ugiriki wa Wayunani ambaye alikuwa anaitwa Laio, naye alikuwa akiongoza mji mkuu wa Thebe. Alioa Jokasta wakazaa Edipode. Kabla ya kuzaliwa kwa Edipode, maaguzi yaliyotolewa na Miungu wa Delfia yalitabiri maafa ya kuleta kifo cha Laio. Na Edipode ndiye ambaye angekuwa mwuaji kabla ya kumwoa mama yake Jokasta. Edipode alipozaliwa, Laio aliamua kumtupulia mbali katika milima ya Kitero ili kuepuka utabiri huo mbaya. Kutupwa tu, mara Edipode aliokotwa na Mfalme Polibo aliyemlea kwa kumtunza vizuri huko alikoishi katika mji wa Korintho. Miaka kadhaa ilipita ndipo Edipode alipopata kugundua maaguzi ya Delfia akafanya hofu kubwa asije akamwua kikweli baba yake Polibo akaamua kuwakimbia wale aliowafikiria ni jamaa zake. Kumbe alikimbilia Thebe kuelekea maajaliwa yake. Njiani katika ukimbizi huo alipishana na msafiri ambaye aligombana naye. Katika ugomvi huo, Edipode aliwahi kumwua msafiri huyo wala hakujua kwamba naye alikuwa ni baba yake mzazi. Alipofika Thebe, aliukuta mji huo umekumbwa na balaa ya njaa huku ukiwa umeonewa na aina ya Zimwi ya kike aliyetisha kila mja asiyeweza kutambulisha kitandawili alichomtegea. Mtu kushindwa kujibu humezwa. Edipode kwa ujasiri wake aliwahi kutambulisha kitandawili hicho na kumwua Zimwi huyo. Kisa hicho kilimwongoza katika mji wa Thebe alikopata kupongezwa na wananchi kisha akajaaliwa kuoa Malkia wa mji, yaani Jokasta aliyekuwa ni mama yake. Edipode na Jokasta walipata watoto wanne, wawili wa kiume ambao ni Eteokile na Polinisi, na wawili wa kike ambao ni Antigone na Ismene. Ndipo Edipode alipoambiwa ukweli kuhusu mkasa huo huku akikomeshwa na mwaguzi kipofu Tiresia. Edipode kwa kutambua kile kilichomkusa akajipofusha na Jokasta alijiua. Kisha aliondoka akaukimbia mji wa Thebe huku akifuatana na binti yake Antigone. Nao watoto wake wa kiume waliobaki Thebe ndio waliotawala mji kwa zamu, kila mmoja akiwa anachukua madaraka kwa awamu ya mwaka moja. Ikawa baada ya mwaka moja, Eteokile akang’ang’ania zamu yake akakataa kuondoka katika madaraka ikawa vita ya mwenyewe kwa mwenyewe. Polinisi akafukuzwa akajisalimisha katika jimbo la Argo ambako aliwahi kuchangamana wakuu wa miji sita ili warudi pamoja kupindua serikali ya Eteokile. Ndugu hawa wawili walipigana mjini kwa Thebe hadi Kreoni, ndugu yake Jokasta, alipoingilia kati akachukua kiti cha mfalme. Katika vita hii, Eteokile na Polinisi walikufa. Eteokile pekee ndiye aliyestahikia maombolezo adhimu wakati maiti wa Polinisi alitupiliwa mbali bila ya kuzikwa akatafunwe na wanyama wa porini. Adhabu hiyo ilitolewa na Kreoni. Aidha Kreoni ndiye aliyepitisha uamuzi wa kupiga marufuku mazishi ya Polinisi na kutoa adhabu ya kifo kwa yeyote atakayekiuka utaratibu huo. Ina maana ya kwamba Kreoni alivunja sheria za kidini ambazo zilisimikwa katika jadi zilizokuwa zikizingatia utakatifu wa mauti. Kukufuru Miungu katika jamii ya Wagiriki ilikuwa miongoni mwa vitendo vya kutia unajisi mkubwa katika utaratibu wa jamii. Iliaminika kwamba nafsi ya Polinisi ndiyo ambayo ingetapatapa ovyo duniani pasipo na nafasi hiyo ya kujiliwaza katika dunia ya waliokufa. Antigone na Ismene walipopata taarifa hiyo wakafadhaika ikawa Antigone alijitolea mwenyewe kumsaidia Polinisi apate kuzikwa kufuatana na sheria ya kidini. Hapo ndipo mchezo huo wa Antigone unapoanza. 

Masomo mengine :

Kwenye blogu hii HAPA
Mfalme Edipode, tafsiri ya Samuel S. Mushi, Oxford University Press, Eastern Africa, 1971.
Mfalme Edipode, mwongozo mtimilifu, James M. Nderitu, Dotline Graphic, Nairobi, 2009.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni