19/10/2015

Hebu nani kabildi Kilwa sivilizeshen ? Golo, Ponjoro, Mlami au Mmanga ?


Katika ujirani wangu ninaye mwanablogu mwenzangu ambaye hivi karibuni amechapa makala kuhusu Kilwa iliyonitamia sana. Kwa kuwa mimi niliishi muda mrefu sana huko Kilwa — nikapiga hodi kwa mwenzangu nikaomba kusoma makala yake inayoitwa « Who built Kilwa's swahili civilization - Arabs, Africans or Arab-africans/African-arabs ? » (msomaji tafadhali usikose kumtembelea mwenzangu HAPO). Makala hiyo imenigusa kwa kuzungumzia hoja ambayo mimi ilinichekesha sana. Hoja yenyewe inahusiana na asili ya utamaduni wa kiswahili huko Kilwa, swala ambalo linataka mtu awe gwiji katika kupiga ramli au kutumia falaki — sijui kama mbuzi hapo amechinjwa au kama ruguza zimesomwa kwa kutumia mawano — yaani vijiti vya kutabiri yasiyotabirika — lakini mimi nikavutiwa na makala hiyo kwa sababu hiyo hiyo. Wengine wangalisema kwamba swala hilo linakufuru Mungu.

Basi msomaji nawe pengine utacheka pia. Kwanza tuzingatie kwamba mstaarabu wa blogu hiyo ametumia lugha ya kikoloni, pengine kwa sababu alijua wazi kwamba lugha hiyo ina uwezo wa kunasa waliokuwemo na wasiokuwemo. Ndiyo, mtego wa panya. Kumbe windo aliowapata ni watu wakubwa sana, yaani maprofesa wa ngazi ya juu sana, hata nimeshangaa mimi kuona kwamba wamekubali kushuka ngazi hiyo ili kuongea na watu wa « kawaida »… ambao hawajui kizungu. Hawa ndio waliokuwemo. Mfano Prof Chami ambaye ni bingwa sana katika sayansi ya akiolojia. Namkumbuka sana Prof Chami wakati tulipofuatana Kilwa Kisiwani katika mradi huo ulioletwa na Ubalozi wa Ufaransa… Siku ile mashua yetu ilipopwelewa Fundi Hussein huko Kisiwani, bwana huyo mara alishuka kwenda kugubuga ndani ya tope ya maji haba, kisha akakoroga ndani ya tope, akapata sijui aina ya kigae fulani akakichambua kisha akasema : « hicho kigae jamaani, si mnakiona ? Afrika hicho ! Ndiyo Afrika, kigae hicho ni cha zamani sana ! Karne 13, ndiyo, kabla ya Waarabu walipokuja ! ». Nami niko na jamaa zangu wa Kilwa kwenye maskani ya mzee Sharifu, tumeotama tunasubiri bwana mkubwa huko tumeachama. Basi siku ya pili yake, tayari bwana huyo kakurupuka jii, hatumwoni ng’o, keshapata jawabu la swala la asili ya Kilwa ! Kilwa ni mji wa Afrika. Alikuwa hodari sana bwana huyo, jinsi alivyochapa kazi chapu chapu si mchezo. Mimi miaka miwili baada ya tukio hilo, bado nipo Kisiwani. Ndiyo maana katika makala hii ya blogu ya Udadisi, bwana huyo hana maneno mengi.

Katika waliokuwemo tunamkuta pia bwana mwingine mkubwa sana. Nadhani kwamba katika utaalamu hakui tena. Mheshimiwa huyo anaitwa bwana Abdul Sheriff. Huyo bwana kasimama jadidi hapo jinsi hoja yake kidogo inavyosigana na bui yangu Chami na ile ya mwanablogu mwenzangu aliyedare kusema kwamba eti waarabu wapo. Yeye mheshimiwa mkwasi anatafuta kugonga pointi fulani kwa kukosoa itikadi ya mkoloni (na ile ya Udadisi ?). Mkoloni ati anaamini sana mambo ya ugozi. Ndo maana wakati wa ukoloni mtu mwovu huyo alipendekeza kuainisha jamii ya kiswahili katika vikundi mbali mbali, nao ni wahindi, wazungu, waarabu na waswahili ambao, kwa mujibu wa Prof Sheriff, hawakuwepo. Kwa hivyo kosa tunalofanya hapo ni kasumba hiyo inayoturejesha nyuma wakati tunapambana na swala hilo la asili ya waswahili. Ishu si ugozi bali ni matabaka ya kijamii katika historia. Kwa kifupi, tusiangalie sura ya mtu bali hadhi yake au wadhifa wake katika jamii. Si uso wake au rangi ya ngozi bali ndara au kubadhi zake.

Katika wasiokuwemo tunakuta waatalamu wengine wenye hoja mbali mbali. Wa kwanza anasema kwamba mswahili ni mtu chotara tu, yaani suriama au afukasti. Naye ni mzungu, kanaitwa Deborah Bryceson, kama sijakosea. Mwingine hapo amenichekesha sana kwa kuwa alionyesha kwanza kwamba atatumia lugha ya kikoloni kama wenzake lakini mara lugha hiyo ikamshinda. Sijui kama ngeli hapo haikumpanda au kimombo hicho hakikukorogeka barabara au pengine ametanabahi kwamba kikoloni hicho hakifai kabisa kutumika katika mjadala huo unaohusiana na watu halisi — si watu wangali wanaishi Kilwa, ambao wanaongea kiswahili (hawajasomeshwa kizungu mboni ?) ? Ukweli ni kwamba bwana huyo pekee ndiye aliyeleta hoja ya kupata kitu kizuri, kwa kusisitiza yale niliyokwisha andika katika blogu yangu, ya kwamba mwafrika alishindwa kufuatisha mifano ya ujenzi ulioletwa na waarabu !

« That such great structures were something in part or wholly erected by 'visitors' I take for granted; but more to is why didnt 'we' emulate or learn such great arts/sciences? Tumeweza kwa mfano kuiga (sorry i mean kufuata) such complex ustaarabu as their religion, hadi makanzu yao, vibaraghashia hata bakora nk, lakini kwanini ujenzi huu ulitushinda kabisa ? Je walituficha ? It appears to me this continues today - Tunajifunza ufisadi na upuuzi wote wa kimagharibi, lakini tumeshindwa sana kujifunza uzalendo na maono ya mbali kwa maslahi ya taifa kama walivyo wamagharibi hawa. Kunani hapaaaaa BONGO!!!? » Adam Lingson.


Huyo bwana mimi namsifu sana — kwa kuwa anaonekana si mtaalamu — kwa kuwa ametumia macho yake tu kabla ya kutumia upuuzi wa kimaghiribi, ikiwemo nadharia ya kimarxisti au lugha ya kizungu ambazo hazina maana yoyote katika kuelewa asili ya binadamu katika kanda hiyo ya dunia !! Mtalaamu yupo katika dhahanio ya mambo tu, ni mtu ambaye huwa amejichunga na dunia ya mashiko, hajui kulinganua maada na dhana. Anashindwa kutofautisha shubiri na shera, kwinini na kashata, shemali na kuvuli, mtu na utu, dume na jike. Hekima na busara zimemkimbia. Ukimwambia tabianchi ni mchakato ambao umekithiri siku hizi, atakwambia kwamba hilo si ishu kwa sababu limeletwa na wazungu ambao wanataka kukandamiza nchi za Afrika zisije kujiendeleza tu. Ukimwonyesha mwezi, atakwambia huo si mwezi bali ni kivuli cha jua. Na hali kadhalika. Mimi hapo nawapenda sana kwa kuwa dunia yetu ni siriasi kabisa, nao ndio watu wacheshi sana ambao hawana habari kwamba wanachekesha. Waama kujitambua si rahisi. Kwa hakika akili nyingi huondoa maarifa !Hakuna maoni:

Chapisha Maoni