04/10/2015

Fasihi, maadili na siasa


Hivi karibuni nimesoma riwaya ya Ken Walibora inayoitwa Siku njema. Kitabu hiko ni kizuri sana ingawa — kwa sababu nimezoeleka kusoma riwaya za kila aina kutoka dunia nzima — sijavutiwa sana na jinsi mwandishi anavyopambana na swala la « mwafaka ». Sijui kwa nini waandishi takriban wote katika fasihi ya kiswahili — kwa kuwa naweza kusema kwamba nimesoma asimilia kubwa ya vitabu vya fasihi katika lugha hiyo — hupenda kuwa « safi » au kuonyesha kwamba hupenda sana « maadili ». Kila nikisoma kitabu cha fasihi katika lugha hiyo, najiuliza kwa nini wahusika hawawakilishi — au hawaonyeshi dalili ya kuakisi — yale ambayo yanatukumba katika maisha yetu ambayo kwa kifupi yapo katika nususi ya mambo. Kila siku, katika jamii yoyote duniani — Tanzania na Kenya nako pia — watu hutukanana, hurushana matusi, hupeana tombovu, hubonga lugha ya mitaani na hupendelea kutunga maneno machafu kuliko mashairi mazuri. Na sidhani kwamba nitakosea kusema kwamba mashairi siku hizi yamekuwa tunu kabisa. Na mifano mingi tunayo kila siku katika sekta ya siasa, sina haja ya kutaja ile ninayoifikiria, kwa kuwa msomaji bila shaka hupenda maadili (kuliko fasihi halisi), hivyo hapo nitapita na zangu.


Sio kwamba mimi, nikiwa miongoni mwa wasomaji wa vitabu hivi, nimeraghbika au nimechukia kila nikikutana na matusi au kisa cha ngono katika riwaya, ila sipendi mwandishi ajipendekeze kwa kunishawishi mimi msomaji nikubali hali hiyo na taswira ambayo bila shaka atakuwa nayo yeye peke yake. Nikitaka kusoma au kusikia hotuba yenye maadili ndani yake, basi nitakwenda kanisani au katika pahala popote pa ibada, hapo ndipo nitakapopata kutakisisha nafsi yangu. Nikitaka kusikia maneno ya kunihimiza nifanye hivi au vile, basi nitajiunga na chama fulani cha siasa. Lakini sitasoma riwaya kwa kuwa riwaya ni tungo ambayo aghalabu — na hapo natumaini iwepo hivyo — hutungwa kwa ajili ya wasomaji huria. Ikiwa mwandishi anajali sana wasomaji wake — kwa maneno mengine akijizuia kuandika anacholenga kutunga — basi sidhani kwamba kazi yake itapata thamani kubwa katika miaka ya mbele. Najua kwamba ni changamoto kubwa sana kwani kuandika fasihi kunataka kutotegemea kitu chochote kile ambacho kitazusha aina ya kizuizi katika ubunifu. Hatimaye hofu ya mwandishi — ikiwa anazingatia sana maadili na siasa — itampelekea katika msimamo wa kutegemea sana mfumo huo unaotuangamiza sisi sote ambao tunapenda ubunifu, nao ni soko huria. Kuandika fasihi kwa ajili ya kupendwa na wasomaji si kujitoa muhanga tu bali ni kujiua. « Shinikizo hizo za nje », yaani maadili, siasa na kisha uchumi ndizo zinazovuruga fasihi. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni