15/10/2015

KILWA PAMEKAGA

Leo alfajiri hii mbichi, nimetunga shairi hili. Kilwa imeingia mnadani, ikauzwa na washtiri wa juu. Msomaji ukitaka kujua maana ya baadhi ya maneno magumu yaliyomo, angalia chini ya shairi.

Bui wa Mti Mbangi, pamwe Kuya Malalani
Mie kauli ya Mawi, naitia maanani
Wendani wa Kisiwani, nyote nnawaiteni
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Sangamla na Kindumba, Sake na Sanga daweni,
Kikoni hadi Mbanga, kuzuru hakunishindi,
Ngwame maji ya kisima, ukulutu sijikuni
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Maji ya Buni mitoni, na mawimbi Ntandura
Na mbwipwi utandani, mguu wa kunitoga
Utibabu wa Chaani, mlulutu ndio dawa
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Si mshipi mkononi, si madema mtumbwini
Fundi Hussein tukirudi, twagubuga majibwini
Mganga mjarabati, kumbe ni jina kamili
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Bahari na utalii, kindu gani ni dafina
Jua latipika tipi, kibwengo kanyemelea
Hali guduri guduri, kilingeni utapona
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Utalii si rupia, kwa yakini nakwambia
Vigogo wametafuna, vinono na meremeta
Shangingi zinatembezwa, na makreti kumwagika
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Wacheni wabweregeshe, mapiswa ya magalacha
Miharo yao ya zimwe, eti kifuu ni pawa
Mchana kutwa waseme, si usiku watalala ?
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Bulazizi hawafiki, wataangushwa piningu
Sheik Ndembo sikwambii, urogo utamu mtupu
Sake ukitaka shari, ndipo shake ya kupiku ?
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Sheikh arobaini ndipo, kweli raha mustajaba
Kwa maini ya kondoo, mkondo ulipasuka
Sharifu kufa kikondo, vigogo si kufaana ?
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Nguvumali si mtalii, ufundi uleta zogo
Zama kale wakoloni, kwa umahiri wa bango
Kawashinda kwa uchawi, katepua pa kisogo
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Kaditama tumefika, uhasidi ninanena
Si mchezo wa kufupa, ufisadi wa wakubwa
Hukumu yao hakika, kuramba unga wa hoka
Nyama ya uvundo sili, naiogopa kuhara

Maarufu Mwalimu Johni


Maneno magumu :

ukulutu : aina ya upele unaosababishwa na kutooga maji

mbwipwi : aina ya mdudu wa pwani anayejifukia katika mchanga ; anauma sana akikanyagwa
mlulutu : mti wa porini, majani yake yanasaidia kutibu majeraha
twagubuga : tunatembea katika maji
mjarabati : aina ya masomo ya kiarabu katika kutengeneza ufundi au dawa maalum

kindu : kitu
tipi : jua limetua kabisa
guduri guduri : kutembea kwa kuchechemea
piningu : kuanguka chini kwa vishindo
hoka : unga aliotumia Nguvumali akitaka kutepua wachawi


                       Hakuna maoni:

Chapisha Maoni