13/10/2015

Kupiga picha urithi na kufotoa mrithi : « kweli chungu » au « uwongo mtamu » ?


Ama kweli kuona ni kuamini. Lakini pia kusema kweli ni thawabu. Hivi karibuni tumeletewa kitabu cha picha kuhusu Kilwa (hapa). Kitabu hicho kimesheheni picha ambazo zinapendeza sana. Kitabu hicho kinalenga shabaha moja tu : kutangazia kanda maskini hiyo ya Tanzania ili wawekezaji wavutiwe nayo wakajenge mahoteli ya kuleta maslahi chungu nzima. Lakini maslahi ya nani ? Je kweli wananchi wa mkoa huo watanufaika ? Na kivipi ? Eti wataalamu wanajua. Mimi hapo nilipo, kwa kuwa nimeishi miaka mingi katika mkoa huo, siwezi kukubali taswira hiyo jinsi ilivyofinyangwa na vigogo wale katika kitabu hicho. Mkoa wa Lindi kwa jumla unakabiliwa na masaibu na mashaka mengi sana, sijui ukame — mikorosho ya Pande inakufa, visima vinakauka na bahari imelaanika — sijui ukosefu wa zana katika kilimo, sijui shule zenye madawati mabovu, mbali na vijana ambao hukimbilia mjini na hali kadhalika. Wala tusiambiwe kwamba utalii utakuja kunusurisha jamaa hawa ! Uwongo huo tunaujua wazi. Tunajua kwamba utalii si tasnia ya kawaida na athari zake katika sekta mbalimbali zimedhihirika tangu zamani sana. Au tururisti ni teroristi !

Hapo basi nimeking’oli baadhi ya picha zangu za Kilwa kwenye ukurasa wangu, si kwa sababu nataka kudhalilisha jamaa zangu wa Kilwa niliowahi kuishi nao, bali nakusudia kuonyesha dhahiri kwamba picha za kitabu hicho hazijawekwa ndani ya mizani. Wasemavyo wahenga wa kale, penye urembo ndipo urambo !   

   

   

   

                   

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni