12/10/2015

Nchanchera ya ufadhili imewafikia : tayari Kilwa ni Zoo ya ziro ?


Zamani nilipokuwa mdogo nikiishi Unguja baadhi ya wenyeji wangu walikuwa huitikadi kwamba magwiji katika uganga wa kienyeji walikuwa na uwezo wa kuruka angani, licha ya kuwa na nyenzo nyingine mithili ya kumzuga mtu usiku na kumtembeza katika mashamba ya giningi au kumshughulisha katika ndoto zake apambane na biti Makiniki ili jongoo asipande mtungi tena. Waswahili hawa wangekuwa bado wana nyenzo hizo, kweli vita ingepamba moto wakati vigogo na mabosile wanaposhuka vijijini ili « kuelimisha wanyonge »… lakini vinabo wote wamerudi katika hali duni ya utwana au ujakazi na wamenyimwa kila kitu — shule za vijijini zimesambaratika, ufukara umetapakaa mote, utengano umekithiri, ukabila unarudi. Maisha magumu zaidi ya kifuu cha nazi. Nacho kifuu — pamoja na moto ule wa zamani — vyote ni zimwe. Tupu, kavu.Hapo nikisema kwamba ukabila unarudi katika vijiji, pengine ni maoni yangu. Lakini ukweli umedhihirika tukiangazia gurupu ya magalacha na wataalamu wa hapa na pale, zikiwa zimekusanya njemba weusi kwa weupe, Wachina kwa Wadigo, Wazambarau kwa Wafaransa, njorinjori kwa wabilikimo, kwani wote wamevaa sare moja. Ukabila hapo umekufa. Hakuna adui tena. Kila mtu na bui yake au, kwa maneno ya kisasa, mdau wake. Na wanaonekana mote Tanzania. Na kama hujawaona, utapata harufu zake ukipita vijijini kwenye warsha zao, hapo ndipo vinono na maji matamu yanapomwagika. Utawasikia pia, vicheko vyao, uchangamfu wao, utawachangamkia masuti yao, pamba zao na meremeta chungu nzima. Hawakanyagi chini hawa, hapana. Wanakuja na shangingi zao na wakikutana na mcountry bumpkin njiani, ukisikia sauti ikirindima kama mwangwi : « wee ambaa huko mporipori ! », basi umempata. Si mkubwa anataka kupita ?


Basi hivi karibuni, Ubalozi wa Ufaransa pamoja na mamlaka ya Tanzania — sijui idara ya mambo ya kale, yaani Antikwitiz, Yunesico na mabosile wengine wenye vitambi — wamefanya shoo na kuku pati huko katika himaya ya Kilwa. Na janibu hilo lina dafina kibao eti ! Ndo maaaaaana ! Na wazungu humo humo, heria tuvuke kwenda Kisiwani, ado ado usione soo, wengine wakiduru kwa baiskeli, wengine wakitalii katika mashua — tanga ya homu ! — wamejitolea sabili jamaani ! Hiyo ndiyo adventure ! Basi baada ya kujionyesha huko, katika showing off ya kulewesha mshamba apate kulewa mataputapu ya kufa mtu — si ulevi huo bali berere berere za mtaalamu — basi wametema aina ya kabrasha la ndani, la kuwakidhi hamu na hanjamu zote za « wahusika ». Sasa mapaparazi hawa wamesevu na wasomi hawa ambao wamerundikiwa rundo la vipawa wamepata posho zao, lakini wameacha buku ya picha, msomaji unaweza kuidownlodi hapo kwenye neti. Shehena ya picha tu ! Hata huna haja ya kusoma, just in case hujui kusoma. Usione noma kama hujui kubukua, wataalamu hawa watakuletea mtambo.

Maneno ya Prof Chachage tunayakumbuka, ila naona kwamba wengi katika majibwa wa kitandawizi ambao wakati wa Makuwadi walitapika nyongo ya ukoloni mambo leo, sasa tayari wametanasarika — au wametandawazika — wakajifunga vibwebwe na visese ili muradi Kilwa pauzwe au pachuuzwe. Kilwa kumeingia mnadani, kweli tu, lakini washtiri wa siku hizi tunawafahamu, wametambulika wazi, ndio hawa wa Delta ya Rufiji wanaosanjari kuuramba mtapishi wa zamani kama kelbu afanyavyo. Si wanasafiri kwenda Uzunguni ili wasome zaidi, wakabobee katika uketo wa utaalamu kisha warudi makwao ili kusomesha wale wale waliopigwa foto ndani ya kabrasha hilo ? Chambilecho mabingwa hawa wa « maendeleo endelevu aushi ya milele », tunajenga sera mpya, falsafa mwafaka, upendo wa ulimi na mate (au mtapishi ?). Wakilwa wamekalia juu ya hazina lakini hawakujua. Sasa wametanabahi, wamepata akili tambuzi na nadhari kubwa, kwa mujibu wa Ubalozi wa Ufaransa. Asante sana, ufadhili umefika, tumeupokea, mambo kamili gado ! Vifijo na nderemo zikufikieni !

Mimi hapo nilipo ni mkimbizi. Nilitaka kuomba uwenyeji wa Tanzania, yaani kujiandikisha uraia. Kuona vile, yaani kinyang’anyiro hicho cha wakubwa, tayari nimeghairi. Si nchi hizo mbili zinalingana tu, Ufaransa imejiafrikanisha ilhali Tanzania imejizunguzisha ? Eti wakubwa na wadogo tuheshimiane…

Je swala hilo la Chachage — Jambo hili kweli lina maslahi kwa taifa ? — kweli lingali lina maana ?                          

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni