18/10/2015

Nyimbo za kasia


Katika maboksi niliyokuwa nikiishi nayo huko Kilwa, leo nimegundua filam moja niliyopiga wakati nilipokwenda na jamaa zangu kupakia boriti na fito zilizokuwa zimekatwa karibu na Chaani huko Kilwa Kisiwani. Kwa kuwa ilikuwa msimu wa maleleji basi siku ile ikabidi tupige kasia. Na kasia hizo zinakuja na nyimbo spesheli ambazo zimejaa uchangamfu na bashasha. Kweli raha ilikuwepo siku ile !Zifuatazo ni baadhi ya nyimbo chache ambazo jamaa zangu waliziimba : 


Mvuta kasia kasema (leo)
Kwanza tuombe Mungu
Kwa baraka za Mashehe
Tuombe Mungu
Mvuta kasia kasema (leo)
Ya Rabi tuombe Mungu
Kwa baraka za walii
Kwanza tuombe Mungu
Kwa baraka za Masharifu leo
Tuombe Mungu...

Kuna wakubwa wenye nundu
Na sisi hatuwajali
Kwa tabia za utundu
Kwa mengi wanayofanya
Tunamshukuru Mungu
Tunakwenda zetu leo
Tunaona uchungu
Kwe heri tunakwenda zetu

Sijaolewa nikaachwa
Lakini bahati yangu mbaya
Wenzangu wamepata vitengee
Bahati yangu mbaya
Nalia na Mungu wake
Naweka makafara
Kuolewa siolewi

Tunagombana na mke wangu
Sababu ya nyumba ile
Kesho nitamwacha
Majirani wanasema
Kina babu wanasema
Kesho nitamwacha

Ukenda pwani uniambie
Usichomwe na kikoa
Kikoa kidudu cha pwani`
Nyama ya kuliwa
Wameng'amua ng'amu wezenu

Mnaitwa Songosongo twende
Kiro kirongo wee
Kina baba kina babu
Maadhamu kiunoni pembe
Ata Gandi naye
Karera mwana si wake

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni