13/11/2015

Haji Gora katika dunia yetu ya fedha


Mwaka 2001 nilipokwenda « kutwalii » Unguja kumtembelea mshairi Haji Gora, sikujua wakati huo kwamba ningefaulu kuchapisha kitabu cha mashairi kadha niliyochagua kutafsiri kwa kifaransa kutoka diwani fulani ya msanii maarufu huyo wa Tumbatu. Cha kutilia maanani hapo ni kwamba nimefanikiwa kukichapisha kitabu hiko mimi mwenyewe, kwa uwezo na satua zangu, bila ya kutegemea mhariri yeyote wala kampuni ya aina yoyote. Yalipatikana matoleo kumi ya kitabu hiko ambayo niligawanya na wasomi wengine wa kwetu Ufaransa, ambao wengine ni washairi pia, wala hayakuuzwa bali yalipewa bure. Hiyo ndiyo ilikuwa kusudio langu. Kitabu kilichopatikana hapo kilikuwa kinapendeza sana kwa kuwa kilichapishwa na michoro maalum ya msanii Mfaransa ambaye alikuwa hodari sana katika usanii wa kaligrafia.


                               


Kuchapisha vitabu kwa njia hii ilikuwa kitu cha maana nyingi katika historia ya nchi mbali mbali ambapo fasihi ilipoanzishwa awali, hususan Japan, Italia na Ufaransa. Kabla haijaanikwa juu ya chanja za dukani kama ng’onda ndani ya kibanda cha wavuvi, fasihi ilikuwa kitu cha kuenziwa wala si kitu cha kuuzwa kama vipuri vya gari. Ukoloni na ubepari ndio ulioathiri sana mchakato wa kutunga fasihi hadi kufika hatua ya kutaka kuuza kila tungo la fasihi kwa thamani ya kiuchumi. Hapo ndipo fasihi, hasa riwaya ambayo ni utanzu duni katika tanzu zote, ilipoanza kutumiwa ili kufikisha ujumbe kwa jamii — kwa kuwa kufikisha ujumbe ni kama kufikisha mifuko ya sembe. Lakini fasihi, hasa Ufaransa na Japan, ilikuwa haina thamani yoyote ya kifedha kabla ya hapo. Ilikuwa tunu ya kupeana, hususan kwa sababu fasihi ni aina ya sanaa iliyoundwa katika tabaka la juu la jamii — ambalo si tabaka lenye fedha kama walivyo mabwanyenye wa siku hizi bali lenye mirathi ya zamani. Ndiko kulikosomwa fasihi, ndiko mwana wa kindakindaki alikopata « kujilimisha » katika nafsi yake.

Tukizingatia jinsi ubepari huo ulivyoathiri dunia yetu ya ubunifu, si jambo la kushangaza kuona kwamba tunashindwa kupima ubora au uzuri wa vitabu hivi vya fasihi. Hatujaingia katika kipindi cha usasa bali tumeingia katika kipindi cha "sasa hivi" na "umimi". Huko Japan au Ufaransa, tunaposoma mashairi fulani kutoka karne 14 tunajua kwamba tunasoma mashairi bora kwa sababu mashairi haya yanazidi kusomwa hadi leo. Ubora wa mashairi hayo pia umedhihirika wazi kwa kuwa waandishi wengi wengineo kutoka karne ile ile wamepotea kwa kuwa walipuuzwa na wasomaji katika karne zifuatazo. Tukirudi katika tungo za Haji Gora — na za washairi wote wa siku hizi, si Watanzania si Wajapani — swala la ubora wa mashairi limekuwa ni changamoto kubwa sana. Haji Gora anaelekea mshairi bora (na mimi ni mpenzi wake) kwa sisi viumbe tunaoishi leo ambao tutafariki kesho, lakini katika mfululizo wa makarne na makarne, nani anajua ? Tukutane karne 25… hapo ndipo tutakapojua kama alikuwa mshairi bora. Lakini hadi hapo, tutengeneze mshiko !!

Ifuatayo ni mifano ya kurasa za kitabu changu. Hapa kuna shairi la "Miujiza", "Ukulivu" na "Bahari" kwa kiswahili na kifaransa. 


Maoni 2 :

 1. Nimependezwa na juhudi yako ya kumwenzi mtunzi maarufu Haji Gora Haji. Ingawa ninakifahamu ki-Faransa kidogo sana, nimesoma kwa uangalifu mashairi uliyoyaweka hapa pamoja na tafsiri zako. Nimeguswa na utamu wa mashairi hayo na tafsiri zako. Nimevutiwa sana na michoro inayoambatana na mashairi hayo.

  Suala la uandishi katika mfumo wa ubepari ni zito. Limewakera watu wenye tafakari nzito tangu zamani, kama vile akina Karl Marx, Vladimir Lenin, na Ernest Hemingway. Himaya ya pesa, imehujumu uhalisia wa utunzi na kuigeuza sanaa kuwa bidhaa. Ni balaa.

  Lakini kuna waandishi ambao wamekataa kuhujumiwa na himaya ya pesa. Hao ndio wale waandishi ambao maandishi yao yanadumu na yatadumu karne hadi karne. Mifano ni akina Tolstoy, Dostoyevsky, Dickens, Dumas, Shaaban Robert na Haji Gora Haji.

  Ninavyoona, nikizingatia ukweli kwamba waandishi kama Haji Gora Haji wanafanya kazi muhimu sana kwa jamii, ingefaa wapate kipato kutokana na uandishi wao. Hakuna ubaya, kwani wao wanazingatia sanaa, sio pesa. Ingekuwa jamii imejipanga vizuri na inawathamini watu hao, ingewapa nyumba, chakula, na mahitaji yao mengine ili waweze kuandika kwa amani kabisa, bila kuhangaika watakula nini, watavaa nini, au watatibiwa vipi wakiumwa. Labda hilo wazo langu ni la kinjozi, yaani utopia, lakini ndilo wazo langu.

  JibuFuta
  Majibu
  1. Asante mpendwa Joseph Mbele kwa mchango wako mzuri ambao kama ilivyo kawaida kwako unagusia hoja muhimu sana. Bila shaka, Haji Gora ni miongoni mwa watunzi bora katika mapokeo ya mashairi ya kiswahili. Hilo nadhani halipingiki.

   Tatizo zito lililopo kwangu ni hadhi ya fasihi katika dunia yetu iliyokumbwa na kutawaliwa na matumizi ya fedha katika vipengele vyote vya maisha yetu. Matokeo yake katika sekta hiyo ya ubunifu yameshadhihirika wazi hususan katika nchi nyingi za Ulaya ambapo kila siku waandishi « bushoke » wanajipeleka mbele ili kujiuza ; kwa kifupi,

   - fasihi haitahiniki kupitia ujumi bali kupitia hoja za siasa au za ukabila (na ukabila wa kisasa tunaujua : eti kuna fasihi ya kimagharibi, fasihi ya kiafrika, na kadhalika ambazo hazilingani).
   - fasihi si mapokeo wala mapisi ya aina yoyote. Yaliyoandikwa zamani — haswa yale « matini » yatokayo nchi za magharibi, hususan nchi zile zilizotawala kiukoloni — si kitu, hayana thamani wala sifa.
   - fasihi ni aina ya bidhaa kama ilivyo vipuri vya gari.

   Endapo mchakato huo utakithiri kikweli, nadhani kwamba fasihi itaingia katika msimu wa mapukutiko na kina Haji Gora watakombwa na kimbunga hicho cha kipuuzi. Kama ulivyosema, Haji Gora hana uwezo. Hivi karibuni, hapa nilipo Kampala, nimeshtukia kukuta kitabu cha « mwandishi maarufu » wa Kenya kilichoandikwa kwa Kikuyu (mbali na vitabu vyake vya kiengereza, vinavyopatikana kwa wingi) wakati ambapo hata vitabu vya kiswahili haviuzwi seuze kamusi ya kitumbatu ya Haji Gora ! Afadhali mtu awe Mmarxisti wa mstari wa mbele (na hapo fedha itapatikana) kuliko mvuvi wa madema kama alivyo bui langu sahibu Haji Gora !

   La mwisho hapo kwa kuwa Haji Gora anastahiki kusaidiwa, kama ulivyosema. Nadhani kwamba hakuna cha kumsaidia zaidi kama si kununua vitabu vyake, na kuhimiza « vitoa » vitabu vya Tanzania kuchapisha vitabu vyake bila ya kumdanganya. Viko wapi vitabu vya kiswahili katika duka la Samora Avenue ?

   Futa