10/11/2015

Kweli neno hili « utamaduni » lina maana ?


Muhtasari : utamaduni ni neno au dhana ambayo inatumika sana siku hizi. Lakini lina utata ndani yake. Tukichambua asili yake tunakuta mikondo miwili ya falsafa. Wa kwanza ni mkondo ule utokeao Ugiriki wa zamani wa kale ukanywesha mkondo wa kilatini kupitia maandishi kadha kama yale ya Cicero. Wa pili ni ule uliomea hivi karibuni huku ukibebwa na maono mapya yaliyoibuka wakati anthropolojia ilipozaliwa karne 19 na 20. Mikondo hii miwili inakinzana kabisa wala hailingani. Wakati maana ya dhana ya utamaduni katika anthropolojia inapojadilia mila na desturi za jamii fulani kwa kuzingatia matokeo yoyote yanayoletwa na watu (na baadhi ya wanyama) — utamaduni hapo ni jinsi watu wanavyokabili maisha katika mazingira yao — utamaduni katika falsafa ya kilatini huzungumzia jinsi mtu anavyokabiliana na ubunifu na uvumbuzi katika nafsi yake. 

                                                                          --------------------------------------------

Sisi sote tunaoishi katika dunia hii ya usasa tunajua, au pengine tunahisi kwa mbali kidogo, maana ya utamaduni, ijapokuwa hatujui neno hilo linakotoka. Wengi katika wanaolitumia kila siku hawajui kwamba asili yake inapatikana Marekani kunako chimbuko la taaluma iitwayo anthropolojia. Fasiri nyingi za neno hilo zinapatikana katika vitabu vingi vya anthropolojia, kamusi zake ama katika mazungumzo ya kitaaluma. Kwa mfano nimenakili uchambuzi huo kutoka tovuti ya wikipedia : « utamaduni ulifafanuliwa kama uwezo wa kiubia wa binadamu wa kuainisha na kusimbika tajiriba zao kiishara na kuwasilisha kiishara tajiriba zilizosimbikwa kijamii ». Tukichambua au tukifafanua zaidi, tunaweza kukuta fasiri nyingi nyinginezo na itakuwa si vigumu hatimaye kuona kwamba kila kitu kina utamaduni wake. Vijana wa bongo flava, wafanyakazi wa viwanda, wanamuziki, mashoga, washabiki wa kandanda, wapenzi wa ngoma fulani, na kadhalika, wote wana utamaduni. Makabila kwa wananchi, wakristo kwa wabudisti, wachawi kwa wana sayansi, wabunifu kwa wasanii, wavuvi kwa rubani, wote wana utamaduni. Wahalifu, washenzi, majambazi, vibaka pia wana utamaduni wao. Hata sokwe, nyuki na pomboo. 

                


Utamaduni ni neno la kubeba mengi. Limekua sana kiasi cha kuvaa akili zetu tusiweze kulitafakari vingine. Kwa sababu kuna viwanda au tasnia za kitamaduni, ukandarasi na soko ya kitamaduni, tunahakikishwa kila siku kwamba kitu hiko kipo. Wataalamu wengine husema utamaduni unaeleweka vizuri tukiwa tumesisitiza kwamba upo katika muundo wa mahusiano ya kijamii. Mtu atakuwa na utamaduni akiwa amejinasabisha katika jamii fulani, kama ametengeneza ubia fulani na watu wengine anaoishi nao. Katika istilahi ya wataalamu wa sayansi ya jamii yapo maneno mengi ambayo yanadhihirisha kwamba hakuna mtu duniani asiye na utamaduni. Lakini je, ikiwa ni hivyo, nini maana yake tena ? Tatizo kubwa lililopo na « nadharia » hii (ambayo si nadharia bali ni maono ya kiitikadi fulani) ambayo imeimarika katika maoni ya watu kote duniani — pengine kupitia mtandao na asasi mbalimbali kama ile ya Unesco — ni kwamba inafeli kuelewesha jinsi wanadamu wanavyopambana na ubunifu. Utamaduni ni mila na desturi, maadili na kaida, maarifa na itikadi, mkabala na tabia, na kama kila jamii ina utamaduni wake, kama isemekanavyo siku hizi, tutalielewa vipi swala hilo la ubunifu, uvumbuzi na uundaji wa dhana ya kisayansi ? Hakuna watu wabunifu, kwa maana ya kuweza kubuni pamoja, si kweli. Wagiriki hawakuwa wabunifu, ni uwongo. Socrate, Sofokile, Plato, Eshile na wengine wengi ndio waliokuwa wabunifu. Kila mmoja alileta ubunifu wake.

             


Kikubwa hapo ni kukumbuka kwamba Wagiriki hawa niliokwisha kutaja hawakuwa na neno lolote ili kujadilia tunachochukulia sisi ni « utamaduni », kitu ambacho kwetu kimegeuka « ng’ombe wetu mtakatifu ». Tungekuwa na uwezo wa kuunda maabadi kwa ajili ya utamaduni, nadhani tusingejinyima kuwa nayo. Ni neno lililojikita katika fikra zetu kiasi kwamba tunashindwa kulikosoa. Na nchi kadhaa duniani wameshajipatia sijui wizara ya utamaduni na asasi mbalimbali kuhusu shughuli hizo za kitamaduni. Wagiriki wa zamani nao hawakujali. Ndiyo maana pengine waliturithisha mambo mengi —tamthilia ya huzuni, na sayansi kadhaa. Na Walatini ambao walikuja baada ya kupotea kwa jamii ya Wayunani walijua fika kwamba Wayunani walikuwa na wabunifu wengi wa hali ya juu. Miongoni mwa Walatini tunakuta Cicero ambaye ndiye mwana falsafa wa kwanza aliyetafakari dhana hiyo kwa kuunda neno « cultura » ili kuzungumzia urutubishaji wa ardhi inayolimika. Hatimaye neno hilo likawa sitiari katika maandishi yake maarufu, hasa katika usemi « cultura animi ». Kwa kutunga usemi huo Cicero alikusudia kusisitiza kwamba mtu anapaswa kukuza (« kulimisha ») nafsi yake kwa kusoma maandishi yaliyohalilishwa katika mapokeo ya jamii ambayo pia ni mifano mizuri ya kufuatia. Katika mapisi haya, utamaduni ukawa neno lililotumika kuelezea jinsi mtu anavyopambana na pingamizi zinazomzuia asijijengee katika nafsi yake (hapo nafsi ni sawa na hekima, maarifa na akili).

Utamaduni kama dhana ya kianthropolojia imependwa na watu wa sasa kwa sababu kwanza ni neno lililofuta neno lingine, nalo ni « ustaarabu » au « kultur » kwa kijerumani. Lakini ustaarabu ni neno lililorejelea uteuzi wa vigezo ama vipengele fulani ambavyo vilichukuliwa na makarii wa karne au enzi ya Nuru kama vina maudhui mahususi yasiyopingika. Kwa mfano, mwenye utamaduni wa nafsi — ambaye ni mstaarabu — ana haki ya kujitenga na wenzake wasio na utamaduni — ambao ni washenzi. Katika utamaduni huo wa nafsi hakuna usawa — neno ambalo lina uzito mwingi katika itikadi zetu za watu wa sasa. Ndiyo maana imani inayozingatia usawa wa kila kitu (« anything goes » au relativism) ambayo imeitikadiwa sana na wanaanthropolojia inasigana pakubwa na msimamo wa wana falsafa wa zama hiyo ya ukale wa Wagiriki, pamoja na wana falsafa wengine wa enzi ya Nuru na wengine wengi wa siku hizi. Kwa mfano, kukeketwa kwa vigori wenye umri wa miaka kumi ni aina ya utamaduni kwa watu wa jamii ambao huamini kuwa kitendo hiko kina sababu zake katika kaida, masharti, jumla ya mitizamo, malengo na maadili kadhaa. Wanaanthropolojia wangesema hapo kwamba athari hizo zote za kijamii ni aina ya mchango muhimu katika kujenga tabia na mwenendo wa vigori ambao wanapaswa kuwa « wanawake bora ». Ni utamaduni wao ! Wagiriki au walatini wasingefahamu msimamo huo kwa kuwa utamaduni kwao ni mchakato (ukuzaji, « ulimishaji ») unaohusisha utu wa mtu, wala si « utu » wa jamii fulani (kauli ambayo haina maana).

                        

Msimamo huo — ambao ulianzishwa enzi zile za Wayunani ukienziwa hadi leo katika nchi mbali mbali — unachukulia kwamba kila mtu ana uwezo au satua ya kujenga utamaduni wake, si kwa sababu yupo katika jamii fulani (akiwa na mila na desturi za jamii hiyo) bali kwa sababu amepewa uwezo (maumbile) wa akili. Wengi katika jamii wanashindwa kujenga utamaduni huo wa nafsi, wachache wanafaulu. Kila mtu katika upweke wa nafsi yake amepewa, kutokana na maumbile yake, uwezo wa kubuni, kuvumbua na kutunga mawazo ya kufikirika kwa sababu ana uwezo (kupitia akili yake) wa kukataa yamwathiriyo katika tajiriba yake. Lakini wengi wanashindwa kwa sababu kujenga na kukuza nafsi ni mchakato wa kibinafsi ambao unapingana na baadhi ya athari hasi za kijamii. Mila na desturi zinazochangia kujenga ubia au ushirikiano ndizo pia ambazo zinadunisha zinduo la utamaduni wa akili kwa kudhoofisha ujasiri unaotakikana katika kujenga nafsi ya mtu. Galileo si Mussolini ingawa wana utambulisho mmoja, kwa sababu Galileo alikuwa na ujasiri wa kufikiria huria. Na jamii kwa jumla ndiyo ambayo huvuruga uwezo huo wa nafsi upate kupanuka vizuri ; tujikumbushe mfano huu wa Galileo na wenye akili wengine jinsi walivyopuuzwa kwa kubezwa na jamaa waliokuwa wakiishi nao. 

Kwa maneno mengine, utamaduni wa nafsi ni mchakato ulio wa kipekee kwa kuwa hufinyanga nafsi ya kila mtu, mbali na ushirikiano mtu atakaokuwa nao na jamaa zake. Mtu anaweza kuwa mtu maridhia mwenye mrahaka na watu wa jamii yake huku akiwa hana utamaduni wowote, kwa maana ya utamaduni wa nafsi. Katika falsafa hiyo, mila ni mila na utamaduni (wa nafsi) pekee ndio unaokuza akili ya mtu. Ni kama kusema kwamba mtu anafanana na wenzake (kutokana na athari ya mila) lakini hana mfano wake (kutokana na « nafsi » yake). Kila mtu ni mmoja japo ana wandani wake. Utambulisho katika falsafa hiyo ni kama ajali, si majaaliwa. Sofokile angalikuwa Mchina (kuzaliwa kwake Ugiriki si jambo la kutilia maanani). Utamaduni ni mchakato ulio katika historia : watu hubadilika kila wakati kwa kuwa binadamu ni kiumbe anayetaka kujiboresha. Katika muktadha huo wa utamaduni wa nafsi, nadhari ya mtu mwenye utamaduni mwingi huwa ni imara, kwa sababu imeerevuka, imepevuka sana kiasi kwamba mtu anajitambua (kabla ya kujitambulisha) akiwa hujijua sana. Pengine ni sababu mojawapo inayoelewesha kwa nini Ugiriki wa zamani ilikuwa ni nchi iliyojaa watu wenye utamaduni mkubwa katika fani mbalimbali kama vile falsafa (Sokrate, Plato, Aristotele), mantiki, hesabati, astronomia na kadhalika.

Kinyume na dhana ya utamaduni ilivyofasiliwa na wana anthropolojia, « utamaduni wa nafsi » wa Cicero ni usemi (si dhana) ambao haueleweki tusipozingatia neno lingine, nalo ni « maumbile ». Maumbile ya mtu ni kigezo kikubwa sana katika kuelewa tabia na mwenendo wa kila mtu. Ina maana kwamba binadamu ni maumbile kwanza — wanadamu wana mwelekeo fulani kutokana na maumbile hiyo. Wanadamu hawatofautiani kufuatana na maumbile hiyo. Katika falsafa hiyo, uhayawani au ubedui kwa mfano ni baadhi ya vipengele ambavyo huzingatiwa sana na wataalamu wa falsafa hiyo (mfano mzuri ni falsafa ya Immanuel Kant (1724-1804) na Hannah Arendt (1906-1975). Ina maana kwamba uhayawani upo katika utu wetu wala hayo si kusema kwamba kikundi fulani cha wahalifu wana utamaduni wa kijeuri. Badala ya hayo, tutasema kwamba kikundi hiko hakina utamaduni. Na tukizidi kusonga mbele katika uchambuzi huo, tunaona kwamba utamaduni wa nafsi ni kichocheo kikubwa katika kujikomboa, ikiwa mtu ana matakwa ya kujikomboa (haina maana kusema kwamba tunaweza kuwakomboa watu wengine). Kujikomboa inahusisha utaratibu wa kujitoa katika maumbile hiyo inayoturudisha katika uhaba wetu wa nafsi ile ya Cicero. Ndipo kusema kwamba kujitia utamaduni ni kama « kujilimisha » katika nafsi yetu. Ni kujikomboa kwa kujitenga na athari zile zinazozuia tusikue katika nafsi yetu, au uhatinafsi wetu. Na katika vizuizi au pingamizi hizo tunakuta « asili » yetu, kile ambacho kinatuunganisha na athari ya nje ya nafsi yetu (kabila yetu, itikadi na imani zetu kadhaa, na kadhalika) kupitia hisia zetu. Falsafa hiyo inazingatia utu kuliko utambulisho. Socrates alikuwa mwana falsafa mwenye utamaduni mkubwa, si kwa sababu alikuwa Mgiriki bali kwa kuwa « alijilimisha » kwa kupania kusoma na kupanua akili na nafsi yake. Katika falsafa hiyo, baadhi ya wana anthropolojia maarufu kutoka mkondo ulioitwa « French theory » walipinga sana nadharia hiyo kutoka Marekani (the so-called cultural studies) inayochukulia kwamba kila jamii, kila asasi, kila kikundi na kadhalika, ina utamaduni wake. Miongoni mwao, hatuna budi kutaja Claude Levi-Strauss pamoja na René Girard ambaye amefariki juzi hii, tarehe 4 ya novemba 2015.

                            


Hapo nitapenda kumaliza makala hii na kutaja dondoo ya kitabu changu cha Antigone nilichotafsiri hivi karibuni (HAPA) kwa kiswahili kutoka kwa mwandishi maarufu wa kifaransa Jean Anouilh. Kitabu hiki hakipatikani katika maduka ya vitabu wala hakitapatikana kamwe kwa kuwa hakina umuhimu kwa watu wanaoishi Afrika mashariki. Hata hivyo, katika utangulizi wake ninazungumzia baadhi ya hoja ambazo zinaendana na mada hiyo ya leo. Kwa mfano, najiuliza kwa nini hatuwezi kusema kwamba tamthilia hizo za huzuni kutoka Ugiriki ambazo takriban zote zimetafsiriwa katika lugha nyingi za dunia (ila kiswahili na lugha ndogondogo za Afrika) zimekuwa maarufu hadi leo. Jawabu ni wazi : kwa sababu Wagiriki walikuwa wameerevuka sana katika huo utamaduni wa nafsi kiasi cha kujua kwamba mila na desturi zao hazikuwa na maana kuzungumzwa katika thamthilia. Kama nilivyoandika katika utangulizi wangu :

« …Tusisahau kwamba wasanii ni wabunifu. Na ubunifu ni mchakato unaokusudia kurekebisha au kugeuza kile tunachoona — au tunachogusa — kwa kukiweka katika hali shani ambayo ni ya kigeni. Ni kama kuchuja au kupitua maoni yetu yapate kupinduka kisha yaibuke katika hali mpya ya kiajabu. Tusisahau pia kwamba Wagiriki walikuwa hawana neno la kumaanisha « utamaduni ». Lakini walijua jinsi ya kubuni kwa kusahilisha wahusika wa tamthilia ili wasije wakaonekane « Wagiriki » halisi, walijua kunyepesisha uchezaji wa jukwani ili watazamaji wasije wakayakumbuke mazoea yao ya kila siku, walijua kurahisisha ufahamu wa maonyesho yao ili watu wapate kupurukusha mazonge waliyokumbwa nayo katika maisha yao. Kughalifika kwa matatizo na masaibu ya maisha ndiyo dhima kuu ya tamthilia hiyo. Antigone wala Edipode si Wayunani, na kweli Sofokile alifanikiwa « kuwasiriba » wahusika wake wasije wakaonekana « Wagiriki ». Sofokile alifaulu kuwatoa wahusika hawa katika « utamaduni » wao ili wawe wanadamu wenye uwezo wa kuongea na watu wote. Ndiyo maana Wagiriki walitumia vinyago, ndiyo maana mapambo na maonyesho ya jukwani yalikuwa si ya fahari ya kikwao, ndiyo maana tamthilia ni aina ya katharsis, yaani utakasaji wa hisia zilizochemka… »

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni