04/11/2015

Mahuruji ya pembe za ndovu yamekomeshwa ?


Siku moja niliwahi kusimama Nangurukuru kwenye njia panda inayoelekea Kilwa. Wakati ule nilikuwa njiani ya kurudi Kilwa Masoko kutoka Mandawa ambako tulikwenda, mimi na rafiki zangu Hassan na Sudi, kwa mzee Maarifa ambaye kwa wakati ule alikuwa mganga maarufu sana katika shughuli za kuendesha kilinge. Basi siku ile tukaamua kumpitia rafiki yetu Hamisi aliyekuwa akiishi Nangurukuru. Kufika tu, tukakaribishwa ndani ya nyumba yake, na kwa kuwa ilikuwa muda wa kula chakula, basi tukaambiwa tusubiri chajio itengenezwe. « Shemeji » yetu akaanza kuteleka na kuipua vyungu vyake na sisi wanaume tukavuta subira barazani hadi « utamaduni huo utekelezwe ».

Hamisi alikuwa ni kijana mzuri sana ambaye alibahatika kupata ajira kutoka biashara ya pembe ya ndovu, yaani ya tembo kwa waswahili wa bara. Na wakati ule, ilikuwa mwaka 2004, biashara hiyo ilikuwa imepamba moto sana katika kanda hiyo ya Tanzania. Kwa kuwa mimi nilikuwa mgeni kabisa katika shughuli hizo, nilimhoji mwenzangu kuhusu pirika zake. Alinifahamisha mengi sana, jinsi kazi hiyo ilivyompatia maslahi ya kumsaidia kutosheleza mahitaji yake barabara, na jinsi shughuli hizo zilivyopangwa vizuri sana kwa kufuata mpangilio uliokuwa umekamilika. Yeye kazi yake ilikuwa kusafirisha « wagonjwa » (yaani pembe zile) waliomfikia kutoka porini hadi « wahusika » waliokuwa ni kama wakadamu wake kutoka Kivinje ambako pembe zile zilikuwa zinaingizwa katika magogo yaliyosafirishwa katika meli za kwendea China. Basi katika maelezo yake mengi alituelewesha jinsi vijana wengi walivyoinuka « kimaisha » kutokana na biashara hiyo, wengi wakiwa makuli wa porini waliokwenda kubeba pembe zile, wengine wakiwa kambini mle wa Selous kunako ndovu wale, wengine wakiwa Kivinje ili kusafirisha mahuruji hayo.

Iko siku tulifuatana na jamaa zangu huko porini wala hatukufika mbali sana tukakuta mizoga mingi ya ndovu na wengine waliokuwa wameshageuka mifupa tu. Tukapiga picha, tukaangazia mazingira vile yalivyokuwa kimya kabisa sasa, tukarudi Kilwa. Nayakumbukia sana matembezi hayo jinsi tulivyoyachamgamkia, na kweli raha ilikuwepo, na vicheko pia tosha. Lakini juzi tumepata habari rasmi ya kwamba mlanguzi mkubwa sana wa pembe za ndovu « ameswekwa rupango ». Kwa jina lake huyo mpunjaji ametambuliwa kama « Shetani ». Msomaji unaweza kufuata kiunganishi hiki (HAPA na HUKU) kama unataka kujua zaidi kuhusu umaarufu wake. Inasemekana kwamba Shetani huyo alikuwa na vikosi vyake vingi vya majangili kote Afrika mashariki, vikosi na vikundi ambavyo aliviunganisha vizuri sana kupitia utaratibu uliokuwa umekamilika vizuri. Inasemekana kwamba katika miaka mitano iliyopita, asimilia 70 ya ndovu wa Tanzania wameshapotea kabisa. Na kweli duniani Tanzania imejitangazia vizuri katika biashara mbali mbali ya kusafirisha nje vitu vingi ikiwa ni pamoja madini, gesi, mafuta na pembe ya ndovu. Hapo ndipo wasiwasi inapowajia marafiki zangu wa kule Nangurukuru. Je, si watapoteza ajira zao, kazi na tija zao ?


   

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni