26/11/2015

Nimetafsiri mchezo wa kuigiza wa Sony Labou Tansi unaoitwa « La parenthèse de sang »...


…kwa kiswahili ni « Kitambo hiki kimejaa damu ».

Huo mchezo unazungumzia hali ya udikteta ulioshamiri katika nchi ya kufikirika. Wanajeshi wanasaka Libertashio ambaye ni « gaidi » aliyepinga udikteta. Katika msako huo mbaya wanajeshi wanajifanya hawajui kwamba Libertashio ameshafariki ili kujenga dunia ya longolongo. Mchezo unatuingiza katika mazingira ya kuruta na sajini ambao wanamalizana. Katika machafuko haya raia ya kawaida nao pia wanakalifiwa na kuteswa kupindukia.  


Sony Labou Tansi (1947-1995) alikuwa ni mwandishi kutoka Kongo. Mchango wake katika fasihi una thamani kubwa, kiasi kwamba wengi katika makarii au wasomi duniani husema kwamba ni kinara mmojawapo wa fasihi bara ya Afrika. Na bila shaka, tukishawataja Ahmadou Kourouma (1927-2003) na Yambo Ouologuem, Sony Labou Tansi atachukua nafasi yake. Mimi hapo nisingesita kusema kwamba amechukua nafasi ya kwanza — na anaacha nyuma sana mwandishi Chinua Achebe (1930-2013) —, angalau kwa sababu moja. Ni mwandishi ambaye yupo katika historia ya fasihi, si kwa sababu maandishi yake yalijaa mafunzo na hekima kubwa — kwa kuwa vipengele hivi hata mwandishi wa habari au mtu yeyote mwenye balagha ya kisofistiki atavitimiza kirahisi — bali kwa sababu alikuwa na satua ya kuelezea mazingira yake kwa kutumia lugha mahiri. Lugha yake imejaa ubunifu wa kila aina na alikuwa mwandishi huria asiyeogopa kutopendwa, asiyejizuia kutumia maneno fulani ati kwa sababu si maadili — na tombovu na matusi kweli zimeshamiri sehemu nyingi za tungo zake — na vipengele vingi sana — hususan ilhamu yake iliyopanuka sana — ambavyo vinamwekea mtunzi huyo katika mlolongo wa waandishi maarufu wa duniani. Sony Labou Tansi ni mjukuu wa Gabriel Garcia Marquez na Arthur Rimbaud. Kiujumi, lugha yake imejaa upinduzi wa maneno, utele wa semi za kumkengeua msomaji, umwingi wa methali za kipuuzi, na fasiri nyingi juu chini. Sony Labou Tansi hupenda ukemi, unajisi wa mwafaka, upinduzi wa kila kikubalikacho haraka haraka.


Ni mwandishi mwenye ujeuri, ujuba mzuri usio na kifani, uchokozi safi na hasira murua. Hivyo ni mwandishi mjasiri na mwasi. Kwa machache alikuwa si mwandishi mwafaka (lakini je, ipo fasihi inayozingatia mwafaka ?) bali mwandishi mhuni — katika maandishi yake — kama alivyokuwa Shakespeare na François Villon. Tamthilia yake haswa ni ya kushangaza : msomaji akisoma michezo yake hajui anakokwenda, si kwa sababu wahusika wenda wazimu au watu wenye kichaa wako tele katika tungo zake, lakini pia kwa kuwa tumezidiwa hadi kukinai na mwonjo wa mwandishi wa kufinyanga wahusika wapendao ufukufuku, ukejeli na mikabala ya kutaka kupindua ujinga. Sony Labou Tansi ni mwandishi anayependa kuteka akili ya msomaji asije akajifanya baadaye kuwa ni bora kuliko wenzake. Ni mwandishi mwenye utu mwingi. Msomaji ukisoma vitabu vyake, utarajie kwamba ujinga utakuvuka. Dhima yake kuu ya fasihi inapatikana kwake : kukukaba wewe msomaji mpaka utakubali kutapika kiburi chako ! 

                                              
 


Alain Mabanckou alipokwenda kumtembelea Sony Labou Tansi ili kumhoji kuhusu kazi yake na ilhamu yake, Labou Tansi alimjibu yafuatayo (kutoka HAPA) :

SLT : « Mimi nasema hivi, nawambia washairi chipukizi kwamba niliwahi kuandika mashairi, tena mengi, lakini wahariri hawapendi mashairi hata kama nilikuwa nimeshapata dibaji kutoka washairi bora wa dunia nzima ! Unajua dunia imesambaratika, imekuwa kama hatupendi mashairi kwa sababu tumepitwa na kina Senghor, Damas na Césaire. Lakini pengine wewe unaweza kubahatika, usikate tamaa, jaribu tu… Na umeshatunga maandishi ya nathari ?
Mabanckou — Bado…
SLT — Siku hizi afadhali kuandika nathari kuliko mashairi. Nina uhakika kwamba wahariri wengi hurudisha tungo nyingi za mashairi wanazopokea bila hata kuzisoma. Na unasoma washairi gani ?
Mabanckou — Hasa wale walio katika mapokeo ya Ufaransa na wengine kutoka kwetu Kongo.
SLT — Si haba lakini wako wengi zaidi ya hawa ! Lazima ujikomboe yaani utembee sana dunia yetu, ujipanue kiakili, ukasome kina Pablo Neruda, Octavio Paz, Giacomo Leopardi, Pouchkine na wengi wengineo !
Mabanckou : Hapo akaniandikia majina hayo niliyokuwa siyafahamu wala kusoma… »


Tafsiri yangu kwa kiswahili haipatikani katika maduka ya vitabu Afrika mashariki wala haitapatikana kamwe miaka ya mbele. Msomaji bila shaka unajua kwa nini… longolongo za wanazuoni ? Sauti zinasikika tayari : huyo mwandishi mwafrika hana itikadi za umoja wa Afrika ? Yaani hana imani hiyo ya Afrika  kuwa  chanzo  cha  mawazo mengi ya kifalsafa ? Inawezekana ? Kwani si ana ngozi nyeusi ? Halafu kazaliwa Kongo ? aaah… au ni kibaraka ya Mkoloni ? Kumbe huyo kikaragosi ! Na kadhalika...

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni