08/12/2015

Nimeandika tamthilia kwa kiswahili inayoitwa « Kaburi la kaboni »


Tamthilia hii imegawanyika miongo mitano. Dondoo lifuatalo penye ukurasa wangu wa leo ni sehemu ndogo (inayoitwa kinibu katika mchezo) kutoka katika mwongo wa tatu, wakati wa majira ya nchanchera ya tindiswiti. Wahusika kutoka nchi iitwayo Kaputi, nchi mojawapo ya Afrika yenye makaazi milioni mia nne na thelathini na tatu, wako nyumbani kwa Prof Bombomu ili kujadiliana mbinu mpya ya kuweza kutengeneza kalibu la kusubia kaburi la kaboni. Mbinu hiyo inaaminika kwamba itasindika gesi ya kaboni ambayo hulinasa joto la jua na kusababisha waafrika wasizae kama kawaida.

Muktadha :

Afrika, mwaka 2064. Watu bilioni 4. Tuko mji mkuu wa Lindilandi katika mtaa uitwao Kalafati Nyororo. Wakaazi milioni 30. Nyumbani kwa Prof Bombomu, maarufu sana Afrika kote kwa maandishi yake murua aliyoandika kuhusu ukoloni mambo mtondogoo.

Usiku mbichi, saa nane. Nje kelele ya jenereta, moshi wa plastiki umehanikiza kote. Unaingia ndani. Mtumishi Mzungu Mbukuku anakwenda kufunga madirisha. Pembeni mwa ukumbizo mna tundu la njiwa wa zamani. Si njiwa hai, bali ni nyara.

Tuko ukumbini kwa Prof Bombomu. Masofa yenye kasabu, gudulia la kigae feki lenye maua ya plastiki, feni kubwa za rangi za dhahabu ya kupaka, viwambo vya kompyuta za aina ya Olekaboni vinameremeta ovyo. Mende mkubwa anakata hewani kuelekea jikoni.


(…)

Kaka Bambam na Prof Bombomu wamekaa ukumbini wanaongea.

PROF BOMBOMU  (akiwa amevaa kizungu, pamba ya mikunjo safi, sandozi za ngozi ya tembo, manukato ya Ufaransa ; amekania shati vizuri sana, nayo inatoka Swizelandi, mkononi amevaa saa ya Rolexi) — Mimi nakwambiaje, muhali si zohali ! Umesikia ? Nimesemaje hapo ?
KAKA BAMBAM (akiwa amevaa kaptula, fulana Fly Karagosi, na slipa miguuni) — Muhali si zohali !
PROF BOMBOMU — Enh enh ! Naomba kufuta basi ! (anafuta) Hivyo, tufanye chapu chapu, unajua wazungu wale walisema…. Walisemaje ? enh enh… nyuzi mbili, bwana ! Nyuzi ngapi ?
KAKA BAMBAM (amekaa ndani ya kocha huku amepiga nne) — Mbili…
PROF BOMBOMU — Eee wala ! Sasa unaniambiaje ? enh ! Sijui nazi zimwe ? Sijui makaa zimwe ? Sijui matunda yametumburujika… Ahh ! Nenda huko katika msitu asiliya ile basi, si unakumbuka ? Sasa ndo msimu wa mapukutiko, nenda basi ukacheki kama zile fruti zinapati…
KAKA BAMBAM — …msitu umefyekwa zamani, mzee.
PROF BOMBOMU — Khaa ! Hii hujuma ya wazungu tena. Wao ndio wametuzidishia nyuzi mbili tena, hivyo tumepata nne sasa. Tutakwenda wapi ? Hawa wametumalizia mali zote, halafu wanatuchafua vibaya ! Hewa ya ukaa na kaboni, wao ! Tindikali ndani ya bahari, wao !… Halafu walikuja zamani, mie namkumbuka… nani huyo ? eti mwalimu Johnson, si unamkumbuka yule bwana ? Basi siku ile kwenye kongamano kuu niliyoiongoza mimi, katuambia sisi Waafrika tusizae, umesikia ? Alisema sisi Waafrika hatuzai kwa maana tunabwagala ! Umesikia hapo, tunabwagala… mshenzi mkubwa sana huyo, kwani sisi panya ?
KAKA BAMBAM  (akitikinyika, slipa inamtoka) — …kama buku, mzee ! (akicheka)
PROF BOMBOMU (hapo amekunja uso) — Acha mas’hara bwana, huo si mchapo, unachekani ?
KAKA BAMBAM (sasa ameushumburua mdomo) — Ah… nawakumbuka wale buku tuliokuwa tunawasaka sana zamani… tulifaidi sana msosi huu… mmm, kwa mchuzi ! Hawa wadudu wamepotea kabisa siku hizi…
PROF BOMBOMU — Hayo yote nimeshasema mimi, wee nenda kwenye tovuti…
KAKA BAMBAM — Siku hizi hatuna mtandao, mzee… unajua umeme taabu…
PROF BOMBOMU — Vitabu vyangu vipo !
KAKA BAMBAM (sasa amejipweteka ndani ya sofa) — Unajua karatasi imeisha… tunasubiri mikalatusi kutoka Uarabuni…
PROF BOMBOMU — Mpango wa kizungu huo, nakwambia, wametukalia mguu wa kausha hawa, tusimame tisti, tuwe macho…
KAKA BAMBAM — Lakini katika makada yetu wengi wana mtoto wa jicho, mzee… macho yao yanafanya kama kiwi… tayari wanatutusa katika giza…
PROF BOMBOMU (akisema huku ameghadhibika sana) — Tumevamiwa, tumevamiwa ! Ubeberu unarudi ! Mpaka macho yetu wanatuharibia ? Lakini sisi tuna utamaduni wetu, umesikia ? Sisi si wazungu, wacha na michezo yao ya makashkuli, wao wanataka kutonesha kidonda, eti uzazi wa mpangilio… na hawa ndio watoaji mimba, halafu si hufunga ndoa ya kijinsia ! Na wengine bado wanakuja kwetu kuchuuza mbinu zao za kuzuia mimba, zile koili ni nini ? enh ? na hizo dawa homoni na mambo mengine machafu… Akhh, sisi utamaduni wetu kuzaa, twend’zetu tukazae basi… »

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni