31/01/2016

Msanii wa fasihi na kipaji chake


"Kuandika mchezo wa kuigiza ni kuumba sanaa. Na sanaa hukataa maelezo ; kamwe haitaki sheria" Ebrahim Hussein.


Imekuwa dhahiri kwamba katika fasihi hakuna usawa. Kuna fasihi bora na fasihi uchwara. Pengine tunaweza kubainisha kigezo kikuu kimoja katika kulinganua fasihi katika matokeo yake na jinsi waandishi wanavyopambana na uhalisi wa mambo. Kuna wale wanaoelezea vitu vilivyo duniani kama vilivyo, bila hata kuvigeuza kimawazo, ambao huchukulia mazonge na matukio ya maisha yetu kama yalivyo bila hata kuzidisha chochote. Imekuwa kama dunia haina siri. Hakuna kitandawili cha kutegea. Vitu vyote vya dunia vinavyotajwa na kukaririwa na mwandishi katika riwaya yake huchukuliwa moja kwa moja kana kwamba binadamu asingekuwa na kipaji cha kusaili misingi ya mashiko ya dunia. Mbuyu ni mbuyu, samaki ni samaki, ndege ni ndege. Mwandishi atajitahidi pengine kuainisha baadhi ya samaki na kutaja wale wanao faida katika tungo yake, iwapo kwa mfano mhusika wake ni mvuvi. Kuelezea tajiriba au uzoefu wa mvuvi katika shughuli zake zote inataka mwandishi aimudu istilahi fulani katika mawanda hayo ya maisha ya binadamu. Lakini kuainisha jodari na kibua ni katika ustadi wa mtu yeyote mwenye kuvutwa na uvuvi. Hivyo mwandishi hajaonyesha ustadi wala ubora wake katika sekta ya ubunifu ikiwa amejisabilia kutaja uelewa wake wa kitu fulani bila hata kuonyesha kwamba kile kitu kinatakiwa kufasiriwa kiumbuji.

Ina maana kwamba uhalisia katika fasihi si kitu cha kutilia maanani kama haujazidiwa na kiwango fulani cha udhanifu. Mwandishi maarufu Marcel Proust (1871-1922) ndiye aliyepiga hatua kubwa katika juhudi za kuinua ubora wa fasihi hadi kilele cha ubunifu. Ndiye aliyejenga msimamo mpya katika mapokeo ya fasihi kwa kusisitiza kwamba mwandishi bora hana budi kupenyeza mtizamo wake katika nususi ya mambo. Kwa maana nyingine, mwandishi bora lazima avuruge maudhui yaliyomo katika dhana hiyo ya uhalisia. Ufundi wake ni kufinyanga, kuchonga na wakati mwingine kutibua mapokeo ya lugha. Kwa mtu wa kawaida pakacha ni kapu lililosukwa kwa makuti ya mnazi. Lakini kwa mwandishi bora wa riwaya pamoja na kwamba ni kitenga kile kilichofasiliwa vile katika kamusi, pia ni kitu kingine ambacho mwandishi pekee, kutokana na satua yake katika kuvuta ilhamu au pia uwezo wake wa kufuga hisia za kila aina, basi atakuwa na umahiri huo wa kukitafsiri vingine hadi kukisawiri upya.


Marcel Proust anadhihirisha kwamba mwandishi mzuri ndiye anayeshinda kuonyesha kwamba kile kitu anachoelezea katika mtiririko wa mikasa ya tungo yake lazima kiwe adimu ili msomaji akichukulie kama tunu ambayo haibadilishiki. Kwa mfano kusema kwamba samaki huyo aliyevua mvuvi Kirovi anaitwa jodari si picha ambayo inaweza kukidhi mahitaji ya msomaji kwa kuwa haitimizi vigezo vinavyotakikana katika fasihi bora. Mfano mwingine, kama nsese yule aliyeelezewa na Mohamed Suleiman katika riwaya yake « Nyota ya Rehema » ni ndege yule ambaye tunamfahamu sisi, yaani mimi na wewe msomaji, basi ina maana kwamba mwandishi hajafaulu kubuni taswira ya kuweza kuweka dondoo hiyo ya matini yake katika mawanda ya fasihi.

« … (Rehema) alipokuwa mtoto katika nyumba ile ile, na uwanja ule ule, mahaba yake yalikuwa ndege. Alikumbuka jinsi alivyokuwa akiwazowesha uwanjani pao kwa chenga za mchele na mtama, ndege wa kila aina, tokea msese mwenye kia refu pamoja na wakeze wasiokuwa na ibadi, hadi makundi ya tongwa na zuwardi. Na bado alitamani kuviona vinyama vyenye mbawa vikipitapita chini yake, vinyama vya kijitukizima…. » Nyota ya Rehema, uk. 102.

Lakini kama mwandishi amewahi kufinyanga ndege yule kwa kusanifu kitu kingine cha kuletea shani au ibra — jambo la kushangaza ambalo sisi wasomaji bila shaka tutashtuka nalo — basi tunaweza kusema kwamba kitu cha ubunifu kimepatikana. Rehema katika riwaya ya Mohamed Suleiman anakumbuka ndege aliowazoesha zamani, lakini ndege hawa wanamsisimua hisia gani ? Wanamweka katika hali gani ? Nini maono yake ambayo yatakuwa tofauti na mhusika mwingine au msomaji mwenyewe ? Kwa mfano mbayuwayu kutoka katika shajara ya mwandishi Mswisi C.F. Ramuz (1878-1947) — ndege huyo hutukabili katika maisha yetu tukiwa kwenye roshani ya nyumba zetu kwa kuwa hujenga kiota chake kwenye vipenu au chini ya milizamu ya majengo ya wanadamu —, basi ndege huyo atatudhihirikia kama kiumbe mwingine akisawiriwa na mwandishi halisi :

« Mbayuwayu wametangulia kufika, wanacheza juu ya uso wa ziwa ambalo sasa limechachuka. Kwa wepesi wao usiokuwa na mashiko, wanateleza katika hewa tuli kwa vikundi vikundi vinavyopendana, mara wakijifanya kutua hadi kugusa viwimbi vya maji, mara wakipaa juu kwa kuchapa hewa kwa mbawa zao, vitu vidogo vyeusi na vizuri vinavyoucheka upepo na maji huku vikipurukusha hali ya hewa. Havina kitu ila kasi yao, harakati zao za kuruka mbio mbio na hizo zinatosha. Angalia michezo yao ya kudeka na kujitapatapa huku na huku kwa uchangamfu, jinsi vinavyokutania, wewe kiumbe maskini ambaye umepaswa kusota chini katika tope mithili ya nyoka ya Eva. Havijinyimi nafasi ya kukumbatiwa na kimande kinyevu, mara vikiganda mbinguni mara vikiwayawaya kama jani lililopeperushwa na upepo. Vinakucheka, kwa kukucheka wewe mlimwengu uliyegongomelewa katika ardhi tasa, vinakucheka wewe ambaye asilani hutawahi kutamwa na raha hiyo ya kukatisha hewa kwa kupiga mbawa. » C.F. Ramuz, Journal, 13 mai 1897 (Shajara, 13 mai 1897)

                       

Kinyume na Suleiman Mohamed katika dondoo nililotaja hapo juu, Ramuz anaangazia ndege kwanza — kitu ambacho S. Mohamed amekifanya naye pia — kisha anavuta taamuli yake ili kutujengea picha ambayo ni ya kigeni kwa uelewa wetu wa kawaida. Picha hiyo mpya itakuwa na nguvu ya kubadilisha maono yetu tuliyo nayo juu ya mazingira ambayo hadi siku ile tuliposoma kitabu hiko tulikuwa hatuna habari nayo. Dhima kuu ya fasihi imetimia hapo kwani ubunifu umetuzindua kwa kutukomoa kutoka kwa fadhaiko na uzoefu wa kijinga. Mwanariwaya mzuri ndiye yule anayebainisha vipengele vya maisha yetu ambavyo vilishinda katika hali ya gubiko kwa kuwa tulikuwa hatujapata zinduko hadi hapo.                                


Kwa tabia yake na nyenzo zake, huwa tunasema kwamba mwandishi ni mtu mwenye kipaji kikubwa, ilhali kipaji chake hakipo katika ufanisi wa akili zake, bali hasa katika hisia zake na mielekeo yake ya kugusia yale yanayomkumba yeye peke yake. Sisi katika maisha yetu ya kila siku, pengine kwa sababu tumeelemewa na shughuli na mazonge mengi, hatujali ndege hawa. Wala hatuna raghba yoyote nao. Kinachomvutia yeye mwandishi, si ukweli wa mambo, jinsi unavyoibuka katika nyanja mbalimbali kama vile sayansi au bayolojia ya ndege, bali ni undani wa mambo. Anachotaka ni kudadisi na kuchambua kila kitu kutoka ndani ili kufichua kiichofutika chini ya gombo la mashiko. Anacholenga hasa ni kukomboa uzuri uliofungwa ndani ya vitu kutokana na matumizi mengi ovyo ya kijamii yaliyosambaratisha vitu vile pamoja na lugha ya kawaida inayotia unajisi mwingi katika msamiati. Marcel Proust hana tamaa hiyo ya kuweka miongozo ya fasihi wala hana lengo hilo la kutunga nadharia nzito. Alikuwa si mtu wa kujishaua kama mwanazuoni. Alikuwa hana imani hiyo ya watu wa siku hizi katika nadharia. Alikuwa kama Ebrahim Hussein niliyetaja juu ya makala yangu, kwake sanaa hukataa maelezo na sheria. Hata hivyo riwaya yake imejaa madokezo kuhusu fasihi. Katika kitabu chake maarufu, msimulizi anatuongoza katika kuelewa vizuri msimamo wake kuhusu fasihi bora. Anasema kwamba mhusika wake anataka kuandika riwaya, naye msimulizi ndipo anapokumbuka kwamba nia hapo haitoshi hadi mtu awe na taamuli na nadhari kubwa :

« Mbali na kanuni hizo zote zinazohusiana na fasihi, ni vivutio vingine vikubwa ambavyo vilinigusia, kama vile paa ya nyumba, mwakisiko wa mionzi ya jua iliyopiga penye uso wa jiwe ama harufu nzuri iliyohanikiza kote njiani, hayo ndiyo yaliyonisimamisha nikawa nimetaanisika, navyo vivutio vilinialika niende kuvikabili nikavipakate kwa sababu vilinidhihirikia kama vilificha kitu ambacho sijawahi kuona bado, licha na juhudi zangu za dhati ambazo hazijafua dafu kuvumbua siri zake. Lakini kwa kuwa nilihisi kwamba siri hiyo ilikuwemo ndani ya vivutio vile, basi nilisimama cheni, huku nikiangalia, huku nikivuta pumzi, huku nikijitahidi kuvuta mawazo kwa kuyapeleka mbele ya picha au nje ya harufu nilikuwa nazo. » Marcel Proust.


Marcel Proust asingesisitiza nguvu hiyo ya hisia na uzito wa mguso katika mchakato wa kubuni fasihi — mbali na kupurukusha nadharia ya fasihi — kama asingezingatia kigezo kingine muhimu ambacho ni chocheo kikubwa katika kuvuta ilhamu ya mwandishi, nacho ni ukumbusho. Mwandishi bora si lazima awe na akili nyingi, kwa maana ya kujua mambo mengi — kwa mfano si lazima awe na taaluma au ujuzi katika uwanja wa uhakiki wa fasihi, mathalan ajue kutofautisha maana ya tashihisi na takriri — bali ni mtu mwenye kipaji cha kuungaunga mtiririko wa vituko vilivyomtokeza katika maisha yake na kuvisuka kupitia hulka, mienendo na tabia yake. Na jinsi anavyofuma na kufumua mtiririko huo haiambatani na upeo wake wa akili bali inategemea vile atakavyochochea hisia zake, hasa katika kuunganisha vituko na mikasa vyote vilivyomkumba. Hapo ndipo inasisitizwa uzito wa ukumbusho kuliko ufanisi wa akili kwa sababu hisia hazina msimamo imara wala haziongozwi na akili ya mtu bali huibuka ghafla katika muktadha mahususi. Kupatwa na harufu fulani, kukutana na sauti ya ndege, kuonja ladhaa fulani na kadhalika ndiyo matukio ambayo yana uwezo wa kusisimua ukumbusho wa mwandishi papo kwa papo bila hata kuelekezwa na akili zake.

                                                                                                              
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni