08/03/2016

Kutunga fasihi katika lugha ya kigeni


Kuandika kazi ya fasihi katika lugha ya kigeni ni jambo la kawaida kwa waandishi wengi katika dunia nzima tangu zamani ya kale. Mashairi ya kijapani huandikwa kwa kutumia herufi nyingi za kichina na waandishi maarufu kutoka nchi hii hawakutumia lugha yao ya kuzaliwa ili kutunga vitabu vyao. Ulaya nako pia hadi karne 15, waandishi wote walitumia lugha ya kilatini ambayo ilikuwa si lugha ya kienyeji. Kote Ulaya tunakuta mifano mengi ya waandishi maarufu, kama vile Franz Kafka (1883-1924), Elias Canetti (1905-1994), Joseph Conrad (1857-1924) na siku hizi Milan Kundera ambao huandika katika lugha ambayo hawakuzaliwa nayo. Mwanafalsafa Emmanuel Levinas (1906-1995) ambaye aliandika vitabu vyake vyote kwa kifaransa alikuwa na asili ya Lithuania. Alikuwa ni mzoefu wa kilithuania, kijerumani na kiebrania ambazo alizotumia katika maisha yake ya kila siku. Wengi katika wasanii hawa walikiri kwamba kuandika katika lugha ya kuzaliwa ni kama kujilemaza wakapendelea kutumia lugha nyingine ya kigeni. Kuandika katika lugha ya kigeni ina manufaa mengi kwa kuwa mwandishi hujikuta amejitenga na « malimwengu », hususan visa na mikasa ya kisiasa, uzoefu wa kuishi katika jamii moja ambayo inahujumu uvumbuzi na wakati mwingine kukandamiza kipaji cha ubunifu. Kwa kutumia lugha ya kigeni, mwandishi hukwepa yale mazonge yanayomduru kichwani mwake akawa amejitenga pembeni na nukhsi za kuishi sasa hivi katika jela ya umimi wa hapo alipo.
                                                         

Mwana falsafa na sayansi Roger Bacon (1214-1294) ambaye alivumbua mambo mengi alikuwa anatumia kilatini, kama wanazuoni na « wadhani » wote wa Ulaya katika enzi zile, ambacho kilikuwa si lugha ya kienyeji wala lugha ya mama, bali kilikuwa lugha ya kigeni kwa kila mtu. Bacon aliwahi kuandika kwamba lugha za kienyeji kama vile kiengereza na kifaransa, kwa enzi zile, hazikukamilika cha kutosha kiasi cha kuendeleza kazi za mantiki alizokuwa anazishughulikia. Lugha za kienyeji zilichukuliwa hazitoshi kidhana ili kusanifu aina ya hoja ambayo si kufu ya chombo cha mawasiliano cha kila siku. Mfano huo unatusisitizia kwamba lugha za mawasiliano, kwa sababu zimepungukiwa dhana na mantiki za kuweza kujenga nadharia ya kisayansi na kifalsafa, mbali na kuwa na upungufu na dosari katika muundo wa kisintaksia na mpangilio wa maneno, basi zilikuwa zina faida katika kuelezea shughuli za kila siku tu, wala si kazi zake kuchangia au kuinua akili tambuzi za kuweza kubuni dhana mpya. Lugha ya mawasiliano ni lugha ambayo aghalabu imejaa utondoti na uzohali katika uvumbuzi. Si lugha nyeti yenye msamiati sahihi.

Kwa mujibu wa maelezo mengi ya waandishi hawa, inahesabika kwamba lugha ya mama ni lugha ambayo inatuteka kwa kutushughulisha kila wakati kiasi cha kutuhangaisha tusiwe na hiari ile ya kuipima vizuri. Sio kusema kwamba lugha ya mama haifai katika kutunga kazi ya fasihi lakini waandishi hawa hudai kwamba ni vigumu zaidi kubuni katika lugha hiyo kwa kuwa lugha ya mama imo katika ung’amu fiche. Kwa kuwa ni chombo tunachotumia kila siku hatuna mkabala ule wa kuitathmini kama ipasavyo. Lugha ya mama inatukomea ndani ya maumbile yetu. Canetti anaeleza vizuri kwamba ilimpasa atumie lugha ya kijerumani ambayo si lugha yake ya kuzaliwa ili kuandika kile alichokuwa moyoni mwake na hivyo kukwepa kukabiliwa na maajaliwa ya kuishi na lugha moja tu. Vyovyote vile, iwe lugha ya mama au lugha ya kigeni, kikubwa ni kuimudu lugha kisanaa, kitu ambacho inabidi jamii ijijengee mazingira mahususi ya kuwapatia waandishi asasi tajiri ya elimu, iwe kupitia familia yenye utamaduni wa kusoma au kupitia jamii kwa jumla yenye shule za kuaminika. Familia na shule ndizo asasi kuu katika jamii ambazo husisimua mshipa wa kutaka kusonga mbele katika kuinua lugha isiwe chombo cha mawasiliano simulizi tu. Tukisoma shajara ya waandishi hawa niliowataja, tutakuta maelezo mengi kuhusu mazingira na athari zake chanya katika kukuza kipaji cha mwandishi chipukizi.


Kwa mfano Samuel Becket (1906-1989) anaelezea kwa nini alijipendekeza kutunga baadhi ya vitabu vyake kwa kifaransa. Kwake kufikwa na hamu kubwa ya kutunga vitabu katika lugha ya kigeni ilimtokea baada ya kutunga vitabu vingi katika lugha ya kiengereza na baada ya kufikwa na hisia fulani hadi ikawa aliona kwamba lugha yake ya kuzaliwa (kiengereza) ilikuwa haitoshelezi mahitaji yake yote hasa katika mawanda ya usanii. Ni kama kusema kwamba hakuna lugha kamilifu. Hapo ni wazi kwamba Becket, ambaye ilimdhihirikia mapema kwamba lugha ya kuzaliwa ni aina ya kitanzi anachotiwa mtu wakati wa kuzaliwa kwake, basi alishinda kuikata kitanzi hicho. Kwa kifupi akasema kwamba ameshindwa kutumia kiengereza kwa sababu ya kuwa na uzoefu mwingi nao, kitu ambacho kinamzuia asiwe na tambuzi ya kutosha katika mchakato wa kutunga tungo la ubunifu. Uzoefu wa kiengereza ukawa ni pingamizi kwake akaamua kuponea kifaransa. Ni jambo la kushangaza kwa yeyote ambaye hutumia lugha yake kila siku huku akiwa na imani kubwa kwamba hakuna ustadi ulioimarika zaidi kuliko ule unaohusika na lugha ya kuzaliwa, ilhali ni dhahiri kwamba kuitikadi vile ni kusahau kulinganua vidato viwili vya lugha, yaani lugha bunifu — hususan fasihi — na lugha chombo kinachotumika hasa kwa ajili ya kuwasilisha au kufikisha ujumbe kwa jamii husika.


Elias Canetti ambaye alipata tuzo ya Nobel mwaka 1981, alizaliwa Bulgaria akapata uraia wa Uingereza baada ya kuishi miaka mingi Uswizi. Aliandika katika kitabu chake « Himaya ya binadamu » (Die Provinz des Menschen - Aufzeichungen 1942-1972) : « Lugha ambazo angepaswa kujua kila mtu ni kama ifuatayo : kwanza, ile lugha aitumiayo na mama yake ambayo angeitupilia mbali akiwa ameshabaleghe ; pili, lugha nyingine ile kwa ajili ya kusoma tu ; tatu, lugha nyingine ya kutumia wakati wa kusali ambayo haieleweki kwake ; nne, lugha nyingine ya kumsaidia ashughulikie pirika zake zote za kibiashara kama vile kupiga hesabu, kuendesha uchumi wake kwa jumla ; tano, lugha ambayo angeitumia ili kuandika maandishi yote isipokuwa barua zake ; sita, lugha nyingine ambayo angeitumia wakati anaposafiri ikiwa ni pamoja na kuandika barua zake ». Maelezo hayo yanathibitisha kwamba lugha ya kuzaliwa ilikuwa haina uzito kwake. Na kweli katika maisha yake Canetti alikuwa anatumia kibulgaria akiwa anaongea na wafanyakazi walioitumikia familia yake nyumbani, na kiromania kila alipotoka nje. Lakini lugha ya kiutamaduni ilikuwa lahaja ya kiebrania iliyokogwa na kihispania, licha ya kijerumani ambacho ilimbidi akitumie kila alipozungumzia maswala ya usanii na wazazi wake, na kiengereza katika sekta ya biashara.


Tukizikazia macho yetu Tanzania na Kenya hatuna budi kubaini kwamba ni waandishi wachache ambao hutumia lugha waliyozaliwa nayo ili kutunga vitabu vya fasihi. Sina habari kama Shaaban Robert alikuwa mzoefu wa lugha yake ya kuzaliwa (kiyao). Wakina Kezilahabi, Gurnah, Vassanji, Kitereza na wengi wengineo huwa wana lugha yao ya kuzaliwa ambayo si lugha ya kuandika. Ni jambo ambalo watu wengi hulisahau. Na tukija kugusia swala lingine, hata waswahili wa visiwani na mwambaoni wana lahaja zao na wakati mwingine lugha zao za kienyeji kama vile kimwera, kimatumbi na kadhalika. Huko Kilwa alikozaliwa Ebrahim Hussein, kiswahili kimeingiliwa na maneno mengi yatokayo katika lugha nyingine. Chambilecho « waswahili » wa bara huitikadi kwamba « wabantu » wa pwani wamekopa msamiati mkubwa kutoka kiarabu, kitu ambacho sio kweli hata kidogo. Tukigeukia Kenya ambako nako pia asimilia kubwa ya waandishi huandika katika lugha za kigeni, ndiye Ngugi wa Thiong’o ambaye, kinyume na kinachofanyika kote duniani, anataka kuandika katika lugha yake ya kuzaliwa, kitu ambacho kinaonyesha wazi, hasa katika muktadha wa siasa ya Kenya, kwamba ametawaliwa na kasumba au msimamo wa kikoloni. Lakini hilo si jambo la kutilia shaka kwa kuwa Ngugi wa Thiong'o ni mwandishi bora duniani nzima ambaye amewapiku wasanii wote waliotangulia kiamboni mwake na ng'ambu (soma HAPA).


                        

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni