20/04/2016

Uislamu na Ukristo : kweli dini hizi mbili ni ndugu « simba kwa simba » ?


Katika kumshawishi mtu apate kukiri imani ya mtu mwenye dini nyingine, inabidi kuchukua njia zenye mizunguko na hadaa nyingi. Ndani yake kuna uwongo mwingi na laghai kupindukia. Hasa ikiwa dini hizo mbili hazilingani hata kidogo. Nazo Uislamu na Ukristo hazishabihiani wala hazina mtazamo mmoja. Kwa sababu sosholojia na sayansi nyingine ya jamii zimejaa itikadi na siasa, pamoja na kuwa na mkabala wa juujuu, hatuna budi kutumia mbinu na njia nyingine katika kuchanganua maudhui ya dini hizi mbili, nazo ni kusoma vitabu vile vitakatifu, yaani Biblia na Kuran kwa njia ya teolojia (ingawa hakuna teolojia katika Uislamu, ipo kinachoitwa « tafsir » na « kalam »). Hapo katika makala hii ni aina ya teolojia linganishi inayoitishwa wala si mbinu nyingine. Kwa kuwa nimeshawahi kufanya utafiti mwingi kuhusu Uislamu na jinsi watu wengine kutoka dini ya Ukristo na dini za kienyeji (ambazo watu wengi Afrika mashariki huziita « dini za kishenzi » ambazo kwa maneno yakinifu ni dini ya upagani) wanavyosilimu. Miongoni mwa makala zangu, moja muhimu inapatikana HAPA (kwa kifaransa). Hapo leo nitahoji maana ya maneno au dhana muhimu chache za dini hizo mbili ili kuonyesha kwamba Waislamu na Wakristo hukengeuka wakati wanapokutana ili kujadili dini zao husika. La kutilia maanani hapo ni nadharia tete ya kimantiki ifuatayo : tutashindwa kuendeleza uelewa wetu wa dini ikiwa hatujasaili kwanza maana halisi ya maneno tunayotumia wakati tunapozungumzia dini hizo.

Ushirikiano au mikataba ?

Dini ya Ukristo, kihistoria, ni Ushirikiano baina ya jamii fulani ambayo watu wake wanaitwa Wayahudi na Mungu. Na Ushirikiano huo au, kwa jina lingine Agano, si mkataba kwa sababu jamii hiyo imeteuliwa na Mungu, ikapatikana ushirikiano huo kwa wakati wake. Ndiyo maana Ukristo ni dini iliyopo katika historia ya wanadamu ingawa historia hiyo pia ni aina ya Ufunuo. Ushirikiano huo ni aina ya uhusiano kwa sababu Mungu amewaandama watu wake huku akiwa amejifunua kama Mwokovu. Imani hiyo kubwa katika dini ya Ukristo haikubaliki katika dini nyingine, hasa katika Uislamu.

Katika Uislamu, hatuna Ushirikiano bali tuna mikataba (kiarabu mîthâk). Mkataba wa msingi unapatikana katika Kuran (7-712 ; 2-27) ambao unadai kwamba Adam alipofinyangwa na Allah alikuwa Mwislamu. Kutokana na imani hiyo wanadamu kwa jumla ambao walikuja baada ya Adam wanachukuliwa wote ni Waislamu, na mitume na manabii wote nao pia walikuwa ni Waislamu kutokana na maumbile yao (kiarabu fitrah). Katika hawa tunakuta Isa, Musa, Ibrahim, Lut, Ismael, Daud, Suleiman, na kadhalika. Wengi katika wataalamu wanaotafisiri Kuran huhesabu kwamba, kutokana na hali hiyo, Uislamu ni dini ya ki-Adamu. Hapo tunaona kwamba hakuna Ushirikiano wa kiokovu kwa sababu Mwislamu hawezi kumshirikisha Allah ambaye si mwokovu. Tukisoma kwa kina msahafu Kuran hatupati jina hilo lenye maana kubwa kwa Wakristo ambao wanaongea kiarabu, yaani « Mukhalisi » au « al Fâdî » linalomaanisha « mwokozi ».
                                       Résultat de recherche d'images pour "quran kiswahili"                                

Mungu mmoja ?

Mara nyingi tunasema kwamba Uislamu na Ukristo ni dini ambazo zina Mungu mmoja. Kweli kauli hiyo ni sahihi ? Nini maana yake ya mmoja ? Na kauli hiyo inakubalika kimantiki au kihesabati ? Na kweli endapo tunaangazia imani yetu kutoka nje hatuna budi kukubali kwamba dini hizo zina imani ya Mungu mmoja, yaani Mungu pekee. Lakini kwa juujuu, kwa kupekua dini hizo ahlan wa sahlan tu ! Sababu yake ni wazi : Wakristo wana mkabala wao wa kipekee ambao si ule wa Waislamu. Tuwasikilize Wakristo : kwanza, Wakristo husema kwamba Mungu ni Imanueli (‘ibn’Allah), yaani Mungu pamoja nasi, imani ambayo ni ya kuchukiza kwa Mwislamu (Mt 1 :23 : « Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi ».). Kwa sababu hiyo, Ukristo ni dini ya uokovu. Mwamini Mkristo yumo ndani ya Mungu, katika moyo wake, wakati Mwislamu yupo mbele ya Mungu, ambaye yuko mbali na waamini wake. Mkristo si « mtumwa » wa Mungu (‘abd’Allah) kama ilivyo katika Uislamu bali ni rafiki (Yh, 15, 15 : « Siwaiti tena watumwa ; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake ; lakini ninyi nimewaita rafiki ; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu ».) Pili, imani ya Utatu, ambayo ni imani ya msingi katika Ukristo (ingawa wakristo wa madhehebu kadha hawana imani hiyo), haieleweki kwa Mwislamu. Haieleweki kwake kwa sababu mbili :
 • kwanza katika kiarabu hakuna neno lenye kubeba dhana ya utatu ambayo kilatini peke yake (au lugha za enzi za Yesu Kristo) huibeba. Kwa kilatini neno « persona » ndilo linalotumika ili kuelewa dhana hiyo ya utatu. Hutafsiriwa mara nyingi kwa kutumia neno « nafsi », jambo ambalo si la kuridhisha. Ithibati ya kuthibitisha kwamba Waislamu hukosea wakati wanaposema kwamba imani hiyo ya Utatu ni namna ya kushirikisha Mungu tunaipata katika lugha ya kiarabu kwanza, kwa kuangazia jinsi inavyotumika katika dini ya madhehebu mbalimbali ya Ukristo wa nchi za Mashariki. Wakristo wenye lugha ya kiarabu husali kwa kiarabu na hutumia kila siku neno mahususi ili kutafsiri dhana ya ‘persona’. Katika ibada yao, wao hutamka « Nasadiki kwa Mungu mmoja, Baba Mwenyezi, Mwana na Roho Mtakatifu, Mungu mmoja katika akanim tatu ». Akanim (moja uknuum) ni neno ambalo linatoka katika kiaramu ambacho ilikuwa ni lugha ya Yesu Kristo (si neno la kiarabu kwa kuwa kiarabu hakina dhana hii). Kwa kifupi, kuamini Utatu ni kubaini kwamba Mungu ni mmoja lakini kwa kuongeza kwamba umoja wake umeingiliwa na « uanuai » fulani. Kwa sababu Mungu ni kielelezo cha uokovu, upendo, na ushirikiano (au Agano). Vinginevyo Mungu angekuwa ni hakimu mkuu tu mwenye nguvu nyingi isiyobadilika na wafuasi wake wangekuwa ni watiifu tu, vipengele ambavyo kwa kweli vinatimiza maana ya Allah kwa Mwislamu. Mkristo naye ana uhusiano wa kina na Mwenyezi Mungu kwa sababu Mungu ni ushirikiano katika « uanuai » (hapo ndiyo maana ya komunyo au karamu takatifu).
 • pili kwa sababu hakuna, katika nchi zenye Uislamu kama dini ya watu wengi, taasisi au vyuo vikuu ambapo watu wanaweza kusoma dini ya Ukristo kwa undani na uketo mwingi kama ilivyo katika nchi zilizoendelea. Hakuna katika nchi hizo kozi inayoitwa Ukristolojia wakati katika nchi za magharibi Wakristo wanaweza kusoma Uislamulojia. Ndipo katika nchi hizo pia za Magharibi ambapo mtu ana uhuru wa kuamini na kusoma dini au madhehebu yoyote ya dunia nzima. Katika nchi zenye Uislamu ambazo huzipiga marufuku dini nyingine zote, kusoma Biblia au msaafu wowote usio na uhalali wala maudhui ya kiislamu ni kujitia hatarini. Kwa mfano, Ukristo na dini nyingine, katika nchi nyingi za kiislamu ni dini zinazopigwa marufuku na waamini wake ama wanateswa kila siku, ama wanauawa. Katika nchi hizo ujinga na ubwege kuhusu tamaduni na dini za mapokeo na imani nyingine hauna kikomo.

« Dini za kitabu » zilizodhihirishwa kwa kuletwa na Mungu ?

Tuna kawaida ya kusema kwamba Ukristo na Uislamu zimeletwa na Mungu. Hapo tena lazima tujiulize, mchakato huo unaoitwa ufunuo, je kweli ni sawa katika dini hizo mbili ? Tuwe makini na waangalifu kabisa. Tuchambue kwanza swala hilo katika Ukristo. Kama nilivyosema hapo awali Ukristo ni dini ya ushirikiano baina ya Mungu na wanadamu. Ina maana kwamba Yesu Kristo ndiye aliyetimiza utabiri wa manabii wa kale ambao wanapatikana katika Agano la kale. Mwenyezi Mungu alijifunua kidogo kidogo katika historia ya wanadamu. Biblia kwanza ni mkusanyiko wa hadithi ambazo zimeandikwa kwa kalamu ya binadamu akiwa na ilhamu ya Roho Mtakatifu. Biblia si maneno ya Mungu bali ni maneno ya Mungu yaliyoingia katika maumbo ya binadamu, kwa maana ya kwamba mafundisho ya Mungu yalipokewa na wanadamu wakati fulani katika jamii fulani kutokana na msuko wa visa fulani. Mwenyezi Mungu ameshirikiana na wanadamu ili kuleta habari njema. Wakristo si watu wa kitabu ingawa wanacho kitabu kinachoitwa Agano la kale na Agano jipya. Lakini kitabu hicho hakitoshi kwao kwa sababu Mungu yungali hai. Wakristo ni watu waaminio Yesu Kristo kabla ya kuamini kitabu chao Biblia. Ndiyo maana kwamba Wakristo wanapaswa pia kufuata amri na mafundisho ya Mkuu wa Kanisa (Papa) ambaye ni mwakilishi wa Kristo duniani. Ufunuo katika Ukristo haukuwaangukia wanadamu bali uliwadhihirikia kupitia Roho Mtakatifu kwa wakati wake. Ndio ufunuo ulioingia mwili wa binadamu. Na sisi Wakristo tunaposoma Biblia tunapaswa kuzingatia kwamba matukio yote ya Biblia ni aina ya ushahidi ya uwepo halisi wa Mwenezi Mungu duniani tangu zamani ya kale hadi leo.

Kinyume na hayo, inaaminika kuwa Kuran ni maneno ya Mungu yaliyoshushwa moja kwa moja kupitia jibril juu ya Mtume Mohamed aliyekuwa mtu ummi (si msomi wa dini yoyote). Uislamu pekee ni dini ya kitabu kilichoshushwa (mchakato huo unaitwa tanziil kwa kiarabu) kutoka katika kitabu kingine kilichopo kwa Allah, nacho kinaitwa « mama ya Kitabu » (um’ al kitab, kwa kiarabu) na kimehifadhiwa kwenye « meza takatifu ». Na inaaminika kwamba kitabu hicho Kuran hakikushushwa mara moja tu kwa kuwa vitabu vingine vinachukuliwa vilishashushwa kabla ya Kuran kuletwa. Waislamu huamini kwamba mitume wengine ambao ndio wanawaita kwa majina ya kiarabu Adam, Nuh, Lut waliwahi kuletwa maneno ya Mungu kwa njia ya mdomo tu wala si kupitia maandiko. Wengineo pia kama vile Ibrahim, Musa, Dawud na Isa huchukuliwa ndio walioletwa vitabu au karatasi ambazo hazikuhifadhiwa. La nyongeza hapo ni kwamba Waislamu husema kuwa Isa ndiye mtume aliyewahi kuandika kitabu kiitwacho injil (ikiwa ni moja tu), kitu ambacho kinathibitisha wazi kwamba Isa si Yesu, kwa sababu Yesu, kwa Wakristo, hakuandika chochote.

Kwa kuwa Kuran na Biblia si vitabu vyenye vipengele sawa vyenye hadhi sawa, namna ya kusoma vitabu vile pia si sawa. Mwamini akisoma Biblia hutumia mkabala wa kihistoria, ambao si mbinu unaoeleweka kwa Mwislamu. Mkristo anajua kwamba Biblia ni kitabu kilichopo katika maendeleo ya binadamu. Mwislamu naye anatakiwa kusoma Kuran kwa kufuata maneno ya Allah kama yalivyoshushwa kwa kuwa ni usemi wa Allah. Sura na aya zake zote hazibadilishiki wala hazikosoleki. Ndio maana kwamba hakuna fasiri (interpretation) kwa maana ya ijtihad katika kusoma Kuran bali kuna tafsir na kalam (explanation, comments and paraphrases). Wakristo nao wana teolojia kwa sababu hiyo hiyo : Ukristo ni dini ambayo imejaa mafumbo na siri za ajabu ambazo mwamini ana haki na hiari ya kuzisaili na kuzihoji. Hapo tena dini hizo mbili zinasigana kwa kuwa Mwislamu atasema kwamba ni kukufuru Mungu kuchambua siri zake kwa sababu Kuran haiathariki katika historia (Kuran 6, 161 ; 9, 36 ; 12, 40 ; 98, 5). Aidha, Allah ana siri zisizoshikika na zisizotambulika (112,2) na hakuna kiumbe duniani aliye sawa naye (112,4). Isitoshe, kusema kwamba « Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui » (2,216) au « Hakika Mimi nayajua msiyo yajua » (2,30), haina maana kwa Mkristo ambaye inampasa atumie juhudi zake zote pamoja na akili zake ili kuwa karibu na Mungu.

Mitume na Manabii sawa ?

Mara nyingi tunasoma katika makala mbalimbali, hususan katika ngebe za tovuti au katika magazeti mengi kwamba dini hizo mbili zinafanana kwa sababu ya kuwa na baba mmoja Ibrahimu. Hapo pia lazima tujihadhari. Nini maana yake ? Na kweli Ibrahimu ni Abrahamu ?

Kwa wakristo, Abrahamu (si Ibrahimu) amepewa nafasi kubwa sana katika Biblia kwa sababu ndiye aliyeanzisha historia ya Ushirikiano unaozingatia Uokovu ukakamilika katika Agano jipya (kwa maana hiyo kusoma Agano jipya bila kusoma Agano la Kale ni usomaji usiokuwa na maana). Ndiyo maana Abrahamu ni « Baba ya waamini » (« tunaye Baba, ndiye Abrahamu » Mt 3,9). Tukisoma Biblia kwa makini tunakuta sifa zake kadha ambazo hazimo katika Kuran.

Katika Kuran, Ibrahimu hakuanzisha chochote kwa sababu alitanguliwa na Adamu na Nuh. Si sahihi kusema kwamba Uislamu na Ukristo ni dini zenye Baba mmoja kwa sababu Kuran haitambulishi Ibrahimu kama ni mwanzilishi wa imani ya kiislamu. Visa vya Ibrahimu, katika Kuran, ni aina ya « dhikiri » au ukumbusho unaokumbusha ujumbe wa zamani, ule alioushushiwa Adamu kwa mara ya kwanza. Kikubwa hapo ni kwamba Kuran inasema kwamba Ibrahimu amepokea kitabu cha kale (20,133 ; 53,37 ; 87,18-19), kitu ambacho hakipo kabisa katika historia ya Abrahamu wa Biblia. Aidha, Abrahamu hakuenda Makka ili kushushiwa kitabu fulani kama ilivyo kwa Ibrahimu wa Kuran. Hapo tena tukilinganisha vitabu vitakatifu hivi viwili, tunakuta kwamba hatuzumgumzii jambo moja. Huenda ndiyo sababu Waislamu husema kwamba Wakristo ndio walioipotosha (kiarabu tahrif) Biblia, kauli ambayo ina uwiano wa kina na mtizamo wa waislamu unaopania kufuta yale yote yasiyokuwa na uhalali kwao. Hali kadhalika, inawasaidia kujenga msimamo unaokanusha kila kitokanacho katika misaafu mengine. Uislamu, kutokana na msimamo huo, una mwelekeo wa kukuza na kuimarisha itikadi kali zisizolingana na ustawi wa uhuru katika jamii.

Kwa mfano, Uislamu unajidai kwamba unatambulisha mitume na manabii wote waliotangulia na waliokuja kabla ya kuteremshwa kwa Kuran. Kauli hiyo si sahihi kwa kuwa mitume wengi muhimu katika Biblia hawapo katika Kuran, kwa mfano Yeremia, Isaya, Ezekieli, Danieli. Isitoshe, wengi kama Ibrahimu na Isa wamepewa majina ambayo hayahusiani na wahusika halisi wa Biblia. Tukiangalia jinsi Kuran inavyogusia visa vya Isa, ambaye Waislamu wanaoamini kwamba ni Yesu, pia tunavutwa kwanza kwa kugundua kwamba kweli Kuran inakiri baadhi ya sifa ya Yesu lakini tunapoendelea masomo yetu tunang’amua kwamba Kuran inatupa kisogo, hasa juu ya sifa muhimu zinazohusiana na utambulisho kamili wa Yesu. Kwa Mkristo, Yesu ana hali mbili, ubinadamu na uungu, sifa ambayo imekataliwa na Waislamu (wao wakisema kwamba ni imani potofu). Tukizidi kubobea katika kusoma Kuran, huku tukijaribu kujua zaidi kuhusu Yesu, mara tunajiuliza : kweli Kuran inazungumzia Yesu Kristo ? Kwa nini Kuran inatumia neno Isa wakati kwa kiarabu, Jesus au Yesu, ni Yasu ? Katika makanisa yote ya madhehebu ya kisiria au kimaroni, Wakristo wote hutumia neno Yasu kwa kiarabu. Kwa nini Kuran haikutumia neno hilo ? Isitoshe, Kuran inasema kwamba Yesu hakusulubiwa juu ya msalaba wala hakufufuka. Aidha, katika Kuran tunakuta visa ambavyo havipo katika Biblia. Kwa mfano Isa anarusha ndege wa udongo aliyefinyanga (5, 110) na anazalisha kijito cha maji kwenye shina la mtende ule unaochukuliwa na Kuran kuwa ndiko alikozaliwa (19,24). Taarifa hizo hazimo ndani ya Biblia. Hivyo, ama habari hizo zinamhusisha mhusika mwingine (Isa) ama ni habari za kughushi ambazo hazilingani kabisa na Yesu (au Yasu).

Yapo mambo mengi mengineo ambayo yangepaswa kuchambuliwa hapo. Kwa mfano, Musa si Moses, Mariam si Maria, na hali kadhalika. Uislamu ni dini ya kipekee ambayo ilitokeza wakati fulani katika nchi Arabia. Ni dini ya watu walioishi katika jangwa ya Arabia ambao kabila lao ni Wabedui. Kinyume na dini ya Ukristo, ambayo ilikuwepo Afrika kabla ya bara hiyo iliposhambuliwa na Waarabu na Wazungu (Ukristo wa Ethiopia, nami nashukuru sana kwa kujifunza mengi kutoka dini hiyo), Uislamu ni dini ambayo inakataa katakata tamaduni na mila za jamii nyingine. Mifano mingi tunayo ya jamii za kiafrika ambazo zilipoteza mila na desturi zao hadi lugha zao ziliposhambuliwa na Uislamu. Kwa mfano jamii ya Wadogon kutoka Mali ilikuwa na imani na dini yake kubwa ya kipagani hadi miaka ya sabini ya karne iliyopita. Siku hizi utamaduni wa Wadogoni umepotea kabisa, si kwa sababu ya ukoloni au utandawazi, bali kwa sababu ya Uislamu. Jamii nyingi mno kutoka Chadi na Sudani nazo vile vile zimeathirika vibaya sana hivi karibuni kwa sababu ya Uislamu ambao unadharau tamaduni zile ambazo si kufu yake.

Maoni 2 :

 1. Nimeipenda makala hii. Inafikirisha na kufungua akili.

  JibuFuta
  Majibu
  1. Asante. La nyongeza kutoka kwako : http://hapakwetu.blogspot.ug/2016/03/dini-ni-siasa-tu-asema-mwandishi-nawal.html
   na hapo : http://hapakwetu.blogspot.ug/2016/02/u-islam-ni-dini-ya-amani.html

   Futa