19/05/2016

Ucheshi katika fasihi ya kiswahili upo ? Merci Mheshimiwa Walibora !


Nakumbuka siku moja nilipokuwa nikiishi Kilwa tuliwahi kwenda, mimi na jamaa zangu, Kilwa Masoko kutazama uchezaji wa mchezo mzuri sana wa Ebrahim Hussein. Mchezo huo uliochapishwa zamani unaitwa « Alikiona ». Basi siku ile, hadhira yote ilikuwa hoi kabisa kwa kucheka, mbavu zikiuma, nami pia niliifurahia sana tamthilia hiyo kwa sababu ilinikumbusha michezo mingi niliyokuwa nimeshaisoma na kutazama katika maisha yangu, kuanzia Shakespeare (1564-1616) hadi Molière (1622-1673, na HAPO msomaji utakuta tafsiri moja ya mtunzi huyo kwa kiswahili), kutoka Rabelais (1483-1553) hadi Oscar Wilde (1854-1900), wala sina haja ya kutaja waandishi wengi wa jana kutoka Uingereza (P.G. Wodehouse, Evelyn Waugh, John Irving) na kwingineko duniani. Fasihi haina mipaka, haina kabila, haina mila, haina rangi. Na fasihi bora ndiyo ile haswa inayotuchekesha.

                

Hapo leo sitazumgumzia uhakiki wa fasihi cheshi kwa kuwa nadhani kwamba hauna maana, wala sioni sababu ya kupiga mbiu ya fasihi hiyo kwa wananchi wengi waishio Afrika mashariki, ila najua kwamba « Waswahili » wa Kongo ndio waliopiku sana katika kutunga aina hiyo ya utanzu wa jukwaani. La kushangaza kwangu ni kuona jinsi Watanzania walivyo ni wacheshi na wachangamfu katika pirika zao za kila siku — hawakosi michapo na mikasa ya kusimulia barazani au kwenye « maskani » za « washkaji » — lakini walivyo « siriasi » kila wakikamata kalamu au wanapotumia kompyuta. Inaonekana kuwa kuandika kwao ni kama kutalii maabadi, kuingia kilingeni (ingawa mimi mwenywe nimeshawahi kucheka sana katika kilinge cha wenzangu wa Pande, Kilwa bara) au kuabudu sijui visanamu fulani. Swala hilo la kuandika ni la kitakatifu. Hacheki mtu hapo !

Waama mwokozi katika fasihi ya kiswahili yupo ! Si Yesu, hapana, kwa sababu amezaliwa hivi karibuni, naye anaitwa Ken Walibora, na sidhani kama atafufuka baada ya kifo chake. Ametutokea Kenya. Si haba, kwa sababu tangu alipoandika « Wakati Ukuta » na « Alikiona », Ebrahim Hussein amekatiza kuandika vichekesho vingine. Ikawa fasihi ya kiswahili ikaingia katika nyumba ya barafu. Poa, kwa sababu akaibuka mzee Walibora. Akatunga Ndoto ya Almasi, wakati wenzake walipendelea kutoa mawaidha na nyaadhi, labda kwa sababu wamejisahau. Au pengine ndoto za waandishi wale hazijatimia ndo maana wamerudi kulala ? Kwa maoni yangu, nahisi kwamba waandishi maarufu wa Tanzania na Kenya, takriban wote, wamefanya hofu ya kupikwa majungu — ingawa jiko la kisasa si mafiga ya mama — na tungo zile za kuchekesha zikaadimika kama pembe za ndovu. Matokeo yake mwandishi akasahau kwamba chipsi hazina ukoko.

                           


Wengine pia wakasahau kwamba kalamu haihitaji vocha kuandika. Isitoshe kazi ya fasihi hailipwi. Na gwiji mwenzangu Walibora kavaa njuga, chapuo tayari kwapani, msondo mkubwa umemsimamia, tayari kutosa mgwisho wake ndani ya kidau cha ucheshi. Hamna takalifu bhana ! Wee ambaa huko kama umemwendea na viongozo vyako, mkwara hauhitaji mafuta. Kwani sifa ya ndege ni mabawa yake ? Yeye ametuletea uhondo mzuri, amejitahidi kufufua ucheshi katika fasihi, si mchezo ! Hilo linatosha, lakini wengine katika magimba ya Chuo Kikuu tayari watakuja na viongozo vyao, hotuba zao, risala zao na watapandisha jukwani kama alivyofanya mzee Masasi katika riwaya Ndoto ya Almasi. Hapo msomaji nimesindika dondoo moja kutoka riwaya hiyo, wakati Almasi, mtoto wa mzee Masasi ameitwa na kukabidhiwa zawadi na mgeni rasmi shuleni :

« (Almasi) alimtazama baba’ake kwenye jukwaa rasmi. Mzee Masasi meno yote ya manjano yalikuwa nje kwa tabasamu ya namna yake. Alitazama upande wa halaiki ya wazazi wa kawaida. Akamwona mama’ake kayaanika meno yote nje. Kijoyo kikamdunda. (…) Akaipokea zawadi kutoka kwa Meya Masika. Alikuwa anaelekea kujiunga na wanafunzi wenzake ndipo alipomwona baba’ake ameamka ghafla na kumkimbilia mkuu wa sherehe. Mzee Masasi akakinyakua kipazasauti kukawa na mzizimo.
« Epu Alimasi mwanangu ngocha kwansa » alisema.
Watu wote wakaanza kucheka kwa mshangao. Almasi alisalimu amri ya baba’ake. Hisia za aibu na hasira zilimkuta.
« Ntiyo. Unakumbuka yaani sauti ilitoka pinguni Yesu alipotoka katika mutoni Yortani, ehe ? Wewe ni mwanao wangu mupentwa, nimekukubali wewe. Hii mutoto ni kama mimi mwenyewe. Mutoto wa nyoka ni nyoka mtoko. Angalia vile yeye anafwanana mimi. Nilikuwa number one kwa mtihani ya Common Entrance kwa shule ya Kiminini ninenteen sasi six »
Watu waliangua kicheko tena. Almasi hakujua uso auweke wapi. » (Ndoto ya Almasi, uk. 37-38)


Ama kweli, himili mzaha, hamna jeraha !
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni