01/08/2016

Kwa nini nimekatiza kutafsiri riwaya ya Ahmadou Kourouma « Majua ya huru » (« Les soleils des indépendances »)
Mwaka jana nilianza kutafsiri kitabu kizuri sana cha marehemu mwandishi Ahmadou Kourouma (1927-2003). Kourouma alikuwa ni mwenyeji wa Kodivaa (Côte-d’ivoire) na alitunga vitabu vingi kwa kifaransa. Ni miongoni mwa waandishi maarufu wa bara ya Afrika katika lugha hiyo, pamoja na Amadou Hampâté Bâ, Sony Labou Tansi na Yambo Ouologuem. Vitabu vyake vinasomwa dunia nzima, na vingi vimeshatafsiriwa katika lugha nyingi. Niliamua kutafisiri kitabu hiki « Majua ya huru » kwa sababu ni kitabu ambacho niliwahi kusoma zamani sana wakati wa ujana wangu. Nasikitika kusema kwamba nimeshindwa kumaliza tafsiri yake, si kwa sababu kiswahili kimeniweza, bali kwa sababu zifuatazo :

— kwanza tuzingatie kwamba haki za kutafsiri kitabu chochote duniani zimehifadhiwa na kukiritimbwa na hairuhusiwi kutoa tafsiri yoyote bila idhini ya kampuni husika (taasisi, mchapishaji, dhuria za mwandishi, n.k.). Mara nyingi, sheria hiyo ni halali na lazima izingatiwe ikiwa mwandishi yungali hai au amefariki katika miaka 70 au 50 nyuma (kutegemea na sheria za kila nchi). Mfano kutafsiri vitabu vya Shakespeare au Molière haina vipingamizi kwa sababu waandishi hawa wamefariki zamani sana lakini kutafsiri Sony Labou Tansi au Jean Anouilh kama nilivyofanya hivi karibuni (HAPA na HAPA) inabidi mfasiri apate haki zote kutoka mwenye haki, na aghalabu ni mchapishaji. Ndiyo maana sikuchapisha vitabu vya Labou Tansi na Anouilh. Na Kourouma, ambaye alifariki mwaka 2003 naye pia. Si kazi yangu kufuatilia haki hizo.

— pili, wachapishaji huona vibaya kuacha haki hizo ikiwa lugha ambayo wewe mfasiri unayoilenga katika kazi yako ni « lugha ndogo » (hapo natumia alama hizo za koma kuonyesha kwamba ni kauli ya mchapishaji, si yangu), na kiswahili nacho kinachukuliwa ni maskini au ndogo. Kwa kifupi, kiswahili kinadhaniwa hakina maslahi au faida kwa sababu hakina soko. Juu ya hayo, inajulikana wazi kwamba wenyeji wa Afrika mashariki hawasomi. Hivyo mchapishaji anahisi kwamba atajiponza akajifilisisha kwa vile atakavyokubali kuchapisha kitabu chochote katika lugha hiyo maskini.

                   Résultat de recherche d'images pour "kourouma books"       Résultat de recherche d'images pour "kourouma books"Résultat de recherche d'images pour "kourouma books"Résultat de recherche d'images pour "kourouma books"

— tatu, hakuna vitoa vitabu au wachapishaji wenye nidhamu na maadili ambao wanaaminika Afrika mashariki. Wakati uchapishaji wa kitabu cha fasihi unachukua muda mdogo sana (mwezi moja hadi miezi sita kwa riwaya) katika nchi tajiri, Tanzania na Kenya utaambiwa « njoo kesho » mara mia kabla hujapewa jawabu. Katika nchi hizo, inaelekea kwamba kuendeshewa resi au, kwa maneno mengine, kuzungushwa na kuongopewa, si tabia inayokosoleka. Pengine ni katika utamaduni wa watu. Katika nchi zenye uhuru, nadhani kwamba wateja wangesusa kununua vitabu katika shirika lolote lile lenye ufisadi kama huo.

— nne, mchapishaji ambaye kazi yake ni kuchapisha vitabu tu, huwa amejifaragua kiasi cha kujua yeye peke yake kinachotakikana katika mswada wa fasihi. Mwandishi wa riwaya au tamthilia, ambaye yeye ndiye pekee anayejua maana ya kubuni, basi anapaswa kuwezwa na kuonewa na « mfanya kazi » huyo ambaye, kwa kuwa amejipa kilemba kikubwa, anajua kila kitu. Ajabu kweli.

                                           Résultat de recherche d'images pour "kourouma books"      Résultat de recherche d'images pour "kourouma books"


— tano, inaelekea kwamba kiengereza kinazidi kutawala Afrika mashariki, na kimejikita katika fikra za watu. Siku hizi, ukiingia katika duka la vitabu Nairobi, Kampala au Dar-es-Salam, utakuta kwamba vitabu asilimia 80 (au zaidi) ni vya kiengereza, yaani lugha ya elimu ya eneo hilo (mandhali kiswahili kinachukuliwa na watu wengi kwamba si lugha ya elimu na sayansi).


Swali : wako wapi wanazuoni na vichwa vikubwa wa nchi hizo ambao wanasikika kila siku huku wakidai kwamba wamebanwa na kazi nyingi na majukumu mazito ? Wanafanya nini ? Kwa nini vitabu vya Adam Shafi, Kezilahabi (HAPA), Said Mohamed vinatafsiriwa na wageni katika lugha tajiri, na vitabu vile vingine vya dunia nzima havitafsiriwi katika kiswahili ? Kwa sababu ya ukoloni mambo leo ? Ubepari ? Utandawazi ? Au kwa sababu ya uzembe, ajizi, uroho, ujinga wa akili, choyo, husuda, rushwa, tabia mbaya wa « vichwa » vile ?
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni