25/09/2016

Unyama wa binadamu au ubinadamu wa wanyama ?


Katika lugha nyingi tunakuta usemi unaoelezea baadhi ya vitendo vya binadamu kwa kutumia maneno « unyama wa watu ». Usemi huo hauna msingi wowote kwa kuwa wanyama, hususan wale ambao wanaaminika ni wakatili sana kama simba au taiga, hawajafikia kiwango kile cha uhayawani ambao binadamu pekee anakuwa nao. Kila siku binadamu ndiye anayeonyesha bayana kwamba huwapita viumbe wote wa dunia yetu kwa ushenzi. Ukatili na ubedui ni miongoni mwa sifa ya binadamu ambayo imejikita katika maumbile yake. La kudhibitisha kwamba tumezidiwa na uhabithi huo usio na kifani limedhihirika katika namna zile ambazo tunajiliwaza nazo tunapolikabili swala nyeti la uharibifu wa dunia yetu. Kwa sisi sote mada hii ya uharibifu wa dunia si hoja. Na hata kama wasayansi watatuambia kwamba binadamu yupo hatarini kwa sababu ya kupotea kwa bayoanuai, hatujali. Na wengi katika wasomi pia husema kuwa ishu hilo ni uwongo, ilhali wengine watakubali kulitilia maanani lakini kwa kulisokomeza katika mjadala wa siasa. Ndipo Mwafrika atakapokwambia kwamba ni kosa la Wazungu, wakati Mchina atasema si shauri yake na Mwarabu naye atataja Allah ! Kwa kifupi, swala hilo halitupigi mshipa. Tunavuruga nyumba yetu, tunasambaratisha makaazi yetu, tunafuja maslahi yetu lakini hatujali. Isitoshe, tunasikia raha. Raha ya maovu !

Mnyama hana akili hiyo. Akili hiyo ya kuweza kuteketeza misingi ya uhai. Afadhali iwe hivyo. Ndiyo hekima yake ambayo binadamu amepungukiwa nayo. Mwache binadamu aendelee kusoma Foucauld, Derrida, Mbembe na wapuuzi wengine wenye akili hiyo betebete, ajishughulishe na demokrasia na udikteta, ajifanye ana maadili kwa kuwa yeye si mnyama, ajidai kwamba yeye ni bora kuliko mwingine kwa sababu ana utamaduni wa udugu, kikubwa hapo ni kumshughulisha binadamu na kumteka kiitikadi ili asije akatambue kwamba yuko hatarini. Vinginevyo angeacha kununua vimeremeta, blingbling, kompyuta, gari na kadhalika. Ingekuwa shida na balaa kwa kuwa viwanda ndivyo vinamtawala na kumtia shemere. Na vichwa vya hapa na pale duniani wangegundua kwamba vita vyao dhidi ya ukoloni mambo leo, utandawazi na ubeberu havina maana. Hivyo wangenyimwa majikwezo yao. Pengine wangesoma vitabu vile vya wasayansi ambao, katika miaka thelathini nyuma, wameshabainisha kwamba huenda binadamu hatakiuka karne hiyo ijayo. Lakini kwa msaada wa watu wakubwa hawa tunazidi kujitia hamnazo na kuwasilisha visababu tu, kwa madoido na maringo kupindukia, huku tukijidai kwamba sisi tunayo akili na wanyama wale hawana chochote. Na tutapania kukuza shughuli zile zile ambazo tayari zinachukuliwa na wasayansi kwamba zitafanikisha mpango wetu wa kuangamiza ulimwengu. Tuko njiani tu, kufyeka misitu yote, kumaliza spishi zote za viumbe, kukausha vyanzo vyote vya maji, kuchafua hewa na kujaza hili tufe la dunia hadi turundikane mpaka kileleni kwa milima yote. Kweli binadamu si mnyama. Ubinafsi na ubedui umemvaa.Mwana falsafa Levi-Strauss aliwahi kuandika kwamba dunia itazidi kuangamia na kwenda tenge ikiwa hatuzingatii swala la demografia. « Nilipozaliwa kulikuwa na wakaazi bilioni moja na nusu duniani. Nilipoingia kazini, mnamo mwaka 1930, tulikuwa bilioni mbili. Sasa hivi, tuko bilioni 6 na tutafikia bilioni 9 baada ya miongo michache tu, kwa mujibu wa tabiri zile za wana demografia. Hata wakisema kwamba idadi hiyo itafikia kilele hicho wala haitaongeza zaidi ya hapo, kiasi cha kwamba idadi ya watu itapungua kuanzia kilele hicho, hatuna budi kutambua kwamba spishi yetu itakuwa imeingia hatarini. Tutakuwa tumeshamaliza kuumbua uanuai wa kila kitu, katika mawanda ya utamaduni na bayolojia kwa sababu tutakuwa tumemaliza asilimia kubwa ya viumbe, wanyama pamoja na uoto wa asili. »

Levi-Strauss alifariki mwaka 2009. Alikuwa mtu mwenye hekima na nadhiri kubwa. Katika miaka hiyo arobaini iliyopita, dunia imepoteza asilimia 40 ya bayoanuai. Kwa sababu ya ongezeko la watu duniani. La kusikitisha ni kuona kwamba takriban wanadamu wote hawajui maana yake wala athari zake. Tanzania nimeshawahi kukutana na watu wengi ambao wanaitikadi kwamba spishi za wanyamapori hawapotei kabisa kwa sababu wanaibuka tu, kutoka katika ardhi. Hawajui kwamba binadamu atashindwa kuishi ikiwa idadi kubwa ya viumbe hai wanaotuzonga watatoweka. Na Afrika kunako bayoanuai ya kiasiliya yenye uketo mkubwa sana duniani ndiyo bara ambayo itakumbwa na hilaki na angamizi kubwa sana. Wakoloni walipofika Afrika mashariki walikuta wakaazi milioni nne. Sasa hivi, nchi hizi tatu za eneo hili — Uganda, Kenya na Tanzania — zinajumlisha wakaazi wasiopungua milioni mia moja na hamsini. Mwaka 2050 na mbele kidogo, Afrika nzima itakuwa imeshapata bilioni tatu. Ina maana kwamba bara hiyo itakuwa bara ya spishi moja tu, yaani binadamu. Waama binadamu mharabu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni