02/10/2016

Uzuri wa kodi na ushuru

Siku hizi, hapa na pale, katika berere berere za vyombo vya habari, teknohama na uana-habari jamii, masikio yetu yanafundukia mishindo ya ngoma tutu. Na ngoma hiyo inarindima, mdundo wake ukitoka ko-di ko-di ko-di ! Eti mheshimiwa Magufuli anapenda maduhuli ! Nd’o maana wakina mawakala wa sekta ya utalii wamejibuta kwa ghadhabu, huku wakimtolea rais mtukufu jicho la kifaru na kumkalia kifuani kama ngoma ya kimanga. Wamesema tayari ! Utalii umepungua. Na utazidi kupungua. Wageni wamesusia nchi ya Kilimanjaro. Hawaji kama kawaida. Kwa nini ? Kwa sababu ya kodi ! Kiingilio ndani ya mbuga kimegeuka maingilio. Na tayari wafanyakazi wengine wa Bongo wamesharudi makwao kuchimba mihogo na kuitokosa na kuitafuna mitupu bila hata kinofu cha kitimoto. Watalii wabaya. Si wana mshiko ? Wanataka nini tena ?

Kumbe katika msururu wa watalii hawa, sijui kama ni watu, wapo wasayansi, wapo wasomi, wapo waandishi. Wachache wanajua kiswahili, lakini wengi wana ujuzi mkubwa kuhusu mazingira asiliya pamoja na wanyamapori waishio Afrika. Si wazungu wa reli, kama wale wa aisee (NGO). Usiwachezee hawa. Kuona uhai wa maumbile umekuwa chapwa ndani ya hifadhi, wengi wemegoma kutoa dola 70 kwa siku moja. Wanakataa kutembezwa katika mbuga na hifadhi zenye migunga mizuri na misitu ya tupiatupia. Mboni si buku na tumbili wapo ? Basi katika hawa wazungu magalacha, wengine wamechakarisha matawi yale, si unajua yale ya Selous, thubutu ! Mizoga tu, ambayo ingali inang’ong’wa na nzi, ndiyo iliyogunduliwa. Si mas'hara, mtalii ametemwa katika dunia ya mizoga tele na uhaba wa wanyama, ambao pengine hawakulipa ushuru ! Bahati mbaya, ujanja wa kiafrika umeshindikana hapo. Hawa wamerudi makwao pia, huku wamechukua picha zao, rekodi zao na wengine hata uvundo wa mizoga ile. Kaifa zote zimetoka wazi.

Hivyo basi. Ushuru si sababu. Au ni sababu katika kijiji cha Bongo. Ng’ambu, au kwa maneno mengine kwa Mamtoni, sifa ya Tanzania imepotea. Watalii wamechoka kuzungusha macho yao duru katika mbuga ambako hifadhi ni jina tu, wamechoka taaban kusota kwenye barabara ya mchangamawe, inuka inama, yallah yallah, simile simile, Pajero ipishwe, mpaka mgongo unawatoka kibyongo. Hata mazibra wameingia mitini ! Lakini haidhuru. Tanzania si bakuli la kufugia samaki. Urani, makaa ya mawe, dhahabu, tanzanaiti na gesi zipo chungu nzima. Binadamu amenusurika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni