18/11/2016

Kuhusu tuzo ya Nobel : jina la Nobel limenajisika tena


Mwaka huu tuzo ya Nobel katika fasihi haikuacha taathira ya mvutio. Bali imetuletea mzubao. Tena mkubwa. Manju mmoja kutoka soko huria ya kidunia ameteuliwa kuwa ni msanii bora wa mwaka 2016. Naye anaitwa Bob Dylan, kutoka Marekani. Inajulikana wazi kwamba tuzo hiyo, tofauti na nyinginezo kama za fizikia au udaktari, hutiliwa shaka. Fasihi si sayansi. Sisi sote tutamchangamkia msayansi yeyote atakayetuletea uvumbuzi mkubwa wa kutusaidia tupate chanjo mbalimbali kama zile tulizokuwa tumeshazipata za kutibu kichaa, mchochota wa maini, surua, pepopunda na kadhalika. Lakini fasihi imechukuliwa na watu wengi ni burudani tu. Katika dunia ya sayansi, teknolojia na maendeleo endelevu, fasihi imeshushwa hadhi. Na bila shaka itazidi kushushwa hadhi kwa msaada wa marehemu bwana Nobel ambaye jina lake limenasijika tena mwaka huu.


Fasihi imegeuka ni kipeperushi. Imekuwa nuksi. Wakati umepotea sasa fasihi ilipotia nanga katika bandari yenye uketo mkubwa sana. Hivyo ilikuwa ni mapokeo, tarehe, kwa kifupi historia. Na wakati ule kulikuwa hakuna mwandishi asiyekuwa na mtangulizi. Mfumo wa siasa unaovuma kwa nguvu katika dunia yetu siku hizi unapendelea vimulimuli vipwitepwite katika mazingira tambarare. Na vimulimuli hivyo visije vikarejelee nuru iliyong’ara zamani katika giza. Tusije tukaendeshwe na nguvu za watu wa zamani ambao vionjo vyao, mienendo yao na tabia zao zinasemwa na vipaza sauti vya sasa kwamba wamepitwa na wakati. Kinachotakikana hapo ni wazi. Tusiwe na nadhari wakati tunaponyanganywa utepe ule wa kupima vidato vile vya kitu — fasihi — ambacho kina umbo wa ngazi. Kwa kuwa kuna fasihi ya chini, fasihi uchwara ambayo mara nyingi huitwa fasihi pendwa na fasihi ya juu ambayo husomwa na watu wachache. Gogo la mbuyu si la mvule. Changamoto ni hiyo tu, ya kwamba tunakabiliwa nayo siku hizi, kutoka Umakondeni hadi ndani ya ukumbi wa Wall Street, nayo inahusiana na mkaliano huo halali uliokuwa ukifinyanga mzao wa vitu katika tabaka hili lenye maana ambao tayari sasa umeingia katika itikadi ya kwamba matokeo yoyote yanayoletwa na watu yana manufaa sawa kwa jamii husika (relativism). Na imani hii kubwa inabebwa na mfumo wa soko huria.


Hivyo tusishangae kwamba manju huyo Bob Dylan, ambaye alikua katika kitalu cha soko huria ameteuliwa mwaka huu ili kutunukiwa kombe la mshindi katika fasihi. Kwa mchango huu mpya wa Nobel, Bob Dylan ni sawa na Coetzee, Soyinka, Bergson na kadhalika. Uliberali ambao ni mfumo wa siasa ulioenea sana katika dunia yetu miaka 50 iliyopita, hasa katika nchi zenye siasa ya kisoshalisti (iwe ujamaa au ukoministi) umekoga akili za watu kiasi cha kuwakomoa wapinzani wengi. Sote tumezoeleka kuishi katika usawa huo. Ni jambo la kuchekesha kwa kuwa tungali tunapenda kushangilia ushindi wa timu ya mpira bora katika mashindano ya kidunia au tunapenda kuifyagilia kampuni ile iliyopata soko kubwa kuliko kampuni nyingine, lakini tutakataa kutambua kwamba Coetzee ni mwandishi bora kuliko Bob Dylan au Ngugi wa Thiong’o. Tabaka katika kipindi chetu cha utawala wa soko huria imepoteza maana yake ila katika sekta ya uchumi (na kandanda ni uhondo mkubwa wa sekta hiyo).  
Fasihi, hadi leo, imegoma kuingia katika mfumo huu wa usawa. Sasa mambo yamebadilika. Tuikumbuke tuzo ya mwaka 2015 iliyomtuza mwandishi Svetlana Alexietch aliyeandika mahojiano tu. Maji yamezidi unga. Si vigumu kufikiri kwamba katika miaka ijao tutatajiwa waandishi wengine tapeli na laghai ambao wataonekana ni bora kuliko wote. Mtu yeyote akiwa amekubuhu katika upigaji wa ngezi, msondo au chapuo, mbali na msewe na ngoma nyingine ya mizuka, basi ana haki ya kuzua heba zake za udanganyifu na kujikokota hadi Stockholm. Wala si lazima awe mrithi katika kuwasilisha usanii wake. Ikubalike, kwa punde kidogo, katika jazanda ya kufikirika, kwamba Shaaban Robert alikuwa hayupo katika dhuria za wasanii wakubwa katika kiswahili, kwa kurithi ufundi wake kutoka wasanii wengine waliotangulia. Je, angalikuwa msanii mkubwa katika waandishi wote wa kiswahili ? Tunajua, kinyume na hayo, kwamba alikuwa amesoma tenzi zile za zamani ambazo zilimwathiri kiasi cha kumweka katika hali ya kuweza kujenga mtindo mpya wa kuandika. Hivyo mshairi Haji Gora naye pia, ingawa hakusoma sana yale yaliyoandikwa katika enzi za kale, bila shaka ni msanii mrithi ambaye amefundishwa mengi kutoka wazee waliofariki zamani.

Turejee kwenye tuzo ya mwaka huu. Tunaambiwa kwamba Bob Dylan ni manju mzuri anayestahili kupata ushindi huo. Hapo ndipo tunapohisi kwamba tumesingiziwa. Udanganyifu ni mkubwa mno. Rai hiyo inakuja na ushawishi nyemelezi. Swala letu ni hilo tu : je, kweli kazi za mwimbaji huyo zina chanzo katika kazi na tungo zile za waasisi waliotangulia zamani ya kale ? Wengi wamesema kwamba nyimbo zake nyingi zina ushairi fulani ambao unafaa kulinganishwa na baadhi ya mashairi wa Emily Dickinson (1830-1886). Wengineo wameleta hoja nyingine wakisisitiza kwamba fasihi simulizi ndiyo iliyoshangiliwa hapo. Wengine pia, hasa bara ya Afrika, wamepaza sauti kama kawaida huku wakikumbusha kwamba swala hilo la Nobel limejaa ubaguzi na ni mchezo unaopigwa Uzunguni tu. Kauli hiyo inayosikika takriban kila mwaka wakati wa uteuzi wa Nobel, huletwa na wakili wa itikadi za umoja wa Afrika wanaokariri kwamba nchi za Magharibi zina sheria kali kandamizi. Kwa wakubwa hawa, urithi katika fasihi si hoja. Ishu ni siasa tu. Hoja hizo zote ambazo zinashughulisha akili za watu zina upurukushaji mkubwa kwa kutoweka katika mizani shinikizo ile inayosukuma jamii zote za dunia kuelekea upande mmoja tu, nao ni shinikizo ya soko huria.


Shinikizo hii ina vipengele viwili katika athari zake. Kufuta historia na kusawazisha vitu vyote visije vikatofautiana tena katika mfumo wa tabaka. Soko huria hupenda kidaka, kitale na dafu viwepo lakini visiwe tofauti katika hadhi, ubora na uzuri. Anything goes. Soyinka na Bob Dylan. Na katika fasihi tanzu zile zisiwe na uzito tena. Mshairi si msanii bora kama hajapiga manyanga na kufuga manywele ya rasta. Mshairi awe na gita, fidla, njuga au nai. Na mtu akisema kwamba Soyinka ni msanii bora kuliko mwimbaji yeyote wa Bongo na Congo, ataambiwa ni mbabe, ana kiburi na majivuno wa kupindukia (na atakuwa ni mbabe kweli kama ni mzungu). Kwa kifupi tunaambiwa kwamba utanzu si kitu cha kung’ang’ania sana. Bob Dylan ni mwimbaji na mshairi. Mawanda hizi mbili — wimbo na ushairi — ambazo hazilingani katika mfumo wa tabaka, sasa zinaingia katika usawa. Manju wa zamani au wa nchi nyingine ambaye huenda bado anaimba tenzi anadaiwa awe pamoja na waimbaji wa sasa katika kundi moja ya wasanii. Uwongo huu umefunikwa na mafumbo ya soko huria ambayo ndiyo inayoimarisha shughuli zile ziletazo faida. Bob Dylan si manju wa mapokeo bali ni mwimbaji ambaye kila siku hupewa misaada ya soko huria ili jina lake, sifa zake na hasa nyimbo zake ambazo ni bidhaa zinazotengenezwa kwa wingi katika viwanda na makampuni zitembezwe dunia nzima kupitia teknohama na nguvu za tasnia ya usanii huo. Manju wa mapokeo naye aghalabu hatoki katika kijiji chake, haendi mbali kwa sababu usanii wake unategemea jamaa zake ambao wamezaliwa pahala fulani katika nasaba fulani — ufundi wake hautegemei uchumi usioshikika.

Fasihi kwa sasa iko katika hali mbaya. Hasa katika nchi zenye fasihi chipukizi ambapo fasihi imeibuka si zamani sana. Kamwe katika nchi hizo fasihi itakuwa ni mapokeo wala urithi. Itakuwa ni vigumu kujenga tarika ya mitindo, mapisi wala tarehe ya kiujumi (aesthetics). Fasihi itabaki ni maudhui na dhamira tu, yaani si kitu kwa sababu insha na mazumgumzo ya kawaida nazo pia zina kazi hiyo. Katika nchi hizo fasihi ingali inaathiriwa na siasa, dini na maadili. Msimamo wake unaegemea nguzo za nje ambazo hazijasimamishwa na wasanii wenyewe. Ikiwa fasihi ni taaluma yenye dhima katika jamii — kuelimisha, kukamilisha mkakati wa upatanishi, kuhamasisha na kujenga itikadi fulani — kwa kifupi kuimarisha udhibiti wa jamii na kujenga uratibu wa mwafaka — basi fasihi haina maana wala haistahili kupewa nafasi katika jamii. Nini maana ya fasihi hiyo isiyo na lengo la kuzusha mgogoro (hususan wa kiujumi) katika jamii ili raia wapate kujenga lugha iliyotajirika, akili tambuzi kusudi waepuke kunyimwa haki zao ? Kufuta historia hiyo ya fasihi ni dhamira ya Nobel ya mwaka huu. Tusiwe watu waasi, tuwe watiifu, wasikilivu na wanyenyekevu. Tupendelee usanii wa mwenye gita au bendi ya mitaani ambao kazi yao ni « kushusha mistari » kuliko kusoma na kubuni ushairi, tamthilia na riwaya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni