07/01/2017

BOMU A NA BOMU D

Tarehe 6 na 9 ya agosti ya mwaka 1945, Hiroshima na Nagasaki, miji miwili ya Japan, ilidondoshwa bomu atomia ambazo zilisababisha wakaazi 200 000 kufariki. Wengi walionusurika waliathirika vibaya na hadi leo wangali wanaumwa kutokana na maradhi mbalimbali zilizoletwa na minunurisho ya kinuklia ikiwa ni pamoja na aina kadha ya saratani. Tukio hili linathibitisha jinsi binadamu anavyoweza kuwa mbunifu na mharibifu pamoja. Bomu mbili tu zilitosha kuangamiza miji miwili. Na bomu ya aina hii kwa jina lake ni bomu A. Tungependa kusema kwamba tukio kama hilo tumeliacha nyuma. Na kwamba binadamu hatarudia. Lakini wapi. Kipindi chetu ni cha kukatisha tamaa. Tungali tunaendelea kutengeneza aina nyingine ya bomu ambayo, kwa kweli, ni hatari zaidi kuliko ile ya kinuklia, nayo ni bomu D, yaani bomu demografia.

                                            
          
      

Hiyo bomu ni tofauti ya ile A kwa kuwa hutumiwa na binadamu mjinga. Kwa kifupi, binadamu alipotengeneza bomu A ilibidi atumie akili nyingi. Tofauti na bomu hiyo mpya, inabidi atumie ujinga wake kupita kiasi. Ujinga wa kuzaa kupindukia kama wafanyavyo sungura na kujaza dunia yetu shinda. Bomu D ndiyo hiyo : mwaka 1830 tulikuwa wanadamu bilioni moja ; mwaka 1930, tukafikia bilioni mbili ; mwaka 1960, tukawa bilioni tatu ; mwaka 1975, bilioni  4 ; mwaka 2000, bilioni 6 ; na leo tumekaribia bilioni nane. Aidha, katika takwimu hizo, namba moja ni ya kutilia maanani : kila baada ya siku tano, idadi ya wanadamu duniani huongezeka kwa milioni moja. Yote hayo tunayajua na hata kama ongezeko hilo linaua zaidi kuliko ile bomu A, hatujali. Kwa kifupi, ongezeko la wanadamu duniani linafuatisha kizigeu cha mtanuko (coefficient of expansion) ambacho kinaonyesha kwamba kila mwaka kinazidisha kasi yake. Tatizo ni hilo : dunia yetu haina maliasili ya kutosheleza mahitaji ya wote. Na maliasili hizo zinamalizika, jambo ambalo watu wengi — hasa bara ya Afrika — hawaamini.

Hivyo ongezeko la watu duniani lina athari na maangamizo makubwa. Mathalan mwaka 2012 peke yake tunaambiwa na WHO (World Health Organization) kwamba binadamu si chini ya milioni 7 wamefariki kwa sababu ya uchafuzi wa mazingira uliosababishwa na ukuaji wa idadi ya binadamu. Lakini si hivyo tu. Athari za ongezeko la watu duniani zinaonyesha uharibifu wake hasa katika mazingira au maumbile asiliya ambayo ni kitalu cha uhai duniani. Kwa mfano, tunajua kwamba leo binadamu na mifugo pekee hutumia asilimia 40 ya chanikiwiti (chlorophill, ambayo ni pigimenti ya majani inayosanisi (synthesize) nuru ya jua na kurekebisha oksijeni). Inajulikana pia kwamba tutapaswa kuzalisha mlo mwingi zaidi katika miaka 50 ijayo kuliko ule tuliozalisha katika miaka 500 nyuma. Hilo kwa sababu ya ongezeko la watu. Lakini haiwezekani kwa sababu ina maana kwamba tutahitaji kujipatia heka milioni 6 ya ardhi kila mwaka ili kutosheleza mahitaji ya watu. Na wakati huo huo, kila mwaka tunapoteza eka milioni 12 ya ardhi limika kwa sababu ya uharibifu wa ardhi ile. Isitoshe, katika miaka hiyo 10 ijayo, takriban watu bilioni 4 watapambana na ukosefu wa maji baridi. Leo hii, zaidi ya watu bilioni 1 hutembea zaidi ya km 1 kila siku ili kuteka maji. Ardhi limika pamoja na mifugo ni shughuli za binadamu ambazo zimesababisha kutoweka kwa asilimia 80 ya vetebrata waishio nchi kavu. Mwisho hapo, uharibifu wa bahari zote kwa sababu ya uchafuzi wenye asidi na dutu nyingine za kemikali utazidi marudufu katika miaka 50 ijayo, mchakato mbaya sana kwa kuwa bahari takriban zote zimeshakumbwa na kupotea kwa asilimia 80 ya spishi zake.Mbali na ubadilifu katika hali ya kemikali na fisikia ya ardhi, hewa, maji ya baharini, ni mfumo mwenyewe unaoongoza uwiano wa ikolojia ambao umevurugika vibaya. Wana sayansi wamethibitisha zamani (lakini hatusomi) kwamba binadamu atashindwa kuishi katika dunia isiyo na viumbe na uoto asiliya. Hivyo binadamu ni mchafuzi mbaya ingawa hakuna usawa katika kuchangia kwa uchafuzi wa dunia. Mmarekani au Mchina siku hizi ana athari mkubwa zaidi kuliko Msudan au Mnepali. Lakini kuna aina nyingi ya uchafuzi na aina nyingi ya mazingira asiliya ambayo yanaangamia kutokana na athari hizo. Aidha kuna athari zinazojitokeza sasa hivi — mathalan kutapakaza kemikali katika mazingira haichukui muda kuchafua maji ya chanzo — na athari za usoni ambazo zinachukua miaka kujitokeza — kuvuruga mfumoekolojia kwa kutojali vidudu na viumbe wanaoishi ndani yake.

Katika nchi za magharibi, uchafuzi uliopo umeshadhihirika wazi ; hasa ni wa aina mbili : uchafuzi wa hewa na uchafuzi wa ardhi. Kwa jumla, katika nchi hizo, mito na misitu haina uchafuzi mkubwa sana (isipokuwa baadhi ya misitu, kama ile ya Canada, ambayo imepatikana na mvua yenye asidi inayounguza miti). Tatizo kubwa nchi hizo zinakabiliwa nazo ni aina za kemikali (nitrati) iliyotapakaa mote katika ardhi, ambayo inazidi kuponza kilimo na mifugo. Pia utoaji wa gesi ya kaboni umekuwa mwingi katika nchi hizo, na inatambulika wazi sasa kwamba gesi hiyo hulinasa joto la jua na kusababisha ongezeko la joto katika maeneo ya nchi kavu na baharini. Utaratibu huo unasababisha uunguzaji wa mafuta ya asilimwamba, kuongezeka kwa hewa ukaa na kupanda kwa halijoto duniani. Changamoto ni kubwa mno tukiangazia jinsi mfumo na mpangilio wa siasa — ambao ndio unaotakiwa kupambana na sakata hiyo — ulivyokumbwa na ubadhilifu mpya unaodhoofisha misingi yote ya jamii. Utawala na uendeshaji wa nchi hizo unahofiwa utachukuliwa na wachache wanaoongoza sekta ya uchumi, hususan sekta ya fedha na benki. Hapo ndipo dunia huenda itaingia katika mipapatikio ya hatima yake. Katika nchi nyingi za Ulaya — mathalan Ufaransa na nchi nyingi za Ulaya mashariki — tayari baadhi ya vyombo vya dola husalimu amri ya asasi za kifedha.

Katika nchi za bara Afrika, hali si nzuri pia kwa sababu ya kukosekana kwa mfumo wa siasa uliowajibika. Uchafuzi ni wa aina nyingine. Haswa unasababishwa na ongezeko la watu. Kikubwa ni athari zile zikumbazo jamii mbalimbali za bara hiyo katika sekta ya chanzo ya maji asiliya na misitu. Kote misitu inazidi kupotea, maji safi kuadimika na viumbe hai wote kutoweka. Kilicho muhimu hapo ni kujikumbusha kwamba mfumoekolojia wa Afrika sio ule wa nchi za magharibi. Afrika, bayoanuai ni maliasili kubwa zaidi kushinda ile ya Ulaya. Kwa mfano, tukiangazia mfumoekolojia wa msitu mkubwa wa nchi yoyote ya Ulaya na msitu wa Kongo, hatuna budi kutambua kwamba ulinganishi hauna maana kwa sababu msitu wa Kongo una dafina mkubwa zaidi ya uanuwai kibiolojia, kitu ambacho msitu wowote wa Ulaya umepungukiwa nazo kiasiliya. Kufyeka msitu wa Ulaya hakuna athari zile kubwa kama ilivyo Afrika. Hivyo kusema kama inavyosikika katika mijadala ya kisiasa mbalimbali kwamba nchi za magharibi pekee ndizo zinazochangia pa kubwa katika kuchafua mazingira ni aina ya longolongo kubwa. Kauli hiyo husababisha uzohali na uzembe katika sekta ya siasa ya nchi zinazoendelea. Kwa kuwa « si kosa letu », tusijali mambo hayo ambayo yanabebwa na « wazungu » wenye itikadi ya kimazingira.

Marehemu mwalimu Nyerere aliwahi kusema « mjinga umwache alale, ukimwamsha utalala wewe ». Nadhani hapo tumefika. Mjinga ameamka, amezindukana kutoka katika lepe lake la usingizi. Hivyo na sisi sote hapo tumerogwa na maruerue mapya ambayo yanatufanya tuteremee usingizi. Imekuwa kama kwamba maungo yetu yote yamepooza na akili zetu zimeparama. Nguvu zetu zimeganda. Na katika ujinga wetu, tungali tunasoma fasihi, tungali tunatunga mashairi, tungali tunashughulikia pirika zetu za kawaida, tungali tunapigania haki za binadamu na hali kadhalika. Tusiwe na akili tambuzi wala tusisome kazi zile zitungwazo na wana sayansi — na kwa kuwa lugha ya kiswahili haijakomaa katika mawanda haya, bila shaka ujinga utazidi kutambaa Afrika mashariki — vinginevyo tutabaini kwamba kweli miaka ya mbele itatutegea laana na hilaki kubwa sana. Laiti watu wangesoma, laiti watu wangeelimika, laiti wanazuoni wasingechanganya siasa na taaluma… lakini kumechelewa. Wengi katika wana sayansi kama Paul Krutzen (HAPA), aliyepata tuzo ya Nobel katika kemia mwaka 1995, wameshakataa tamaa. Kwa kifupi, mustakabali wetu kama spishi mmojawapo duniani hauna uhakika. Inatisha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni