27/01/2017

Kuzaa wengi : utamaduni wa urijali au kasumba ?


Kabla ya enzi ya ukoloni, si miaka mingi nyuma, Afrika ilikuwa ni eneo la dunia ambalo lilikuwa halina watu wengi. Kwa sababu hiyo, tunaweza kuchukulia kuwa maliasili ya bara hiyo, kwa wakati ule, ilikuwa haimaliziki. Na katika jamii zote za Afrika, kama ilivyokuwa bara nyingine kabla ya kuzidiwa na wakazi wengi, watu waliishi kwa kuchuma maliasili kwa kadiri wawezavyo. Kuanzia karne 19, hususan wakati wa majilio ya wakoloni, bara hiyo ilijaaliwa — ama ililaaniwa — kukumbwa na ongezeko la watu, haswa kwa msaada wa utibabu ulioletwa na wakoloni. Idadi ya watu hapo ndipo ilipata kuongezeka kwa kiasi kikubwa.

Siku hizi, idadi ya watu bara ya Afrika inaendelea kuongezeka kwa kiwango kikubwa kushinda bara zote za dunia ambapo mwendo wa ongezeko la watu umeshaanza kulegea hadi kushuka kama ilivyo katika baadhi ya nchi zilizotajirika katika mawanda ya elimu (mfano Japan). Kadiri kiwango cha elimu kinavyoshuka katika nchi yoyote, ndipo ongezeko la watu unaposhika kasi. Tunayo mifano mingi ya nchi za Afrika magharibi kama vile Nigeri au Chadi ambapo kasi ya kuongezeka kwa watu imepungua kidogo ikakua tena hivi karibuni baada ya kusambaratika kwa asasi za elimu (shule na vyuo vikuu). Kwa kifupi, ongezeko la watu linaakisi kiwango fulani cha ukosefu wa elimu. Kote duniani, katika historia ya nchi zote, ujinga ulikuwa — na unazidi kuwa, kwa nchi nyingi —, ni mchango na msukumo mkubwa sana katika kuongezeka kwa watu, kwanza katika familia, pili katika jamii kwa jumla.


Uwiano huo kati ya kiwango cha elimu na kasi ya ongezeko la watu unamaanisha kwamba maendeleo katika sekta ya uchumi si kigezo cha kutilia maanani katika kupunguza kasi hiyo. Uchumi si kitu. Mifano tunayo mingi tu. Katika nchi kadhaa za kiarabu, watu huzaa watoto wengi hata kama ni mabilionea. Nao ni matajiri kiuchumi lakini pia ni watu ambao wengi hawana elimu. Nchi nyingi za dunia ya leo, kama vile India na China, ambazo zinachukuliwa ni mataifa makubwa kiuchumi, bado hazijaingia katika kikosi cha nchi zenye ustaarabu katika kuthabiti na kusimamia kuongezeka kwa wakazi wao, kwa sababu mfumo wa elimu umekuwa dhaifu. Licha ya hayo, nchi hizo bado hazijakomesha umaskini wao ambao kwa kweli umekithiri miaka hii ya hivi karibuni.

Na dalili za kuwa na elimu zinapatikana katika takwimu kadhaa hususan katika tathmini zinazofanyika katika sekta ya ubunifu kama vile vyeti vichapishwavyo kila mwaka katika kila nchi. Na sitakosea nikisema kwamba hakuna ukanda mwingine duniani ambao umeponza na kuzorotesha maendeleo ya sekta hiyo kama ilivyo ukanda wa Afrika. Ni ya kuhuzunisha kwa kuwa bara ya Afrika kwa jumla inaendelea kudidimia kielimu — ingawa teknolojia na miundombinu imepandikizwa ikamea barabara —, baada ya kupata uhuru takriban miaka 60 nyuma, na kujizongoresha akilini rubega ya visingizio vya kisiasa wakati dunia nzima inahitaji kuamsha akili za watu wote tukashirikiane katika kupambana na maafa na janga zijazo.

Hapo naomba (ashakum) kusogeza takwimu chache tu — najua ukweli unauma — ili kusisitiza kilicho wazi kabisa katika sekta ya elimu na ubunifu (wala ubunifu hauambatani na uchumi) : mwaka 2009, dunia nzima imerekodi ikahalilisha vyeti takriban 166 000 katika ubunifu na uvumbuzi ; katika vyeti hivyo vyote, 486 vilipatikana Afrika, ikawa sawa na asilimia 0,3 ya vyeti vyote. Katika 0,3 % hivyo, 90 % vilipatikana Afrika kusini, lakini katika matokeo haya, 80% vilibebwa na Waafrika weupe na 10% na Waafrika wahindi (takwimu hizo zinazoakisi aina ya ukabila na uhasama zingekuwa hazina maana katika nchi yoyote ya dunia, ambapo raia hana rangi, lakini inajulikana wazi kwamba Afrika kusini ni nchi ambayo haijaondokana na ubaguzi wa rangi ingawa jina la apartheid limefutwa). Mwaka huo huo wa 2009, Moroko ndiyo nchi iliyopata 10% ya vyeti vilivyobaki pamoja na Misri iliyopata 41%. Ya kusikitisha sana, hasa msomaji ukilinganisha takwimu hizo na zile za nchi yoyote ya Amerika kusini na Asia.

Maelezo hayo hayana ubabe wala kejeli. Yana ukweli tu. Mtu akivinjari katika tovuti mbalimbali ya kibongo pia atagundua ukweli huo. Kwa mfano nakumbuka wakati waziri mkuu Mizengo Pinda alipotoa onyo kali kuhusiana na ongezeko la watu Tanzania. Ikawa matope, matusi, mawe, kibesi na viwembe. Nusura mheshimiwa kupigwa kitutu. Baadhi ya vijembe vile nimevi-kopy (?) hapo kama ifuatayo (hapo sijakosoa makosa ya kiswahili, au ni mategu ?) :

« Tusipende kukopy kila kitu mzungu anachotuletea mzungu kaleta family planning sasa ndio imekua nyimbo kila siku »

« Tatizo viongozi wetu hawasomi na wanakalili mitizamo hasi ya watu wa magharibi »

« Uzazi wa mpango uzazi wa mpango, uhuni wa wazungu huu viongozi wetu wanauimba kama kasuku, no thinking »

Wadau hawa ni wakweli kabisa. Wazungu ndio wanaohusika katika kuleta « mawazo hasi, madudu mabaya na maadili ya kijinga kuhusu jinsia, kuzaa nje ya ndoa na uzazi wa mpango ». Ishu hiyo haina noma (objection) kwa kuwa inajulikana tangu zamani ya kale kwamba dhana hasi ni kichocheo kikubwa cha ujuzi, falsafa, sayansi na elimu. Si Wazungu wamepiku katika sayansi na udaktari tangu enzi na enzi ? Si uovu umo katika uzuri (kama msomaji umezubaa, soma Ayubu katika Biblia) ? Ningekuwa na nafasi hapo kutaja waandishi na wasayansi maarufu (katika wale ambao walichangia pa kubwa sana katika kuinua maisha ya binadamu) waliodhihaki wenye maoni chanya, nadhani maandishi yangu yangejaza maktaba nzima. Kikubwa hapa ni jinsi dhana chanya ilivyo ni msingi wa muono na mtizamo wenye ubwege. Lakini si hoja yangu ya leo.

Hapo najiuliza : uzazi huo wa ulemete (kutunga mimba na kuwa mtoto mwingine mkononi) na kuzaa kama ncha ya kimondo kweli ungekuwepo leo hii kama wakoloni wasingefika Afrika ? Wao ndio walioleta chanjo, dawa, hospitali na sayansi ya kuongezea miaka ya kuishi na kupata watoto wengi (nisitaje uovu wao wa aina nyingine). Tunajua wazi kwamba wasingekuja, watu wangeendelea kupambana na maafa makubwa kama vile maambukizi na kifo cha mapema. Tangu walipotokezea na sayansi na udaktari zao (mbaya ?) umri wa wastani wa kuishi umeongezeka, vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano vimepungua sana, na hali kadhalika. Yote hayo ni katika maendeleo ya vifaa na mbinu ziletwazo kutoka nje. Lakini je, tabia, mienendo na hali ya kupambana na uzazi, kweli zimebadilika ? Isitoshe, wengi husema kwamba kuzaa ni katika utamaduni wa kiafrika. Hapo pia kauli hiyo haina kichwa wala miguu kwa kuwa dunia nzima, penye ujinga, pana watoto wengi ! Si Afrika, si Ulaya, kote duniani. Msukumo mkubwa wa kuzaa huwa ni urijali na kutokuwa na upeo wa akili, hususan ni ubabe na ubaradhuli wa kiume, mwanamke mja mzito asije akawania elimu na uwezo wa kupigania haki zake.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni