10/03/2017

Serengeti na mbuga nyingine : urithi utakaopotea ?


"Serengeti ni bidhaa. Lakini pia ni jamvi la wageni. Kwetu mtu haoni sababu ya kuhifadhi mbuga iliyojaa wanyama waharibifu. Hivyo mihadhara na hafla nyingi za kienyeji ziitishwe kuamsha akili za watu ili wote waelewe kwamba wanyama wale ni fedha. Kama hawana faida, wana tija gani zaidi ya hiyo ? Bayoanuai ? Acha dhana hiyo ya kizungu. Ni fedha tu. Hivyo tumpembejee mzungu na mfadhili mwema atuletee mshiko tu. Nasi tuwe na uwezo ule wa kuchapisha ramani na bango. Bure ghali. Watalii wasipotee ndani ya pori hiyo kubwa. Si mzungu ndiye aliyeturithisha hifadhi hizo ? Yeye ndiye anayeranda ndani ya mbuga. Sisi Waafrika, hatuna mpango huo. Ndio wao wanaotikita game drive. Sisi jamii yetu kutungamana tu, kushirikiana na kupeana. Burudani yetu ni human drive.


Mzungu hajui kwamba falsafa yetu imekolea viungo vyenye ladha ya maovu. Mfano Serengeti. Yeye mzungu anatuhamasisha tuwe makini kabisa na hifadhi hiyo iliyowekwa katika orodha ya Unesico. Itunzwe vizuri. Sawa, lakini ina gharama. Na sisi ndio tutakaochuuza sehemu hiyo ya Tanzania katika mnada. Tufaidike na sisi. Wazungu wana utamaduni na itikadi ya mazingira. Eti wale hawapendi sisi tujenge barabara kuu ndani ya hifadhi. Watu wasinune. Hilo sakata kubwa ni faida yetu basi. Fidia itozwe hapo. Uendeshaji sisi, mtaji wao ! Yaani miundombinu, barabara na maslahi yote wawekeze wao ! Kama wanapenda mbuga iwepo. Tusisahau wazee waliposema, baniani mbaya, kiatu chake dawa. Wakipenda wasipende, tutajenga viwanda, boma, gridi za umeme, kinu cha kinuklia, treni na mambo mengine ! Ndani ya mbuga. Watakoma !"

 Si tumeshaanza na Selous ? Raha ya maovu !

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni