08/04/2017

Kiswahili cha kisasa kipo ?


Mtu akivinjari katika tovuti na blogu mbalimbali za kiswahili huambiwa kila muda kwamba kiswahili kinazidi kukua. Kwamba kimepevuka, kimepanuka kiasi cha kustahili sasa kujivuta katika medani ya lugha nyingine tajiri za duniani. Maoni haya hayana msingi kwangu. Ni ajabu kubwa, labda kwa sababu natumia lugha nne katika kusoma vitabu, jambo ambalo linachangia sana kuchonga akili ya mtu apate kuchanganua utajiri na umaskini wa lugha. Lakini si hivyo tu. Kila wiki, vitabu kadhaa huwa vinanihangaisha, si riwaya peke yake, bali hasa ni vitabu vya sayansi, vile vyenye uketo wa ndani katika taaluma mbalimbali, ikiwemo etolojia, bayolojia ya wanyama na vidudu fulani, ikolojia na kadhalika. Sina budi kusema kwamba nimebahatika kuzaliwa katika nchi yenye lugha tajiri (kwa maana ni lugha yenye historia ndefu) kitu ambacho kinanipambazukia niwe makini na wenye ari katika matumizi tofauti ya lugha yetu, ikiwemo ushairi na sayansi. Na leo hii, nikitaka kusoma kitabu cha sayansi, bila shaka nitakigeukia kifaransa au kiengereza, lakini nitakitupilia mbali kiswahili. Kitabu changu nachosoma siku hizi kinaitwa « Kutokuwa na kumbukumbu katika kupambana na ubadilifu wa mfumo wa ikolijia… » Na ni kitabu kiuzwacho katika duka lolote Ulaya. Huna haja ya kuwa msomi au Profesa mkwasi wa Chuo Kikuu, kwa sababu mtu yeyote mwenye elimu atakuwa hana tatizo lolote kukisoma. Hata kama dhana na msamiati mgumu zimo, lakini kwa kuwa shule za Ulaya ni shule zenye maana, mtu yeyote atawahi kupambana nacho. Lakini je, Uswahilini mtindo huo umeshapambazuka ? Kwani mtu anaweza kuandika insha au makala kuhusu, kwa mfano, tabia ya kuzaliana kwa mbwa msitu na athari za uchafuzi wa mazingira juu ya tabia hiyo ? Mfano mwingine, siku hizi tunazumgumzia sana mambo ya mabadiliko ya tabia nchi. Lakini viko wapi vitabu vya ndani kuhusu hoja hiyo, kwa kiswahili ? Wangapi, katika wananchi wale waliotimiza kidato cha sita, wataibuka hapo kuwasilisha mjadala uliopo siku hizi katika vikosi vya wana sayansi duniani, huku wakitumia kiswahili ?

Nakumbuka, miaka mingi nyuma, katika miaka themanini ya karne iliyopita, nilipofikwa na jamaa aliyenigaia diwani ya Abdilatif Abdalla iitwayo Sauti ya dhiki. Niliposoma kitabu hicho, wakati ule, raha ilinikunjukia jinsi kiswahili chake kilivyonakshiwa kwa umahiri. Kitabu hicho kilichapishwa mwaka 1973 na kilitangulizwa na dibaji ya bwana mmoja ambaye hakunyimwa nafasi nzuri ya kuchomekea lake. Naomba nitoe baadhi ya maneno yake ili mtu apate kuelewa vizuri nachokusudia kusema hapo, hasa kuhusiana na utaratibu ule uliozidi, kuanzia miaka hiyo ya 70, kukwamisha lugha ya kiswahili isije ikawa lugha ya kisasa. Huyo mheshimiwa, kwa jina lake Shihabuddin Chiraghdin, aliandika :

« (lugha ya kiswahili) tuikuze kwa kuzichanganya janibu zote za kiswahili ; tusiivize kwa kushikilia zile zile ndweo na ndezi za kikoloni, tukawa na lazima na urathi wao. Njia moja ya kuikuza, kuitukuza na kuivyaza lugha ya kiswahili ni kupatikana maandishi kama haya ya Abdilatif — yatoke janibu zote. »

Niliposoma dibaji hiyo kwa mara ya kwanza, nilifurahi sana. Siwezi kuficha kwamba kitabu hicho kilinihimiza sana niendeleze juhudi zangu za kusoma zaidi kiswahili. Lakini leo, nimerudi mkuse, kama tunavyosema katika kisongo kilichoparauka katika « janibu » ya Kilwa. Kwani miaka zaidi ya 45 imepita sasa kutoka 1973. Na maua yale yaliyotarajiwa kuvyaa, kama alivyonena bwana huyo, yako wapi ? Vitabu vile vya mashairi viko wapi ? Vitabu vingapi vinachapishwa kila mwaka ili wasomaji wa kiswahili wapate « kucheza kwa mdundo wa kiafrika » ? Mboni ukapa ukaenea sana ikawa miti yote imelanika (kikilwa hicho !) ? Aidha, kukuza lugha katika taaluma yake mojawapo ni vizuri sana, lakini je, taaluma zile nyingine ? 

                                                               

Tuondokane na bwana huyo mkubwa tumgeukie mwingine. Hapa naomba kutaja kitabu cha marehemu rafiki yangu Alain Ricard, katika kitabu chake kizuri kihusucho mwandishi Ebrahim Hussein ambaye anachukuliwa (na sisi wawili) ni mwandishi mzuri sana katika waandishi wote katika lugha ya kiswahili. Mwandishi huyo aliwahi kuandika tamthilia nyingi ikiwemo Kijinkitile na Mashetani. Basi vijana wa siku hizi waelewe vizuri, kwa sababu si wengi kati yao waliobahatika kwenda shuleni, kwamba msanii huyo maarufu alipondwa na kuzomewa na vichwa vile kwa sababu eti msanii huyo anatumia kiswahili kigumu. Mimi Mzungu niliyesoma vitabu vile Mashetani na Kijinkitile, sijapata taabu kuvielewa. Mboni mzawa mwenye uzalendo mwingi havielewi ? Wacha dhana ya utamaduni, ambayo si hoja noma katika kusoma na kuelewa kitabu chochote cha fasihi, nini maana yake, nini sababu yake ya kusema kwamba « kitabu cha fasihi » si kizuri kwa kuwa si rahisi kukielewa ? Kwa nini Ebrahim Hussein alitupwa na wasomaji wake baada ya kutolewa kwa Mashetani ? Jibu tunalipata katika kitabu cha Alain Ricard aliyebobea katika kuchanganua kazi za uhakiki (au ni hukumu ?) zilizoletwa na baadhi ya « wasomi » wa enzi ile, katika miaka ya sabini. Mfano bwana Kiango ndiye aliyeleta baadhi ya mishale iliyofumwa na kutoswa katika sumu ya siasa dhidi ya michezo ya Ebrahim Hussein wakati ule. Ni vizuri kuitaja hapo angalau tupate kukumbuka utaratibu ule ulioleta kusambaratika kwa fasihi kuanzia miaka themanini :

« Kwa sababu ya umuhimu wa mchezo huu kwa kila Mtanzania, ndiyo hapa namlaumu mwandishi kwa kuandika Mashetani kama alivyouandika. Kwa sababu ni watu wachache watakaouelewa kwa urahisi. Kwa wengi, unakuwa ni kama kujaribu kuvunja chuma kwa meno »

Vijembe kama hivi viko vingi katika maandishi ya « kitaalamu » ya miaka ile Tanzania. Hakuna mtu hapo kuinua mkono na kuuliza : « huyo bwana Kiango ameandika nini mwenyewe, amefanya nini ili kujishaua kiasi hicho ? ». Lakini si ishu. Kikubwa hapo ni kwamba tunaambiwa tusadiki maneno ya bwana mkubwa huyo ambaye alishindwa, kama Maprofesa wengi wa chuo kikuu cha wakati ule, kuzikabili kazi za fasihi kama ipasavyo, yaani kama sekta ya ubunifu unaotakiwa kupimwa kwa kutumia mbinu na mikabala ya kiujumi peke yake. Bwana Kiango angeibuka katika mjadala ule wa ubora wa vitabu vya Ebrahim Hussein huku akijadilia sifa za kiujumi za michezo yake, tungemtukuza sana. Lakini kipindi kile cha usanii wa Ebrahim Hussein kilikuwa enzi ya Ujamaa ambao tayari tumeshang’amua kwamba ulikuwa ni aina ya ukoministi, ingawa ukoministi wa kiafrika.


Hatuwezi kulaumu wananchi wa Afrika Mashariki, na mimi nitahisi kama sitawatendea haki wenzangu niliokaa nao miaka mingi, vijijini na porini (kilingeni na utagalani), kwa kuwa ndio wao wanaojua kiswahili cha ndani Tanzania na Kenya. Si vichwa vile vya mijini ambao maandishi yao yanafanana na visuguzi na vikwabuzi vya kufutilia mbali kiswahili kile cha ndani, kile ambacho kisuguliwacho kwa dodoki na "mafuta ya nyonyo" ya kienyeji. Najitahidi, kila nikiandika kwa kiswahili-hicho-cha-mipasho (kipendezwacho na madikteta), kujizuia nisije nikachanganya kile nachozoea nacho, ambacho kimesheheni msamiati na istihali za kienyeji, si lahaja si lafudhi, ili wasomaji wangu wapate kunielewa. Lakini kujisahilisha ni wajibu kwa mwenye blogu, si kanuni wala sheria ya mwana fasihi. Kiswahili kinachochukuliwa ni kisanifu ndicho kile watumiacho wale vichwa na wanene wa mjini ambao hawajui kinachoendelea vijijini kwao. Ndio wao wanaojitahidi kudhibiti kisichofaa ili jamii ifuate "maadili" na "nyaadhi" za kisiasa.  Fasihi itawezekana katika muktadha huu wa mwafaka ? Bila shaka, kwa misaada ya "vihiyo" vile vya Chuo Kikuu na "vitaalamu" vya gengeni. Si wana nguvu na nyenzo za kuonea mburumatari na waandishi waasi wanaoleta vurugu ya kibinafsi katika jamii ? La kuchekesha ni kuona kwamba hawa vichwa — licha ya kuwazomea waandishi — mara nyingi huona kwamba kiswahili hicho kisanifu kililetwa na wakoloni. Si wazee walisema « kikulacho ki nguoni mwako » ?


Kuhusu Alain Ricard : HAPA 

Kuhusu Ebrahim Hussein : HAPA (katika lugha ya "vihiyo"), HUKUHakuna maoni:

Chapisha Maoni