11/06/2017

Athari za kusafiri

Kuishi katika nchi ulikozaliwa kuna taabu na raha zake. Raha zile tunazifahamu, kama vile chakula kile kile, jamaa wale wale, uzoefu na desturi zile zile kila siku. Na taabu zipo pia kwa sababu si rahisi kwa mtu ambaye hajatoka pahala alipozaliwa kujitambua na kujijua. Kama hujasafiri, huwezi kuelewa vizuri misingi na athari za malezi uliyoyapata. Huna mwangaza wa ulimwengu unavyokwenda na nini kinatokea. Lakini kusafiri kadhalika si dawa ya kukuzia upeo wa akili ya mtu. Hapo Afrika mashariki ninakoishi tangu zamani sana, tunaona watalii wengi jinsi wanavyoranda katika mibuga ama kwenye fukwe za pwani. Wachache sana wana elimu ya kutosha katika taaluma za ikolojia na bayolojia ambazo zinatakikana ili kuelewa mazingira asiliya ya porini. Safari kama hizo hazina maana kwa kutoleta faida yoyote katika uzoefu au tajiriba ya mtalii. Aidha katika Waafrika wanaokwenda Ulaya, ni wachache sana ambao watanufaikia mazingira ya Ulaya kwa kukosa kutembelea pahala penye vivutio vikubwa. Waafrika ni wengi sana Ulaya lakini hawana mikabala wala udadisi ule wa kuweza kuwasaidia wajenge mtizamo unaoleta faida, mathalan kusoma sayansi, usanifu majengo, usanii na kadhalika. Wengi wanatafuta tenda, ajira, posho na misaada. Hawaendi Ulaya kwa sababu wamesukumwa na udadisi ama hamu fulani. Mkabala huu mara nyingi huambatana na mazingira finyu ya elimu iliyopo Afrika. Shule za bara hii kwa jumla ni jina tu.

Kila mwaka ninasafiri Ulaya. Si kwa sababu nataka « tuhesabiwe », kama tunavyosema Bongo wakati tunaposafiri ili kutembelea jamaa zetu. Wala sina hisia zile za mshipa wa nyumbani. Aghalabu nakwenda Ulaya kusudi nijiondoe uchovu fulani wa Afrika. Afrika ni eneo la dunia lisilokuwa na ubunifu. Fikra zote zinachukuliwa na maendeleo ya miundombinu na teknolojia lakini ubunifu na uvumbuzi ni dhana ya kukopea tu, kitu cha kuiba. Leo nitachukua mfano katika ujenzi. Mimi tangu zamani ni mpenzi wa usanifu majengo. Na usanii huo hauna kifani chake katika ubunifu, ila pengine katika uchoraji. Hivyo majuzi nimerudi kutoka Venisi, mji maarufu uliopo kaskazini kwa Italia, ambao umepata sifa fulani Tanzania, angalau kwa jina tu, kufuatana na kitabu cha Shakespeare ambacho Mwalimu Nyerere aliwahi kutafsiri katika kiswahili. Kichwa cha kitabu hicho kwa kiswahili hakina maana kwa kuwa tunajua wazi kwamba Shakespeare hakuandika kitabu chochote kiitwacho Mabepari wa Venisi, kwa sababu katika kitabu cha Shakespeare, hakuna mabepari bali kuna wauzaji. Lakini si kosa kubwa sana kwa sababu huenda ubepari ulianzia Afrika. 


                                      

                                      

                                       


Venisi ni miongoni mwa miji yenye fahari nyingi duniani. Mji huo mdogo kiasi una wakaazi takriban 60 000 lakini unakaribisha watalii milioni 30 kila mwaka (Tanzania inakaribisha chini ya watalii milioni moja kila mwaka). Watalii hawa wanatokea sehemu zote za dunia, ila pengine Afrika. Ni mji mwenye historia ndefu sana kwa kuwa misingi yake ya awali iliwekwa zamani ya kale, mnamo karne 11. Majengo mengi, makanisa, maabadi na makasri mengi yalijengwa karne hizo zilizopita. La kushangaza sana ni kwamba mji huo umejengwa ndani ya maji ya bahari, ingawa karibu na ufukwe. Hapo mwanzo palikuwa na bwawa na dawe na maji yalikuwa si ya kina sana. Watu walipoanza kustakimu katika eneo hilo walitumia nguvu na ufundi mwingi ili kujenga majengo ya kudumu. Na enzi zile, kulikuwa hakuna mashine, umeme au nishati ya aina nyingine zile tanazozitumia siku hizi. Watu huwa walijenga kwa mikono tu kwa kubeba mawe na vifaa vingine kwa mashua na boti nyingine. Leo mji huo ungalipo ingawa umekumbwa na changamoto kubwa sana ya kudidimia kidogo kidogo ndani ya maji.

                                            

                                           

Wengi husema kwamba hatuwezi kulinganisha miji ya fahari kama Venisi na miji mingine ya dunia kama ile ya Afrika. Hata hivyo sielewi kwa nini mambo ya fahari mengi yalitokea katika sehemu fulani za dunia ikawa ujuzi na ufundi ule uliosababisha fahari hiyo haukuenea ukagusa sehemu nyingine za dunia. Venisi si mji wa fahari tu kwani wakaazi wake tangu zamani walizingatia namna ya kuishi — utulivu, matangamano, usikivu, ukarimu, usukuti, usafi, na kadhalika — iliyosifika dunia nzima. Huenda ni utamaduni, kama wasemavyo Wamarekani, ambao ndiyo shinikizo ile kubwa iliyosukuma watu wa Venisi kujenga mji wa ajabu kama huo. Hata hivyo, ni dhahiri kwamba hakuna usawa katika usanii. 

                                      

                                       

                                       

                                       

                                            Bonyeza picha kuzikuza

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni