01/08/2017

Urithi uliopotea Afrika (1)

Makala hii imeandikwa mwaka 2017 kwa ajili ya watu wa mwaka 2050. Hivyo isisomwe sasa hivi. Haina maana kwa sababu sisi wanadamu hatujaelewa kinachoendelea duniani. Hatujapata mwamko huo. Vizazi vya mwaka 2050 vitatukumbuka kwa kuwa sisi ndio wasaliti na wajinga wakubwa. Bado tuko katika itikadi ya kuamini kwamba dunia yetu ni supamarkiti. Na kama imejaa viumbe na maliasili zisizomalizika, sisi tujisaidie tu. Kazi yetu kuchuma tu, bila kikomo. Na mali ikimalizika, tutaunda mbinu. Si teknolojia ipo ? Vizazi ambavyo havijaja vijue kwamba sisi tunaoishi leo hii tuko katika imani ya utele wa kila kitu, upungufu wa hisia na uhaba wa maarifa wakati tunapozumgumzia mada ya uhai. Hatujui uhai ni kitu gani. Ndiyo maana tunaharibu kila kitu, misitu, chanzo cha maji, wanyama, uoto asiliya, vidudu, samaki, na kadhalika.


Courtesy@Big Life Foundation : HAPA

Nyinyi watoto wa mwaka 2050 muelewe vizuri kwamba leo hapa Afrika mashariki, wananchi kwa jumla hawajali enzi zijazo. Huendelea kuzaa — kwa kujidai kwamba « tunapenda watoto » — lakini kwa kutojali mazingira yale ambapo nyinyi watoto wa 2050 mtakapoishi. Hivyo msishangae kwamba mmekumbwa na matatizo makubwa. Mnaishi katika uchafu, uharibifu, uhaba wa maji na chakula safi na mazingira yenu yamesambaratika. Sitaji vita, uhayawani, ubedui wa kila aina na maradhi nyingi mpya ambazo zimeenea kutokana na uchafu wa mazingira. Yote hayo yamesababishwa na sisi tunaoishi leo ambao tunadharau wanachosema wana sayansi. Ndiyo wao pekee wanao uwezo huu wa kutabiri kinachokukabilieni sasa hivi. Waliposema ukweli, walipuuzwa na watu wote. Wakasemwa vibaya, wakaumbuliwa kila wakati, wakaambiwa kwamba wana muono hasi na kadhalika.

Mabadiliko hayo mabaya yalianza kukumba bara ya Afrika katika miaka ya 1980. Ndipo ongezeko la watu wa Afrika lilipoanza kushika kasi likakithiri hadi kuathiri sehemu zote za bara hiyo. Wakati China ilipokata shauri kudhibiti ongezeko la watu wake, nchi zote za Afrika zilipuuza siasa hiyo huku viongozi wake wakisema kwamba hoja hiyo ni ya kizungu. Hivyo haifai. Muelewe kwamba hilaki na nakama hizo kubwa mnazokumbwa nazo siku hizi (mwaka 2050), zote zina asili moja tu : uzembe na upumbavu wa viongozi wa Afrika, mbali na udhaifu wa elimu. Asije mtu kukwambieni kwamba maangamizi hayo yamesababishwa na ukoloni mambo leo au siasa ya nchi za kigeni. Ujinga, ukaidi na ujuba ndio sababu za pekee ambazo zimeingiza bara ya Afrika katika janga hiyo kubwa.

Makala hiyo ni aina ya utangulizi wa makala nyingine ambazo zitakuja baadaye na zitakazohusu mazingira asiliya ya Afrika — ambayo imetoweka sasa (tuko mwaka 2050) — pamoja na wanyama wake wachache ambao wamepotea kabisa kutoka dunia yetu, kama vile simba, duma, ndovu na kadhalika. Urithi huo ulikuwa hauna maana kwa Waafrika walioishi karne 20 iliyopita, hadi leo. Ingekuwa una maana ndege hawa waonyeshwao hapo penye picha nilizobandika wangekuwa wameshapata majina kwa kiswahili. Lakini hawana faida wala uchumi. Si mwaka 2050 wengi katika wao wameshakufilia mbali ?

                                     

                                     

                                     

                                     

                                     

                                     
Kutoka juu, kuanzia kushoto kuelekea kulia :

Bateleur (Terathopius ecaudatus), Superb Starling (Lamprotornis superbus), Fork-tailed Drongo (Dicrurus adsimilis), Arrow-marked Babbler (Turdoides jardineii), Fischer’s Lovebird (Agapornis fischeri), Yellow-throated Longclaw (Macronyx croceus), Wattled Starling (Creatophora cinerea), Nubian Woodpecker (Campethera nubica), Yellow-billed Oxpecker (Buphagus africanus) on zebra, Yellow-billed Oxpecker (Buphagus africanus) on buffalo, Black-headed Weaver (Ploceus cucullatus), Secretary bird (Saggitarius serpentarius), Great White Pelican (Pelecanus onocrotalus).
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni